Search
Close this search box.

TFF Ifanye Uamuzi Mapema Kocha wa Taifa Stars

Haya mambo ya kutaka ushindi kwa nguvu katika kila mechi, yanaweza kutupa picha bandia kuwa tuna timu nzuri, kumbe hatujui hata uzuri wake uko sehemu gani na kushindwa kuuimarisha.

subscribe to our newsletter!

Timu ya taifa ya soka, Taifa Stars, iko nchini Azerbaijan kucheza mechi za michuano mipya ya kirafiki iliyopewa jina la FIFA Series ambayo inaandaliwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).

Katika mechi ya kwanza iliyofanyika Machi 22, Tanzania ilifungwa bao 1-0 na Bulgaria, ambayo ni mwakilishi wa bara la Ulaya katika mashindano hayo yanayoshirikisha timu nne kutoka mabara matatu.

Tanzania itamaliza mechi hizo kwa kuvaana na Mongolia Machi 25. Jambo muhimu kwenye mashindano hayo ni kwamba matokeo yake hujumuishwa kwenye upangaji wa nchi kwa kuzingatia ubora wake na hivyo ni mechi muhimu, hasa pia kwa kuwa inakutanisha timu zilizo katika viwango tofauti.

Ni michuano ambayo inaondoa lile tatizo la kupata mechi nzuri za kirafiki za kimataifa. Kwa hali ilivyokuwa inakwenda, isingekuwa rahisi Tanzania, ambayo katika orodha ya viwango vya ubora ya FIFA inashika nafasi ya 119, kupata mechi ya kirafiki dhidi ya Bulgaria ambayo ni ya 83. 

Ilikuwa ni vigumu kupata mechi za kirafiki dhidi ya hata mataifa makubwa katika soka Afrika kama Nigeria, Cameroon, Morocco, Ghana, Senegal au Afrika Kusini kwa sababu nayo yalikuwa yakisaka mechi dhidi ya England, Ufaransa, Brazil, Argentina na Ujerumani.

SOMA ZAIDI: TFF, TPLB Ziamke, Azam Media Siyo Mfadhili

Kwa hiyo, FIFA Series inayalazimisha mataifa hayo makubwa kucheza na timu ambazo ziko chini katika orodha ya ubora ya FIFA. Hata hivyo, hiyo haitulazimishi kutotumia mashindano hayo kujenga mkakati wetu kwa ajili ya mashindano yajayo makubwa.

Mashindano ya CHAN

Mwishoni mwa mwaka huu, Tanzania, Kenya na Uganda zitakuwa mwenyeji wa mashindano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) ambayo hushirikisha wachezaji wanaocheza soka katika ligi za ndani. Yaani, hayashirikishi mchezaji kama Mbwana Samatta ambaye anacheza soka barani Ulaya.

Awali, ilikuwa ni wachezaji walio katika ligi ya nchi tu, lakini Shirikisho la Soka Afrika (CAF) sasa limepanua wigo na kuruhusu wachezaji wanaocheza nje ya nchi lakini barani Afrika, pia wajumuishwe. Mfano ni Himid Mao, ambaye anacheza soka nchini Misri.

Wakati tukielekea mwezi Aprili, sijaona mkakati wa makocha kwa ajili ya mashindano hayo ambayo nchi hizi tatu za Afrika Mashariki zimepewa kama jaribio la kuona utayari wao wa kuandaa mashindano makubwa kabla ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2027 zitakazoandaliwa pia na mataifa hayo.

Nilitegemea kuona makocha wetu wakiita wachezaji kwa ajili ya kuanza kujenga kikosi cha CHAN 2024, lakini hali imekuwa ni ileile ya kuita wachezaji kwa ajili ya kutafuta ushindi ambao mara nyingi huwajenga makocha.

SOMA ZAIDI: Utitiri wa Marathoni Unakisaidiaje Chama cha Riadha Tanzania?

Isingekuwa rahisi kwa kocha Hemed Morocco na Juma Mgunda kuita wachezaji kwa ajili ya CHAN 2024 wakati hawana uhakika wa kuwepo Taifa Stars hadi Desemba mwaka huu kwa kuwa wamekabidhiwa dhamana hiyo kwa muda.

Kwa hiyo, katika kipindi hiki cha kufanya kazi kwa muda, makocha hawa watataka kila mechi wapange kikosi ambacho kitawapa matokeo mazuri kwa ajili ya kulinda heshima yao badala ya kufanya majaribio ya wachezaji ambayo yanaweza kuathiri matokeo.

Walipewa jukumu hilo la kuiongoza Taifa Stars baada ya kocha mkuu, Adel Amrouche, kufungiwa na CAF kutokana na kulidhalilisha shirikisho hilo kuwa linaburuzwa na Morocco katika maamuzi yake, ikiwa ni pamoja na kupanga siku na muda wa mechi.

Amrouche, raia wa Algeria ambayo kisiasa ina uhasama na Morocco, amefungiwa mechi nane na tayari amekosa mechi nne, mbili za AFCON na mbili za FIFA Series na hivyo kusaliwa na mechi nne.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, alikaririwa na vyombo vya habari wiki hii akisema kuwa wanafikiria kusitisha mkataba wa kocha huyo kwa kuwa kwanza amefungiwa na pili anasemekana hana uhusiano mzuri na wachezaji.

Tuharakishe

Nikiangalia kauli hiyo ya rais wa TFF na hali ilivyo kwa Morocco na Mgunda, nadhani uamuzi wa kumtimua ungefanyika mapema ili shirikisho liwe na uhakika na mtu aliye na dhamana na timu ya taifa na pia, hata atakayepewa dhamana hiyo ajue kuwa ni yake na si ya muda.

SOMA ZAIDI: Mpira wa Miguu Sasa ni Sekta Muhimu, Uratibiwe

Hii itamuwezesha kocha na benchi lake la ufundi kuwa na mipango ya muda mrefu na kuitekeleza kadri mechi za mashindano na za kirafiki zitakavyokuwa zinakuja. 

Haya mambo ya kutaka ushindi kwa nguvu katika kila mechi, yanaweza kutupa picha bandia kuwa tuna timu nzuri, kumbe hatujui hata uzuri wake uko sehemu gani na kushindwa kuuimarisha na hivyo kujikuta tukifanya vibaya mashindanoni.

Ni muhimu sana kuwa na kocha wa uhakika kuanzia sasa kwa kuwa majukumu yaliyo mbele yetu ni makubwa. Tutaandaa fainali za CHAN mwaka huu, tutaandaa fainali za AFCON 2027, tutaanza kutafuta tiketi ya kushiriki AFCON inayokuja na bado hatujamalizia mechi za michuano ya awali ya Kombe la Dunia.

Hii yote haihitaji makocha wa muda kwenye timu iliyopewa dhamana na taifa kuiwakilisha nchi. Ni muhimu TFF ifanye maamuzi mapema katika benchi la ufundi la Taifa Stars.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *