The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Juma Duni Haji: Tafsiri ya Mwanasiasa Mnyenyekevu

Jumatano ya Septemba 4, 2024, ACT Wazalendo tunafurahi na kuenzi maisha ya kisiasa na uongozi ya Juma Duni Haji, kiongozi wetu aliyetuvusha kwenye mapito mengi.

subscribe to our newsletter!

Sikutaka kuandika makala haya. Hukupaswa kuisoma kabisa. Unaisoma kwa sababu ya maneno ambayo nimeambiwa jijini Mbeya na mmoja wa wanasiasa waandamizi katika siasa za upinzani mkoani humo, na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa ujumla.

Niliomba kupata naye kifungua kinywa asubuhi ya siku nimeandika makala haya. Katikati ya mazungumzo yetu marefu ambayo yalikuwa yanapitia hali ya siasa ya mkoa wa Mbeya na mapito yake, mwanasiasa huyu akatamka maneno yaliyoniingia kichwani na moyoni.

“Mwami, siasa za upinzani hapa Tanzania ni sawa na harakati za ukombozi, kila mmoja ana mchango wake,” aliniambia. “Nyinyi ambao mmefanikiwa kupata nafasi za juu huwa mnasahau michango ya wengine na kudhani kuwa ni nyinyi peke yenu mmejitoa katika kujenga vyama vyetu ambavyo mimi naviona ni zaidi ya vyama vya siasa. Ni vyama vya ukombozi.” 

Sikuyanukuu kwa ufasaha maneno yake lakini nilichokinukuu kinabeba ujumbe mzima nilioupata.

Palepale nilianza kuyatafakari maneno haya kwa kina. Nilitoka pale kuwahi uwanja wa ndege wa Songwe ili kurejea Dar es Salaam. Nikiwa ndani ya ndege fikra za maisha ya mwanasiasa mkongwe, Juma Duni Haji, zilinijia na kuunganisha na maneno ya mwanasiasa yule wa mkoani Mbeya. 

Nikakata shauri kuandika machache kuhusu Juma Duni Haji, Mwenyekiti wa Taifa Mstaafu wa chama cha ACT Wazalendo. Nilikata shauri hili kwa kuunganisha maneno ya mwanasiasa wa Mbeya na tukio ambalo linafanyika Septemba 4, 2024, tukio la kuenzi maisha ya Juma Duni Haji katika Siasa za Zanzibar na za Tanzania kwa ujumla. Ninaamini kuwa tukio hili linasaidia kuonesha kuwa tunapaswa kuthamini mchango wa kila mtu katika harakati za kujenga demokrasia hapa Tanzania.

Kazi na Babu Duni

Sijafanya kazi kwa muda mrefu na Mzee Duni, maarufu Babu Duni. Nimefahamiana naye kikazi haswa mara baada ya wanasiasa waandamizi wa Zanzibar, chini ya hayati Maalim Seif Sharif Hamad, na wafuasi wao walipoamua kujiunga na ACT Wazalendo kama jukwaa la kuendeleza mapambano yao ya kupigania demokrasia na haki ya Zanzibar katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

SOMA ZAIDI: Je, Viatu vya Zitto Kabwe Vitamtosha Kiongozi Mpya wa ACT-Wazalendo Dorothy Semu?

Nakumbuka mara baada ya Shusha Tanga, Pandisha Tanga, kama tulivyoita mchakato ule, uteuzi wangu wa kwanza kabisa wa watu kutoka Chama cha Wananchi – CUF ulikuwa ni wa Juma Duni Haji kuwa Naibu Kiongozi wa Chama. 

Mimi binafsi sikuona kama jambo lile ni kubwa mpaka siku nilipokwenda Zanzibar, Ofisi za Chama Vuga na kukutana na Babu Duni, alinishukuru kwa maneno ya hekima kubwa kiasi nikajiona kama Rais vile aliyeteua ama Waziri au hata Waziri Mkuu. 

Kwa Kiswahili chake cha kaskazini ya kisiwa cha Unguja aliniambia, “Babu Zitto, nashukuru sana kuniteua kuwa Naibu [Kiongozi wa Chama] KC, nimetumiwa salamu nyingi za pongezi katika simu, nikasema heee, kumbe wadhifa mkubwa huu!”

Babu Duni alionesha unyeyekevu mkubwa sijapata kuona kwa kweli. Japo kwa muda mfupi, lakini alinisaidia sana katika mpito ule wa kuhakikisha kuwa wanachama wapya waliotoka CUF na wanachama waliokuwepo ACT Wazalendo wanawivana na kujenga chama kimoja chenye utamaduni unaoshabihiana kisiasa.

Tulipofanya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi mwezi Machi, 2020, na kuchagua viongozi wa chama kudumu miaka mitano, Juma Duni Haji alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama upande wa Zanzibar, Mwenyekiti akiwa Maalim Seif Sharif Hamad. Babu Duni alitusaidia kutuvusha katika mpito muhimu sana katika ukuaji wa chama chetu.

Mrithi wa Maalim

Mapema mwaka 2021 tulipata mtihani mkubwa, Mola alipitisha uwezo wake na kumchukua kiumbe wake, Maalim Seif, Allah amhifadhi katika pepo ya daraja la juu kabisa. Kabla ya hapo, tulikuwa tumetoka kwenye uchaguzi mgumu sana uliopelekea maafa ya majeruhi. Wanachama wetu 21 waliuwawa na vyombo vya dola Zanzibar na mamia kuumizwa na wengine kupata ulemavu wa kudumu.

Baadhi ya waliopatwa na madhila haya ni viongozi wetu wa kitaifa, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Chama chetu wakati huo Nassor Ahmed Mazrui na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama, Ismail Jussa Ladhu.

SOMA ZAIDI: ACT-Wazalendo: Mikopo ya Asilimia Kumi ya Halmashauri Itolewe Kupitia Skimu ya Hifadhi ya Jamii

Tukiwa tunahangaika na ama kuwatafuta au kuwatibu viongozi na wanachama wetu kufuatia kutekwa na vipigo vya polisi, tulipaswa kufanya maamuzi ya kushiriki katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. 

Babu Duni, akiwa Makamu Mwenyekiti wa Chama, ilimlazimu kushauriana na mimi na Maalim Seif kila wakati ili kukabiliana na changamoto hizi lukuki. Niliona kwa ukaribu unyenyekevu na utulivu mkubwa kiuongozi kutoka kwake katika kipindi hiki. Ghafla, Mwenyekiti akatangulia mbele ya haki!

Nadhani huu ndiyo ulikuwa wakati mgumu zaidi kwangu kiuongozi. Maalim Seif alikuwa na nafasi mbili muhimu ambazo zinapaswa kujazwa kwa mujibu wa Katiba ya Chama na Katiba ya Zanzibar. 

Hili la Katiba ya Zanzibar lilikuwa la haraka kwani Katiba ilitupa siku 14 tu kujaza nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Lile la Katiba ya chama tulikuwa na muda wa kutosha wa mwaka mzima na Katiba ilishaweka utaratibu wa kukaimu, kwamba Makamu Mwenyekiti wa chama kutoka upande ambao hatoki mwenyekiti hukaimu nafasi hiyo kwa muda usiozidi miezi kumi na miwili.

Kupata Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ni mchakato unaoanzia na Kuishia, au kuamuliwa, na Kamati ya Uongozi ya Chama. Kabla ya marekebisho ya Katiba ya Chama mwaka 2024, Kamati hii ilikuwa na watu tisa tu. Mmoja, Maalim, akiwa ametangulia mbele ya haki na mmoja Mshauri Mkuu wa Chama ambaye hakuwapo. Hivyo tulibaki watu saba tu.

Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi nilibeba jukumu la kufanya mashauriano na kila mjumbe kabla ya siku ya kikao ili kupata mwafaka wa pamoja. Ndani ya kikao, Wazanzibari watatu kati ya wajumbe wote saba walikuwa na sifa zote za kuteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, wakiongozwa na Juma Duni Haji ambaye wakati huo alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Zanzibar na kwa hakika Mwanasiasa Mwandamizi zaidi katika siasa za Zanzibar.

Nilikwenda nyumbani kwa Babu Duni katika mzunguko niliofanya wa mashauriano. Aliniandalia chakula cha mchana kizuri na tukafanya mazungumzo marefu. Mazungumzo yalihusu kujaza nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. 

SOMA ZAIDI: Zitto Kabwe: Kwa Nini ACT-Wazalendo Tumeamua Kuwa na Ofisi?

Alinieleza alivyotayari kama chama kikimpendekeza, lakini pia alivyotayari kumuunga mkono mwanachama mwingine ambaye chama kitampendekeza ikitokea sio yeye. Kwa maneno yake niliyoyanukuu, alisema: “Babu Zitto, sisi vijana wa Maalim Seif tunaamini katika cause, siyo nafasi za vyeo.” Nilimweleza pia fikra za Maalim kuhusu umuhimu wa kuleta kizazi kipya cha viongozi wa kisiasa.

Wakati wa mjadala wa Chama kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Maalim alikuwa ameomba kuwa Chama kisimpendekeze kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais bali tupendekeze jina la mwanachama mwingine kutoka kizazi kingine cha viongozi. 

Mazingira yalikuwa magumu sana baada ya uchaguzi ule wa mwaka 2020, hali iliyopelekea wanachama wengi kutaka yeye Maalim ndiye awe Makamu wa Rais. Hatimaye, Maalim akatoa sharti kuwa basi yeye ahudumu nafasi hiyo kwa miaka miwili na nusu kisha tupate mwanachama mwingine ambaye angemaliza na kutuingiza kwenye uchaguzi mkuu wa 2025. Tukakubaliana naye hilo.

Maalim alikuwa na watu wawili aliowafikiria wakati huo ukifika. Nilimweleza Babu Duni hayo pia kwa ajili ya tafakari zake pia. Nilifanya mazungumzo kama hayo na Nassor Mazrui, Omar Said Shaaban, Ismail Jussa Ladhu, ambaye alikuwa mgonjwa wakati huo na hakuwa katika Kamati ya Uongozi, Said Ali Mbaruk na Pavu Juma Abdallah. 

Vilevile, hao watu wawili ambao Maalim Seif alikuwa amewahi kuwataja kwa ajili ya kuwafikiria kuchukua kijiti cha uongozi kutoka kizazi chao niliwatafuta kwa mashauriano. Mmoja akaniambia yeye hapana, nimfuate mwenzake. Mwenzake huyo naye hakuwa tayari, alikuwa akisita sita. Wote, kwa wakati huo, walikuwa wanachama wa kawaida wa chama.

Siku ya Kikao cha Kamati ya Uongozi hatimaye azimio likawa huyo anayesitasita atafutwe na aombwe kukubali kushika nafasi ile iliyoachwa na Maalim Seif. Sijapata kuona kiwango cha hali ya juu kabisa cha unyenyekevu kama alichoonyesha Babu Duni, kwani yeye, pamoja na kwamba alikuwa na sifa zote za kuchukua nafasi ile ndiye aliongoza timu ndogo ya kumtafuta Othman Masoud Othman ili kumwomba akubali kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Babu Duni aliridhia yeye kuendelea kuongoza Chama kwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa baada ya Uchaguzi Mkuu wa ndani ya chama, lakini kuachia nafasi ya kidola kushikwa na Mwanachama mwingine wa Chama chetu. Unyenyekevu wa Juma Duni Haji uliweka maslahi ya Zanzibar mbele ya maslahi yake binafsi.

Mifano ya Babu Duni

Katika siasa za Uingereza, Juma Duni Haji unaweza kumlinganisha kwa mbali na Rab Butler. Huyu alikuwa mwanasiasa wa Chama cha Conservatives ambaye zaidi ya mara tatu akidhaniwa kuwa atabeba mikoba ya Uwaziri Mkuu wa Uingereza kutoka kwa waliokuwa wakishika nafasi hizo – Winston Churchil, Anthony Eden, Harold Macmillan na Alec Douglas-Home. 

SOMA ZAIDI: ACT-Wazalendo: Uhifadhi Ngorongoro ni Pamoja na Kulinda Maslahi ya Wanajamii wa Ngorongoro

Butler alishika nafasi mbalimbali za uongozi katika chama chake na Serikali ya Uingereza, ikiwemo kuwa Waziri wa Fedha wa Churchil na Waziri wa Mambo ya Ndani chini ya Macmillan. Mara mbili alikaimu nafasi ya Uwaziri Mkuu wakati Eden na Macmillan wakiwa wagonjwa mtawalia. 

Muda wote chama kilipoteua Kiongozi mwingine alitii na kutoa ushirikiano wa dhati mpaka alipostaafu siasa baada ya uchaguzi wa mwaka 1964. Juma Duni, kama alivyokuwa Rab Butler, si mwanasiasa wa ‘leo yupo, kesho hayupo.’ Ni mwanasiasa aliyedumu na kuhudumu kwa unyenyekevu mkubwa katika nafasi zake alizokabidhiwa. Ni muumini wa shabaha inayolengwa bila kujali nani anaongoza ulengaji katika taasisi.

Katika siasa za Kusini mwa Afrika, Juma Duni Haji unaweza kumlinganisha na Walter Sisulu. Mzee Sisulu alifanya kazi kwa karibu na kuhudumu pamoja jela na Nelson Mandela. 

Alipata kuwa Katibu Mkuu wa ANC kabla ya kukamatwa na kuwekwa jela ya Roben Island kwa miaka 25 na hatimaye alikuwa Naibu Rais wa ANC wakati Mandela akiwa Rais wa Chama hicho baada ya kuchukua nafasi kutoka kwa Mzee Oliver Tambo. 

Walter Sisulu alijiona na alionwa na wenzake kama Kiongozi wa nyakati za ukombozi na Mandela akiwakilisha kizazi chao na kwamba wajibu wao ulikuwa ni kuhamisha uongozi kwa kizazi kipya cha wanasiasa wa ANC kuendesha Taifa lao. 

Hakushika nafasi yeyote ya juu ya kidola katika Afrika ya Kusini huru, badala yake, aliwaunga mkono viongozi wapya, vijana wao kama Thabo Mbeki. Walter Sisulu, kama ilivyo kwa Juma Duni Haji, alikuwa na unyenyekevu wa hali ya juu kwa Taasisi yao na viongozi waliopewa jukumu la kuongoza.

Inawezekana mifano niliyotoa hapo juu isiwe sawa kwa asilimia mia moja, lakini dhamira yangu ni kuonesha kuwa duniani kuna mifano ya aina ya watu kama Juma Duni, ambao si wengi kwa hakika, haswa kwenye tasnia ya siasa. 

SOMA ZAIDI: Ni Zipi Fursa, Changamoto za Ukuaji wa ACT-Wazalendo Kama Chama cha Upinzani? 

Mwenyewe Babu Duni hupenda kutoa mifano ya Mzee Mandela anapotuhadithia mapito yake, haswa kuhusu kukaa kwake jela kwa miaka mitatu bila kosa lolote. Lakini walikaa Jela wengi, si wote ni kama Mandela au Sisulu au hata Juma Duni.

Unyenyekevu

Hakika Babu Duni ni tafsiri ya unyenyekevu. Alituongoza kama Mwenyekiti wa Chama Taifa kumaliza muda ulioachwa na Maalim Seif kwa weledi mkubwa na kukabidhi uongozi kwa Mwenyekiti mpya katika namna ambayo taasisi yetu imekuwa mfano wa kuigwa wa sio tu vizazi kupishana, bali pia sasa namna gani tunaenzi viongozi wastaafu.

Jumatano ya Septemba 4, 2024, tunafurahi na kuenzi maisha ya kisiasa na uongozi ya Babu Duni. Sina hakika kama kuna chama kingine cha siasa hapa Afrika Mashariki kina sera maalumu ya kuwaenzi viongozi wake wanaostaafu nyadhifa zao. 

Shughuli ya Jumatano imenipa matumaini kwamba japo ni kweli kwamba tunasahau michango ya kila mmoja katika harakati za mageuzi ya kidemokrasia hapa Tanzania, angalau ACT Wazalendo imeweza kumuenzi na kumthamini Juma Duni Haji akiwa yu hai. 

Labda wanasiasa wanaochipukia sasa, baada ya kuona heshima hii ambayo Juma Duni Haji anapewa na wanachama wa chama chake, wanaweza kuona mwanga mpya kuwa kila mchango unaenziwa. Namwomba sana Mola kuwa ACT Wazalendo ifanye utamaduni huu kuwa wa kudumu katika chama.

Kama inawezekana, Chama kifanye maamuzi mahususi kabisa kuwaenzi na wengine waliotangulia mbele ya haki kwa umoja wao kwa kufanya shughuli kubwa itakayoambatana na dua na sala kwa wana mageuzi wote kwa michango yao kwa demokrasia ya Tanzania. 

Juma Duni Haji amepata bahati ambayo wenzake hawakuipata, basi iwe ni fikirisho kwa siku za usoni!
Zitto Kabwe ni Kiongozi wa Chama mstaafu wa chama cha upinzani, ACT Wazalendo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia zruyagwa@icloud.com au X kama @zittokabwe. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *