The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Jamhuri ya Korea: Nchi ya Bahati na Misaada

Jamhuri ya Korea ya Kusini imekua nchi ya kupigiwa mfano wa namna nchi za Afrika zinaweza kujifunza kwao na kuendeleza nchi zao kufuta umasikini na kua tajiri, tena ikizingatiwa kuwa Korea Kusini haina rasilimali nyingi kama nchi za Afrika.

subscribe to our newsletter!

Saa nne usiku, jamaa mmoja, baunsa, ananiwekea mkono kifuani kunizuia nisiingie kwenye mgahawa mmoja uliyochangamka, katika mtaa wa Hongdae, jijini Seoul, nchini Korea Kusini, au Jamhuri ya Korea kama taifa hilo la kusini-mashariki mwa Asia linavyojulikana. 

Ananiambia, kwa Kiingereza cha kubabaisha, “Hapa Wamarekani hawaruhusiwi kuingia.” Namshangaa! Nami namjibu mimi siyo raia wa Marekani, natokea Tanzania na namuonyesha kitambulisho. Ananiruhusu kuingia baada kuridhika mimi siyo Mmarekani. 

Hali hiyo inanishtua na kunishangaza, baada ya kula na vinywaji, nauliza kwa nini hawaruhusu Wamarekani mule? Mhudumu ananijibu, huku akitabasamu, kuwa, “Hapa kuna kambi kubwa ya jeshi la Marekani. Baadhi ya askari wao wakija mara nyingine wakishalewa wanakua wasumbufu.”

Maisha bwana! Kuna mahala kua Mtanzania kuna maana sana kuliko kua Mmarekani, nikajichekea moyoni.

Korea Kusini ni nchi iliyoendelea sana kiuchumi, kisayansi, kiteknolojia, kiubunifu, na kibiashara, na la kushangaza zaidi ni kua kwenye miaka ya 1960, uchumi wao haukua umepishana sana na baadhi ya nchi za Kiafrika kama Ghana au Tanzania. 

SOMA ZAIDI: Mkopo wa Dola Bilioni 2.5 Kutoka Korea Kusini: Je, Tanzania Imeweka Rehani Bahari na Madini Yake?

Lakini ndani ya miaka 30, watu wa taifa hili walitoka kuwa nchi masikini mpaka kuwa nchi tajiri, hata kutoka kua nchi iliyokua inategemea na kupokea misaada na kua nchi inayotoa misaada kwa nchi zingine!

Jamhuri ya Korea ya Kusini imekua nchi ya kupigiwa mfano wa namna nchi za Afrika zinaweza kujifunza kwao na kuendeleza nchi zao kufuta umasikini na kua tajiri, tena ikizingatiwa kuwa Korea Kusini haina rasilimali nyingi kama nchi za Afrika. 

Binafsi ilikua mara yangu ya tatu kufika Korea Kusini, ila wakati huu nilikua nimeenda kama sehemu ya Ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambae aliamua kuambatana na baadhi ya vijana wajasiriamali ambao wanatokea kwenye ekolojia ya startup nchini.

Pamoja na mambo mengine mengi yaliyotokea kwenye ziara hii, ikiwemo mikataba ya mashirikiano, mikataba ya biashara, misaada na mikopo, pia ilikua fursa nzuri kujifunza kutoka kwa wenzetu: wamefikaje walipo, fursa, na changamoto walizonazo. 

Binafsi, haya ndiyo machache ambayo kwangu nilijifunza Korea kwenye ziara hii:

Msaada wa Marekani

Korea na Marekani ni nchi marafiki sana. Kwa kiasi kikubwa, maendeleo ya Korea yamechangiwa na msaada mkubwa na endelevu walioupata kutoka nchi ya Marekani na washirika wake. 

SOMA ZAIDI: Korea Ilikua Masikini Kuliko Nchi Nyingi Afrika, Leo Inatoa Misaada Afrika. Imewezaje?

Baada ya kuisha kwa Vita ya Pili ya Dunia, rasmi ilianzia vita baridi, ikiongozwa na kambi mbili zilizokua zikiongozwa na Marekani, waliofuata mrengo wa kibepari na soko huria, na upande mwingine Umoja wa Kisovieti (USSR) wenye mrengo wa kikomunisti. 

Korea ya Kusini waliamua kua upande wa Marekani na washirika wake. Kwa wakati huo, Marekani ilichagua bara la Asia kuwa eneo la kimkakati na kuamua kuwekeza kuendeleza nchi zilizokua huko ili kuzivutia nchi zingine kisiasa, kisera na kiulinzi. 

Bahati hii ikawadondokea Korea, na kilichofuata ni kupewa misaada ya fedha, teknolojia, ulinzi na masoko ya kuuza bidhaa zao nchi za magharibi. Msaada waliopata Korea ya Kusini ulikua wa kipekee sana, kwa ukubwa wake na mfululizo wake. 

Kwa mfano, kati ya mwaka 1946-1978, Korea Kusini ilipokea msaada kutoka Marekani wa Dola za Kimarekani billioni sita, na bara zima la Afrika lilipewa Dola za Kimarekani bilioni 6.8 tu. 

Tunachojifunza hapa ni kuwa msaada siyo kitu kibaya, ila ni aina, wingi wake, na uendelevu wake. Afrika na Tanzania bado haijawahi kuwa na fursa ya namna hii. Misaada yetu imekua na masharti mengi, midogo na siyo yenye uhakika.

Chaebols

Uchumi wa Korea Kusini umejengwa na kushikiliwa na makampuni na familia chache, zinazoitwa Chaebols. Kampuni hizi ni kama Samsung, Hyundai, LG, na kadhalika. 

SOMA ZAIDI: Rais Samia, Tunaomba Utuachie Kitabu Chenye Hadithi Nzuri

Miaka ya 1960, Serikali ya Korea iliamua kimkakati kukuza uchumi wake kutoka kua unaotegemea kilimo kuwa na ule wa viwanda kwa kuziwezesha kampuni chache kwa kuwapa mitaji, mikopo, teknolojia kutoka nje, misamaha ya kodi na masoko ya nje. 

Hizi kampuni zikaajiri watu wengi sana na kuzalisha kila aina ya bidhaa, na kusaidia mauzo ya nje ya Korea. Kampuni hizo mpaka leo zinashikilia uchumi wa Korea na kuzifanya familia chache kua tajiri sana. 

Kampuni hizi zinazoitwa Chaebols ni tano kubwa na zinachangia nusu ya uchumi mzima wa Korea, huku kampuni ya Samsung peke yake ikichangia asilimia 22 ya uchumi mzima wa Korea. Kampuni hizi pia zimesaidia maelfu ya kampuni zingine ndogo na za kati kwenye mnyororo wa thamani ya uzalishaji na uwepo wao.

Funzo hapa ni kwamba siyo lazima kila mtu awe mfanyabiashara ili nchi iendelee, badala yake wachache wenye uwezo wanaweza kusaidiwa ili wao wazalishe na waajiri wengine.

Startups 

Mwaka 2017, Korea Kusini iliamua kufanya suala la Startup na biashara ndogo na za kati kua suala la kimkakati na kuamua kuunda wizara maalum ya Startups na biashara ndogo na za kati. 

SOMA ZAIDI: Tukitaka Maendeleo, Hatuwezi Kukwepa Uwekezaji Mkubwa Kwenye Tafiti

Startups ni biashara zinazoanza, zenye ubunifu na uwezekano wa kukua haraka. Korea wamefaidika sana na kukuza biashara zao chache kufanikiwa kama Samsung, ila kwa sasa wamegundua hizi chaebols haziwezi kukua zaidi ya zilivyo sasa. 

Hivyo, kama nchi, wanawekeza kwenye Startups ili ziwe ndiyo kampuni mpya chachu ya maendeleo ya uchumi, ajira na uwekezaji kwa sasa na baadaye. Tayari Korea wana ikolojia ya Startup ya pili kwa ukubwa barani Asia, wakiwa na Startups zaidi ya 2,000 na 14 kati ya hizo zikiwa Unicorn, yaani zenye thamani zaidi ya Shilingi trillioni 2.6. 

Basi Tanzania tunaweza kuziona Startups kama fursa ya kiuchumi na ajira, kwani tayari tuna Startups takribani 700 na ndani ya miaka mitatu zimeshavutia uwekezaji kutoka nje ya nchi wa takribani Shilingi billioni 520. 

Jambo la kupongeza ni kwamba Rais Samia amesema hadharani Startups ni moja kati ya sekta ya kipaumbele kwa Serikali yake.

Demografia

Takwimu zinaonyesha miaka 50 baadaye, idadi ya watu wa Korea itapungua kutoka millioni 51 waliopo sasa mpaka millioni 36. Na nusu ya watu hao watakua wazee wenye umri wa miaka 65 au zaidi! Hii ndiyo changamoto kubwa inayowakabili watu wa nchi ya Korea kwa sasa. 

SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Hatujaweza Kutumia Uhuru Wetu Kuleta Maendeleo ya Taifa Letu

Uwepo wa wazee wengi na watu wachache inamaanisha kupungua kwa nguvu kazi na kuongezeka kwa idadi ya wategemezi. Serikali yao imekua na mikakati mingi ya kuhamasisha raia wake kuzaa watoto wengi, lakini bado inaonekana mikakati hiyo haijafanikiwa. 

Tofauti na kwetu Tanzania, ambapo wastani wetu wa kuzaa bado ni mzuri na tuna vijana wengi kuliko wazee, nchini Korea Kusini idad ya wazee inatishia kuipiku ile ya vijana. Hii changamoto imewalazimu Korea kuanza kufungua mlango wa ajira kwa wageni kwenda kuhamia kufanya kazi nchini huko. 

Moja kati ya nchi zilizoko mbioni kufaidika na fursa hii ni Tanzania ambapo Balozi wetu nchini Korea, Mheshimiwa Togolani Idriss Mavura, ameshaanza mazungumzo na Serikali ya Korea kufanikisha mchakato huu.

Binafsi kwangu haya maeneo manne ndio yalikaa zaidi akilini: bahati ya Kosea Kusini kua katikati ya vita baridi ya dunia; maarifa yao ya kutumia jiografia; misaada waliyopata kuendelea kiuchumi; na changamoto zinazokuja kama matokeo ya maendeleo, kama hili la idadi ya watu. 

Shukrani za kipekee kwa Mheshimiwa Balozi Togolani Mavura kwa kufanikisha ziara ya kihistoria, iliyofanikisha nchi kupata mkopo wa masharti nafuu wa takribani Shilingi trillioni sita na billioni 300. Nchi iliyopata bahati ya kupewa misaada, sasa nayo inatoa misaada.

Kazi Iendelee!
Zahoro Muhaji ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Startup Association. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia zahoromuhaji@gmail.com au X kama @ZMuhaji. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 Responses

  1. Big up uncle! Well crafted article. We can pick some ideas and customize to Tanzania economic environment with our own synergy and thoughts for better outcomes.

  2. Hakika ni somo la kujifunza kama nchi kutoka kwa waliofanikiwa kama Korea ya Kusini……big up Zahoro wa GZF💪🏽👏🏽🙏🏽

  3. Dhairi watz tunapenda maendeleo Kwa maneno ,pamoja na kujionea na kujifunza toka Korea ya kusini,,bado roho za ubinafsi zmetamalaki Kwa watz, ndio maana uongozi tz ni ufisadi Tu ,,, na hii ndiyo inayotumika Sana na viongozi wetu kwani mtaji wao wa kutawala na kuendekeza ufisadi ni kuwa na idadi kubwa ya watu wasiojitambua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *