The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mpira wa Miguu Sasa ni Sekta Muhimu, Uratibiwe

Serikali haina budi kuungalia mchezo wa soka kwa jicho la ziada na kufanya kile kinachowezekana kudhibiti ili kuondoa kuibuka na kupotea kwa klabu na hivyo hata ule mvuto pia kupotea.

subscribe to our newsletter!

Serikali ya Uingereza ina mpango wa kupeleka muswada kwenye bunge la nchi hiyo utakaoanzisha ofisi ya Mdhibiti Huru wa mchezo wa mpira wa miguu, ambaye atakuwa na majukumu ya, pamoja na mambo mengine, kuhakikisha klabu zinakuwa imara kifedha.

Muswada huo umekuja baada ya miezi mingi ya kuahirishaahirisha kutokana na sababu tofauti, ikiwa ni pamoja na tukio la miaka mitatu iliyopita wakati klabu za Manchester United, Liverpool na Arsenal zilipotangazwa kuwa zitashiriki mashindano mapya ya European Super League, yaliyoanguka ghafla kutokana na kupingwa na mashabiki, vyama vya soka vya nchi na Serikali.

Tayari Serikali ya Uingereza ilishatoa waraka, au whitepaper, wenye kurasa 99 unaoitwa A Sustainable Future—Reforming Club Football Governance tangu Februari mwaka jana ukionyesha jinsi gani mchezo wa mpira wa miguu umekuwa sekta kubwa ambayo inastahili kuratibiwa na Serikali ili watu watoe maoni yao kabla ya muswada kuwasilishwa bungeni baadaye mwaka huu.

Miongoni mwa mambo muhimu kwenye muswada huo ni kuanzishwa kwa ofisi ya Mdhibiti wa Mpira wa Miguu atakayehakikisha klabu zinakuwa imara kifedha, mfumo wa utoaji leseni kwa klabu, upimaji mpya wa watu wanaotarajia kuwa wamiliki wa klabu ili kuziepusha kumilikiwa na watu wasiojali, mwongozo uendeshaji klabu kama shirika, mtandao na ushirikishwaji wa mashabiki, kanuni za urithi wa klabu na kanuni zinazozuia klabu kuingia katika mashindano ya uasi kama ilivyokuwa kwa European Super League.

Muswada huo, wa kwanza kwa mataifa makubwa katika soka, una lengo la kuulinda mpira wa miguu wa Uingereza, ambako Ligi Kuu imekuwa na umaarufu usio kifani duniani, huku klabu zikitengeneza mamilioni ya dola na wawekezaji wengi wakimiminika kununua hisa.

Kilichosukuma udhibiti

Udhibiti wa klabu za soka ulionekana haukwepeki baada ya klabu ya League Two, ya nne kwa ngazi kutoka Ligi Kuu, ya Bury kuanguka kifedha ghafla mwaka 2019. Mwaka huo, yaani msimu wa 2018-19, Bury ilishika nafasi ya pili ya League Two na hivyo kupanda kwenda League One. Lakini ikashindwa kuanza msimu kutokana na matatizo ya muda mrefu ya kifedha na kusababisha itimuliwe League One.

Mwaka uliofuatia iliwekwa chini ya msimamizi na baadaye kundi la mashabiki likainunua kutoka kwa msimizi na kurejesha makali yake. Hilo ni mojawapo ya mambo yaliyosababisha Serikali kustuka na kuanza kufikiria jinsi ya kudhibiti hali ya kifedha ya klabu za soka.

SOMA ZAIDI: Baraza la Michezo Lifikirie Kuandaa Olimpiki Yetu Kwanza

Tukio la klabu tatu kubwa za England kujiunga na Super League nalo lilitikisa nyanja tofauti, kiasi kwamba mashabiki waliona wamiliki hawajali tena hisia zao zaidi ya kuangalia fedha tu. Kwa hasira, wakafanya fujo zilizozuia mechi ya Ligi Kuu baina ya Liverpool na Manchester United.

Katika muswada huo, kuna kipengele cha kuzuia klabu kushiriki mashindano ya uasi, yaani yanayoanzishwa sambamba na mashindano mengine yanayotambuliwa na ambayo yanaweza kuathiri mashindano mengine. 

Super League, ambayo ushiriki wake hautokani na ushindani katika msimu husika, iliteua timu zinazojulikana kuwa ni kubwa na ambazo hazingekuwa zikishuka daraja.

Super League, ambayo ilianzishwa na taasisi tofauti na Chama cha Soka Ulaya (UEFA) na haikushirikisha vyama vya nchi, ingeondoa umuhimu wa mechi za nyumbani na za Ulaya na hivyo kuudhi mashabiki ambao kwao burudani kubwa ni kuona timu zao zikipambana na Man United, Liverpool na Arsenal.

Muswada huo ukipita kuwa sharia, klabu hazitakuwa na uhuru wa kujiamulia kushiriki mashindano hadi kwa idhini.

Ushirikishwaji wa mashabiki

Pia kuna kipengele cha ushirikishwaji wa mashabiki, ambacho kinataka klabu ama ziunde bodi kivuli kuwakilisha mashabiki katika kufanya maamuzi yanayowagusa au ziwe zinaweza kuwasilisha ushahidi kwamba uamuzi fulani unaungwa mkono na zaidi ya nusu ya idadi ya mashabiki—si wanachama.

Mfano, Singida Big Stars inaamua kubadili jina na kuwa Singida Fountain Gate, au uwanja kutoka Namfua kwenda Kirumba au rangi ya jezi za nyumbani kutoka njano hadi bluu, haitaweza kufanya hivyo hadi uamuzi huo utakapopitishwa na zaidi ya nusu ya mashabiki wake.

SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Idhibiti Uahirishaji Mechi Kiholela, Kuhama Viwanja

Mwaka juzi, mmiliki wa klabu ya Gwambina, Alexander Mnyeti, aliamua kuiondoa klabu yake Ligi Daraja la Kwanza, akidai kuwa haridhishwi na uendeshaji wa soka na kwamba anadhani klabu yake inaonewa. 

Mnyeti alishajenga uwanja mkoani Mwanza ambao ulikuwa unatumiwa na klabu hiyo, lakini wakati anafikiria kujiondoa alisema, “Ni afadhali niutumie kulisha mifugo kuliko mchezo wa soka.”

Hata kama ana hoja kiasi gani, Mnyeti asingeamua kuiondoa timu kwenye ligi bila ya uamuzi huo kuidhinishwa na zaidi ya nusu ya mashabiki wa nyumbani, kwa mujibu wa muswada huo wa kuanzisha ofisi ya Mdhibiti Huru wa Soka.

Kanuni hizo pia, mbali na kuangalia uimara wa klabu kifedha, pia zinaweka vipimo kwa wamiliki wa klabu na wakurugenzi –Owners and Directors Test (OADT)– kwa maana ya kiuchumi na ushiriki wao kisiasa. Iwapo watu wanaotaka kumiliki klabu watapita vipimo hivyo, wataruhusiwa kutekeleza nia yao, hali kadhalika wakurugenzi.

Chini ya kipengele hicho, mbali na mambo mengine, wamiliki watafanyiwa tathmini ya hali yao kifedha, kuangalia vyanzo vyao vya fedha na watatakiwa kuwasilisha mpango mkubwa wa kifedha.

Udhaifu wa kanuni

Kwetu hapa, kanuni hazijaingia ndani sana kuzungumzia umiliki wa taasisi za soka pekee. Klabu za Simba na Yanga zimeshaanza mchakato wa kubadilisha muundo wa umiliki, lakini wa Simba umegota kidogo kutokana na kasoro zilizoonwa na Tume ya Ushindani (FCC), ikiwemo ya kwenda kinyume na kanuni inayotaka wawekezaji wawe zaidi ya mmoja.

Hadi sasa, mwekezaji anayejulikana ni Mohamed Dewji pekee, ambaye amediriki kusema kuwa alishainunua Simba miaka mitano iliyopita, wakati mchakato bado haujakamiliki. Hakuna tathmini iliyofanyika ya hali ya kifedha ya mwekezaji wala kupima uwezo wa wakurugenzi wanaoingia kwenye bodi kwa kuwa hatuna sheria hiyo kwa sasa. 

SOMA ZAIDI: Sheria, Kanuni za Uchaguzi TFF Ziangaliwe Sasa

Pia, Shirikisho la Soka (TFF) bado halijatoa kanuni za kuongoza mchakato wa kumilikisha wawekezaji klabu na hivyo kuwa kikwazo kwa mchakato wa Simba. Hili ni la kujifunza kwa Waingereza kwamba kunahitajika, situ udhibiti, bali mwongozo. 

Kwa sasa klabu zinazidi kuibuka zikiwa na wamiliki binafsi ambao baadhi vyanzo vyao vya kifedha si bayana, baadhi wakiwa wanasiasa na wafanyabiashara. Klabu hizo zinasajili wachezaji kutoka nje ya nchi ambao hulipwa mishahara mikubwa, lakini si TFF wala Baraza la Michezo la Taifa (BMT) linalojua vyanzo halisi vya fedha vya wamiliki hao.

Hivi karibuni, ilikuwa kama sinema. Singida inasemekana imenunuliwa na wamiliki wengine na hivyo kuhama mkoani kwake, wakati Ihefu imenunuliwa na aliyekuwa mmiliki wa Singida Big Stars na hivyo itahamia Namfua. Awali Singida ilijulikana kama Singida United, lakini kulipotokea msukosuko wa kisiasa, nayo ikatetereka hadi kushuka daraja na kupotea.

Mchezo unaopendwa

Nimezungumzia mpango huo wa Serikali ya Uingereza kutokana na kuona mabadiliko yanayoendelea kutokea katika klabu zetu za soka ambao ni mchezo unaopendwa na mamilioni ya Waanzania.

Yanga na Simba zinaendelea na mchakato wa mabadiliko ambao hauna mwongozo wowote maalum kwa mchezo wa mpira zaidi ya ule wa umiliki wa taasisi za kibiashara. Wakati Simba inaonekana kama kukwama, Yanga inaonekana kuwa mapumzikoni baada ya kufanikiwa kubadilisha katiba ili kuruhusu mabadiliko hayo.

Klabu zinazomilikiwa na watu binafsi zinazidi kuibuka na huanzia ligi ya pili kwa ukubwa – Championship – kutokana na wafanyabiashara kununua timu zinazokaribia kupanda daraja na baadaye kuzibadili majina. Timu hizo hazina mizizi na hivyo hazina mashabiki. Hali inayozifanya Simba na Yanga kuwa kubwa kupita kiasi.

Hatujui ni kwa muda gani hawa wafanyabiashara wataendelea kuwa na utashi wa kuendelea kuzimiliki. Kama Singida United ilipotea kutokana na misukosuko ya kisiasa, vipi kuhusu Namungo, Ihefu, Singida Big Stars, Tabora United, Mashujaa na nyingine zilizo Championship zenye umiliki kama huo?

SOMA ZAIDI: Serikali Itafakari Hili la Mafunzo ya Wachambuzi wa Soka Tanzania

Klabu za wananchi kama Tukuyu Stars (Mbeya), African Sports (Tanga), Majimaji (Songea), Lipuli (Iringa) na Mbeya City, ambazo zina mtaji wa mashabiki, zimefifia kwa kuwa hazina fedha na hazikuwa zikidhibitiwa mwenendo wao wa kifedha.

Hakuna haja ya kusubiri yaliyozikuta timu hizo yazikute nyingine zinazoanza kujitengenezea mtaji wa mashabiki lakini hazieleweki zinapataje fedha, ukiachilia mbali zile zinazotokana na matangazo ya televisheni na udhamini wa ligi.

Kwa kuwa soka ni mchezo mkubwa nchini unaovuta hisia za wengi na kuajiri wananchi wengi, kuanzia wachezaji hadi wafanyakazi katika shughuli zinazoambatana na mchezo huo, Serikali haina budi kuungalia mchezo huu kwa jicho la ziada na kufanya kile kinachowezekana kudhibiti ili kuondoa kuibuka na kupotea kwa klabu na hivyo hata ule mvuto pia kupotea.

Soka sasa ni sekta nyeti, ikiajiri wachezaji wanaolipwa pengine kuzidi maofisa watendaji wakuu wa baadhi ya mashirika, hivyo Serikali kuweka mkono katika udhibiti ni kuilinda sekta hiyo isiporomoke na kuathiri ajira na biashara za kampuni, achilia mbali hisia za Watanzania wengi.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *