The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Uhasama Kati Ya Mataifa Ya Afrika Mashariki Unaipeleka Wapi Jumuiya Hiyo?

Mahusiano ya mataifa ya Afrika Mashariki yako katika sura ya mchafukoge na kizungumkuti. Kila nchi imejiundia hasimu wake. Hakuna mgogoro unapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

subscribe to our newsletter!

Tawala zinazoshindwa kuwa na uhusiano mzuri na raia wao ni vigumu kuwa na uhusiano mwema na nchi zao za jirani. Ikiwa sadaka huanzia nyumbani, vile vile panapohusika uovu nao huanzia nyumbani kabla ya kuenea.

Afrika Mashariki ni jumuiya yenye nchi sita kwa sasa. Wanachama wakongwe wa Jumuiya wanajulikana kuwa ni Tanzania, Kenya na Uganda kisha wakafuatia wanachama wengine Burundi na Rwanda na hatimae mwanachama mpya zaidi ni Sudan Kusini iliyokuwa mwanachama kamili wa Jumuiya hiyo mnamo mwaka 2016.

Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya tawala za nchi hizo hazina uhusiano mzuri na raia wao, kwa kushindwa kusimamia utawala bora; mfano kushindwa kuheshimu katiba na kutunza uhuru wa kisiasa. Tawala hizo ndizo zinakuwa za mwanzo kuyakengeuka mambo ambayo ni muhimu kwa raia na mustakbali wa amani ya kweli.

Kuharibika uhusiano wa raia na tawala zao, kumetanuka hadi kufikia sura ya nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuonekana kila taifa limejenga uhasama na taifa jengine, mwanachama mwenzake wa Jumuiya. Ikumbuke kuwa tabia ya uovu nayo pia huwa na tabia ya kutanua mabawa.

Vuta n’kuvute ya Kenya na Tanzania

Uhusiano kati ya Tanzania na Kenya hutikisika mara kwa mara tangu Tanzania ilipovichoma moto vifaranga vya kuku kutoka Kenya. Kabla ya hapo palizuka msigano baada ya tukio la Tanzania kuwashikilia mifugo ya n’gombe kutoka Kenya. Na hivi karibu kumezuka sintofahamu nyengine iliosababishwa na janga la korona.

Huo ni msururu wa kuharibika kwa diplomasia ya mataifa hayo. Ukiangazia ndani ya Tanzania kwenyewe kuna fukuto la muda mrefu kati ya raia wenye mrengo wa vyama vya upinzani na utawala wa sasa chini ya Raisi anayewania mwongo mwengine wa miaka mitano Dk John Magufuli.

Rais Magufuli amekuwa akishutumiwa kwamba chini ya uongozi wake kumekuwa na uminywaji wa uhuru wa kisiasa na haki nyengine za kiraia kama vile uhuru wa kujieleza. Halikadhalika kumekuwa na malalamiko juu ya uhuru wa wanasiasa wa upinzani, vyombo vya habari na mashirika na kiraia, sanjari na kuasisiwa sheria na kanuni mpya zinazokosolewa vikali kwamba zinazohatarisha uhuru wa kujieleza. Serikali, kwa upande wake, siku zote imekuwa ikikanusha shutuma dhidi yake za kuminya uhuru wa raia wake.

Burundi haina maelewano mazuri na Rwanda. Tangu taifa hilo lilipoituhumu Rwanda kuwa nyuma ya mapinduzi yaliyoshindwa ya kumg’oa madarakani aliyekuwa Rais wake marehemu Pierre Nkurunziza, aliyefariki dunia kwa kuugua ghafla mnano Oktoba 6, 2020, mambo yakaanza kwenda kombo.

Ndani ya Burundi, taifa hilo halina rikodi nzuri katika jicho la kimataifa. Ripoti nyingi zimetoka zikiutuhumu utawala wa Nkurunziza kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu. Taifa hilo lilishuhudia vurugu kubwa mwaka 2015 baada Nkurunzinza kutangaza kugombea muhula wa tatu wa Urais.

Ndani ya Rwanda, taifa hasimu wa Burundi, chini ya rais wake Paul Kagame, limekuwa na rikodi mbaya katika siasa zake, hasa panapohusika uhusiano wa utawala huo na viongozi wa upinzani au wakosoaji wake.

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International linakadiria wanasiasa sita wameuwawa au kupotea nchini Rwanda kuanzia 2016 hadi katikati ya 2019. Aghlabu wanaokumbana na masaibu hayo ni wale wakosoaji ama wapinzani wa utawala wa Kagame.

Burundi na Rwanda mambo si sawa

Nchi ya Uganda chini ya Rais Yoweri Kaguta Museveni, haina uhusiano barabara na Rwanda. Zote zinatuhumiana kuunga mkono makundi ya waasi yanayotishia usalama wa mataifa hayo. Uhusiano ulichafuka kiasi cha raia wa mataifa tajwa kupata tabu pindi wanapofika mipakani kuvuka kwa ajili matembezi au biashara.

Kwa maneno mengine mahusiano ya mataifa ya Afrika Mashariki yako katika sura ya mchafukoge na kizungumkuti. Kila nchi imejiundia hasimu wake. Utakuta mingi ya migogoro yao haijapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Joto hupanda na kushuka kila uchao.

Na kwa sasa hakuna taifa lenye uthubutu wa kukemea taifa jengine ikiwa uvunjifu wa haki za kiraia utatendeka. Wala halijatokea taifa la kusimama na kuwa mpatanishi wa hii migogoro yote. Kila kitu kinaachwa kijiendee wenyewe.

Burundi itaanza vipi kuipatanisha Rwanda na Uganda wakati Burundi ni hasimu wa Rwanda? Uganda itawezaje kuileta Burundi na Rwanda katika meza ya mazungumzo wakati Rwanda na Uganda hazielewani? Kenya na Tanzania zina uthubutu gani kuwapatanisha majirani zao wakati wao wenyewe wanavutana mara kwa mara?

Hata ukiiangalia Sudan Kusini, mwanachama wa karibuni zaidi kujiunga na Jumuiya, iko katika amani ya mashaka. Kuna viongozi wanao gombania madaraka kule, lipo tatizo la ukabila. Hayo yote huifanya amani ya nchi hiyo kuwa mashakani.

Migogoro chimbuko la umasikini

Ripoti ya mwezi April, 2020 ya Benki ya Dunia, inaeleza watu wanne kati ya watano wanaishi katika umasikini uliopindukia nchini Sudan Kusini, huku watu milioni saba, takribani asilimia 60 ya wakaazi jumla wanakumbwa na uhaba wa chakula.

Migogoro ya kisiasa na kibiashara ndani ya Jumuiya inadhihirisha ugumu uliopo katika kuyafikia malengo ya kuundwa kwake. Ndani ya mataifa yenyewe mambo hayaendeshwi vizuri. Kuna serikali zisizoheshimu utawala bora,  wala kutenda haki na kusimamia sheria kwa usawa.

Itakumbukwa kuwa Jumuiya hii iliwahi kusimama kufanya kazi baada ya wanachama kuingia katika mgogoro wa kisiasa, kisha ikaja kufufuliwa tena 1999. Tangu wakati huo hadi sasa ipo hai lakini  migogoro hii ya mara kwa mara kati ya wanachama inazorotesha utendaji wake. La kuogopa zaidi inahatarisha hata uhai wake.

Upo umuhimu wa viongozi wa nchi za jumuiya hii kuheshimu utawala bora, zikiwemo haki za binaadamu na uhuru wa kisiasa. Taifa linaposimika utawala wenye uadilifu katika ardhi yake, hurahisisha kuwa na uhusiano nzuri na majirani zake.

Rashid Abdallah ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa siasa. Huandika makala za uchambuzi katika tovuti ya BBC Swahili na Aljazeera English. Unaweza kumpata kupitia akaunti yake ya Twitter @RashiidAbdallah. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo Initiative.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *