Wanawake Wanavyotumia Takataka Kujipatia Kipato

Wajasiriamali hao hutumia takataka kutengeneza mkaa mbadala ambao huwasaidia kwenye matumizi yao ya nyumbani na kuuza pia na hivyo kuongeza kipato chao.
Jenifer Gilla3 February 20215 min

Umoja ni nguvu si msemo tu kwa Agness Damian, mama wa miaka 50 anayejishughulisha na uuzaji wa mboga mboga. Kwake yeye, kama ilivyo kwa wanachama wenzake wa kikundi cha Fahari Yetu, kilichopo Tabata, Dar es Salaam, msemo huo ni ukweli unaoishi kama inavyodhihirika kwenye maisha yao ya kila siku. Kwa kushirikiana kwenye kutengeneza mkaa kutoka kwenye takataka na kufanya shughuli nyengine kwa pamoja zenye kuwaingizia kipato Agness na wenzake wamepata sababu nyengine ya kufurahia maisha.

Moja kati ya faida ya haraka inayotokana na watu kuja pamoja ili kupambana na changamoto za maisha zinazowakabili ni kwamba uwezo wa watu hao wa kuwa na matumaini hufufuka. Ni ukweli huu ndiyo uliompelekea mwandishi wa vitabu wa Kimarekani Tom Bodett kuja na nukuu yake maarufu kwamba: “Wanasema mtu anahitaji vitu vitatu tu ili aweze kuishi maisha ya furaha hapa duniani: mtu wa kumpenda, kitu cha kufanya, na kitu cha kutamania.” Kikundi cha Furaha Yetu kimewapa akina Agness kitu cha kufanya na kitu cha kutamania pia.

“Nashukuru sana kuwa mwanachama wa kikundi hiki na kupata fursa ya kujifunza kutengeneza mkaa,” Agness anaieleza The Chanzo ilipowatembelea ofisini kwao ili kufahamu zaidi harakati zao za kujikomboa na umasikini. Agness anaonekana ni mtu mwenye furaha sana na anajivunia kuwa sehemu ya kikundi hicho. Akieleza kwa nini yuko hivyo, Agness anasema: “Ni kwa sababu kwa kufanya kazi pamoja kipato changu kimeongezeka kwa kuwa nautengeneza [huo mkaa] halafu nauza, kwa wiki naweza kupata kati ya Sh15,000 na Sh20,000. Inanisaidia na watoto.”

Lakini si kipato tu kinachowafanya Agness na wenzake kuwa na furaha na matumaini ya maisha yao kubadilika. Maimuna Hassan, 73, anasema mkaa anaotengeneza pia unatumika katika shughuli za kupikia nyumbani na hivyo kumpunguzia gharama za maisha. Anaeleza: “Zamani nilikuwa natumia mkaa wa Sh4,000 kwa siku kutokana na ukubwa wa familia yangu na ule mkaa wa kuni hutumika mwingi. Lakini huu mkaa wa taka natumia wa Sh1000 tu siku nzima kwa kuwa ni mzito.”

Mkaa mbadala

Mkaa wanaozungumzia Agness na Maimuna unaitwa Mkaa wa Kisasa au Mkaa Mbadala. Ni mkaa ambao hutengenezwa kwa kutumia takataka kupitia teknolojia maalumu. Mbali na kuwa nafuu katika ununuaji mkaa huo pia unapigiwa chapuo sana na wanaharakati wa mazingira kutokana na uimara wake wa kuweka mazingira safi kwani malighafi yake kuu ni uchafu. Fahari Yetu si kikundi pekee kinachozalisha na kuuza mkaa wa aina hiyo. Wajasiriamali wengi nchini Tanzania pia wanafanya biashara hiyo na wengi wameweza kufanikisha ndoto zao nyingi kupitia bidhaa hiyo.

Maimuna, anayefanya biashara ya kuuza samaki wa kukaanga, anasema kwamba ana mpango wa kuanza kutumia mkaa huo unaotokana na takataka katika biashara yake hiyo kwani kwa sasa anatumia kuni anazosema  si nzuri kwa afya yake kutokana na moshi wake kumuathiri macho na kifua.

Fahari Yetu ni moja tu kati ya vikundi vingi sana vinavyoendelea kuundwa nchini Tanzania ambavyo vinalenga kuwaleta pamoja wananchi wanaopambana na changamoto zinazofanana ili kuweza kukabiliana nazo kwa umoja wao. Kwa kitaalamu vinaitwa VICOBA, au Village Community Banks kwa kimombo. Mfumo wa VICOBA unaweka mkazo katika umiliki wa jamii ambapo wanakikundi wanakuwa ndio wamiliki wa mali yote ya kikundi. Hii ni tofauti na mifumo mingine ya ukopeshaji fedha, kwa mfano benki, ambapo mkopeshaji ndiye anayemiliki mali na mkopaji anakuwa ni chombo tu cha kumzalishia faida.

Akiongea na The Chanzo ofisini kwake, Mwenyekiti wa kikundi cha Fahari Yetu,  Warda Omary, 42, anasema kikundi hicho kiliundwa mwaka 2019 na mwaka huohuo wakapata fursa ya kutembelewa na taasisi ijulikanayo kama Jukwaa la Asasi za Kiraia kwenye Mabadiliko ya Tabia ya Nchi, au kwa kifupi kama Forum CC, ambao waliwafundisha kuhusu umuhimu na njia za utunzaji wa mazingira. Forum CC ni jumuiya ya asasi za kiraia zilizojitolea kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwenye programu zao lakini pia kwenye uchechemuzi. Moja kati ya shughuli zinazofanywa na Forum CC ni kutembelea vikundi kama Fahari Yetu na kuvipa elimu juu ya mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na kuwapa mbinu wanachama wao za namna wanavyoweza kujiongezea kipato kutoka kwenye vitu vinavyoathiri tabia ya nchi.

Ni katika mazingira haya ndipo wanachama wa Fahari Yetu walipata fursa ya kufundishwa kutengeneza mkaa unaotokana na takataka na kupewa elimu ya ujasiriamali ambayo ndio inawaongoza katika shughuli zao za kila siku za kujiongezea kipato.

Warda, mama wa watoto watatu anayefanya biashara ya mama lishe, anaungana na wenzake katika kuusifia mkaa huo kwamba unamuongezea kipato na kumrahisishia gharama za maisha. Anasema: “Mkaa huu mimi nautumia katika biashara yangu ya mama ntilie na unanirahisishia gharama kwa kuwa huu unatumika kidogo ukilinganisha na mkaa wa kawaida, ukiuweka katika jiko unapikia maharagwe mpaka yanaiva bila kuongeza.”

Uendelezaji wa miradi

Malengo makuu ya akina mama hao kupitia kikundi chao hicho ni kuwa na uwezo wa kuwekeza kwenye miradi mikubwa. Amina Mohamedi, 35, Mweka Hazina wa Fahari Yetu, anaieleza The Chanzo kwamba kwa sasa wanakutana kila wiki kwa ajili ya kutengeneza mkaa ambao wanauuza na pesa inayopatikana huhifadhiwa kwenye akaunti ya kikundi kwa ajili ya mambo ya maendeleo. Anasema: “Kwa wiki tunatengeneza mkaa kilo 20 hadi 40 ambao tunauuza kilo moja kwa Sh1,000 ambayo hutupatia si chini ya Sh20,000  tunayoiweka benki.”

Moja kati ya mafanikio ambayo wana kikundi hao wameyafikia mpaka sasa kutokana na faida waliyopata mwaka 2020 ni ununuzi wa shamba la hekari moja eneo la Kisemvule, Mkuranga, Mkoa wa Pwani lenye gharama ya shilingi milioni nne ambalo bado hawajaamua watalifanyia nini, kama ni kulima au kutekeleza mradi mwengine katika eneo hilo.

Pia kuna miradi mingine ambayo wanakikundi hicho pia hujishughulisha nayo. Katibu wa kikundi hicho Getrude Nestory, 38, anaeleza kwamba kikundi chao hujishughulisha na utengenezaji wa sabuni za maji kwa ujazo wa lita moja hadi tano. Vilevile wanatengeneza pilipili ya kulia chakula maarufu kama siki, kuokota na kuuza vyuma chakavu pamoja na kukusanya na kuuza chupa za plastiki ambazo huzigawanya kwa wanakikundi kwa ajili ya kuziuza.

Lakini kama ilivyo kwa wajasiriamali wengine wadogo nchini, bado wanachama wa Fahari Yetu wanakabiliana na changamoto kadhaa zinazowazuia kufanikisha malengo yao. Baadhi ya changamoto hizi ni matumizi ya vifaa duni na vichache, kitu ambacho hurudisha nyuma kasi yao ya utengenezaji mkaa na sabuni.

Warda pia analalamikia kutokuwa na mashine ya kutolea mkaa, mashine ya kuchanganyia na kusagia mkaa kuwa kikwazo katika uzalishaji. Mwenyekiti huyo anawaomba wadau wawasaidie vifaa hivyo ili kuwarahisishia kazi na hatimae kutengeneza mkaa mwingi watakaouuza kwa jumla ili kutimiza malengo yao ya kuwa wazalishaji wakubwa.

Rebeca Muna ni Murugenzi Mtendaji wa Forum CC ambaye anasema kwamba Furaha Yetu ni moja ya vikundi vitatu katika Wilaya ya Ilala ambavyo Forum CC ilivitembelea na kuvipatia mafunzo pamoja na fursa za  ujasiriamali. Muna anasema walitembelea kikundi hicho mwaka 2019 ikiwa ni azma yao ya kutembelea wanawake wajasiriamali na kuwaonyesha fursa zitokanazo na utunzaji wa mazingira kwa kuwa mwanamke ndio mtendaji mkuu wa familia.

“Tumewafundisha jinsi ya kutengeneza mkaa kupitia taka hasa za vifuu, kuuza vyuma chakavu na chupa za plastiki,” Muna anasema wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Hii yote ni katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuepuka athari za mabadiliko ya tabia nchi, pia tumewafundisha kutengeneza sabuni.”

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msimbazi, Tabata, Godfrey Anthony ameiambia The Chanzo kwamba anafurahishwa na uwepo wa vikundi vya akina mama vinavyofanya shughuli za maendeleo katika mtaa wake. Anthony anasema moja ya kumi  ya makusanyo katika kila halmashauri inarudi kwa jamii ambapo asilimia nne inakwenda kwa kinamama kwa njia ya mikopo isiyokuwa na riba. Ofisa huyo wa Serikali ya Mtaa anawasahauri wanawake kutobweteka, kuunda vikundi vya maendeleo ili kujipatia mikopo kutoka Serikalini.

 

Jenifer Gilla ni mwandishi wa kujitegemea wa habari za kijamii, wanawake na vijana anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: jenifergilla2@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatile, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Jenifer Gilla

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

The Chanzo Black@300x

The Chanzo Initiative exists at the interface between advocacy and journalism. It is founded to uplift the voices of the underreported, vulnerable, and marginalized communities in Tanzania with the goal to make Tanzania the best place to live for everyone regardless of class, creed, sexual orientation and nationality.

Subscribe to Our Newsletter

The Chanzo Initiative, 2022 © All Rights Reserved