Dodoma. Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwandisi Hamad Masauni leo amekutana na viongozi wa juu wa Jeshi la Polisi Tanzania kujadili hali ya amani na usalama ikiwemo matukio ya uhalifu yanayotkea nchini na hatua zilizochukuliwa.
Kikao hiko pia kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya ndani, Daniel Sillo, ambapo kwa upande wa Jeshi la Polisi ujumbe wake uliongozwa na Inspekta Jenerali wa Polisi, Camillus Wambura.
Kikao hiki kinakuja ikiwa ni siku chache tangu Jeshi la Polisi kupitia kwa msemaji wake kutoa taarifa za matukio mbalimbali ya kiuhalifu yanayohusu watu kupotea na mauaji ambayo Polisi ilieleza yalitokana na sababu mbalimbali ikiwemo masuala ya kujichukulia sheria mkononi, wivu wa mapenzi na imani za kishirikina.
Lakini pia wadau mbalimbali ikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Asasi za Kiraia na vyama vya siasa wamekuwa wakipaza sauti kufuatia kuripotiwa kwa matukio ya utekaji na mauaji ya watu wazima na watoto. Baadhi ya wadau hao ikiwemo vyama vya siasa wamewatupia lawama Jeshi la Polisi wakiwashtumu kuhusika jambo ambalo wamelikanusha.
Kikao hiko cha Waziri Masauni kilihudhuriwa na viongozi wote wa kamisheni za Polisi ikiwemo Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimaliwatu, Suzan Kaganda, Kamishna wa Fedha na Lojistiki, Liberatus Sabas, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Awadh Juma Haji, Kamishna wa Sayansi ya Uchunguzi wa Jinai, Shabani Hiki.
Wengine ni Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai CP Ramadhani Kingai, Msemaji wa Jeshi la Polisi, ACP David Misime, Naibu Kamishna kutoka Kamisheni ya Intelijensia na Jinai, Kheriyangu Khamis Mgeni, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro.