Serikali kumtafuta mwekezaji mwingine bandari ya Dar.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Serikali inaendelea na utaratibu wa kumpata muwekezaji mwingine katika bandari ya Dar es Salaam atakayekuwa anafanya shughuli za uendeshaji kuanzia gati namba nane hadi 11 kwa lengo la kuongeza tija katika bandari hiyo.
Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo Mei 6, 2024, bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2024/2025.
Profesa Mbarawa ameongeza kuwa utaratibu huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kushirikisha sekta binafsi katika kuiendesha bandari hiyo mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa kukabidhi kwa muwekezaji uendeshaji wa gati namba nne hadi saba.
Suala la kuwapa wawekezaji binafsi uendashaji wa bandari ya Dar es Salaam limekuwa likipingwa vikali na wadau mbalimbali hapa nchini. Oktoba 22, 2023, Tanzania ilisaini mikataba mitatu ya uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam kwa muda wa miaka 30 na kampuni ya Dubai ya DP World licha ya kuwepo kwa ukinzani mkali dhidi ya mpango huo.
Godlisten Malisa na Boniface Jacob wafikishwa mahakamani
Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob na mwanaharakati Godlisten Malisa, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu tuhuma zinazowakabili za uchochezi na kuchapisha taarifa za uongo kinyume na sheria.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani leo Mei 6, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, ambapo kwa mujibu wa Wakili wa Serikali, Neema Moshi, amesema wawili hao wameshtakiwa chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo kesi hiyo imeairishwa mpaka Juni 6, 2024, na wawili hao wameachiwa kwa dhamana baada ya kila mmoja kusaini bondi ya Shilingi milioni mbili.
Jacob na Malisa waliachiliwa kwa dhamana na Jeshi la Polisi Aprili 27, 2024, baada ya kushikiliwa kwa siku tatu katika vituo mbalimbali vya polisi. Kushikiliwa kwao kulihusishwa na taarifa walioichapisha kwenye mitandao ya kijamii mnamo Aprili 13, 2024, kuhusu kupotea kwa kijana aliyefahamika kama Robert Mushi.
Aprili 23, 2024 Jeshi la Polisi kanda ya Dar es Salaam lilitoa taarifa kuwa Mushi alifariki kwa ajali na mwili wake kuhifadhiwa Hospitali ya Polisi, habari iliyozua mjadala mitandaoni. Taarifa hiyo pia ilitoa wito kwa Jacob na Malisa kuripoti polisi kwa kile kilichodaiwa wanasambaza taarifa za uongo.
Polisi wawashikilia watu 10 kwa tuhuma za kujihusisha na mikopo ya ‘kausha damu’
Watu 10 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi katika mikoa ya Songwe na Mtwara kwa tuhuma za kujihusisha na utoaji wa mikopo ya kausha damu ambapo wanatarijiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 6, 2024, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Songwe, Augustino Senga, amesema wamewakamata watu sita kwa kufanya biashara ya kutoa mikopo bila ya kuwa na leseni kinyume cha Sheria ya Mikopo Midogo Namba 10 ya mwaka 2018, Kifungu cha 16.
Naye Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Issa Juma Suleiman, amewaambia waandishi wa habari kuwa wanawashikilia watu wanane kutoka kampuni za Mloganile Microfinance, Soulmate General Supplier Ltd pamoja na Joma Microfinance Company Ltd kwa tuhuma za kujihusisha na kosa kama hilo.
Hivi karibuni bungeni ulizuka mjadala juu ya mikopo kausha damu inayotolewa na baadhi ya taasisi za fedha rasmi na zisizo rasmi.
Mikopo hiyo ilielezwa kuwa inatesa wananchi, hivyo Serikali iliahidi kuchukua hatua za kisheria na kuona namna bora ya utolewaji wa mikopo hiyo.