The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

CAF Ilitafutie Suluhu ya Kudumu Suala la Morocco

Ikiwezekana ramani ya Morocco isijumuishwe kwenye jezi ya nchi hiyo ili michezo ichukue jukumu lake kuu la kuunganisha watu na si kutumika kutangaza siasa ambazo hazijapata muafaka.

subscribe to our newsletter!

Fainali ya Kombe la Shirikisho itazikutanisha klabu za Zamalek ya Misri na RS Berkane ya Morocco ambazo zimepitia njia zenye mazingira tofauti hadi kufika hatua ya mwisho ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa katika ngazi ya klabu barani Afrika.

Wakati Zamalek ililazimika kupata matokeo mazuri katika hatua za awali, ikiwemo ushindi wa ugenini wa mabao 3-0 dhidi ya Dreams FC ya Ghana, RS Berkane haikugusa hata mpira kuitoa USM Alger ya Algeria katika mechi mbili za nusu fainali.

Katika mechi ya kwanza, RS Berkane waligoma kuingia uwanjani wakidai wapewe jezi zao zilizoporwa na mamlaka nchini Algeria kutokana na nguo hizo kuwa na ramani ya Morocco inayojumuisha eneo ambalo nchi hiyo inalikalia kwa mabavu huku Algeria ikiwa na maslahi huko.

Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) likaamua kuipa ushindi RS Berkane licha ya timu hiyo kugoma kuingia uwanjani. Na katika mchezo wa marudiano nchini Morocco, USM Alger iligoma kuingia uwanjani ikiendelea na msimamo wa nchi yake wa kupinga jezi zenye ramani inayojumuisha eneo linalokaliwa kimabavu.

Na kwa kitendo hicho, CAF ikaipa tena ushindi RS Berkane na hivyo kuifanya iingie fainali bila ya kupiga mpira, ikiwa na ushindi wa jumla ya mabao 6-0 ambayo hayakufungwa na wachezaji.

SOMA ZAIDI: Tutapataje Mabondia Bora Bila Ngumi za Ridhaa?

Siasa kali

Huo ni mwendelezo wa siasa kali za kaskazini mwa Afrika ambazo mara kadhaa zimeathiri mechi za soka na sasa zimeingia hadi kwenye michezo mingine baada ya timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ya mpira wa mikono kukataa kucheza na Morocco kutokana na jezi zao kuwa na ramani hiyo.

Inaonekana Morocco imeamua kutumia michezo kuhalalisha kitendo chake cha kukalia kimabavu eneo la kaskazini mwa Sahara Magharibi, ikinufaika na rasilimali zilizoko huko, ikiwa ni pamoja na zile za baharini na madini.

Si Umoja wa Mataifa (UN) wala Umoja wa Afrika (AU) ambao umepitisha azimio la kuunga mkono kitendo hicho licha ya nchi kadhaa kuwa upande wa Morocco, ikiwa ni matokeo ya ziara ya mfalme wa nchi hiyo kutembelea nchi mbalimbali kushawishi viongozi waunge mkono kitendo hicho.

Na kama hali itaendelea hivi, tutashuhudia mechi nyingi zikishindwa kufanyika kadiri mataifa yatakavyokuwa yanawaunga mkono wapiganaji wa Polisario ambao wanataka Sahara Magharibi itangazwe kuwa taifa huru wakipinga ubabe wa Morocco.

Karibu theluthi mbili ya wananchi wa Sahara Magharibi ni wakulima wakubwa kutoka Morocco na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kusafirisha wananchi kwenda kuishi eneo linalokaliwa kimabavu ni kuvunja sheria za kimataifa.

SOMA ZAIDI: Wimbi la Wachezaji Kuvunja Mikataba Lidhibitiwe

Taifa huru

Kanuni kuu ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) katika kuipa nchi uanachama wake ni kuwa taifa huru, yaani lenye Serikali, mipaka, watu na linalotambuliwa na jumuiya ya kimataifa, kwa mujibu wa katiba ya Umoja wa Mataifa iliyoboreshwa baada ya Vita Kuu vya Pili vya Dunia.

Kwa hiyo, kuvamia eneo la nchi na kulijumuisha kwenye ramani ni kwenda kinyume na katiba ya Umoja wa Mataifa kwa kuangalia suala la mipaka katika sifa kuu za taifa.

Kwa hiyo, uamuzi wa CAF kuipa ushindi RS Berkane ni kuonyesha kutambua kitendo cha Morocco kukalia kwa mabavu eneo hilo ambalo sasa linatambulika kama Jimbo la Kusini la nchi hiyo.

Na ikiendelea hivi, Serikali ya Morocco itaendelea kutumbukiza vitu vingi kwenye michezo kwa kuwa inaona ndiko ambako mambo yake yanakubalika kirahisi tofauti na huku kwenye siasa ambako kuna mlolongo mrefu hadi uvamizi utambulike rasmi.

Hivi sasa CAF inaendesha shughuli zake nyingi nchini Morocco, ambako mfalme wa nchi hiyo amejenga miundombinu bora kwa ajili ya michezo. Hivyo, semina, mafunzo, mikutano mikubwa na shughuli nyingi za CAF hufanyika nchini Morocco. Nchi hiyo ndiyo pia itakuwa mwenyeji wa fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025).

SOMA ZAIDI: Kwa Kufundisha Watoto Hujuma, Tunajenga Taifa la Aina Gani?

Fainali zilizofanyika Algeria hazikuijumuisha Morocco kwa sababu za kisiasa. Algeria iliizuia Morocco kutumia ndege ya moja kwa moja kuingia nchini kwake. Morocco ikagoma na baadaye ikajitoa. 

Kuna uwezekano mkubwa Algeria ikagomea pia fainali za AFCON 2025, au ikaenda lakini ikagoma kucheza na Morocco endapo zitakutana katika hatua za juu za mashindano hayo makubwa kwa nchi.

Hoja ya wazi

Kuna hoja inayoonekana ya wazi kwa Algeria au timu zake kupinga kitendo cha Morocco kulazimisha timu zake kuvaa jezi zenye ramani ya nchi hiyo inayojumuisha eneo linalokaliwa kimabavu kwa kuwa kinavuruga hata saikolojia ya wanaohusika katika mchezo huo kama wachezaji na hata waamuzi kutoka nchi pinzani wanaopangwa kuchezesha mechi za soka zinazohusisha timu za Morocco.

Ni hoja ambayo haipaswi kupuuzwa na CAF na hivyo ni muhimu kwa shirikisho hilo kujadili suala hilo kwa mapana na marefu yake na kukubaliana na Serikali na Shirikisho la Soka la Morocco kuhusu kitendo cha timu zake kutumia ramani hiyo kwenye jezi. 

Ikiwezekana wakubaliane ramani isijumuishwe kwenye jezi ili michezo ichukue jukumu lake kuu la kuunganisha watu na si kutumika kutangaza siasa ambazo hazijapata muafaka kwenye jukwaa lake.

Ni muhimu kwa timu kuendelea kupata ushindi uwanjani kuliko hali hii inayozidi kukua ya kushinda kwa sababu za kisiasa.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *