The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Yanga Imefanyiwa Ukatili, CAF Ifanyie Kazi V.A.R

CAF haina budi kufanyia kazi suala la matumizi ya V.A.R na haina budi kuonyesha ukali ili waamuzi wasiendelee kujifanyia mambo watakavyo kwa kuwa tu wanayo mamlaka hayo.

subscribe to our newsletter!

Safari ya wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano ya soka barani Afrika ilikoma Ijumaa baada ya Simba na Yanga kupoteza michezo yao ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya wawakilishi wa Misri, Al Ahly na wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns ambao walinufaika na makosa ya refa na wasaidizi wake.

Simba, iliyokuwa ikihitaji ushindi ili isonge mbele baada ya kupoteza mechi ya kwanza nyumbani kwa bao 1-0, ilipoteza tena mchezo kwa kufungwa mabao 2-0 na Al Ahly kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo nchini Misri.

Yanga, iliyolazimishwa sare ya bila kufungana nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, iliondolewa kwa mikwaju ya penati baada ya mechi ya marudiano iliyofanyika Uwanja wa Loftus Versfeld kuisha tena bila timu hizo kuzifumania nyavu.

Gumzo kubwa baada ya mechi hizo za marudiano ni tukio lililotokea katika dakika ya 59 wakati mshambuliaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, alipopiga shuti na mpira kugonga mwamba na baadaye kuonekana ukidunda ndani ya lango la Mamelodi kabla ya kurejea uwanjani.

Hata picha za marudio zinaonyesha mpira ulishavuka mstari wa goli, lakini mwamuzi Dahana Beida, ambaye alisimamisha mchezo baada ya tukio hilo, aliwasiliana na Mwamuzi Msaidizi wa Video (V.A.R) na baadaye kuamua kuwa halikuwa goli na hivyo kuendelea na mchezo.

SOMA ZAIDI: TFF Ifanye Uamuzi Mapema Kocha wa Taifa Stars

Aibu

“Tumeporwa ushindi,” alisema kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, alipoongea na waandishi wa habari baada ya mchezo. “Kila mtu ameona na sitajibu tena maswali yenu. Siwalaumu Mamelodi, lakini nachosema tumeporwa. Kilichotokea ni aibu kwa mpira wa Afrika.”

Ndiyo, ni aibu kwa soka la Afrika.

Katika matukio tata kama hayo, mwamuzi alitakiwa ajiridhishe kwa kwenda kwenye runinga iliyo pembeni ya uwanja kuangalia picha za marudio ili kufanya uamuzi sahihi, lakini aliamua kuendelea na mchezo akiridhika na mawasiliano yake na V.A.R.

Teknolojia ya video iliruhusiwa kutumika katika mashindano ya soka mwaka 2018 kusaidia waamuzi kufanya maamuzi sahihi ya matukio muhimu ili mchezo huo upate washindi wanaostahili.

Matukio hayo ni kukubali au kukataa goli, kukubali au kukataa penati, uamuzi sahihi kuhusu kadi nyekundu ya moja kwa moja na kuonyesha kimakosa kadi nyekundu au njano kwa mchezaji ambaye hakufanya madhambi.

SOMA ZAIDI: TFF, TPLB Ziamke, Azam Media Siyo Mfadhili

Kanuni za matumizi ya V.A.R zinalazimisha waamuzi wafanye kwanza uamuzi kabla ya mwamuzi msaidizi wa video kuingilia na kutoa ushauri ili kuwaepusha waamuzi kuwa tegemezi wa teknolojia hiyo. Kwa hiyo, baada ya ushauri, na wakati mwingine kuangalia picha za marudio, mwamuzi anaweza kuendelea na uamuzi wake wa awali au kuubadili.

Kwa kuwa kipa wa Mamelodi, Ronwen Williams, aliuwahi mpira uliopigwa kichwa na beki wake kabla haujatoka, na kwa kuwa mwamuzi aliomba apewe mpira ili audunde kuashiria kuendelea na mchezo, haieleweki Baena alisimamisha mchezo baada ya kufanya uamuzi gani.

Alisimamisha mchezo ili kushauriana na mwamuzi msaidizi wa video au alipuliza filimbi kuashiria mpira ulishatoka nje, au alipuliza filimbi kukubali goli?

Na kwa kuwa mwamuzi alionyesha ishara kuwa halikuwa bao, maana yake ni kwamba alishafanya uamuzi wa awali wa kukubali goli na hivyo ilikuwa muhimu kwake kwenda kwenye runinga ya uwanjani kujiridhisha na uamuzi alioufanya awali badala ya kusikiliza anachoambiwa na mwamuzi msaidizi kuhusu tukio ambalo lingeweza kuamua mechi.

Matatizo

Teknolojia ya V.A.R imekuwa na matatizo tangu Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) lianze kutumia katika mashindano ya ngazi ya klabu.

SOMA ZAIDI: Utitiri wa Marathoni Unakisaidiaje Chama cha Riadha Tanzania?

Katika mwaka wake wa kwanza, vifaa vyote viliwekwa uwanjani lakini wakati wa mchezo teknolojia hiyo haikutumika kuamua matukio tata. Mfano, Orlando Piarates walilalamikia teknolojia hiyo kutofanya kazi katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Simba mwaka 2022 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Tukio kama bao la Aziz Ki lilitokea mwaka 2019 katika fainali ya Kombe la Shirikisho wakati mwamuzi wa Gambia, Bakari Gassama, alipoamua kutotumia picha za marudio kujiridhisha uamuzi wake wa kukataa bao lililofungwa na kiungo wa Wydad Casablanca, Walid El Karti, katika dakika ya 58 na kusababisha vigogo hao wa soka wa Morocco kuamua kugomea mchezo na kutoka uwanjani.

Katika fainali zilizopita za Mataifa ya Afrika (AFCON 2023) ambazo zilisifiwa kwa uamuzi bora, Algeria iliandika barua kwenda CAF kulalamikia matumizi ya teknolojia hiyo katika mchezo wao wa makundi dhidi ya Burkina Faso ulioisha kwa sare ya mabao 2-2.

Yapo matukio mengi yanayoonyesha matumizi mabovu ya V.A.R katika soka barani Afrika, lakini pale yanapoonekana dhahiri na kuhusisha timu inayomilikiwa na rais wa CAF, hoja huibuka kwamba huenda waamuzi wanapewa maelekezo, au wana woga kufanya uamuzi hasi dhidi ya timu ya rais, kama lawama zilivyoibuka kwenye fainali za AFCON 2023 dhidi ya Afrika Kusini baada ya kiongozi huyo wa shirikisho la Afrika, Patrice Motsepe, kuonekana katika kila mechi za nchi yake.

Lakini kwa kuwa matatizo ni mengi na yanahusu klabu tofauti, kasoro hizi ni aibu kwa soka la Afrika, na kwa kuwa uamuzi ni kitu muhimu katika michezo, matatizo hayo hayatoi washindi sahihi katika dunia ambayo inategemea sana matumizi ya teknolojia ili kufanya maamuzi sahihi.

SOMA ZAIDI: Mpira wa Miguu Sasa ni Sekta Muhimu, Uratibiwe

Pamoja na kwamba matokeo huwa hayabatilishwi, CAF haina budi kufanyia kazi suala la matumizi ya V.A.R na haina budi kuonyesha ukali ili waamuzi wasiendelee kujifanyia mambo watakavyo kwa kuwa tu wanayo mamlaka hayo.

Kama uamuzi kama huo ulikuwa aibu kubwa kwa Afrika baada ya mechi ya fainali kuvunjika katika dakika ya 58, matukio mengi makubwa yanaweza kutokea iwapo CAF haitachukua hatua zinazostahili kumaliza tatizo la V.A.R.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *