The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Kufundisha Watoto Hujuma, Tunajenga Taifa la Aina Gani?

Ni lazima tujenge taifa linalotaka kushindana kwa haki, kushinda kwa haki na kukubali matokeo.

subscribe to our newsletter!

Michezo ni kati ya njia nzuri za kujenga taifa bora la baadaye kutokana na misingi iliyo ndani yake. Kupambana ili kushinda, kukubali kushindwa, kuheshimu mpinzani, kumuheshimu msimamizi, au mwamuzi, na kufuata maelekezo ya mbinu za kocha ni kati ya mambo yanayojenga misingi mizuri inayomuwezesha mtoto kuwa raia mwema wa baadaye katika taifa lolote lile.

Lakini michezo ikitumika kujenga fikra za hila, hujuma, kutokubali matokeo na mambo mengine, haitaweza kumuandaa mtoto awe raia mwema wa taifa lake. Mambo hayo huzaa waovu, wahalifu, mafisadi, au watu wanaotaka kunufaika kwa mambo ambayo hawastahili, wezi na wabaya wengine katika jamii.

Hivi ndivyo mchezo wa mpira wa miguu umeanza kutumika kubomoa taifa la kesho katika baadhi ya mikoa, au wilaya, hapa Tanzania. Kwa sasa kumeanza kujengeka tabia ya kufundisha watoto wanaookota mipira kwenye mechi za Ligi Kuu kupoteza muda hasa timu kutoka mkoa wao inapokuwa inaongoza, au inataka kulazimisha sare.

Tabia hii imeanza kukomaa na ilijidhihirisha tena katika mechi baina ya Mashujaa FC na Simba iliyofanyika mjini Kigoma takriban wiki mbili zilizopita.

Mara kadhaa mpira uliopokwenda nje ya uwanja, watoto hao walichelewa kuurudisha uwanjani, hasa wakati ambao Simba walikuwa na haki nao. Mara kadhaa watoto hao walionekana wakitembea taratibu kumfuata mchezaji wa Simba aliyekuwa akisubiri kurusha mpira, badala ya kumrushia ili kurahisisha mambo.

SOMA ZAIDI: Yanga Imefanyiwa Ukatili, CAF Ifanyie Kazi V.A.R

Si rahisi kudhani kuwa mtoto kama huyo ana nia ovu kwa kuwa anaonekana anatembea kuelekea sehemu aliyo mchezaji wa Simba, kumbe angemrushia asingepoteza ule muda. Lakini kwa kuwa anajua nia yake ni kupoteza muda, anaamua kutembea akiwa ameshikilia mpira, huku akielekea sehemu aliyo mchezaji wa Simba.

Mara nyingine ilichukua muda mpira kurudi uwanjani, na katika baadhi ya matukio mipira miwili ilirushwa uwanjani ili mwamuzi alazimike kusimamisha mchezo hadi mpira mmoja utolewe uwanjani.

Vitendo hivi vilifanywa na watoto wadogo wanaopewa dhamana ya kuokota mipira wakati wa mechi. Na kwa kuwa vinafanywa kimfumo, ni dhahiri kuwa kunakuwa na mafunzo ya jinsi ya kuchelewesha mpira kwa watoto hao. Tunalipeleka wapi taifa hili iwapo tunaanza kuwafundisha watoto wadogo hujuma katika michezo?

Hawa ndiyo watakuwa viongozi wa baadaye, wachezaji wa baadaye, waamuzi wa baadaye na wenye mamlaka katika taasisi mbalimbali. Kipi kitatushangaza iwapo kutakuwa na hujuma kubwa katika taasisi hizo, au michezo, kama hawa vijana wamefundishwa vitendo hivyo wakiwa bado wadogo?

Si mchezo wa Mashujaa na Simba pekee uliokuwa na vitendo hivyo; hali kama hiyo ilionekana katika mchezo baina ya Ihefu na Yanga. Achilia mbali mechi za Ligi Kuu ya NBC, hata mechi ya makundi ya AFCON 2023 baina ya Tanzania na Niger ilitawaliwa na vitendo hivyo.

SOMA ZAIDI: TFF Ifanye Uamuzi Mapema Kocha wa Taifa Stars

Mara kadhaa watoto hao walirusha mipira mingi uwanjani kwa ajili ya kupoteza muda na mashabiki wakishangilia wakidhani walichokuwa wakifanya watoto hao ni uzalendo wa hali ya juu kumbe ni kujifunza uovu ambao unaweza kuja kuwavurugia mambo yao katika maisha na pia kuliangusha taifa.

Kuna mambo mengi mazuri ya kuwafundisha watoto, hasa hao wanaopewa fursa ya kuwa karibu na wachezaji nyota wa Tanzania na wale kutoka sehemu nyingine za bara la Afrika badala ya kuwafundisha kuhujumu.

Katika baadhi ya nchi, watoto wanaookota mipira wamejikuta wakipigwa na wachezaji nyota kutokana na kuchelewesha mpira kwa lengo la kuisaidia timu ya nyumbani.

Mwaka 2013, mshambuliaji nyota wa zamani wa Chelsea, Eden Hazard, alimpiga teke mtoto aliyekuwa anaokota mipira katika mechi dhidi ya Swansea. Ingawa Hazard alionyeshwa kadi nyekundu kwa kitendo hicho, mtoto huyo, Charlie Morgan, aliachiwa kumbukumbu mbaya. Kwanza alipigwa teke na mchezaji nyota, na pili ni kweli alifanya kosa la kutaka kuihujumu timu.

Ingawa Charlie sasa ni bilionea, kumbukumbu hiyo mbaya haitaondoka pamoja na kwamba alichangia kuiwezesha Swansea kuiondoa Chelsea katika michuano ya Kombe la Ligi.

SOMA ZAIDI: TFF, TPLB Ziamke, Azam Media Siyo Mfadhili

Ili kuondoa tabia hii mbaya ya hujuma za wazi katika mpira wa miguu, Ligi Kuu ya England imepiga marufuku wanaopewa kazi ya kuokota mipira kuwarushia, au kuwapelekea, wachezaji mipira. 

Badala yake, Premier League imeamua kutenga maeneo ambayo mipira itakuwa inawekwa na wachezaji watatakiwa kuifuata mipira maeneo hayo na si kurushiwa au kuletewa.

Maana yake ni kwamba zile hujuma zilizoshirikisha watoto sasa zimeondolewa na kubakizwa kwa wachezaji wenyewe ambao kiakili wameshakomaa. Kwamba mchezaji atachelewa kuufuata mpira kwa kutembea taratibu, hilo ni jukumu lake na asipokuwa makini atakutana na makali ya mwamuzi ambaye ana uwezo wa kumuonya, kumuonyesha kadi ya njano na kumtoa kwa kadi ya pili ya njano.

Kwa hiyo, Premier League imeondoa huo uovu kwa watoto, huku ikiimarisha muda unaotumika kucheza mpira dhidi ya unaopotezwa kwa vitendo kama hivyo.

Hizi ni hatua ambazo Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) haina budi kuzichukua ili kukilinda kizazi kijacho na mafunzo na tabia za hujuma na uovu mwingine, lakini pia kuulinda mchezo ili timu isishindwe kwa hujuma ambazo ni dhahiri bali kwa mbinu za kimchezo.

SOMA ZAIDI: Utitiri wa Marathoni Unakisaidiaje Chama cha Riadha Tanzania?

Shirikisho la Soka (TFF) nalo halina budi kuondoa vitendo hivi kwa watoto wanaopewa fursa ya kusaidia mechi za timu zetu za taifa, au klabu, zinazoliwakilisha taifa katika mashindano ya kimataifa.

Ni lazima tujenge taifa linalotaka kushindana kwa haki, kushinda kwa haki na kukubali matokeo, mambo yatakayotulazimisha kufanya maandalizi mazuri, kuwekeza inavyostahili na kutumia kila mbinu halali kupata ushindi na hatimaye kuendeleza soka letu.


Ile taswira iliyoonekana katika mechi dhidi ya Niger ni aibu kwa taifa na fedheha kwa uongozi wa mpira. Taswira ile inajenga picha kuwa mamlaka zilitumia muda na mali zake kuwafundisha watoto wadogo jinsi ya kuhujumu timu pinzani kwa kofia ya uzalendo. 

Hakuna uzalendo wa kuhujumu wengine bali kushinda kwa haki baada ya uwekezaji na maandalizi sahihi. Tusifikirie sifa tunazopata kwa timu zetu kushinda, bali tujihoji tunajenga jamii gani.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *