The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tunavyoweza Kuwawezesha Vijana Kuwekeza Zaidi Kwenye Uchumi wa Buluu

Bado kasi ya vijana wa Kitanzania kushiriki kikamilifu kwenye kuvuna fursa zinazotolewa na uchumi wa buluu hairidhishi.

subscribe to our newsletter!

Sekta ya uvuvi ni miongoni mwa sekta muhimu za uchumi nchini Tanzania inayochangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa na juhudi za kutokomeza umaskini. Sekta hii inajumuisha shughuli zote za uvuvi wa asili na ukuzaji wa viumbe maji kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisasa. 

Kwa mwaka 2022, kwa mfano, sekta hii ilikuwa kwa asilimia 2.5 na ilichangia silimia 1.8 ya pato la taifa, takwimu za Serikali zinaonesha

Takriban Watanzania milioni 4.5 wamepata ajira kupitia sekta ya uvuvi katika mnyororo mzima wa sekta hiyo, huku ajira za moja kwa moja za wavuvi zikiwa 195,000 na wakuza viumbe vya majini 31,998, takwimu hizo za Serikali zinaonesha.

Tanzania kuna bahari, mito na maziwa ambayo yanaweza kutumika vizuri kwenye uvunaji wa viumbe maji watakaoweza kusafirishwa na kuuzwa kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi kupitia soko huria la nchi wanachama.

Kwa mwaka 2021/2022, meli sita zilipatiwa vibali kwa ajili ya uvuvi mkubwa wa kibiashara ambapo meli tatu ni za nje ya nchi na tatu ni za wawekezaji wa ndani. 

Vijana na uwekezaji

Hata hivyo, kunaonekana kuwepo kwa kusuasua kwa wawekezaji wa ndani, hususan vijana, kwenye kuchangamkia fursa zitokanazo na uchumi wa buluu nchini, hususan ule unaohusisha na kutafuta masoko nje ya nchi.

Kwa kawaida, ni ngumu kwa kijana aliyehitimu chuo na aliyepo mtaani kuzitazama fursa za nje ya nchi kwani wengi wanaamini ni kitu kigumu na kisichowezekana. 

Hali hii inapelekea vijana wengi wajasiriamali wadogo, na muda mwingine hata wakubwa, kuwekeza nguvu nyingi nchini bila kuwa na mawazo ya kuvuka mipaka na kuanzisha viwanda na makampuni nje ya Tanzania.

Pia, ukosefu wa elimu mahususi juu ya uwekezaji na usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi ni kikwazo kwa vijana wengi wa Kitanzania, hususan wanaohitimu vyuo vikuu. 

Kwa kuwa mfumo wa elimu unamtaka mwanafunzi ajue zaidi katika masomo ya darasani, hii imefanya wanafunzi wengi wa vyuo kutojua mambo mengine ya kibiashara nje ya masomo. 

Kwa mfano, mwanafunzi anayechukua masomo ya Kiswahili na Historia, ni ngumu kujihusisha na masomo ya biashara; namna ya kuanzisha kampuni nje ya nchi; namna ya kusafirisha bidhaa bandarini; nakadharika. 

Hii inapelekea vijana kutojiingiza kwenye biashara zinazojumuisha Bara la Afrika, hali inayowaweka vijana wa Kitanzania nje ya ulingo wa kifursa uliopo nje ya mipaka ya nchi yao.

Itakumbukwa kwamba mnamo mwaka 2021, Serikali iliridhia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Bara la Afrika, unaojulikana kama AfCFTA

Kwa kufanya hivyo, Tanzania ilikuwa nchi ya 41 kati ya nchi 55 za Kiafrika zilizoridhia mkataba huo utakaowezesha nchi wanachama kufanya biashara bila vikwazo vya ushuru wa forodha. 

Hatua hii ni ya kupongezwa na kama ikiwekewa mikakati madhubuti basi tatizo la ajira nchini linaweza kupungua kwa kiasi kikubwa.

Nasema hivi kwa sababu Tanzania imebarikiwa maziwa, mito na Bahari ya Hindi ambazo zote, kwa pamoja, zinaweza kutumika kimkakati na kunufaika na ACfTA. 

Hii ni kwa kupitia uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu na kuzisafirisha katika nchi za Kiafrika ambazo hazina bahari.

Hii inaipa Tanzania fursa za kujiimarisha kwenye uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu, zikiwemo aina kadhaa za samaki.

Kinachoweza kufanyika

Kwa hiyo, Serikali haina budi kueneza elimu kwa wahitimu wa vyuo vikuu juu ya fursa zilizopo kwenye sekta hiyo, huku ikiweka mkakati wa kuwawezesha kwa teknolojia za kisasa, kama vile visimba na mabwawa, kwa ajili ya uzalishaji mkubwa na wenye tija ili waweze kushindana kwenye soko hilo la Afrika.

Pia, kulifanya somo la uvuvi kama sehemu ya masomo kwenye mitaala yetu itawezesha vijana wengi kutambua fursa nyingi zilizomo kwenye sekta ya uchumi wa buluu. 

Hii ina maana kuwa kama elimu ya uvuvi na bidhaa zitokanazo na bahari itatolewa kuanzia chini hadi vyuo vikuu, basi vijana wanaohitimu vyuo vikuu watapata mwanga mkubwa juu ya nini cha kufanya kujiajiri kwenye uchumi wa buluu na usafirishaji wa bidhaa zitokanazo na uchumi huo.

Mabalozi wa Tanzania wa nchi kama Uganda, Rwanda na Botswana nao pia hawana budi bali kuweka mikakati ya kutangaza utajiri wa bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu zilizopo nchini Tanzania. 

Hapa kuna haja ya balozi zetu kufanya ushirikiano wa kimkakati na Wizara za Wiashara na zile za sayansi na kilimo katika nchi husika ili kuwezesha upatikanaji wa bidhaa sahihi zinazohitajika katika nchi hizo. 

Sambamba na hilo, kuna umuhimu wa balozi zetu kuratibu ziara za kibiashara na uwekezaji kwa vijana wa Kitanzania wanaojihusisha na bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu ili wakajionee soko na uhitaji halisi wa bidhaa hizo katika nchi husika.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi pia itoe vibali vingi na kwa wakati bila kuwepo kwa urasimu kwa vijana wa Kitanzania walio tayari kusafirisha bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu kwenda kwenye nchi husika. 

Kama vibali hivi vitatolewa kwa wakati na kwa masharti nafuu na rahisi basi vijana wengi watajitokeza kuchangamkia fursa hii itakoyopaisha pato lao na taifa kwa ujumla.

Michezo na muziki ni miongoni mwa vitu vinavyowakutanisha vijana wengi, kama wasanii na wanamichezo wakubwa nchini wakitumika kama mabalozi kwa kuwawezesha kutembelea nchi husika na kutangaza fursa zilizopo huko. 

Kwa kufanya hivyo, bila shaka tutashuhudia ongezeko la vijana wengi wakijihusisha na usafirishaji wa bidhaa zitokanazo na uchumi wa buluu nje ya nchi.

Mwisho, kuna umuhimu wa Serikali kuwahusisha wadau kwenye sekta ya uvuvi kufanya tafiti za kisayansi juu ya mbegu bora za viumbe maji zitakazoweza kuleta ushindani kwenye masoko ya nchi husika na kuchochea matumizi ya njia za kisasa za kufuga viumbe maji ili kuleta uzalishaji wenye tija.

Bakari Mahundu amejitambulisha kama mdau wa maendeleo ya vijana Tanzania. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia bakarimahundu8@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *