Serikali yaahidi kuimarisha ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa waandishi wa habari ili kuhakikisha kwamba wanafanya kazi zao pasipo kusumbuliwa mahali popote wanatakapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Majaliwa ameyasema hayo leo Mei 3, 2024, wakati alipokuwa akizungumza kama mgeni rasmi kwenye siku ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika huko jijini Dodoma.
Kauli hiyo ya Majaliwa imekuja kufuatia taarifa iliyotolewa na Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratius Nsokolo, ambaye katika hotuba yake alieleza kwamba, bado waandishi wa habari nchini wanakumbana na changamoto kutolewa vitisho, kupigwa na kuachwa kwenye misafara wakati wakitafuta habari.
Akieleza juu ya ufumbuzi wa baadhi ya changamoto hizo, Majaliwa amewataka watendaji wa ofisi za Serikali kuhakikisha kuwa wanaandaa magari kwa ajili ya waandishi wa habari kwenye kila ziara ya kiongozi wa Serikali ili kupunguza usumbufu ambao waandishi wa habari wamekuwa wakikutana nao.
Serikali yawataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya kimbunga Hidaya
Serikali imezielekeza mamlaka za mikoa iliyotajwa kuwa katika hatarini kukumbwa na kimbunga Hidaya kuchukua tahadhari na kutoa taarifa kuhusu mwenendo wa kimbunga hicho pale ambapo dalili za uwepo wake zitakapojitokeza.
Akizungumza bungeni leo Mei 3, 2024, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, amewataka pia wananchi ambao wanafanya shughuli zao katika maeneo ya kando ya bahari wachukue tahadhari na kuendelea kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zinazohusiana na kimbunga hicho.
Mei 2, 2024, TMA ilieleza kuwa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa baharini inaonesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kimbunga Hidaya kusogea karibu kabisa na Pwani ya Tanzania na kitaendelea kuwepo hadi Mei 6, 2024.
Baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Unguja na Pemba yalielezwa kuwa hatarini kuathirika na kimbunga hicho.
Idadi ya watu waliofariki kutokana na mvua za El-Nino yafikia 161
Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, leo Mei 3, 2024, amewaambia waandishi wa habari jijini Dodoma kuwa idadi ya watu waliofariki kutokana na mvua za El-Nino kuanzia mwezi Oktoba 2023 imefikia watu 161.
Matinyi ameongeza kuwa idadi ya watu waliojeruhiwa imefikia watu 250 na kaya 52,000 zenye zaidi ya watu 210,000 zimeathirika kutokana na mvua hizo huku nyumba zaidi ya 15,000 pia zikiharibiwa.
Maeneo ambayo Matinyi amesema kuwa yameathirika na mvua hizo ni pamoja na Pwani, Morogoro, Mbeya, Iringa, Tabora, Dodoma, Lindi, Mtwara, Arusha, Kagera, Shinyanga, Geita, Songwe, Rukwa pamoja na Manyara.
Taarifa iliyowahi kutolewa na Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa (TMA) ilibainisha uwepo kwa mvua kubwa kuanzia mwezi Oktoba 2023 hadi Mei 2024 katika maeneo mbalimbali nchini.
Mwezi Oktoba hadi Desemba 2023, kulikuwa na ongezeko la mvua ambapo jumla ya milimita 534.5 zilipimwa ikilinganishwa na milimita 227.2 kwa mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 135.