The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali imeunda kamati ya kukusanya na kuchambua maoni na mapendekezo ya viwango vya nyongeza ya pensheni ili kuwezesha maandalizi ya rasimu ya waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu nyongeza ya pensheni kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina. 

Hayo yamesemwa leo Mei 7, 2024, bungeni jijini Dodoma, na Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, wakati akijbu swali la mbunge wa viti maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taska Restuta Mbongo, aliyetaka kufahamu mikakati ya Serikali juu ya malalamiko ya kikokotoo cha pensheni kwa wastaafu.

Nchemba emeongeza kuwa taarifa ya kamati hiyo na kazi ya uchambuzi wa maoni pamoja na mapendekezo ya wadau inatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 30, 2024.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na malalamiko ya wafanyakazi na wadau juu ya kikokotoo kipya katika mifuko ya hifadhi ya jamii kilichoanza kutumika Julai 1, 2022, kutokana na malipo ya wastaafu ya mkupuo kupungua kutoka asilimia 50 mpaka asilimia 33, kitu ambacho watu hao wameonekana kutokiunga mkono. 

Zaidi ya Shilingi bilioni 11 zalipwa na Serikali kwa wananchi walioathiriwa na wanyama

Serikali imelipa zaidi ya bilioni 11 kama kifuta jasho na kifuta machozi kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi Machi, 2024 kwa wananchi waliothirika na changamoto mbalimbali za wanyama wakali na waharibifu.

Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 7, 2024, bungeni jijini Dodoama, na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dunstan Kitandula, wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu kupitia CHADEMA, Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, aliyetaka kufahamu katika kipindi cha mwaka 2017 hadi mwaka 2022 ni kiasi gani cha fedha kimelipwa kama kifuta jasho kwa waathirika wa uharibifu wa mazao na mauaji yaliyofanywa na tembo.

Kitandula ameongeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii tayari imezifanyia marekebisho kanuni za kifuta jasho na machozi, na sasa ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na Wizara ya Fedha ili kupata ridhaa ya matumizi ya viwango vipya vya fidia kwa kuwa viwango vilivyopo sasa vimepitwa na wakati.

Uharibifu mkubwa wa mazao na mauaji hapa nchini yamekuwa yakifaywa na wanayama wa porini aina ya tembo. Baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia changamoto hii ni wilaya za Liwale na Nachingwea huko mkoani Lindi, lakini wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma pamoja wilaya ya Handeni iliyopo mkoani Tanga.

Serikali kuongeza idadi wa wanafunzi wanaopata mikopo ya elimu ya juu

Serikali imesema itaongeza fursa za utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka wanafunzi 223,201 hadi 252,245 kwa mwaka 2024/2025 ili kuwezesha na kuimarisha huduma ya utoaji na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa na uhitaji.

Hayo yamebainishwa na  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda,  leo Mei 7, 2024, bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha hotuba yake ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara yake kwa mwaka 2024/2025.

Akifafanua namna ya utolewaji wa mikopo hiyo, Profesa Mkenda amesema kuwa Serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi 84,500 wa mwaka wa kwanza ambapo shahada ya kwanza itahusisha wanafunzi 80,000, shahada za juu zitahusisha wanafuzni 2,000, wanaosoma nje ya nchi itakuwa wanafunzi 500, udhamanini wa masomo wa Samia utahusisha wanafunzi 2,000 na pia itatoa mikopo kwa wanafunzi 157,745 wanaoendelea na masomo.