Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Emmanuel Nchimbi, amewataka Watanzania kuepuka kufarakanishwa na Polisi hii ni baada ya kuwepo na malalamiko yanayohusisha Jeshi hilo juu ya watu kutekwa na kupotea.
Nchimbi ameyasema haya leo Septemba 13,2023, katika ofisi za CCM, Lumumba Dar es Salaam, wakati akitoa msimamo wa chama hicho juu mauaji ya kiongozi wa CHADEMA na matukio ya utekaji ambayo Nchimbi ameeleza yameikasirisha sana CCM.
“Kuna jitihada kubwa tu ambayo inafanywa ya kujaribu kufarakanisha Jeshi la Polisi na raia, hili mimi nataka niwaambie katika mambo mabaya unayoweza kufanya ni hili,” aligusia nchimbi.
Hata hivyo, wakati malalamiko ya wananchi yameendelea kushamiri juu ya utekaji, tafiti mbalimbali za Serikali zinaonesha kuwa Polisi ni taasisi yenye changamoto kubwa ya kuaminika na jamii.
Kwa mfano, Utafiti wa Uadilifu wa mwaka 2022, wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora unaonyesha Kitengo cha Jinai cha Polisi na Trafiki ni sehemu inayo onekana kuongoza kwa rushwa Tanzania.
Pia Utafiti wa Rushwa (2020) wa TAKUKURU uliohusisha watu 3,163 ulionesha kuwa Polisi ndio taasisi inayo ongoza kwa rushwa Tanzania ikifuatiwa na sekta ya afya. Wakati utafiti huo unaonesha Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania linaongoza kwa kuwa na maafisa waadilifu na waaminifu (60.9% ya watu walieleza), Polisi ilitajwa kama taasisi iliyo ongoza kwa kuwa na maofisa ambao wananchi wanaowaona sio waaminifu.
Nchimbi kwa upande wake anaamini wananchi wengi wana imani kubwa na Jeshi la Polisi na hivyo sio haki kwa maafisa wachache wasio waaminifu kulichafua jeshi hilo.
“Kwa wananchi wa kawaida,Polisi wanafanya kazi zao vizur. Sasa haiwezekani kukitokea Polisi wawili watatu wenye matatizo ninyi mnataka wananchi wawakasirikie polisi nchi nzima, hii haikubaliki hili ni jambo la hovyo kuliko yote ninayoyafahamu,” alisisitiza Nchimbi.
Utekaji
Chama cha upinzani cha CHADEMA kimeendelea kuwahusisha Polisi na utekaji wa wanachama wake akiwemoDeusdedith Soka and Jacob Godwin Mlay, waliotekwa mnamo Agosti 18,2024. Soka na Mlay walitekwa pamoja na Frank Mbise, ambaye alikuwa dereva bodaboda wa Soka.
CHADEMA wanaeleza kuwa Soka aliitwa Polisi Chang’ombe kwenda kuchukua pikipiki yake iliyoibiwa, baada ya kujulishwa na watu ambao CHADEMA inaeleza ni maafisa wa polisi na alifuatana na Mlay na Mbise ambapo waliishia kuchukuliwa na gari aina ya Noah na hawajapatikana mpaka leo hii.
Sio CHADEMA pekee wanaowahusisha Polisi na utekaji. Edgar Edson Mwakabela aliyetekwa mnamo Juni 23,2024 na kupatikana Juni 27, 2023 akinusurika kuuwawa anaeleza kuwa alipelekwa kwenye kituo cha Polisi cha Oysterbay baada ya kutekwa. Mwakabela amesambaza taarifa za mmoja wa Maafisa waandamizi wa Polisi akieleza kuwa ni mmoja ya watu waliomhoji baada ya kutekwa na kunusurika kuuwawa.
SOMA: Utata Kupotea Kwa Kiongozi Mwingine wa CHADEMA. Polisi Rukwa Wasema Hakuna Utekaji
Watanzania wengine ambao Wapendwa wao wametekwa na wamenyoosha kidole kwa Polisi ni pamoja na marehemu William Sije Rubanda. Katika mahojiano yake na The Chanzo wiki tatu kabla ya kufariki alieleza kuwa mashahidi walishuhudia mtoto wake akichukuliwa na Polisi mnamo Agosti 17,2021. Toka wakati huo mtoto wake aitwaje James Sije hajaonekana tena.
“Mimi mpaka huyu mtoto anakufa sijawahi kupata amani kwa sababu wamefuata na mama yake,” Sije aliiambia The Chanzo akimueleza mtoto wake aliyepotea kuwa amekufa.
“Sijawahi kupata amani kabisa katika maisha yangu, na mpaka sasa hivi nikimuwaza huyu mtoto natokwa machozi tu, nashangaa sana imeshanichukua muda lakini nimeshindwa kusahau, ndiyo hatari kubwa ninayoiona,” alieleza zaidi kwenye mahojiano hayo yaliyofanyika Julai 25,2024, wiki tatu kabla Sije hajafariki mnamo Agosti 17,2024, ikiwa ni tarehe ambayo mtoto wake huyo alipotea.
Malalamiko kama hayo pia yalielezwa pia na Johari Rajab Songoro ambaye mume wake Isaya Lilenga alipotea mnamo Mei 11,2024, akiacha familia yake yenye majonzi. Johari ana amini mumewe amekamatwa na Polisi kwani alishawahi kupotea kwa mwezi mmoja mnamo April 29,2022, lakini baadae ilikuja kugundulika alikua Polisi.
Polisi wameendelea kusisitiza hawahusiki na matukio ya utekaji huku IGP Camillus Wambura akieleza tuhuma hizo ni kulikosea adabu Jeshi hilo linalotegemea kusherehekea kuadhimisha miaka 60 mnamo Septemba 17.
Katika mazungumzo yake na waandishi, Nchimbi anaeleza kuwa matukio ya utekaji ni moja ya changamoto kubwa inayoikabili Tanzania, n ani matukio ambayo yanaihitaji jamii kuwa wamoja.
“Kama kuna jambo halitasaidia taifa letu ni watu kujielekeza katika kufarakanisha polisi na umma, mwisho wa saa maumivu ni ya umma sio ya Polisi au IGP, inakuwa unaliumiza taifa bila sababu yeyote ya msingi,” alifafanua Nchimbi.
“Kwa hiyo nadhani tunao wajibu mkubwa sana wa kuhakikisha kwamba tunaacha kunyoosheana vidole tunahakikisha kwamba uchunguzi wa kweli na wa kina unafanyika,” aliongeza Nchimbi.
Matukio Mapya
Nchimbi aliweza pia kulielezea tukio lililotokea la mnamo Septemba 11,2024, huko Geita ambapo wananchi walivamia kituo cha Polisi baada ya kuwahisi watu wawili kuwa ni watekaji wa watoto. Baada ya Polisi kuzuia watu hao wasiwadhuru watu waliohisiwa kuwa watekaji wa watoto, wananchi walivamia kitua cha Polisi na kuharibu mali. Katika tukio hilo watu wawili waliuwawa, huku mmoja akiwa mwanafunzi ambaye risasi ya Polisi ilimpata akiwa nyumbani kwao.
Tukio hili limefuatana na lile la Lamadi Simiyu lililotokea Agosti 21, ambapo waandamanaji waliokuwa wakitaka Polisi kuwajibika zaidi juu ya mtukio ya watu kutekwa na kuuwawa kuvamia kituo cha Polisi na kujaribu kukichoma. Tukio hili lilisababisha kukamatwa kwa watu 108 na mwanafunzi mmoja aliuwawa baada ya polisi kutumia silaha za moto.
Kwa upande wao chama cha CHADEMA kimeeleza kuwa Polisi hawana uweledi wa kujichunguza hivyo wamependekeza taasisi ya uchunguzi ya nje ije ifanye uchunguzi wa matukio yote ya mauaji na utekaji wa watu.