Ukarabati wa kivuko kilichozua mjadala cha MV Magogoni kukamilika Disemba 2024
Serikali imesema kuwa ukarabati wa kivuko ambacho kilizua mjadala mkubwa kutokana na gharama zake cha MV Magogoni unatarajiwa kukamilika Disemba mwaka huu na kurejeshwa nchini ili kuendelea kutoa huduma.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi ya Mei 30, 2024, bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, wakati akijibu swali la mbunge wa Kigamboni kupitia Chama cha Mapinduzi, Dk Faustine Ndungulile, aliyeuliza ni lini matengenezo ya kivuko hicho kilichopo nchini Kenya yatakamilika na kurejeshwa nchini ili kianze kutoa huduma kwa wananchi?
Kasekenya ameongeza kuwa kuwa ukarabati unaofanyika kwenye kivuko hicho ni wa kukijenga upya kwa sababu kilikuwa kimechoka kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, hakuweza kutaja tarehe rasmi ya mwezi Disemba ambayo kivuko hicho kitawasili na kuanza kazi.
Februari 2023 Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) alisaini mkataba wa ukarabati wa kivuko cha MV Magogoni wenye thamani ya Shilingi bilioni 7.5. Kitendo hicho kiliibua mjadala mkubwa kwa sababu kivuko hicho kilinunuliwa kwa gharama ya Shilingi bilioni nane.
Kivuko cha MV Magogoni kilianza kazi mwaka 2008 kikiwa na uwezo wa kubeba tani 500, ambazo ni sawa na abiria 2,000 na magari madogo 60 na ni kiunganishi muhimu kati ya maeneo ya Kigamboni na Magogoni.
Mtoto mmoja kati ya wanne nchini Tanzania yupo katika utumikishwaji
Mtandao wa Kupinga Utumikishwaji wa watoto Tanzania umesema kuwa licha ya jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali na wadau wengine nchini, bado kumekuwa na changamoto ya watoto kuendelea kutumikishwa katika ajira zilizopo kwenye sekta mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia takwimu kuonesha kwamba takribani watoto milioni tano nchini yaani wastani wa mtoto mmoja kati ya watoto wanne wapo katika utumikishwaji wa watoto unaoendelea kwa hivi sasa.
Haya yameelezwa leo Alhamisi ya Mei 30, 2024, jijini Dar es Salaam, wakati mtandao huo na washirika wake walipokuwa wanatoa tamko lao mbele ya waandishi wa habari katika kuelekea maadhimisho ya siku ya kupinga utumikishwaji wa watoto duniani.
Maadhimisho hayo hufanyika Juni 12, kila mwaka tangu ilipozinduliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2002, kama njia ya kuonesha madhila wanayokutana nayo watoto wanaohusishwa katika utumikishwaji katika sekta mbalimbali duniani.
Kwa mwaka huu mtandao huo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu wanatarajia kufanya maadhimisho ya kitaifa ya siku hiyo mnamo Juni 12, 2024, huko mkoani Simiyu.
Lakini kabla ya kufanyika kwa maadhimsiho hayo, Juni 5, 2024, mtandao huo utafanya mjadala wa kitaifa wa kuangalia utekelezaji wa jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali na wadau wengine katika kutokomeza utumikishwaji wa watoto nchini.
Wahitimu 188,787 kidato cha nne wachaguliwa kujiunga kidato cha sita.
Wahitimu 188,787 kati ya 197,426 waliofaulu mitihani ya kidato cha nne mwaka 2023, wamechaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita pamoja na vyuo mbalimbali kwa mwaka 2024.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi ya Mei 30, 2024, jijini Dodoma na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, wakati akitangaza kuhusu uchaguzi wa wanafunzi hao mbele ya waandishi wa habari.
Mchengerwa amesema kuwa wanafunzi 131,986 wakiwamo wasichana 66,432 na wavulana 65,554 wenye sifa wamechaguliwa kujiunga na shule za sekondari za kidato cha tano 622 zikiwamo shule mpya 82 zinazoanza mwaka huu wa 2024.
Aidha, wanafunzi 1,462 wakiwamo wasichana 669 na wavulana 793 wamepangwa katika shule za sekondari nane zinazopokea wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi huku wanafunzi 6,576 wakiwamo wasichana 3,449 na wavulana 3,127 wamepangwa katika shule za sekondari za kutwa za kidato cha tano.