Dar es Salaam. Leo, Septemba 2, 2024, Bunge linatarajia kupitisha au kutupilia mbali marekebisho yanayopendekezwa kwenye Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2024, hususan kifungu 10(b) kinachoeleza kwamba mtu ambaye atabainika kudai au kushwawishi kutoa rushwa ya ngono basi naye atashtakiwa.
Kipengele hicho kimeenda mbali zaidi na kueleza kuwa endapo mtu huyo atakutwa na hatia basi atahukumiwa kulipa faini au kufungwa jela na pengine kukumbana na adhabu zote kwa pamoja.
Wakitoa tamko lao mbele ya waandishi wa habari Agosti 31, 2024, Mtandao wa Kupinga Rushwa ya Ngono Nchini ulieleza kwamba endapo mapendekezo hayo yatapitishwa basi sheria hiyo itakwenda kuhalalisha na kuendeleza matumizi mabaya ya mamlaka kwa njia kumhukumu muathirika wa rushwa ya ngono kama mbinu ya kumnyamazisha na kuzima moto wa mapambano dhidi ya rushwa ya ngono.
Mtandao huo ukaendelea kueleza kwamba kifungu cha 25 kilichopo kwenye Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 kinajitosheleza na wala hakihitaji marekeisho yoyote kwani hakina mapungufu kwenye falsafa ya sheria kwa sababu kinamlinda muathirika wa rushwa ya ngono.
Kifungu hicho cha 25 cha Sheria ya Rushwa ya Ngono ya Mwaka 2007 kinamlinda muathirika wa rushwa ya ngono kwa kuwadhibiti maofisa wakuu wanaotumia nyazifa zao na madaraka vibaya kuomba kupokea na kuomba rushwa.