Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuwa uwepo wa kimbunga Hidaya maeneo ya karibu na pwani kimepelekea vipindi vya upepo mkali na mvua maeneo tofauti tangu jana.
Kwa mujibu wa taarifa ya TMA hadi kufika saa tisa usiku wa kumkia leo, kimbunga hiko kilikuwa umbali wa kilomita 125 kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi), Kilomita 93 kutoka Pwani ya Mafia na kilomita 128 kutoka pwani ya Dar es Salaam kikiwa na kasi ya upepo inayofikia kilomita 120 kwa saa.
Hali hii imepelekea kuwepo kwa mvua kubwa juu ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Mtwara na Lindi, huku maeneo ya Dar es Salaam, Mtwara, Kilwa na Zanzibar yakishuhudia upepo mkali unaoenda kilomita 50 kwa saa.
TMA imeeleza kuwa kimbunga HIDAYA kitaendelea kusogelea maeneo ya pwani na kinatarajiwa kupungua nguvu kuelekea usiku wa Mei 5, 2024. Hivyo wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari.