The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mamlaka Ngorongoro, Wananchi Wavutana Ufadhili wa Wanafunzi Elimu ya Juu

Wanafunzi wadai kusitishiwa ufadhili wa masomo, au kucheleweshewa malipo, bila taarifa, hali wanayosema inawasababishia usumbufu mkubwa.

subscribe to our newsletter!

Kuna sintofahamu inaendelea kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Baraza la Wafugaji Tarafa ya Ngorongoro (NPC) inayohusiana na madai kwamba mamlaka hiyo imesitisha, bila taarifa, ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka Ngorongoro wanaosoma katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini, au kuchelewesha malipo kwa wanafunzi hao.

NCAA, ambayo inaendesha eneo hilo la Hifadhi ya Ngorongoro, imekuwa na utaratibu wa kufadhili masomo kwa wanafunzi kutoka kaya masikini zinazopatikana kwenye eneo hilo tangu angalau mwaka 1994, huku watu takriban 14,000 wakikisiwa kunufaika na utaratibu huo unaowalenga wanafunzi wa elimu ya awali mpaka wale wa chuo kikuu wanaopendekezwa na NPC.

Lakini kwa siku za hivi karibuni, vyombo hivyo viwili vimejikuta vikiwa kwenye sintofahamu baada ya NPC, na baadhi ya wanufaika, kuishutumu NCAA kusitisha ufadhili kwa baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu, au kuwacheleweshea malipo, kinyume na utaratibu, hali inayoripotiwa kuwasababishia wanafunzi usumbufu mkubwa na kuwalazimisha wengine kufikiria kusitisha masomo yao.

Kwa mujibu wa maelezo ya wanafunzi waathirika na viongozi wa NPC, Serikali imekatisha ufadhili wa wanafunzi 55 wa vyuo vikuu na vyuo vya kati kwa mwaka wa masomo 2023/2024, huku ikiwatelekeza wanafunzi wengine wapatao 99 wa vyuo vikuu na vyuo vya kati wa mwaka wa masomo 2022/2023, katika kile wanajamii wanasema ni kinyume na makubaliano ya awali.

Hata hivyo, Msemaji wa NCAA, Hassan Dammbaya, amekanusha madai hayo, akidai kuwa kilichotokea kwa mwaka 2023/2024 ni kuwa NPC lilipeleka watoto wengi zaidi ya idadi iliyohitajika na mamlaka.  

Bajeti

“Baraza lilituletea wanafunzi wa vyuo vya kati 110, kinyume kabisa na bajeti iliyotolewa ya kusomesha wanafunzi 55 wa vyuo vya kati,” Dammbaya aliiambia The Chanzo. “Kwa hiyo, walipotuletea wanafunzi hawa 110, sisi tuliwaambia bajeti yetu ni [wanafunzi] 55.

SOMA ZAIDI: Serikali Ilikamata Mifugo 30,000 Mwaka 2022. Kilio Chaendelea Mifugo Zaidi Ikitaifishwa Loliondo, Ngorongoro

“Lengo ni kusomesha wanafunzi. Fedha hizi siyo za mhifadhi wala mimi Dammbaya, ni fedha za Serikali. Fedha zikiwepo, wanafunzi wote watasomeshwa, lakini kama fedha hatuna, tunafanyaje? Tunasomesha kulingana na bajeti tuliyokuwa nayo.”

Wakati Mwenyekiti wa NPC, Edward Nduleti, hana shida na ufafanuzi huu kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa masomo wa 2023/2024, anahoji kwa nini Serikali haikutoa ufafanuzi huo kwa wanafunzi takriban 99 wa mwaka wa masomo 2022/2023, ambao nao pia wamesitishiwa ufadhili.

“Kama kungekuwa kuna mabadiliko yoyote, basi [NCAA] wangetuambia kwamba kutokana na matatizo ya kibajeti hatutaweza kupeleka watoto 110 tutawapeleka hawa,” alilalamika Nduleti. “Mpaka sasa hivi sisi tunajua bado mamlaka itawalipia wale watoto ada na inabidi iwalipie kwa sababu ni jukumu lao la kisheria siyo hisani.” 

Lakini akizungumza na Watetezi TV kuhusu madai haya ya wanafunzi wa 2022/2023, Dammbaya alisema hakuna kesi ambapo NCAA imekatisha ufadhili wa masomo kwa wanafunzi ambao ilikubali awali kufadhili masomo yake ya elimu ya juu.

“Tukishakubali kukosomesha, kama hakuna changamoto ya kuachishwa masomo, au kufariki, ule mchakato wa wanafunzi kusoma unaendelea mpaka pale [mwanafunzi] atakapohitimu,” alisema afisa huyo. “Kama kuna kesi za aina hiyo, kwamba kulikuwa na mwanafunzi anafadhiliwa na NCAA lakini ghafla tu halipiwi tena, sisi hatujapata malalamiko hayo.”

Tumetelekezwa

Laraposho Leizer, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ameiambia The Chanzo kwamba yeye na wenzake wamekuwa wakilipiwa ada na kupewa fedha za matumizi na NCAA, lakini tangu mwaka 2021 zoezi hilo limekuwa likifanyika kwa kuchelewa sana. 

SOMA ZAIDI: Ufafanuzi Mdogo wa Kile Kinachoendelea Ngorongoro

Leizer ametolea mfano kuwa kwa mwaka huu wa 2024, muhula wake wa pili wa masomo ulianza tangu mwezi Machi, lakini wamekuja kupewa fedha hizo mwezi huu wa Mei, kitu ambacho anadhani kuwa si sahihi.  

“Ada tunalipiwa kweli, na pesa za matumizi tunapewa, lakini hazifiki kwa wakati, kuanzia mwaka 2021 kumekuwa na hiyo changamoto,” anasema Leizer. 

“Hebu fikiria kwamba umempeleka mwanafunzi kuanzia Januari, unakuja kumpa fedha mwezi Mei, unafikiria kama umempeleka mwanafunzi Dar es Salaam ambapo anakuwa amepanga, anahitaji kulipa fedha ya vitabu, anahitaji kula, anahitaji kulipa umeme, anahitaji kulipa maji, vitu kibao unalipa, hiyo miezi minne, mitatu mwanafunzi anakuwa anaishi katika mazingira gani?” alihoji Leizer. “Kwa hiyo, unakuta wanafunzi wanakuwa wanapitia hali ngumu kitu ambacho siyo sawa.”

Megoliki Naidosi ni mkazi wa kijiji cha Endulen kilichopo wilaya ya Ngorongoro na mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es Salaam, akisomea shahada ya uhasibu, akifadhiliwa na NCAA tangu darasa la kwanza, ambaye anafikiria kuacha masoma baada ya kudai kusitishiwa ufadhili.

“Itanibidi niingie mtaani sasa,” anasema Naidosi kwa sauti inayoashiria kukata tamaa. “Masomo itabidi nisitishe kwa muda kidogo, nitafute fedha, kwa sababu kama mtu alikuleta halafu akaja akakutema, unakuta ada ni kama Shilingi 2,000,000 unaipatia wapi, na mtu alikwambia anakulipia?” 

SOMA ZAIDI: Kuwaondoa Wananchi Ngorongoro ni Shambulio Dhidi ya Ufugaji wa Asili

“Wametufanyia kitu ambacho siyo cha kibinadamu kabisa, unafikiria yaani huyu mtu alikuwa na maana gani? Kwa sababu huwezi ukamtoa mtu nyumbani halafu ukaja ukamtema bila kumtaarifu. [Ni bora] ungemtaarifu mapema kwamba [wewe] haupo, baada ya hapo angeondoka au angetafuta namna nyingine ya kuishi.

“Umetoka huko nyumbani, walikuwa wanakufadhili kwa sababu ya ugumu wa maisha, wamekuleta huku halafu wanakuja kukutema [kwa hiyo] lazima usitishe masomo,” alilalama Naidosi.

Kukatwa huduma za jamii

Madai haya kusitishwa kwa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Ngorongoro au kucheleweshewa malipo yanakuja wakati ambapo Serikali imedaiwa kukata huduma za msingi za kijamii katika eneo la Ngorongoro kama sehemu ya mkakati wake wa kuwahamisha watu kutoka kwenye eneo hilo linalotambuliwa kama urithi wa dunia.

Mmoja wa watu waliowahi kuyaeleza wazi madai haya ni Mbunge wa Ngorongoro kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Emmanuel Oleshangay, ambapo Arili 8, 2024, akiwa bungeni jijini Dodoma, aliishutumu Serikali kusitisha huduma za kijamii kwenye eneo la Ngorongoro. 

Hata hivyo, Dammbaya ameiambia The Chanzo kuwa hakuna usitishwaji wa huduma za kijamii kwenye eneo la Ngorongoro, akidai kwamba zoezi la kuhama ni la hiari na kwamba huduma mbalimbali za kijamii zinaendelea kutolewa ndani ya eneo hilo.

“Shule zinaendelea, zahanati zinaendelea, vituo vya afya vinaendelea na shughuli nyingine za wananchi zinaendelea na ni kitu ambacho ni kizuri sana,” alisema Dammbaya. “Wafugaji wanaendelea kufuga mifugo yao, hakuna mtu yeyote anayezuiwa, hakuna mtu yeyote anayesukumwa, hakuna kitu chochote kibaya ambacho wananchi hawa wanafanyiwa.”

Modesta Mwambene ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka Mbeya anayepatikana kupitia mwambemo@gmail. Lukelo Francis amehariri habari hii.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *