The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tunawezaje Kuwa na Baraza la Vijana Huru na Lenye Sura ya Kitaifa?

Matarajio ya vijana wengi ni kuona wanakuwa na chombo kitakachoweza kuwaunganisha vijana wote nchini bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, kidini na kikabila

subscribe to our newsletter!

Ni mwaka sasa umepita tangu Waziri Joyce Ndalichako atoe taarifa kuwa Serikali ipo mbioni kuanzisha  Baraza la Vijana la Taifa la Tanzania Bara mara baada ya kukamilika kwa mchakato wa maboresho ya Sera ya Taifa ya Vijana ya mwaka 2007 unaoendelea.

Ikumbukwe kuwa Sheria ya Baraza la Vijana ilitungwa tangu mwaka 2015 na kanuni za Baraza hilo zilitangazwa kwenye gazeti la Serikali namba 348 tarehe 15 Septemba 2017. Ni miaka sasa imepita lakini bado hakuna kilichotekelezwa.

Matarajio ya vijana wengi ni kuona wanakuwa na chombo kitakachoweza kuwaunganisha vijana wote nchini bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, kidini na kikabila katika katika kutambua, kuchambua na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Baraza la Vijana siyo jambo geni katika mataifa mbalimbali hata hapa Afrika. Nchi za Kiafrika yenye mabaraza rasmi ya kitaifa ya vijana ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Afrika Kusini, Namibia na nyingine nyingi. Hata kwa hapa Tanzania upande wa Zanzibar lipo Baraza la Vijana tangu mwaka 2013.

SOMA ZAIDI: Je, Ni Kweli Ushirikishwaji wa Vijana Kwenye Uongozi Tanzania Ni Hafifu?

Chombo hiki kinapaswa kuwa sauti ya vijana kwenye mambo ya msingi ya kitaifa, mathalani hivi karibuni wakati Waziri wa Mipango na Uwekezaji akizindua Kamati ya  Dira ya Taifa 2050, kama Baraza lingekuwepo, basi vijana wangekuwa na uhakika wa uwakilishi wa maoni yao juu ya Tanzania waitakayo miaka 25 ijayo kupitia chombo chao. 

Ukiacha masuala ya ndani ya nchi kama hayo, kuna uwakilishi wa kimataifa vijana wa Kitanzania wanakosa kutokana na kutokuepo kwa Baraza hili. Matokeo yake tunakua na wawakilishi ambao wanatuwakilisha kibinafsi. Kwa hili hatuwatendei haki vijana wa Kitanzania.

Sasa kama niliovyoeleza, kwa vile serikali ya Tanzania ilishaanza mchakato wa kuunda Baraza hilo na Waziri alitoa taarifa juu ya mchakato unaoendelea wa mapitio ya Sera ya vijana ya mwaka 2007, naona ni vyema nikafanya mapitio kidogo ya Sheria na Kanuni ambazo ndio zitakuwa msingi wa kuanzishwa kwa chombo hiki..

Nitajikita zaidi kujadili na kuuchambua muundo wa Baraza uliopendekezwa kwa kuangalia ngazi ya taifa kama unaakisi kuwa na Baraza la Vijana huru na lenye sura ya kitaifa. 

SOMA ZAIDI: Vijana wa Siku Hizi ni Zao la Wazee wa Siku Hizi. Tuwe na Akiba ya Maneno Tunapowasimanga

Muundo wa Baraza la Vijana

Muundo wa Baraza una ngazi tano ambazo ni Baraza la Vijana la Taifa, Baraza la Vijana la Mkoa, Baraza la Vijana la Wilaya, Baraza la Vijana la Kata na Sekretarieti. 

Kwa mujibu wa sheria hiyo  kifungu 4(3), uanachama wa Baraza unaanzia kwenye ngazi ya kata na utakua wa wazi na wa hiari kwa vijana kutoka kata husika, Asasi za Vijana zilizo sajiliwa kitaifa, na vijana waliochaguliwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata kwa mujibu wa sheria.

Kwa mujibu wa Sheria, katika ngazi ya taifa Baraza litakuwa na wajumbe 29 ambao ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mtendaji na wajumbe 26 kutoka mikoa ya Tanzania Bara.

Baraza litakua na mkutano mmoja kila mwaka. Majukumu ya mkutano huo  ni: Kumchagua Mwenyekiti na Makamu, kupendekeza wajumbe wa Bodi ya Ushauri, kuridhia mipango ya maendeleo, mikakati na programu za Baraza, na kupokea, kutathmini na kuridhia utekelezaji wa mipango, mikakati na programu.

Sasa mpaka hapo sina tatizo na muundo wa Baraza na utendaji kazi kama ilivyopendekezwa. Changamoto inayoibuka ni namna hawa watu watakavyopatikana kwa mujibu wa Sheria na kanuni.

SOMA ZAIDI: Vijana Wachachamaa Wakitaka Umri wa Kugombea Upunguzwe

Mfumo wa upatikanaji wa wajumbe na viongozi hawa unapaswa kuhakikisha hautoi  fursa ya kuwa na Baraza la Vijana ambalo kwa kiasi kikubwa litaathiriwa na siasa za vyama na kuingiliwa kiutendaji na Mamlaka za Serikali.

Hivyo naona ni muhimu yafanyike marekebisho ya Sheria  ambayo yataweka mipaka kama vile kuzuia makada na viongozi wa vyama vya siasa kuwa wajumbe wa mabaraza haya kuanzia ngazi ya sekretarieti mpaka  kitaifa. 

Mtu yoyote ambaye ni kiongozi au amewahi kushika nyadhifa kwenye vyama vya kisiasa  inabidi azuiliwe kua na ujumbe kwenye mabaraza haya. Hii itasaidia Baraza lifanye kazi kwa maslahi ya wote bila kuangalia itikadi za kivyama.

Bodi ya Ushauri ya Baraza la Vijana

Chombo kingine muhimu kwenye muundo wa Baraza la Vijana la Taifa ni Bodi ya Ushauri ya Baraza ambayo itaundwa na Mwenyekiti atakayeteuliwa na Raisi, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana, Afisa Sheria na vijana 5 watakaochaguliwa na Baraza na kuridhiwa na Waziri.

Kazi ya Bodi hii itakua ni kulishauri Baraza kwa ujumla katika utekelezaji wa mamlaka na kazi zake zilizoainishwa chini ya sheria, Kufanya kazi zingine kama itakavyopewa au itakavyo elekezwa chini ya sheria ya Baraza la Vijana.

Sina shida na huu muundo, ila nina maoni ya marekebisho kadhaa ili kuwezesha kuwa na Baraza la Vijana litakalokidhi matarajio na malengo ya vijana kama nilivyoeleza awali.

Mosi, hakuna sifa ya umri kwenye Bodi hiyo. Japo kuna wajumbe kwa mantiki ya nafasi zao watakua ni vijana ila nafasi kama ya Mwenyekiti wa Bodi, na Mkurugenzi wa Vijana hazionyeshi vigezo vya umri. 

Kwa kuwa nafasi hizo zitahitaji mtu mwenye uzoefu fulani wa kitaalamu sina shida wakiwa na umri zaidi ya 35 ila busara zioneshe kuwa hupaswi kuwa na wazee kwenye Bodi ya Baraza la Vijana. Ningeshauri Mwenyekiti wa Bodi na kwa Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka wizarani  awe mtu asiezidi umri wa miaka 40. 

Haitaleta  maana kama Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Vijana na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeo ya vijana ambao ni wazee kuwa wajumbe wa Bodi ya Ushauri.

SOMA ZAIDI: ‘Samaki Mkunje Angali Mbichi’: Shule Zinavyoandaa Vijana Dhidi ya Vitendo vya Rushwa

Ukakasi mwingine niliokua nao ni Mwenyekiti wa Bodi kuteuliwa na Raisi na vijana watano kuridhiwa na waziri. Kuhusu Mwenyekiti wa Bodi ningeshauri nafasi itangazwe wazi na wenye sifa na vigezo waombe kazi hiyo na kufanyiwa usaili. Iundwe jopo la wataalamu ambao watapitia wasifu wa kila muomba kazi na kuwafanyia usaili ambao utakua wa wazi. 

Hii itaepusha muonekano wa Raisi kumteua mtu ambae ataonekana ni mtu wake kwenye nafasi ambayo haipaswi kuripoti moja kwa moja kwake. Pia wale vijana watano wanaochaguliwa na Baraza wapite bila kuhitaji ridhaa ya waziri husika. 

Nia na madhumuni ya haya ni ili Baraza lisionekane kwa namna moja au nyingine kuegemea upande wowote ule wa kisiasa au kuonekana kama chombo kilichopo kwa manufaa ya Serikali na sio vijana.

Kamati ya Uchaguzi ya Baraza

Kipengele kingine muhimu cha kutazama ni Kamati ya Uchaguzi ya Baraza. Kwa mujibu wa kifungu  24(2) cha kanuni za sheria za Baraza la Vijana la Taifa, kutakua na Kamati ya Usimamizi wa Uchaguzi yenye wajumbe 9 watakaoteuliwa na waziri anaehusika na maswala ya vijana. 

Wajumbe hao ni watu watatu kutoka  wizara inayohusika na masuala ya vijana, Mjumbe mmoja kutoka wizara inayohusika na masuala ya maendeleo ya jamii, jinsia na watoto, Mjumbe mmoja kutoka TAMISEMI, Mjumbe mmoja kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe watatu wenye uelewa wa masuala ya vijana kutoka Sekta ya Umma

Wajumbe hao 9 watachagua miongoni mwao Mwenyekiti na Katibu ambao ndio watasimamia na kuratibu shughuli za chaguzi wa Baraza kwa ngazi zote. 

SOMA ZAIDI: Tunavyoweza Kuwawezesha Vijana Kuwekeza Zaidi Kwenye Uchumi wa Buluu

Hapa tatizo ni lilelile, kwamba Serikali itakua imehodhi mchakato mzima wa uchaguzi haswa ukizingatia wajumbe wote 9 watakua ni waajiriwa wa Serikali wanaoteuliwa na Waziri. 

Muundo wa Kamati hii unawezwa boreshwa kupunguza ushawishi wa Serikali kwenye chaguzi za Baraza. Japo hatuwezi kuiondoa kabisa Serikali kwenye mchakato huu tunaweza walau kupunguza uhusika  wake kwa kiwango kikubwa kwenye Baraza.

Mimi nashauri kuwepo na wajumbe watano wa Serikali wanaoteuliwa na Waziri na wajumbe watano kutoka Asasi za Kiraia na Sekta Binafi ambao si wateule wa waziri. 

Kwa kuongeza, kwa ujumla muundo wa Baraza ulipaswa kuzingatia nafasi ya kundi kama la wanataaluma tofauti na sasa. Muundo uliopedekezwa kwa sasa unafanya kazi nzuri ya uwakilishi wa kimaeneo nchi nzima lakini sijaona taaaluma ikizingatiwa. 

SOMA ZAIDI: Sababu za Mwamko Mkubwa wa Vijana Kugombea Nafasi za Uongozi Zatajwa

Baraza la Vijana kabla ya 2025

Rai yangu kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako, ni kukamilika kwa mchakato huu na kuhakikisha tuna Baraza la Vijana linakuwepo  ifikapo mwaka 2025. 

Asilimia 60 ya Watanzania ni vijana hivyo yawapaswa kuwa na chombo chao kitakachopigania maslahi yao haswa kwenye maswala ya kisera. Kinachohitajika tu ni utashi wa kisiasa kuweza kulikamilisha hii. Na rai yangu kwa vijana, haswa kwa wale waliobahatika kuwa na sauti au ushawishi waweze kulipigania hili swala ipasavyo. 

Thomas Joel Kibwana ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na uhusiano wa kimataifa. Unaweza kumpata kupitia thomasjkibwana@gmail.com au Twitter kama @tkibwana. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com  kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *