Tarehe 3 Februari 1960, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Harold Macmillan alilihutubia bunge la Afrika Kusini enzi za utawala wa kibaguzi wa wazungu wachache, hotuba iliyopewa jina “Wimbi la Mabadiliko.” Katika hotuba hiyo, Bwana Macmillan alisema kwamba wimbi la mabadiliko haliepukiki barani Afrika. Bila ya shaka alikuwa akiwaonya makaburu na kuitanabahisha Serikali yake ya chama cha kihafichina cha Conservative nyumbani kwao Uingereza, kwamba hatua ya kuanza kuyapa uhuru makoloni yake barani Arika haiepukiki. Mjini Cape Town, Macmillan alikuwa akirudia aliyoyatamka kabla mjini Accra, Ghana, koloni la zamani la Uingereza, na nchi ya kwanza Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kuwa huru, Machi 1957.
Hivi sasa ni zaidi ya karne moja tangu wimbi la mabadiliko kutoka ukoloni hadi kujitawala wenyewe lilivyoanza kupiga katika bara hilo. Pamoja na hayo miaka iliyofuata ilikuwa ya misukosuko kuanzia mapinduzi, tawala za chama kimoja na ukandamizaji wa haki za kiraia. Wapiga kura wamekuwa wakati wote katika hatua ya kutaka mabadiliko, iwe ni kupitia vyama vilivyoko madarakani au kutafuta mabadiliko hayo upande wa vyama vya upinzani, wanapoona waliowaamini kabla wameshindwa kuwapa matarajio yao.
Mchakato huo katika sehemu kubwa ya la Afrika umeandamwa na vizuizi vingi kutoka vyombo vya dola kwa amri ya watawala, hali inayoendelea na ambayo kwengineko inazidi kushamiri. Sababu kubwa ni watawala kutokuwa tayari kuheshimu matakwa na maamuzi ya umma, wananchi.
Miaka michache iliopita kulifanyika chaguzi katika nchi karibu 20 ikiwemo Nigeria taifa lenye idadi kubwa zaidi ya wakaazi katika Afrika. Kwa mara ya kwanza kukafanyika makabidhiano ya amani ya madaraka kutoka kwa kiongozi aliyekuwa madarakani kumuendea kiongozi mpya aliyeshinda uchaguzi, kutoka kwa Goodluck Jonathan kwenda kwa mpinzani wake Muhammadu Buhari. Buhari mwenye umri wa miaka 77 alimaliza muhula wake wa miaka minne na akachaguliwa kwa muhula wa pili Februari 16, 2020.
Nigeria taifa lenye hali ngumu ya kiuchumi ilikuwa la kwanza kutumbukia kwenye janga la mapinduzi ya kijeshi ulipouangusha utawala wa kiraia wa Waziri Mkuu Abubakar Tafawa Balewa 1966, miaka 6 baada ya uhuru. Katika tukio hilo Balewa aliuwawa kikatili, miaka michache tu baada ya uhuru. Hata tawala za kiraia zilizofuata hazikudumu muda mrefu. Wanajeshi wakakamata mpini. Mapinduzi yakafuata, Ghana, Mali na kwengineko.
Hivi sasa kumeibuka mtindo mpya. Watawala wanazibadili katiba ili waendelea kubakia madarakani na baadhi yao kwa njia za ulaghai na matumizi ya nguvu. Katika kundi hilo kuna waliokwenda kinyume na kauli zao wenyewe kwamba wameingia madarakani sio kubakia kama wale waliowatangulia bali wataondoka watakapomaliza mihula yao kikatiba. Kauli zao hawakuziheshimu na miongoni mwao ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda. Orodha ya viongozi wa sampuli hii, kwa bahati mbaya imeongezeka, wakiwemo Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Congo (Brazaville) na Azali Asumani wa Comoro. Alpha Konde wa Guinea na Alassane Ouattara pia wamejiunga na safu hiyo. Nchi zote mbili zinapanga kuwa na uchaguzi wa Rais Oktoba mwaka huu 2020. Wote wawili waliwapinga watangulizi wao walipojaribu kurefua kubakia madarakani.
Mnamo miaka ya 1990, aliyekuwa Rais wa Marekani Bill Clinton, akiyazungumzia mabadiliko yaliyokuwa yakijitokeza barani Afrika kisiasa na kiuchumi, aliwataja viongozi vijana wa wakati huo Rais Paul Kagame wa Rwanda, Isayas Afewerki wa Eritrea aliyefariki dunia 2012 na Waziri Mkuu wa Ethiopia marehemu Meles Zenawi kama matumaini ya mabadiliko barani Afrika.
Miongo zaidi ya miwili sasa Eritrea imekumbwa na giza. Rais wake amegeuka kuwa mtawala wa kimabavu kiasi cha nchi yake kufananishwa na Korea Kaskazini, ikipewa jina la dhihaka, “Korea Kaskazini ya Afrika.” Mabadiliko ya uongozi katika Ethiopia baada ya kujiuzulu Waziri mkuu Haile Mariam Deselegne na kushika hatamu Dr Abiy Ahmed, kuna matarajio makubwa miongoni mwa raia kwamba hatimaye taifa hilo la pembe ya Afrika linapiga hatua kuelekea demokrasia, itakayogeuka kuwa mfano kwa mataifa mengine ya kiafrika.
Licha ya kukabiliwa na changamoto kubwa ukiwemo upinzani hata kutoka kwa wanasiasa wenzake ndani ya chama tawala, Dk Abiy ameonesha ujasiri kwa kufanya mabadiliko makubwa ya kisiasa ikiwa ni pamoja na kuwaachia huru mamia ya wafungwa wa kisiasa na kuwaomba waliokimbilia uhamishoni kurudi nyumbani na pia kufanya mageuzi katika Tume ya Uchaguzi na kumteuwa mwanamke, mwanaharakati na mpinzani kuiongoza tume hiyo bila ya ushawishi wowote wa kisiasa.
Tume za uchaguzi katika nchi nyingi barani Afrika ni moja wapo ya vikwazo katika kujenga na kuimarisha demokrasia na zinachangia pia katika kuzuwia haki na kuzuka kwa migogoro baada ya uchaguzi. Tatizo kubwa sio tume kuteuliwa na viongozi wa kitaifa lakini uteuzi hufanyika kwa utashi wa kisiasa kuhakikisha mwenyekiti na wengi wa wajumbe wanabaki watiifu kwa mtawala na serikali yake na kuhakikisha utawala ulipo unabakia madarakani kwa gharama yoyote ile.
Kuna maoni yanayokinzana miongoni mwa wakaazi wa barani la Afrika kuhusiana na swali, jee! demokrasia imepiga hatua au imerudi nyuma kinyume na matarajio? Mtazamo wa wengi miongoni mwa wadadisi ni kwamba hoja zote mbili zina mashiko. Demokrasia imeendelea kushamiri katika mataifa yaliohesimu misingi ya demokrasia tangu uhuru na mfano unaozungumzwa sana ni wa nchi kama Mauritius, Botswana na Senegal. Miaka ya hivi karibuni Ghana imejiunga na orodha hiyo. Afrika Magharibi, eneo lililokuwa na doa linalohusiana na uongozi, sasa linaongoza kuwa alau ni mfano wa kuigwa.
Historia inatufunza kwamba mapambano ya kupigania haki kule kwenye ukandamizaji hayaepukiki na watawala wanaoongoza kwa mkono wa chuma hawawezi kudumu milele. Wapiga kura wengi leo hii ni vijana ambao wanadai mabadiliko kutoka kwa viongozi wanaowaona ni wakandamizaji na sio wakombozi na wenye dira ya kuwajengea mustakbali mwema. Turufu nzito ya kupata mafanikio ni kuendeleza kilio chakudai utekelezaji wa demokrasia ya kweli kutoka kwa wale wanaoipigia debe kwa maneno matupu na kuendeleza ukandamizaji dhidi ya wapinzani wao.
Kuna dhana potofu ya kufikiria kwamba demokrasia ni pamoja na kuwa na kikomo cha utawala au utitiri wa vyama vya siasa. Suala la kikomo halina uzito pale ambapo katiba inaheshimiwa na sio lazima katiba ziwe na kifungu hicho, isipokuwa vyovyote iwavyo yawe ni maamuzi ya umma wa nchi husika. Mataifa mengi duniani yakiwemo yale yalioitawala Afrika, kama vile Uingereza na Ufaransa, hayana ukomo wa madaraka ndani ya katiba zao. Nchini Ujerumani, Kansela Helmut Kohl alitawala miaka 16. La msingi ni uhuru wawapiga kura kujimulia na maamuzi yao kuheshimiwa.
Kichekesho ni kwamba hotuba ya Macmillan ya “Upepo wa Mabadiliko Barani Afrika,” ilikuwa ya kujitoa kimasomaso, kwani dola ya kikoloni ya Uingereza yenyewe iliitawala Afrika kwa zaidi ya karne na kuwanyima watawaliwa uhuru na demokrasia ambavyo walilazimika kuvidai kwa njia zote na bado wanaendelea kuvidai wakati huu katika mazingira tunayoyaita ya kujitawala wenyewe.
Maendeleo kwanza ni kumpa uhuru binadamu ukiwemo uhuru kutoa maoni na kujieleza ambayo ni haki yake ya kuzaliwa. Uhuru huo unakamilika tu pale demokrasia, utawala bora na haki za binaadamu kwa jumla zinapoheshimiwa. Vyenginevyo wakati kuna nchi zitakazopiga hatua, nyenginezo utakuwa ni muendelezo wa DOMOkrasia, zikiwa bado haziko tayari kwa DEMOkrasia. Watawala wanahisi hiyo kwao ni njia ya kubakia madarakani, kinyume na matakwa ya raia. Wanachosahau ni kwamba leo wapo na siku moja wataondoka, lakini taifa linabaki na taifa ni watu.
Mohamed Abdulrahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Alishawahi kuwa Naibu Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, DW, katika idhaa yake ya Kiswahili. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mamohamed55@hotmail.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.