Mchango wa mwanamke katika jamii ni mkubwa na adhimu na kwa kweli thamani yake haiwezi kufananishwa na kiwango chochote cha malipo.
Lakini kwa bahati mbaya bado unapozungumzia hali ya mwanawake katika jamii yoyote husika, sura unayoipata ni ile ya kudhani kwamba wanaume ndiyo wenye haki ya kutamalaki mustakbali wa mwanamke. Mfumo dume unaendelea kuwatenga wanawake na pale wanapopewa fursa fulani basi inakuwa ni kwa bahati tu au fursa yenye mipaka fulani. Tukio la aina hiyo linapojiri basi hupigiwa upatu kama kwamba ni zawadi iliyo tunu badala ya kuwa ni haki yake aliyepewa fursa hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, wanawake ni karibu asilimia 66 ya kile ilichokieleza kama muda wa kazi ulimwenguni, lakini ni asilimia 10 tu ya pato la dunia. Kwa tafsiri rahisi ni kuwa wakati wanawake ndiyo wachangiaji wakubwa wa maisha na maendeleo ya binadamu – kwenye kilimo au maeneo mengine – manufaa wanayopata ni duni. Kwa maneno mengine, mchango wao ni mkubwa lakini tija ni haba.
Ukombozi wa mwanamke maana yake ni kumpa nafasi ya kujihisi kwamba ana thamani, uwezo, haki ya kuchaguliwa pamoja na haki ya kuwa na nafasi sawa na mwanamme katika kila sekta ya jamii; ikiwemo siasa, uongozi na usimamizi wa rasilimali pia.
Lakini ni kwa namna gani mwanamke anaweza kukomboka na kuwa na nafasi ya kupata mahitaji yake yote muhimu, ikiwemo elimu na ajira? Tunaposema kila mmoja wetu ana mchango wa kutoa katika jamii, tukumbuke kwamba bila ya mwanamke, haiwezekani, kwasababu bila ya yeye jamii haijatimia.
Kwanza kabisa la msingi ni kuuvunja mfumo dume uliopo na ambao katika baadhi ya jamii umeota mizizi na ukosefu wa usawa, ili kuhakikisha ubaguzi wa jinsia unakoma. Siku moja nilikuwa nikinywa kahawa katikati ya jiji la Cologne, Ujerumani ninakoishi. Nilikuwa na rafiki yangu mmoja Mwaafrika mwenzangu kutoka Ghana, taifa la Afrika magharibi, taifa la kwanza kujinyakulia uhuru barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Nakumbuka ilikuwa tarehe 8 Machi siku ya Kimataifa ya Mwanamke. Mazungumzo yetu yalijikita katika siku hiyo kwa kumkumbuka mwanamke kwa mtazamo wa kuwa ni mama, pamoja na mchango wake katika jamii na mwenendo wa maisha duniani kwa jumla. Mara tulijikuta tukitafautiana kimtazamo. Msimamo wake ulipingana sana na wangu katika kile kinachoitwa “jitihada za mwanamke kujikomboa.”
Hoja zake zilituwama zaidi kwenye yale aliyoyaona kuwa ni utata wa mwanamke na sio jukumu lake zito na mchango wake wa kutukuka, kuanzia uzazi hadi malezi ya familia. Ilikuwa kama vile kwake yeye, sisi wanaume tumekamilika, hatuna tatizo.
Wakati tukizungumza nikatoa hoja zangu kwanini mwanamke anahitaji kujikomboa na ni wajibu wetu kama wanaume kumuunga mkono katika hilo. Baada ya muda, nilihisi kama anazikubali lakini hakuwa tayari kukiri moja kwa moja. Nilihisi pia akizingatia mifano ya upande mmoja. Pengine kuna yaliomsibu yeye binafsi yaliofanya kuyageuza kuwa ya jumla jamala.
Mwisho alicheka na kuniuliza, “Sasa kwanini tusiwe na siku ya kimataifa ya kina baba?” Swali lake lilinifanya na mimi nicheke kidogo. Jibu langu lilikuwa, siku hiyo ipo Novemba 19 lakini haina shauku kubwa wala kutiliwa maanani. Sababu kubwa ni kwamba sisi wanaume ndiyo tuliyouunda huu mfumo dume na kudhibiti mwenendo wa maisha kwa muda mrefu. Kadhalika ndio chanzo cha janga analokabiliana nalo mwanamke kama mama. Hali hii lazima tuirekebishe kumpa nafasi ya kujihisi kweli yeye ni sehemu ya jamii na mchango wake ni nguzo muhimu katika kuiendeleza na kuilinda jamii.
Kusisitiza hoja yangu kwa mzaha nikamwambia, “Angalia hata wewe unapobanwa na maumivu, kinachotoka kinywani mwako ni maneno mawili, ‘Mungu wangu weee’ au ‘Ooh Mama yangu.” Alicheka sana na kunambia “my brother you are absolutely right” (ndugu yangu uko sahihi kabisa). Nyanja moja wapo ambapo mwanamke amedhulumika na kuachwa nyuma ni katika elimu. Lakini hayo yameanza kubadilika kwa kasi kubwa tangu kipindi cha miongo miwili na nusu. Maamuzi ya mkutano wa wanawake wa Umoja wa Mataifa mjini Beijing 1995 ulioongozwa na Bibi Getrude Mongella kutoka Tanzania kama Mwenyekiti, yaliwazindua akina mama na kuwapa changamoto wanaume. Miongoni mwa mafanikio ni kushiriki kwao zaidi katika masuala ya kisiasa mbali na kujiendeleza kitaaluma. Kama ilivyokuwa tayari barani Asia. India kwa Indira Ghandi, Sirimavo Bandaranaike nchini Sri Lanka (zamani Ceylon), Benazir Bhutto wa Pakistan, hawa wote walikuwa Mawaziri Wakuu au hata Bangladesh na Khaleda Zia hapo kabla na sasa Sheikh Hasina. Afrika nayo imepiga hatua. Kwa mfano katika siasa za dunia iliweza kutoa Naibu Katibu Mkuu wa kwanza wa Umoja wa Mataifa Bi Asha Rose-Migiro kutoka Tanzania. Afrika pia ilipata marais wa kwanza wanawake kama Allen Johnson Sirleaf wa nchini Liberia na Joyce Banda wa Malawi pamoja na Makamu wa Rais katika nchi za Burundi, Afrika Kusini, Tanzania, Zambia, Uganda, Zimbabwe na Gambia.
Ni mafanikio makubwa katika suala la usawa wa jinsia lakini bado katika nchi nyingi kumekuwa na hali ya kusota kwenye ngazi za diplomasia na uongozi wa taasisi za umma yakiwemo mashirika na makampuni. Maazimio yaliofikiwa Beijing ikiwemo kukabiliana na udhalilishaji wa kingono na matumizi mengine ya nguvu, haki ya mwanamke katika elimu, afya, vyombo vya habari na kinga kwenye maeneo ya vita, bado yanabakia kuwa msingi wa hatua za kivitendo na mafanikio yanayoendelea kupatikana.
Inafurahisha kwamba katika kinyang’anyiro kinachoendelea kujaza nafasi ya Katibu Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) wanawake wawili kutoka Barani Afrika wameingia duru ya pili ya wagombea wanne. Hao ni waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje wa Kenya Bi Amina Mohammed na Dk Ngozi Okonjo-Iweala, waziri wa zamani wa fedha wa Nigeria ambaye sasa ni mjumbe wa bodi za mashirika kadhaa ya kimataifa. Katika kinyang’anyiro hicho cha wagombea watano yumo pia mwanamke wa tatu ambaye ni waziri wa biashara wa Korea Kusini Yoo Myung-hee na wanaume wawili, Mohamed al-tuwaijri kutoka Saudi Arabia na waziri wa zamani wa Uingereza Liam Fox. Shirika la biashara duniani, halijawahi kuongozwa na Mwafrika achilia mbali mwanamke!
Lakini wakati mwanamke analalamika na kuendelea kupambana na kutamalaki kwa mfumo dume, naye hana budi kuachana na tabia ya kusema, “ Nina uhuru wangu.” Ana kila haki ya kuyasarifu maisha yake, lakini bila ya kukiuka taratibu za sheria na utaratibu wa kuhifadhi utamaduni wa jamii husika. Upande wa pili masuala ya utamaduni na jadi hizo pia yasitumiwe kuwa kikwazo na kisingizio cha kuzuwia maendeleo yake.
Suala liwe si kumkomboa na kumpa nguvu mwanamke au mwanamme bali kumpa nguvu binadamu bila ya kujali jinsia yake, ili kila mmoja katika jamii achangie kwa ujuzi na maarifa aliyonayo. Ni hapo utakapopatikana usawa wa kweli wa kijinsia.
Katika uzowefu wangu kwenye tasnia ya habari na utangazaji, nimeshuhudia ujasiri wa wanawake katika kujiamini zaidi, iwe katika mahojiano au mijadala. Huo ni mfano mmoja mdogo . Ninaamini wakati umefika kwa kina mama kuibadili kauli mbiu yao inayotumiwa sana ya “Tukiwezeshwa Tunaweza.” Badala yake sasa iwe “Tukijizatiti, Tukashikamana na Kujiamini, Tutaweza.”
Mohamed Abdulrahman ni mwandishi wa habari mstaafu na mtangazaji gwiji wa kimataifa. Alishawahi kuwa Naibu Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, DW, katika idhaa yake ya Kiswahili. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni mamohamed55@hotmail.com au kupitia akaunti yake ya Twitter ambayo ni @mamkufunzi. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.