Search
Close this search box.

Baraza la Michezo Lifikirie Kuandaa Olimpiki Yetu Kwanza

Kwa nini BMT isikusanye wadau na kujadili jinsi ya kuanzisha Olimpiki ya Tanzania, ambayo itahusisha michezo yote na kwa umri tofauti kulingana na ukubwa wa mchezo?

subscribe to our newsletter!

Kuanzia Julai 26, 2024, macho ya wapenzi wa michezo duniani yataelekezwa jijini Paris, Ufaransa ambako wanamichezo mbalimbali watakuwa wakipambana kuwania medali katika Michezo ya Olimpiki.

Michezo hiyo itakuwa ikifanyika Paris kwa mara ya tatu na kuwa jiji la pili duniani kuandaa Olimpiki mara tatu.

Karibu kila nchi iko katika maandalizi ya mwisho kabla ya michezo hiyo mikubwa duniani itakayoshirikisha maraifa 204. Kwetu hapa matarajio makubwa ni kufuatilia nchi za Afrika zitakazofuzu kushiriki upande wa soka na baadaye kuhamia ama Hispania, England, Brazil au Argentina katika hatua za mwisho.

Labda Jumapili ya Agosti 11 ndipo angalau tunaweza kuona wanariadha wetu wakipambana katika mbio za marathoni, mchezo pekee ambao Tanzania ina uhakika si tu wa kufuzu, bali hata kujipatia medali moja. Hadi sasa Tanzania ina medali mbili za Olimpiki na zote ni katika riadha.

Timu ya taifa ya soka ya wanawake Ijumaa ilikuwa inacheza mechi ya kwanza ya raundi ya tatu ya michuano ya kufuzu dhidi ya Afrika Kusini, mechi ambayo ni ngumu kwa wasichana wetu na iwapo watapata matokeo mazuri katika mechi zote mbili watakutana na mshindi wa mechi baina ya Cameroon na Nigeria mwezi Aprili.

SOMA ZAIDI: Bodi ya Ligi Idhibiti Uahirishaji Mechi Kiholela, Kuhama Viwanja

Iwapo timu hiyo, maarufu kama Twiga Stars, itafuzu, itakuwa imeandika historia ya mafanikio kwa soka la wanawake, uchambuzi unaoweza kutoa picha halisi ya matarajio ya Tanzania. Ikifuzu, hali inaweza kuwa tofauti na wale machawa –watu wanaojitoa akili kusifia wengine– maarufu kujitokeza.

Timu ya soka ya Olimpiki iliondolewa mapema na Nigeria baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani na baadaye kulala kwa mabao 2-0 ugenini, katika mechi ambayo viongozi wa Serikali za majimbo walitoa ahadi za mamilioni ya fedha kwa wachezaji ili waishinde Tanzania.

Katika riadha, tayari Alphonce Simbu, Gabriel Geay, Magdalena Shauri na Jacqueline Sakilu wameshafikia viwango vya kushiriki mbio za marathoni. Muda unaotakiwa kufikiwa na wanariadha wanaotaka kwenda Paris ni saa 2:0.26 kwa wanaume na saa 2:26.50 kwa wanawake.

Chama cha Riadha kinataka kiweke rekodi ya ushiriki wake kwa kutuma wanariadha sita wa mbio hizo. Emanuel Giniki na Faraja Lazaro wanasubiri mashindano yatakayofanyika mwezi Aprili kujaribu nafasi yao ya mwisho wakati Josephan Gisamo anasubiri kuchukua nafasi ya mmojawapo iwapo ataumia au atapata tatizo lolote lile.

Mchezo wa ngumi

Bado kuna changamoto katika mchezo wa ngumi ambao pia hufuatiliwa kwa karibu wakati mabondia wa Tanzania wanaposhiriki. Mchezo wa ngumi za ridhaa, ambao ndiyo mtambo wa kuzalisha mabondia wa ngumi za kulipwa, unaonekana kupoa na imekuwa ni tatizo kuandaa mashindano ya taifa ambayo yamekuwa yakizalisha timu ya taifa.

SOMA ZAIDI: Sheria, Kanuni za Uchaguzi TFF Ziangaliwe Sasa

Tanzania haikutuma mabondia katika michezo miwili iliyopita ya Olimpiki na mara ya mwisho, mwaka 2012, ilituma bondia mmoja, Selemani Kidunda, huku ikiweka rekodi ya kutuma mabondia wengi mwaka 1980 ilipowakilishwa na mabondia tisa.

Mabondia hufuzu kwa kushinda katika mashindano ya kanda, kama ilivyo kwa michezo mingine kama ya wavu, kikapu na mpira wa mikono.

Mchezo mwingine ni judo ambao pia umekuwa na changamoto zake, licha ya kuwa matumaini ya medali huonekana kwa wanamichezo wake.

Hakuna matumaini halisi ya ushiriki wa mchezo wa mpira wa wavu, mikono, kikapu na michezo mingine ya riadha kama kurusha tufe, mkuki, kuruka juu na chini, mbio fupi na ndefu.

Katika maandalizi, Kamati ya Olimpiki (TOC), ilianzisha mradi wa Twende Olimpics ambao ulihusisha mafunzo kwa viongozi wa vyama vya michezo mbalimbali ya jinsi ya kuweka mikakati kwa ajili ya michezo hiyo mikubwa.

SOMA ZAIDI: Serikali Itafakari Hili la Mafunzo ya Wachambuzi wa Soka Tanzania

Lakini hakuna matarajio ya kuongeza idadi ya wanamichezo wa Tanzania kwa sababu uhai wa michezo ambayo si soka wala marathoni unaonekana kuwa katika mashine za kupumulia. Na pengine mafunzo ya mradi huo yatumike kujiandaa kwa Olimpiki ya 2028.

Changamoto ya kifedha

Tatizo kubwa linaonekana kuwa kwa vyama kuendesha shughuli zake kitaifa. Inaonekana changamoto ya kifedha imekuwa tatizo kubwa kwa ushiriki wa timu, kiasi kwamba haionekani tatizo tena kwa chama cha mchezo fulani kushindwa kuandaa mashindano ya taifa.

Mchezo wa soka ambao umekuwa ukivutia mashabiki wengi na kampuni za udhamini, huku chama kikipokea ruzuku kubwa kutoka Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) ndiyo pekee unaonekana kujimudu, huku riadha ikitegemea jitihada binafsi za wanariadha wake.

Lakini Chama cha Riadha (AT) kimekuwa kikishindwa kuandaa mashindano makubwa ya kitaifa, ndiyo maana hatuoni tena wanariadha wa mbio fupi, warusha mkuki, kisahani, kuruka juu na michezo mingine.

Wakati fulani baada ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuanzisha Shule ya Sekondari Makongo na mwanariadha gwiji, Filbert Bayi kuanzisha shule yake Kibaha, ilionekana michezo hiyo ya riadha ingefufuliwa.

SOMA ZAIDI: Tumejitahidi AFCON, Lakini Tunajipangaje Upya?

Walijitokeza wasichana na wavulana wadogo katika michezo kama kurusha tufe na kisahani na baadhi mbio fupi na za masafa ya kati ambazo ndizo zimetuletea medali pekee mbili za Olimpiki baada ya Suleiman Nyambui kutwaa medali ya fedha mwaka 1980 jijini Moscow akishiriki mbio za mita 5,000, na Filbert Bayi kushinda medali kama hiyo katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi jijini humo.


Lakini baadaye shule hizo zikafifia katika michezo na hali kadhalika chipukizi wa michezo tofauti na soka pia kutoweka.

Kuamsha michezo mingine

Nini kifanyike? Moja ya majukumu ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ni kuendeleza michezo, lakini jukumu hilo limekuwa ni gumu kwa sababu fedha za maendeleo katika bajeti zinazoelekezwa katika michezo ni ndogo, labda kuwe na miradi mikubwa kama ujenzi wa viwanja.

Wakati Serikali ikiwa katika maandalizi ya kujenga viwanja vipya viwili na kuboresha baadhi, ni muda sasa kwa BMT kuangalia itawezaje kuamsha michezo mingine ili viwanja hivyo vitumike kikamilifu, hasa kutokana na ukweli kwamba Serikali hujenga viwanja vya viwango vya Olimpiki.

Kwa nini BMT isikusanye wadau na kujadili jinsi ya kuanzisha Olimpiki ya Tanzania, ambayo itahusisha michezo yote na kwa umri tofauti kulingana na ukubwa wa mchezo?

SOMA ZAIDI: Kamati ya Hamasa Bila ya Mkakati wa TFF

Olimpiki ya Tanzania, kama wazo lilivyo kwa All Africa Games, itasaidia kuvifanya vyama viwajibike kuamsha ari mikoani na hatimaye wanamichezo wapambane katika jukwaa kubwa ambalo litasaidia kuunda timu za taifa.

Kama timu za mikoa za michezo tofauti zitakutana Uwanja wa Benjamin Mkapa kumenyana kwa wiki mbili au tatu kuwania medali, hilo litakuwa tamasha kubwa la kimichezo Tanzania kuliko mengine yote na litaanza kuwapa wanamichezo picha halisi ya mashindano kama ya Olimpiki.

Tatizo linaweza kuwa ni fedha za kuandaa Olimpiki ya Tanzania, lakini kikao cha wadau kinaweza kutatua tatizo hilo kwa kuwa kadri mipango itakavyopangwa vizuri, ndivyo kampuni zitavutiwa na kuamua kuweka fedha zake. Na bila shaka, hayo yatakuwa maandalizi mazuri kwa Olimpiki ya 2028.


Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *