Search
Close this search box.

Bodi ya Ligi Idhibiti Uahirishaji Mechi Kiholela, Kuhama Viwanja

Ratiba ndiyo chombo kikuu cha kuwezesha ligi kuwa bora, ikiwezesha klabu na wadau wengine kutengeneza fedha, watangazaji na wadhamini kujipanga vizuri.

subscribe to our newsletter!

Wiki iliyopita, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ilitangaza tena mabadiliko ya tarehe za mechi na viwanja vinavyotumiwa na klabu kutokana na sababu tofauti, ikiwa ni pamoja na maombi na mazingira.

Haya ni mabadiliko mengine yaliyofanywa takriban baada ya raundi mbili tangu Ligi Kuu irejee uwanjani baada ya kupumzika kwa karibu mwezi mmoja kupisha fainali za mashindano ya Mataifa ya Afrika zilizofanyika nchini Ivory Coast.

TPLB ilitangaza kusogeza mbele mchezo baina ya Simba na Mtibwa Sugar kuwapa nafasi wawakilishi hao wa Tanzania muda wa kutosha kwa safari yao ya Ivory Coast ambako watacheza na ASEC Mimosas katika mechi ya Ligi ya Mabingwa.

Awali, mchezo huo ulikuwa uchezwe Februari 18, yaani Jumapili, kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, wakati mchezo dhidi ya ASEC utakuwa Ijumaa ya Februari 23. Simba ilikuwa ni viporo vilivyotokana na sababu kama hizo ambavyo ilivimaliza Alhamisi.

Pia, mchezo baina ya Yanga na KMC umehamishiwa Uwanja wa Jamhuri kutokana na maombi ya wenyeji, wakati mchezo baina ya Simba na JKT ulihamishiwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ambao unasemekana una mashimo mengi na hauna hadhi ya kuchezewa Ligi Kuu.

SOMA ZAIDI: Sheria, Kanuni za Uchaguzi TFF Ziangaliwe Sasa

Kwa maneno mengine ni kwamba muda mfupi ujao, Bodi ya Ligi itatangaza kuufungia uwanja huo kwa maelezo kuwa umekosa sifa za kuchezewa mechi za Ligi Kuu.

Bado klabu kama Singida Fountain Gate haijaamua kabisa itumie uwanja gani, maana kuna taarifa kwamba inataka kutumia uwanja wa Sheikh Amri Abeid au Kirumba Stadium, huku KMC ikiwa haijatulia Morogoro.

Ni kama mabadiliko ya tarehe na viwanja kwa ajili ya Ligi Kuu sasa ni mazoea ambayo ni vigumu kuyaacha na vile mabadiliko hayo hayana athari zozote kwa klabu, TPLB, Shirikisho la Soka (TFF), wadhamini, watangazaji, na wadau wengine.

Kwamba jukumu la hao wote ni kusubiri TPBL itangaze mabadiliko halafu wafikirie nini cha kufanya na si kwamba bodi iwafikirie wadau wake kabla ya kufanya mabadiliko.

Ratiba

Moja ya nyenzo kubwa kwa klabu, TPLB yenyewe, wadhamini, watangazaji na wadau wengine kujipanga ili kufanya shughuli zao vizuri ni ratiba. Kadri ratiba inavyokuwa imara, ndivyo wadau wote wanavyojipanga kufanya shughuli zao kwa ufanisi mkubwa na hatimaye kuiwezesha Ligi Kuu kuwa bora.

SOMA ZAIDI: Serikali Itafakari Hili la Mafunzo ya Wachambuzi wa Soka Tanzania

Fikiria tu shabiki ambaye amepanga aangalie mechi labda sita za Mashujaa msimu huu, tatu za nyumbani na tatu za ugenini. Huyu atajipanga vipi kwa safari iwapo hana uhakika wa mechi hizo? Kama muajiriwa ni lazima atengeneze mazingira ya ruhusa ofisini, kama ni mfanyabiashara ni lazima ajue ataachaje shughuli zake katika kipindi hicho. Atafanyaje bila ya kuwepo ratiba imara?

Fikiria kampuni inayodhamini ligi. Katika kila mechi ni lazima iwe na shughuli za kunogesha udhamini, yaani inatuma wafanyakazi wake kwenye mkoa ambao mechi inachezwa. Itajipangaje kibajeti kwa ratiba inayobadilika kila mara?

Fikiria mfanyabiashara wa pale Mwanza ambaye baada ya ratiba ya kwanza kutoka, alijipanga vizuri kutumia fursa hizo kutengeneza fedha lakini leo anaambiwa Geita imehamisha mechi zake kwenye viwanja vya nje ya mkoa.

Fikiria watangazaji wa Ligi Kuu, yaani Azam Media, ambao hulazimika kutuma jopo lao katika kila mechi. Watajipangaje kibajeti iwapo ratiba inabadilika hovyo? 

Fikiria vyombo vya habari vya ndani na nje, ambavyop vingependa kutuma waandishi wake kwa ajili ya zile mechi kubwa, halafu vinaambiwa kuwa baadhi ya mechi zimesogezwa mbele hadi zitakapotangazwa tena.

SOMA ZAIDI: Tumejitahidi AFCON, Lakini Tunajipangaje Upya?

Fikiria kampuni ya kuendesha matukio ambayo ilipanga kunogesha mji fulani kwa kuweka onyesho la muziki, ikitegemea kuwa siku hiyo mashabiki baada ya kutoka uwanjani watapata sehemu ya kwenda kuburudika. Leo wanaambiwa wasubiri hadi itakapotangazwa tena, wakati washaingia makubaliano na wasanii kuhusu siku hiyo.

Na vipi klabu ambazo hutafuta wadhamini wa siku ya mechi kulingana na eneo wanalochezea? Yanga imeingia makubaliano na benki moja ili wanachama watakaolipia kadi ya Shilingi milioni moja wawe na tiketi za kuona mechi kumi za nyumbani na marupurupu mengine. Vipi mechi hizo zikihamishwa?

Udhibiti

Ni lazima Bodi ya Ligi ijirekebishe na kuanza kudhibiti uahirishaji mechi kiholela. Kanuni ni lazima ziboreshwe kwa lengo la kudhibiti klabu kuomba kuhamisha viwanja. Ni lazima kanuni zieleze mazingira yatakayowezesha klabu kukubaliwa kuhamisha au kubadili kitu chochote. Kanuni zisiishie mabo ya siku saba kabla ya mechi.

TPLB pia haina budi kuwa makini katika kuruhusu matumizi ya viwanja. Kabla ya msimu kuanza, TPLB hutuma wakaguzi kwenye viwanja vyote vilivyoombwa na klabu kwa ajili ya Ligi Kuu. Lakini huwa tunashuhudia baada ya raundi moja tu, uwanja unafungiwa kwa kukosa sifa. Vipi waliokagua na kuihakikishia TPLB kwamba uwanja huo unasifa zote? Huwa wanachukuliwa hatua gani?

Ili klabu zisihamehame ni lazima suala la ukaguzi lifanyike kwa ufasaha ili kusiwepo hatua za kuufungia uwanja na klabu kulazimika kutafuta viwanja vingine.

SOMA ZAIDI: Kamati ya Hamasa Bila ya Mkakati wa TFF

Ratiba ndiyo chombo kikuu cha kuwezesha ligi kuwa bora, ikiwezesha klabu na wadau wengine kutengeneza fedha, watangazaji na wadhamini kujipanga vizuri. Ligi isiyo na ratiba imara huondoa mipango mingine mingi ya wadau kujihusisha nayo na matokeo yake mechi za ligi huwa ni dakika tisini tu.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *