The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uzoefu wa Wanasiasa Wakongwe na Ushauri Wao kwa Wagombea Vijana, Wanawake Kuelekea Chaguzi 

Vijana na wanawake wametakiwa kuchangia ujenzi wa vyama vyao kwani hiyo itaongeza uwezekano wa wao kupewa ridhaa na vyama hivyo kwenye chaguzi za nchi.

subscribe to our newsletter!

Mtwara. Vijana na wanawake ambao wanatarajia kugombea kwenye kura za maoni ndani ya vyama vyao vya wametakiwa kujitoa kwa kiasi kikubwa kushiriki katika kujenga na kuimarisha chama, lakini pia wajiamini na kujiweka katika nafasi za kupigiwa kura ili watakapoomba ridhaa ya kugombea iwe rahisi kupata. 

Aidha, makundi hayo pia yametakiwa kuhakikisha yanatimiza matarajio ya wanachama wao kwa kiwango cha juu pale ambapo watawapa nafasi ya kugombea uongozi fulani na kushinda kwa ajili ya kujenga imani kwa wanachama wao na kuwawezesha kuendelea kupewa nafasi ya kugombea. 

Haya yalibainishwa Juni 13, 2024, kwenye mkutano ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la International Republican Institute (IRI), mkutano ambao umepewa jina la Ready to Run and Serve For Women and Youth in Tanzania.  

Mkutano huo ambao unamalizika Juni 14 umeandaliwa kwa lengo la kuyajengea uwezo makundi hayo kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu hapo mwakani, 2025, ukiwaleta pamoja wanasiasa ambao wamewahi kushika nyadhifa mbalimbali na vijana na wanawake wenye nia za kugombea kwa ajili ya kubadilishana maarifa. 

Kwenye mkutano huo, IRI imetumia mtaala wake ulioboreshwa unaofahamika kama ‘Kutoka Kushinda Hadi Kutawala,’ wenye lengo la kuwalea na kuwasaidia wagombea vijana kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa ya nchi yao.

Changamoto 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi Mkazi wa IRI Tanzania, Sentell F. Barnes, alibainisha kuwa wamewakutanisha pamoja vijana na wanawake kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kiuongozi kutokana na kwamba licha ya kuwa makundi hayo yana idadi kubwa ya watu, wao ndiyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi kwenye jamii.

SOMA ZAIDI: Je, Tuwatazame Vijana Kama Kundi Maalumu Tanzania?

“Ongezeko la vijana hapa Tanzania linaweka changamoto kwa viongozi wa baadaye,” alisema Barnes. “Viwango vya juu vya ukosefu wa ajira kwa vijana, upatikanaji mdogo wa elimu bora na huduma za afya, na fursa zisizotosha za ushiriki wa maana katika michakato ya kufanya maamuzi ni miongoni mwa changamoto kuu zinazowakabili vijana nchini.”

“Baadhi ya fursa na changamoto ni za kiujumla kati ya vijana na wanawake; wanawake wanakabiliwa na masuala ya upendeleo wa kijinsia, ubaguzi, na upatikanaji usio sawa wa rasilimali ambao unaweza kuzuia mchakato wa uchaguzi kwa wanawake,” aliongeza Barnes. 

“Wanawake katika siasa mara nyingi wanakabiliwa na uchunguzi mkubwa zaidi wa muonekano wao, maisha yao binafsi, na uwezo wao wa uongozi kuliko wenzao wa kiume.

“Hivyo, ni muhimu wanawake na vijana kugombea nafasi za uongozi. Tunataka kuhakikisha kwamba kuna kundi tofauti la watu mezani tunapojadili masuala muhimu yanayoikabili nchi. Tunahisi kwamba wanawake na vijana wataleta mitazamo mipya na uzoefu mbalimbali kwenye meza ya majadiliano.”  

Maandalizi makubwa 

Zitto Kabwe ni mwanasiasa mkongwe ambaye amewahi kugombea kupitia vyama viwili vya upinzani vya CHADEMA pamoja na ACT-Wazalendo na akashinda. Si hilo tu, mwanasiasa huyu amewahi pia kugombea ubunge katika majimbo mawili tofauti ya Kigoma Kaskazini na Kigoma Mjini na akashinda. 

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwa na Baraza la Vijana Huru na Lenye Sura ya Kitaifa?

Kwa mara ya kwanza aligombea mwaka 2005 katika jimbo la Kigoma Kaskazini na akarejea tena kwenye jimbo hilo mwaka 2010, kisha mwaka 2015 akagombea jimbo la Kigoma Mjini na mara zote hizo alishinda kabla ya kushindwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 aliogombea kwenye jimbo la Kigoma Mjini. 

Uzoefu huu wa Kabwe unamfanya aeleze kuwa ili vijana na wanawake waweze kushinda kwenye kura za maoni za vyama vyao ni muhimu wakafanya maandalizi makubwa ya kujenga taasisi za vyama vyao kwani kwa kufanya hivyo wanachama wenzao hawataweza kuwatupa kwa sababu watakuwa wanafahamu kama ni wanachama wenzao halisi. 

“Kazi ya kwanza ambayo nyinyi mnapaswa kufanya, kwa wale ambao mnatoka vyama ambavyo ni vipya, kwa maana vyama vya upinzani ambavyo tayari vina muundo wa chama na chama tawala ambacho tayari kina muundo wa chama, wajibu wa kwanza ni ama kuimarisha chama kwa kufanya kazi na wale viongozi ambao utakutana nao, au kuwa na ukaribu na viongozi ambao watakuja kupiga kura kwa ajili ya kuchagua wagombea,” alisema Kabwe.

“Kwa watu wa upinzani ambao chama unakuta hakipo, inabidi wewe ndiyo ukipeleke, kazi ya kwanza muhimu kuliko yote ni kujenga mtandao wa chama,” aliongeza Kabwe. “Mara nyingi huwa nawaambia vijana, mtandao wa chama ukiwepo ni uhakika wa ushindi kwa asilimia 30, kama huna mtandao wa chama hauwezi ukashinda.”

Kwa upande wake, Zainab Mdolwa, ambaye ni mbunge wa viti maalum mstaafu kutoka Chama cha Wananchi (CUF), alisema kuwa vijana na wanawake wengi wamekuwa na hofu kubwa linapokuja suala la kugombea, hali inayowafanya kubaki kuwa wapiga kura kwenye chaguzi. 

SOMA ZAIDI: Vijana Wachachamaa Wakitaka Umri wa Kugombea Upunguzwe

Mdolwa, 54, anaeleza kuwa kwa mara ya kwanza alijitosa kuomba ridhaa ya kukiwakilisha chama chake kwenye uchaguzi wa mwaka 2000 na akakosa, lakini hakukata tamaa mpaka alipokuja kupata ubunge wa viti maalumu mwaka 2015.

Baada ya kuitumikia nafasi hiyo kwa ufanisi aliomba ridhaa ya kuwania ubunge jimbo la Temeke kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 na chama chake kikampa nafasi hiyo aliyoipigania lakini hakushinda na sasa anajipanga upya. 

“Ili vijana waweze kushiriki kikamilifu katika chaguzi za ndani ya chama ni lazima wajitahidi wasiwe wapiga kura tu, waingie moja kwa moja kushiriki [kugombea],” anasema Mdolwa ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi wa CUF. “Kwa sababu tunaona kundi kubwa la kina mama ni wapiga kura, wanatumika kupitisha viongozi.” 

“Ninachoomba vijana tuwe karibu na wanachama wetu, zinapotokea fursa, hususan mwaka huu 2024, tujaze fomu kuanzia Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji tujitokeze na mbinu ni kuwa karibu na wanachama wako muda wote. 

“Siyo wakati wa uchaguzi ndiyo unaonekana unaenda kugombea, kila mtu anauliza huyu katoka wapi, kaletwa na nani? Kwa kushiriki katika shughuli za kisiasa kwenye kata, kwenye majimbo, kwenye wilaya hii itakupelekea kuweza kushinda na kuweza kujulikana.” 

Mnakatisha tamaa

Catherine Ruge ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia amewahi kuwa mbunge wa viti maalumu kati ya mwaka 2017 na 2020. Ruge anaeleza kuwa pamoja na kwamba kumekuwa na juhudi nyingi za kuwapa nafasi za uongozi wanawake na vijana, makundi hayo yamekuwa yakiwakatisha tamaa wapiga kura baada ya kupewa nafasi. 

SOMA ZAIDI: Sababu za Mwamko Mkubwa wa Vijana Kugombea Nafasi za Uongozi Zatajwa

Ruge amesema hali hiyo imepelekea vijana wasipewe nafasi wakati mwingine kutokana na wale ambao walipewa nafasi walishindwa kukidhi matarajio makubwa ambayo wapiga kura wengi walikuwa nayo kwao. 

“Wengi wetu, hasa wanawake na vijana, tumekuwa tukiwakatisha watu tamaa,” anasema Ruge ambaye kwa sasa ni Katibu wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA). Hata kwenye Serikali, vijana wameaminiwa lakini wamewakatisha watu tamaa.” 

“Hii inawafanya watu wanaondoa imani kwenye jamii wanasema hawa vijana wameaminiwa lakini hawafanyi kazi vizuri au mwanamke fulani ameaminiwa lakini hafanyi vizuri,” anaongeza mwanasiasa huyo. “Kwa hiyo, sisi ambao tunapewa nafasi, uwe mwanamke, uwe kijana hakikisha unaonesha uwezo wako ili kuifanya jamii iendelee kuwaamini wanawake au vijana.”

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com. Lukelo Francis amehariri habari hii.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *