The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wimbi la Wachezaji Kuvunja Mikataba Lidhibitiwe

Kwa sababu soka ni mchezo wa kitimu, ni muhimu wachezaji wakawa pamoja kwa muda fulani ili walimu waweke mbinu zao vichwani mwao na kujenga timu wanayoifikiria.

subscribe to our newsletter!

Ilianza kama utani wakati kiungo wa Azam Football Club, Feisal Salum, alipojiondoa Yanga na kuandika barua ya kuvunja mkataba, ikiambatana na muamala wa Shilingi milioni 112 kama fidia ya kuvunja mkataba.

Baadhi waliona kuwa ni jaribio la kuutingisha uongozi wa Yanga ili usalimu amri na kukidhi mahitaji yake ya kuboresha maslahi kwenye mkataba wake, na wengine kudhani kuwa ilikuwa ni njama za kuihujumu klabu hiyo yenye makao yake makuu katika makutano ya Mtaa wa Twiga na Jangwani.

Lakini kadri siku zilivyokwenda ndivyo hali ilivyoonekana kuwa tofauti. Hoja za kutaka kuvunja mkataba hazikuonekana kuwa na mashiko lakini haja ya kuondoka ilionekana dhahiri, shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliamua kujitosa na kuiomba Yanga iridhie matakwa ya kiungo huyo kutoka Zanzibar.

Yanga iliweka sokoni na muda mfupi baadaye Azam wakajitosa kulipia dau lililowekwa na Yanga ili kumuondoa kiungo huyo ambaye alikuwa amebakiwa na mwaka mmoja kwenye mkataba wake.

Siku chache baadaye, kiungo mwingine wa Kagera Sugar, Abdul Aziz Makame, akatoweka kambini kwa kile kilichoelezwa na viongozi wake kuwa amejiongezea muda wa wiki mbili aliopewa kwenda kutibu jeraha. Ilisemekana kuwa kiungo huyo wa zamani wa Yanga hakuwa na mawasiliano yoyote na waajiri wake hadi Kagera Sugar walipotangaza kuachana naye kwa makubaliano.

SOMA ZAIDI: Kwa Kufundisha Watoto Hujuma, Tunajenga Taifa la Aina Gani?

Baadaye mchezaji huyo akaeleza kuwa aliamua kuachana na Kagera kwa sababu mshahara aliokuwa akiingiziwa benki ulikuwa na makato ambayo yalifanywa bila ya ridhaa yake. Akatimka.

Wiki chache zilizopita, kipa wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya, alidaiwa kuondoka kambini wakati klabu hiyo ikijiandaa kucheza na Yanga. Singida walisema kwa kawaida meneja wa timu hana mamlaka ya kutoa ruhusa kwa wachezaji na kwamba ombi lake lilikataliwa. 

Kakolanya akaeleza kuwa alishindwa kufikia makubaliano na uongozi na akaomba ruhusa kwa meneja na kuruhusiwa, jambo lililoonekana kama njama za kuihujumu Singida dhidi ya timu yake ya zamani ya Yanga.

Lakini baada ya mechi hiyo, kiungo wa Singida FG, Yusuf Kagoma, alijiondoa kambini jijini Mwanza, akipinga kutolipwa haki zake na ikasemekana wachezaji wengine wako kwenye mweleekeo huo wa kuachana na timu zikiwa zimesalia takriban raundi saba msimu kumalizika.

Kuchukua hatua

Kwa mujibu wa kanuni za sasa, si Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wala Bodi ya Ligi inayoweza kuchukua hatua dhidi ya wachezaji wanaoondoka kutokana na klabu kushindwa kutimiza matakwa ya mikataba yao. 

SOMA ZAIDI: Yanga Imefanyiwa Ukatili, CAF Ifanyie Kazi V.A.R

Kinachowezekana ni TFF kuridhia nia yao ya kuvunja mikataba kwa kurejea sheria za Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) kuhusu hadhi na haki za wachezaji.

Wakati ni rahisi kwa wachezaji kuvunja mikataba kutokana na klabu kushindwa kutimiza utashi wa mikataba, ni vigumu kwa TFF au TPLB kudhibiti uimara wa kiuchumi wa klabu zinazoshiriki Ligi Kuu, huku baadhi zikiwa hazina wamiliki ambao ni bayana hadharani.

TFF na TPLB hazina utaratibu wa kufuatilia hali ya kiuchumi ya klabu zinazoshiriki mashindano yake, kiasi kwamba moja ikitetereka kiuchumi inaweza kuathiri mwenendo mzima wa ligi, au kusababisha mashindano kupoteza ladha.

Kwa mfano, mchezo wa Singida FG na Yanga ulitawaliwa na habari za tuhuma za kutoweka kwa Kakolanya, zikihusishwa na njama za kuihujumu timu hiyo ambayo imebadilisha mmiliki hivi karibuni kutoka kwa wale waliokuwa wanaimiliki Singida Big Stars na baadaye kuiza kwa Fountain Gate na wao kuinunua Ihefu Football Club na kuigeuza kuwa Singida Black Stars.

Tuhuma hizo za njama ziliimarishwa na matokeo ya kipigo cha mabao 3-0 walichopewa Singida na kutaka kuaminisha umma kuwa kulikuwa na mpango wa hujuma. Lakini kuondoka kwa Kagoma kumeweka bayana tatizo la ndani la Singida Fountain Gate kuhusu hali yake ya kiuchumi.

Hali ngumu ya kiuchumi

Feisal Salum, maarufu kama Fei Toto, hakuondoka kwa sababu ya hali ngumu ya kiuchumi kwenye klabu ya Yanga bali madai yake kuwa hakuwa akitendewa haki kimkataba. 

SOMA ZAIDI: TFF Ifanye Uamuzi Mapema Kocha wa Taifa Stars

Na wengi wanaona pamoja na mchango mkubwa kwenye klabu hiyo, mshahara wake ulikuwa mdogo kulinganisha na nyota wengine waliosajiliwa baadaye, kitu ambacho ni kawaida katika ajira kwa mwajiriwa mpya kukubaliana mkataba mnono, huku aliowakuta wakisubiri kufanya mazungumzo ya kuboresha mikataba yao.

Sakata la hivi karibuni linamuhusisha mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube, ambaye aliutaarifu uongozi nia yake ya kuvunja mkataba na baadaye klabu kuafiki lakini ikaweka dau kubwa la kuvunja mkataba, kwa madai kuwa mshambuliaji huyo kutoka Zimbabwe alishasaini mkataba mwingine unaoisha Juni 2026.

Lakini Dube amefungua madai TFF akisema mkataba wake unaisha Juni mwaka huu, hali itakayomfanya aondoke akiwa mchezaji huru, asiyetakiwa kulipiwa chochote kama ada.

Awali ya yote kulikuwa na sinema ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Bernard Morrison, ambaye bila ya kutarajiwa aliandika barua TFF akidai kuwa amesikia Yanga wanasema wana mkataba naye wa muda mrefu, kitu ambacho alidai si sahihi. 

Baada ya shauri lake kusikilizwa, ilionekana ni kweli alisaini mkataba huo, lakini Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ikasema kulikuwa na kasoro katika mkataba huo na hivyo kuubatilisha, hali iliyompa mwanya mchezaji huyo kutoka Ghana kujiunga na Simba.

SOMA ZAIDI: TFF, TPLB Ziamke, Azam Media Siyo Mfadhili

Kwa hiyo, kunaonekana kuna wimbi la wachezaji kuchoka kucheza sehemu moja na kutafuta mianya kwenye mikataba ili watimke katikati ya msimu, hali inayoweza kuathiri Ligi Kuu ya NBC, ambayo ilipanda hadi kufikia nafasi ya tano kwa ubora barani Afrika kabla ya mwaka huu kushuka hadi nafasi ya sita.

Mchezaji ambaye yuko kwenye klabu iliyo imara kiuchumi anatafuta sababu za nje ya maslahi ya kifedha kuondoka, huku mchezaji aliye kwenye klabu iliyo hoi kiuchumi anatafuta sababu za kutotimiziwa maslahi yake kuondoka.

Na kwa mujibu wa sheria na kanuni, vyote vinawezekana ikiwa mchezaji atakuwa amejipanga vizuri. Kujua mchezaji atachukua uamuzi huo wakati gani, ni vigumu kujua, anaweza kutumia mechi muhimu kama fimbo ya kuwachapia viongozi ili wakubaliane naye kama ilivyotafsiriwa katika sakata la Kakolanya na kidogo la Fei Toto.

Anaweza kuamua baada ya mechi muhimu ambayo ameonyesha ubora wake na watu kuukubali kama alivyofanya Yusuf Kagoma. Au anaweza kufanya uamuzi huo katika kipindi ambacho klabu yake ina majukumu muhimu kitaifa na kimataifa kama ilivyotafsiriwa katika sakata la Fei Toto wakati Yanga ikicheza mechi muhimu za michuano ya Kombe la Shirikisho.

Sumu kwa soka

Kilicho sumu kwa mpira wa miguu ni wachezaji hao kufanya maamuzi katikati ya msimu, au kabla ya msimu kumalizika, kipindi ambacho klabu haziwezi kuziba mapengo yao ingawa ni kweli pia kuwa hata wao hawawezi kucheza tena hadi msimu uishe.

SOMA ZAIDI: Utitiri wa Marathoni Unakisaidiaje Chama cha Riadha Tanzania?

Katika mazingira haya, TFF na TPLB zinawezaje kudhibiti hali hii ambayo ni tishio kwa maendeleo ya mashindano yetu ya ndani? Hadi sasa hatuna kanuni tulizotunga zinazolingana na mazingira yetu. Kanuni nyingi ni zile zilizoundwa kulingana na mwongozo wa FIFA kuhusu haki na hadhi za wachezaji.

Ni muhimu sana kwa TFF, TPLB na Chama cha Wanasoka (SPUTANZA) kukaa chini na kutafuta suluhisho la pamoja la jinsi ya kudhibiti, au kuweka mazingira mazuri ya wachezaji na klabu kuishi pamoja hadi mwisho wa msimu, au angalau katikati ya msimu wakati dirisha linapofunguliwa kwa ajili ya kuboresha usajili.

Kwa wenzetu ni rahisi kudhibiti masuala ya maslahi ya wachezaji kutokana na sheria zinazodhibiti matumizi ya fedha, lakini pia mwenendo wa kifedha wa klabu unaoweza kuifanya iwekwe chini ya uangalizi inapoonekana mambo yanaenda kombo na msimamizi akajihusisha na matumizi ya mambo muhimu tu kama vile mishahara na gharama za kwenda vituoni kucheza mechi za mashindano.

TFF na wadau wanaweza kuangalia wadhibiti wapi katika vyanzo vya fedha ili haki za wachezaji zisikiukwe, huku wakiangalia pia jinsi ya kudhibiti tabia hii inayokomaa ya wachezaji kujivunjia mikataba na kutimka kabla ya msimu kumalizika.

Mpira wa miguu ni mchezo wa kitimu na si wa mchezaji mmojammoja kama ilivyo riadha au ngumi. Na kwa sababu ni wa kitimu, ni muhimu wachezaji wakawa pamoja kwa muda fulani ili walimu waweke mbinu zao vichwani mwao na kujenga timu wanayoifikiria. 

SOMA ZAIDI: Mpira wa Miguu Sasa ni Sekta Muhimu, Uratibiwe

Kuondoka kwa wachezaji kama hao, ambao wengi ni tegemeo, huvuruga mbinu za kocha na kulazimika kuanza kuziba mianya bila ya sababu za msingi.

Kwa hiyo, mchezo wowote wa kitimu lazima uwekewe kanuni za kuhakikisha wachezaji wanakaa pamoja kwa kipindi fulani hadi muda unapofika wa kufunguliwa dirisha ili waondoke kwenda kutafuta maisha kwingine.

Bila ya hivyo, tutavuruga mpira wetu.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *