The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Simba Inahitaji Kutathmini Safari Yake ya Mabadiliko

Badala ya wana-Simba kurushiana shutuma, hawana budi kukaa chini na kutafakari upya safari yao ya mabadiliko na mageuzi ili kuongeza ufanisi.

subscribe to our newsletter!

Kama kuna mwaka mashabiki wa klabu ya Arsenal walichukia, basi ni 2016 baada ya gazeti la The Evening Standard kuchapisha habari iliyoonyesha kuwa mwekezaji mwenye hisa nyingi, Stan Kroenke haoni kama ubingwa ni kitu muhimu kilichomsukuma ainunue klabu hiyo.

Gazeti hilo la nchini England lilichapisha habari iliyomkariri Kroenke akisema, “Sikuinunua Arsenal [kwa ajili ya] kutwaa vikombe,” wakati kwa nchi yenye wendawazimu wa mpira wa miguu kama England, kutwaa mataji ndiyo kitu kikubwa kuliko vingine vyote kwa klabu ya soka.

The Evening Standard lilimkariri Kroenke akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na taasisi ya MIT Sloan Sports Analytics, ambayo hufanya uchambuzi wa taarifa zinazosaidia klabu kujua aina ya wachezaji zinaowataka, matarajio ya matokeo ya msimu unaofuata, aina ya kocha anayetakiwa, biashara na mambo mengine muhimu yanayotakona na tafsiri ya takwimu.

Lakini Kroenke, ambaye alinunua hisa za Arsenal mwaka 2007 na kujiimarisha zaidi kuwa mmiliki mwenye hisa nyingi mwaka 2011, hakuwa anamaanisha kile kilichoandikwa na The Evening Standard na wala hakukuwepo na sentensi iliyosema sikuinunua Arsenal kutwaa mataji. Gazeti hilo liliongeza chumvi katika tafsiri ya alichosema.

Alichokuwa anazungumzia ni jinsi kunavyotakiwa kuwe na uhusiano kati ya kutwaa mataji na biashara na ndiyo maana akaponda uwekezaji wa taasisi, au watu binafsi kutoka Mashariki ya Kati ambao alisema inaweza kufikia wakati wakapoteza utashi wa soka na kuamua kuondoka zao, hali ambayo inaweza kuwa mbaya kwa klabu na hasa mashabiki.

SOMA ZAIDI: Olimpiki ya Paris Imeshatupita, Tujiandae ya 2028

Alisema watu hao, kama mmiliki wa Manchester City, wanamwaga fedha kwa kuwa wanataka vikombe na si kufanya biashara kama anavyofanya, lakini akasema hilo linawezekana tu kama kutakuwa na biashara nyingine ya kuweza kuchukua fedha na kuziingiza kwenye kusaka ubingwa.

Msimu uliotangulia kabla ya kauli hiyo, Arsenal ilikuwa na fedha taslimu Pauni milioni 160 za Kiingereza kwa ajili ya kununua wachezaji, lakini ikatumia Pauni milioni 10 tu kumchukua kipa Petr Czech kutoka Chelsea, wakati Man City ilitumia Pauni milioni 150 kuwasajili Kelvin de Bruyne, Raheem Sterling an Nicolas Otamendi, huku Chelsea ikitumia Pauni milioni 65 kununua wachezaji nane. Kwa ujumla klabu hizo mbili zilitwaa mataji sita tangu Arsenal itwae ubingwa kwa mara ya mwisho mwaka 2004.

Faida ya uwekezaji

Kauli ya Kroenke ilikuwa ya kikatili lakini yenye ukweli kwamba lazima mwekezaji aone faida ya uwekezaji wake ndipo amwage fedha. Kwa mwekezaji huyo Mmarekani, soka nchini England linaweza kutengeneza fedha nyingi ambazo zitatumiwa kununua wachezaji, akitoa mfano wa shabiki anayeweza kupanda ndege kutoka Johannesburg, Afrika Kusini na kwenda London kushuhudia mechi na kurudi Afrika.

Utamaduni wa mashabiki wa soka wa England kusafiri umbali mrefu kufuata timu yao ni fursa kubwa ya kufanya biashara.

Hapishani sana na utamaduni wa kampuni inayomiliki asilimia kubwa ya hisa za Liverpool, ambayo haimwagi fedha nyingi katika kununua wachezaji bali inategemea chapa ya klabu hiyo kuzalisha fedha nyingi.

SOMA ZAIDI: Kwa Hili, Serikali Imeheshimu AFCON 2027

Hata hivyo, mwanae aliwatuliza mashabiki wa Arsenal mwaka 2019 aliposema pamoja na kwamba hakukuwa na matarajio ya kutwaa ubingwa, aliona mwanga mbele baada ya Arsenal kufanya marekebisho muhimu kwenye muundo, ikimuajiri kwa mara ya kwanza mkurugenzi wa ufundi, Edu na Per Mertesacker kama meneja wa shule ya soka. 

Na tangu mwaka huo, mambo yameanza kwenda vizuri baada ya Arsenal kupambana na Manchester City mara mbili hadi siku za mwisho kuamua bingwa.

Hali inayoonekana kuendelea katika klabu ya Simba ni hiyo ambayo Kroenke aliikataa Arsenal. Wana-Simba wanaamini kuwa mafanikio yatakuja kwa mwekezaji kumwaga fedha kwa ajili ya kununua wachezaji wazuri, huku wakituhumu kwamba fedha anazotoa Mohamed Dewji zinaliwa au kutapanywa na viongozi.

Huu ni msimu wa tatu sasa Simba anapishana na ubingwa na msimu huu hali imekuwa mbaya zaidi kwa kuwa haitashiriki Ligi ya Mabingwa wa Afrika, ambayo ni mashindano makubwa kuliko yote barani kwa upande wa klabu, baada ya kushika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu.

Mashabiki wanawapigia kelele wajumbe wa bodi, na hasa wenyeviti wa upande wa klabu na mwekezaji, wajiuzulu ili waingie watu wengine wenye mapenzi na timu na wasiomtapeli mwekezaji, huku wengine wakimsihi aendelee kutoa fedha ili kupata Simba iliyo bora.

Mageuzi

Hakuna anayezungumzia muundo bora utakaowezesha Simba kuongozwa kisasa zaidi na kutumia ukubwa wa jina lake kufanya biashara itakayoiwezesha klabu kusimama imara bila ya kuyumbishwa na mabadiliko ya mwekezaji au viongozi.

SOMA ZAIDI: Ni Muda Makocha Wazawa Tanzania Waanze Kufanya Kazi Kisasa

Hakuna anayezungumzia kutokamilika kwa mageuzi ambayo yalilenga kuifanya Simba iendeshwe na kumilikiwa kisasa na kuachana na hali ya sasa ambayo uongozi unafanya mambo kwa shinikizo la mashabiki na wanachama bila ya kuzingatia mipango thabiti ya muda mrefu na mfupi ya kuiondoa Simba katika uzamani.

Mabadiliko yaliyofanywa ni ya usoni yasiyoakisi usasa, huku watu walewale wakibadilishana nyadhifa na kuendelea na utaratibu uleule wa uendeshaji klabu.

Hakuna anayehoji ufanisi na mafanikio ya uwekezaji, kwamba baada ya Dewji kuweka Shilingi bilioni 20, kumekuwepo na mabadiliko gani katika uendeshaji, au hata makusanyo ya fedha, kiasi kwamba mara kwa mara mwekezaji analalamika kwamba anapata hasara. 

Ni mambo gani yanayosababisha klabu yenye chapa kubwa kama Simba isifikie wakati ikawa inakusanya mapato ya kujitosheleza kutokana na haki za televisheni, udhamini, mauzo ya bidhaa kama fulana, kofia na leso, mapato ya mlangoni na ubunifu mwingine wa kibiashara. Hayo mageuzi ya kutaka klabu ijiendeshe kisasa ni yapi? 

Ni ya kutaka Dewji amiliki kila kitu au ya kutaka kuona klabu inajiendesha kwa jinsi ambayo itatengeneza fedha na kuonyesha kuwa ni sehemu ambayo wawekezaji wengi zaidi wanavutiwa kuweka fedha zao?

SOMA ZAIDI: Tathmini Inahitajika Kuondoa Mazoea Kwenye Soka la Tanzania

Na mara kwa mara Dewji anapoibuka ama kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii au mahojiano na vyombo vya habari, huonyesha kwamba ama anafanyiwa mizengwe asifanikiwe lengo lake la kuimiliki klabu au alishainunua klabu hiyo, wakati mchakato ulimzuia kukamilisha kuinunua klabu peke yake baada ya kanuni kutaka asilimia 41 za hisa zinunuliwe na watu kuanzia wawili.

Kwa hiyo, haijulikani mageuzi yaliyofanywa yalilenga kuimilikisha klabu kwa mwekezaji au kuifanya Simba kuwa taasisi inayoendeshwa kwa faida na kuwa kivutio kwa wawekezaji. 

Dewji ashike hatamu?

Inavyoonekana ni kwamba mashabiki na wanachama wanataka Dewji ashike hatamu na kuwa mwamuzi wa kila kitu, na ndiyo maana lawama na mashambulizi yote yanakwenda kwa Salim Try Again, ambaye ni mwenyekiti wa bodi aliyeteuliwa na Dewji, na Murtaza Mangungu, ambaye ni mwenyekiti wa klabu aliyechaguliwa na wanachama.

Katika kipindi ambacho mageuzi hayajakamilika, ni vigumu kuwa na uamuzi madhubuti unaohusisha au kukubaliwa na pande zote. 

Hakuna mtu aliye juu ambaye ana kauli ya mwisho na ndiyo maana inasemekana Dewji amewaomba wajumbe wa bodi ya wakurugenzi aliowateua, wajiuzulu ili apande safu yake upya, lakini hana mamlaka kwa wajumbe walioingia kwa tiketi ya wanachama.

SOMA ZAIDI: CAF Ilitafutie Suluhu ya Kudumu Suala la Morocco

Kulihitajika usahihi kama uliowekwa na Kroenke kwamba ni lazima klabu ijikite kukuza chapa yake ili itengeneze fedha na hilo haliwezi kushuka kama mvua, bali kwa mipango. 

Ndiyo maana Arsenal ikaanza kujenga misingi ya uendeshaji imara wa klabu, kuweka sera za usajili, kuunda idara muhimu katika soka la sasa kama kurugenzi ya ufundi, na kutafuta watu muafaka na wenye ufanisi katika nafasi hizo.

Walikuwepo watu wengi wa muda mrefu ambao wangeweza kubadilishwabadilishwa kwenye nafasi hizo, lakini tathmini iliwaona Edu na Mertesacker kuwa ndiyo wanaweza kushirikiana na Michel Artete kuijenga Arsenal mpya; na mambo yanakwenda vizuri. 

Arsenal kwa sasa ndiyo klabu inayotoza kiingilio cha juu cha tiketi za msimu kuliko klabu nyingine yoyote Ligi Kuu England, maana yake chapa imekuwa kubwa zaidi.

Kroenke angeweza kuchukua njia ambayo Manchester City au Chelsea zilivyochukua, yaani kumwaga fedha kununua wachezaji kwa ajili ya kutafuta vikombe, lakini akaona hiyo si njia sahihi. 

SOMA ZAIDI: Tutapataje Mabondia Bora Bila Ngumi za Ridhaa?

Chelsea imekuwa mfano wa klabu ambazo badala ya kujenga jina zilijikita katika kutafuta mafanikio na mwekezaji wake, Roman Abrohamovic alipoyumbishwa na siasa za Mashariki na Magharibi, klabu pia ikayumba.

Kwa nini klabu za michezo mingine zilizo chini ya Kroenke zimepata mafanikio lakini Arsenal bado inasota? Los Angeles Rams ilishinda fainali ya mpira wa miguu wa Kimarekani mwaka jana, Colorado Avalanche ilishinda Kombe la Stanley, na Denver Nuggets ikatwaa ubingwa wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani (NBA) kwa mara ya kwanza mwaka jana.

Kwa hiyo, kuna siri ya mafanikio ambayo Kroenke anayo ndiyo maana anaendelea kuwa na dola kubwa ya michezo chini yake.

Maamuzi

Leo wana-Simba hawana budi kuamua; wanataka mafanikio yasiyo na mizizi kama ya Manchester City na Chelsea, yaani yale ya tajiri kutoa fedha kila zinapohitajika kwa ajili ya kusajili wachezaji, au mafanikio yanayolenga kujenga taasisi imara. 

Ni kweli kwamba walichotaka ni Dewji awe na sauti kubwa kuliko wote au fedha anazotakiwa kuwekeza ziiimarishe klabu kiuchumi na kuwa moja ya taasisi bora nchi na Afrika kwa ujumla. Njia ipi ni sahihi?

Na kufikia njia hizo mbili, wanajua kuwa mradi wa mabadiliko haujafikia mwisho na kwamba kikwazo kikubwa ni sharia na kanuni za nchi?

SOMA ZAIDI: Wimbi la Wachezaji Kuvunja Mikataba Lidhibitiwe

Hata Dewji leo akimwaga fedha kadri zitakavyohitajika, itakuwa dawa ya matatizo yaliyoikumba katika misimu mitatu iliyopita?

Badala ya wana-Simba kurushiana shutuma kwamba fulani ndiyo mwenye makossa, hawana budi kukaa chini kutafakari upya safari yao ya mabadiliko na mageuzi na kuona wamefikia wapi na nini kirekebishwe ili kupata uongozi wenye ufanisi utakaotokana na mfumo wenye ufanisi.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *