Ni Zipi Fursa, Changamoto za Ukuaji wa ACT-Wazalendo Kama Chama cha Upinzani? 

ACT-Wazalendo kuwemo ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar ni moja ya fursa muhimu inayoweza kusaidia ukuaji wa chama hicho. Moja ya changamoto ni je, chama hicho kitafanikiwa kutafsiri mafanikio yaliyopatikana huko Zanzibar na kuyahamishia Tanzania Bara?
Evarist Chahali2 February 20225 min

Hatimaye mnamo Januari 29, 2022, chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo kilifanya mkutano wake mkuu jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kupata Mwenyekiti mpya Juma Duni Haji, anayejaza nafasi iliyokuwa wazi baada ya kufariki kwa Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki Februari 17, 2021.

Katika maandalizi ya mkutano huo mkuu ambao pia ulihudhuriwa na wawakilishi wa baadhi ya vyama vya upinzani vya nchi jirani, kama vile Nelson Chamisa kutoka nchini Zimbabwe, chama cha ACT-Wazalendo kilifanya moja ya kampeni ya kihistoria za kukusanya michango.

Binafsi, nilikuwa miongoni mwa watu walioguswa na kampeni hiyo kiasi kwamba kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, nilitoa mchango kwa chama hicho. 

Kabla ya kuruhusiwa tena kwa mfumo wa vyama vingi nchini ilikuwa ni lazima kukichangia chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia masharti mbalimbali, kama vile kulipia kadi ya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM).

Licha ya kutoa mchango huo, niliwaunga mkono ACT-Wazalendo kwa kuwahamasisha niliowaita “wadau wa demokrasia” kuunga mkono kampeni hiyo. Ni hivi, huku nchi za Magharibi, suala la michango kwa taasisi za demokrasia, hususan vyama vya siasa, ni la kawaida. 

Moja ya vyanzo muhimu vya taasisi hizo ni pamoja na michango ya “raia wema” wanaoelewa bayana kuwa uimara wa taasisi hizo ni muhimu kwa ustawi wa taifa husika.

Utamaduni wa kuchangia vyama Tanzania

Kwa bahati mbaya – au pengine kwa makusudi – vyama vyetu vya siasa nchini Tanzania havijajenga mazingira rafiki kwa watu wasio wanachama wa vyama hivyo kutoa michango yao ya hali au/na mali.

Japo kwa muda mrefu CCM imekuwa ikipokea michango kutoka kwa watu na taasisi mbalimbali, michango hiyo imekuwa zaidi katika mazingira ya “nipe nikupe,” ambapo kwa upande mmoja watoa michango hutegemea fadhila kutoka kwa chama hicho tawala au Serikali zake, ilhali CCM nayo ikitarajia “ushirikiano” wa hiari na hata wa vitisho.

Lakini michango ya wafanyabiashara mbalimbali kwa chama hicho tawala imekuwa ikitajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia chama hicho “kuwatelekeza wakulima na wafanyakazi” na badala yake kuwakumbatia wafanyabiashara wakubwa.

Kadhalika, michango kwa CCM imekuwa moja ya njia maarufu kwa wafanyabiashara kujipenyeza kabla ya kuomba ridhaa ya uongozi.

Kwa vyama vya upinzani, michango imekuwa ni suala la vyama binafsi na wanachama wake. Hata hivyo, “mapinduzi” yaliyofanywa na ACT-Wazalendo kuelekea uchaguzi wao mkuu, na ufanisi wake, unaandika historia mpya kwa Tanzania yetu.

Nilipohamasisha wadau wa demokrasia kuwaunga mkono ACT-Wazalendo katika kampeni yao ya mchango kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wao mkuu, nilikumbusha kwamba mara nyingi wananchi wamekuwa wepesi kuvilaumu vyama vya siasa, hususan vya upinzani, kwa “maamuzi mabovu” lakini michango ya wananchi hao kwa vyama hivyo ni finyu.

Nikatoa rai kuwa hii ni fursa ya kuanza zama mpya za kuzisaidia taasisi za kidemokrasia, hususan vyama vya siasa vya upinzani, ambavyo tegemeo kubwa la vyanzo vya mapato ni ruzuku na ada za uanachama ambazo hata hivyo hazikidhi mahitaji.

Mbali ya ufanisi wao katika kuhamasisha michango kwa ajili ya mkutano huo, yayumkinika kuhitimisha kuwa ACT-Wazalendo hawana sababu ya kuwazuwia wao “kuchukua nafasi ya CHADEMA” kama chama cha pili kwa ukubwa nyuma ya CCM.

Mitaji ya kuipaisha ACT-Wazalendo

Chama hicho kina mitaji kadhaa muhimu kisiasa ambayo ikitumika vizuri inaweza kukipaisha. Mtaji muhimu zaidi ni uzoefu wake kama chama cha upinzani kinachounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar.

Kwa kuzingatia yaliyojiri kwenye uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 2020, ambapo wana ACT-Wazalendo kadhaa walipoteza maisha na wengi zaidi kujeruhiwa kutokana na vitendo vya ukiukwaji haki za binadamu vilivyofanywa na vyombo vya dola “kuibeba” CCM, ilikuwa vigumu sana kwa vyama hivyo kuweka kando tofauti zao za kiitikadi na kukaa pamoja kwa ajili ya maslahi mapana ya Wazanzibari.

Lakini hicho ndicho kilichotokea. Licha ya kuwa wahanga wa uchaguzi mkuu huo, hatimaye ACT-Wazalendo waliafikiana na CCM kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Uamuzi huo ulipelekea chama hicho kuandamwa vikali, hususan kwenye mitandao ya kijamii, kikituhumiwa kwa “usaliti.”

Kadhalika, ACT-Wazalendo imeshiriki chaguzi ndogo kadhaa, ambazo wenzao wa CHADEMA walisusia. Na hili la ushiriki kwenye chaguzi ni moja ya vitu vinavyovitofautisha vyama hivyo vya upinzani.

Msimamo wa CHADEMA umekuwa ni “kususia kila kitu” hadi Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi vitakapopatikana, ilhali ACT-Wazalendo wamekuwa wakishiriki.

Japo maamuzi ya CHADEMA yanapaswa kuheshimiwa lakini kwa upande mwingine kuna haja ya kuangalia ufanisi wa mbinu hiyo ya kususa.

Mantiki ya kususa kwao ina mashiko; kushiriki chaguzi haramu ni sawa na kuhalalisha kufuru, lakini kususa tu pasi kuchukua hatua makusudi za kurekebisha sababu zilizopelekea kususa, hakuwezi kubadili chochote.

Mtaji mwingine muhimu wa ACT-Wazalendo ni kufanya siasa zao kistaarabu.  Ukiangalia maongezi ya viongozi na wanachama wa chama hicho kwenye mitandao ya kijamii, hutoshindwa kubaini ustaarabu wao.

Baadhi ya makada wa CHADEMA wamekuwa wakitumia lugha zisizo za kistaarabu dhidi ya ACT-Wazalendo na viongozi wake, lakini “wana zambarau” hao wamekuwa wakijibu hoja kistaarabu.

Kwa nini hili la ustaarabu ni muhimu? Kwa sababu kwa kiasi kikubwa Watanzania ni wastaarabu wasiopendezwa na lugha za matusi na kejeli. Kwa bahati mbaya, baadhi ya wana-CHADEMA ni kama wameiga mfano kutoka kwa baadhi ya wana-CCM, ambapo njia pekee ya maongezi nao ni kuafikiana na wanachoamini wao, kinyume chake ni matusi na kejeli.

ACT-Wazalendo wana fursa muhimu ya kuwavuta wana-CHADEMA wasiopendezwa na “utamaduni wa matusi” sambamba na wana-CCM wasiopendezwa na mwenendo wa chama hicho tawala.

Lakini kama kuna kundi muhimu zaidi ambalo ACT-Wazalendo inaweza kuvuna wafuasi, ni “sie tusio wanachama wa chama chochote cha siasa.” Hili ndio kundi kubwa zaidi katika siasa za Tanzania.

ACT-Wazalendo inakabiliwa na changamoto pia

Miongoni mwa changamoto kubwa kwa chama hicho ni tatu. Kwanza, ni kufanikiwa kutafsiri mafanikio yaliyopatikana huko Zanzibar na kuyahamishia Tanzania Bara. Hili linahitaji juhudi za makusudi.

Pili, ni chama hicho kuondokana na “mentality” kuwa “wao ni chama kidogo.” Yayumkinika kuiona ACT-Wazalendo kama “imeridhika kubaki nyuma ya CCM na CHADEMA.”

Tatu, ni kwenye mitandao ya kijamii ambako sasa ni moja ya maeneo yanayoweza kukisaidia chama cha siasa kuvuna wafuasi. Mara kadhaa ACT- Wazalendo “wamekuwa wakiongea wenyewe kwa wenyewe,” kiasi kwamba si ajabu hata “tweets rafiki” (zinazoongelea chama hicho vizuri) zisionekane kwao.

Nihitimishe kwa kutanabaisha kuwa ACT-Wazalendo haina sababu ya kutokuwa “kubwa zaidi ya CHADEMA,” kwa vile uwezo wanao lakini pengine kinachokosekana ni udhati kwenye nia ya kuona hilo likitimia.

Evarist Chahali ni mchambuzi wa siasa anayeishi nchini Scotland. Unaweza kumpata kupitia evarist@chahali.com au kupitia Twitter kama @chahali. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com. 

Evarist Chahali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved