The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, Tuwatazame Vijana Kama Kundi Maalumu Tanzania?

Swali siyo vijana tunafeli wapi, bali tunafeli wapi kama jamii?

subscribe to our newsletter!

Nchini Tanzania, kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana, 2007, kijana ni mtu yeyote mwenye umri kuanzia miaka 15 mpaka 35. 

Japo kuwa makundi mbalimbali yamekuwa yana tafsiri tofauti ya umri kuhusu vijana, vipo vyama vya siasa nchini vinavyotafsiri kijana katika umri huo, huku vingine vikiweka ukomo wa ujana kuwa ni miaka 45, na vingine vimeanzia miaka 18. 

Ubishani wa ukomo wa umri wa ujana umeenda mbali zaidi hadi wengine kusema ujana ni fikra tu, na wengine wameangalia kijana kwa dhana tu ya ulinganifu, hata kama una miaka 50, kama tunakulinganisha na wenye miaka 70, basi wewe ni kijana. 

Lakini ni ukweli kuwa ni muhimu watu wote kuongozwa na tafsiri ya kijana kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 kwa lengo la kuwa na mtazamo wa pamoja na kulinda fursa zinazotolewa kwa vijana.

Sasa, kumekuwepo na hoja nyingi linapokuja suala la haki na wajibu wa vijana, na swali muhimu limekuwa je, tunahitaji kuangazia masuala ya vijana kwa upekee kama tunavoangizia masuala ya wanawake, watoto na watu wenye ulemavu? Je, vijana watazamwe kama kundi maalumu? 

SOMA ZAIDI: Kijana wa Miaka 18 Anaweza Kuwa Kiongozi. Tuondokane na Ubaguzi wa Umri

Mara nyingi nimepata nafasi ya kushiriki na kuwasilisha mada juu ya maslahi na ushiriki wa vijana, na maswali haya yameibuka mara kadhaa, na waibuaji wake hufanya hivyo wakiwa na hasira, wakihoji, kwa nini vijana wanataka kutengenezewa mazingira ya ‘kupewa’ vitu wakati wana nguvu? Watu hawa wanauliza, kwani vijana wanafeli wapi?

Vijana wana nguvu?

Hoja imekuwa kwa sababu ya wingi wao, na nguvu walizonazo, vijana hawapaswi kulialia kuhusu fursa za kiuchumu, au nafasi katika vyombo vya maamuzi. Kwamba vijana ni wengi sina ubushi nalo hata kidogo. 

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, Watanzania wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 35 ni 21,312,411, ambayo ni sawa na asilimia 34.5 kwa kulinganisha na idadi wa Watanzania wote ambao ni 61,741,120. 

Kwa mujibu wa Sensa, nguvu-kazi yetu ni kuanzia miaka 15 mpaka 64 ambao kwa idadi ni 33,000,224. Hi ina maana kwamba vijana ni asilimia 64.58 ya nguvu kazi ya taifa. Kwa hiyo, hoja kwamba vijana ni wengi ni kweli kabisa, na hakuna ubishi wowote katika hilo.

Lakini tujiulize, vijana kuwa wengi ina maana kuwa wana nguvu? Natambua kuwa pamoja na vijana kuwa wengi siyo lazima iwe na maana kuwa wana nguvu. 

SOMA ZAIDI: Mpango Mkakati Wa Upatikanaji Wa Fedha Kwa Vijana Wazinduliwa Zanzibar

Nguvu za mwili, yaani misuli inayotakana na umri wao tu, wanayo, lakini tukiangalia nguvu kwa maana ya umiliki wa rasilimali na ushiriki katika vyombo vya maamuzi, tafiti mbalimbali na hali halisi inaonyesha wazi kwamba vijana wengi siyo wamiliki wa njia kuu za uzalishaji mali, japo wanaweza kuwa wazalishaji wakuu, kama ilivyo tu kwa wanawake. 

Sababu mbalimbali, kama mifumo ya umiliki wa ardhi, ugumu katika upatakanaji wa mitaji na ukosefu wa ujuzi sahihi unaohitajika, zinatajwa kuhusika kwa vijana kushindwa kumiliki nguvu ya uchumi.

Ukiangazia nguvu ya vijana kushiriki katika uongozi na vyombo vya maamuzi, hapa napo ni mahali penye maswali mengi ambayo vijana wanatafuta majibu kwa wenye nguvu na wenye nguvu wanaona vijana hawako tayari, au wanafeli. 

Lakini zipi hasa ni njia za kufikia vyombo vya maamuzi na kuchukua nafasi? Kwa mfumo wa utawala wa nchi yetu, ukiondoa nafasi za kuajiriwa, nafasi nyingi ni kwa kuteuliwa, au kugombea kupitia mchakato wa uchaguzi.

Ili kufikia nguvu zinazotokana na madaraka ya kuchaguliwa, kuteuliwa ama kuajiriwa vipo vigezo vilivyowekwa kisheria na vile ambavyo siyo rasmi, lakini jamii husika ina vizingatia. Kwa mfano, kigezo cha kijana kutokuwa na mke, au makazi yake binafsi, kimetumika mara nyingi kuondoa vijana katika ushindani wa nafasi mbalimbali za kuongoza. 

SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwa na Baraza la Vijana Huru na Lenye Sura ya Kitaifa?

Zipo sheria ambazo ni mageti yenye kufuli kubwa na funguo zake zimepotea, au aliyeshika funguo hizo amesafiri safari ya mbali. Mijadala imeibuka mara kadhaa kama tunamwamini kijana wa umri wa miaka 18 kupigia kura, iweje asubiri mpaka awe na miaka 21 kugombea nafasi katika ngazi za Serikali za mitaa, udiwani na ubunge? 

Ile haki ya kuchagua na kuchaguliwa ingependeza kama ingetekelezwa kwa kuruhusu mtu aliyefikia umri wa kupiga kura kuwa na haki ya kugombea pia.

Kundi maalumu

Ukweli utabaki kuwa vijana ni kundi maalumu tukiliangazia katika dhana ya wakati walionao na mazingira yanayowakabili; ni kundi linalohitaji hatua za kipekee katika kutatua changamoto zinazolikabili.

Ili vijana waweze kushiriki katika uongozi ni wajibu wa makundi mbalimbali kuwekeza katika mikakati mbalimbali ya kuwajenga vijana. Kuanzia katika ngazi ya familia, ni lazima jamii yetu iwe na hatua za wazi za kutekeleza dhana ya ujumuishi wa vijana. 

Hatua rahisi kama kumpa kijana nguvu ya kufanya maamuzi ya kila siku yanayohusu matumiza ya pesa ambayo mlezi umempa ni hatua muhimu katika kujenga vijana watakaojiongoza na kuwaongoza wengine.

SOMA ZAIDI: Vijana wa Siku Hizi ni Zao la Wazee wa Siku Hizi. Tuwe na Akiba ya Maneno Tunapowasimanga

Badala ya kuuliza vijana mmefeli wapi, kwa nini usijiulize mimi binafsi nachukua jitihada gani kuhakikisha vijana wanakuwa imara na kutimiza wajibu wao kwa jamii kama inavyowapasa? 

Vijana tulivyo ni matokeo tu ya jamii ilivyo. Kwa hiyo, swali siyo vijana tunafeli wapi, bali tunafeli wapi kama jamii?


Ocheck Msuva ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bridge For Change, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utetezi wa vijana. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ocheck.msuva@bridge4change.co. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Kwanza nakubaliana na wewe katika tafsiri ya umri wa kijana kama ulivyofafanua na kuongeza kuwa baadhi ya makabila nayo yanatafsiri vijana kwa mila zao. Katika masuala ya uongozi bado kuna changamoto kwani vijana hawapewi nafasi kwa hofu kubwa ya kukosa uzoefu na kuwa hawana Guilt Consciousness katika maamuzi yao. Lakini bado wana fursa kubwa ya kushiriki katika michakato ya kiuongozi. Sasa tukirudi katika suala la kumtazama kijana kama kundi maalumu, ni wazi kuwa kunahitaji kuwa na tafsiri ya mahitaji muhimu gani anayohitaji kijana kumjengea utimamu katika kushika nafasi na kuchapa kazi. Sasa mahitaji gani kijana anayohitaji, ni yale yanayomfanya ashindwe kufikia ndoto zake na kushindwa kutoa mchango katika ujenzi wa jamii. Ni mjadala mrefu na siku kukiwa na mjadala huo naomba nishirikishwe. Kwa kuhitimisha naomba nikupongeze sana kwa kutufikirisha vijana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *