Wakati Serikali ikiendelea na juhudi zake za kukomesha matumizi ya mkaa na kuni nchini ikisema nishati hizo si salama kwa afya za watumiaji na mazingira pia wananchi wengi wa kipato cha chini wameonesha wasi wasi wao kwamba juhudi hizo zinaweza zisizae matunda kwani wao binafsi hawataacha kutumia kuni na mkaa kwa sababu bei zake ni nafuu ukilinganisha na ile ya gesi.
Kulingana na tathmini iliyofanywa na The Chanzo katika maeneo mbali mbali ya jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, wananchi wengi, wakiwamo wale wanaojishughulisha na biashara ndogo ndogo, wamebainisha sababu kadhaa za wao kushindwa kuacha kutumia nishati hiyo inayopigwa vita na wadau kadhaa nchini ikiwemo kipato duni kinachowazuia kutumia nishati bora kwenye matumizi yao ya kila siku.
Moja kati ya wananchi hawa ni Mwajabu Athumani, 31, mkazi wa Tabata Segerea anayejishughulisha na biashara ya uuzaji wa samaki wa kukaanga. Wakati wa mahojiano na The Chanzo yaliyofanyika katika eneo lake la biashara, Mwajabu anasema kwa kipato chake cha Sh.150,000 kwa mwezi hawezi kuacha kutumia kuni.
“Siwezi kuacha kutumia kuni katika biashara yangu,” Mwajabu, mama wa watoto watatu, anaiambia The Chanzo huku akifikicha macho yake kutokana na moshi mkali wa kuni unaotoka kwenye jiko lake la kukaangia samaki. “Sasa nikiacha nitatumia kipi cha haraka, gesi ipo juu siwezi imudu kutokana na biashara yangu ni ndogo. Natamani kutumia gesi lakini nina familia kubwa kidogo. Siwezi maana mtungi mkubwa wa kilo 28 unaofaa kwa familia na ambao naweza kuutumia mwezi mmoja tena kupikia vyakula vyepesi tu unauzwa Sh. 50,000. Nikinunua gunia la mkaa la Sh. 30,000 natumia miezi miwili. Hii ni nafuu zaidi kwangu.”
Mwajabu ni moja kati ya wakazi wengi wa Dar es Salaam na maeneo mengine nchini wanaoendelea kutumia nishati ya kuni na mkaa licha ya juhudi za Serikali na wadau wengine kuhimiza wananchi wahamie kwenye matumizi ya nishati ya gesi kwani matumizi endelevu ya mkaa na kuni yameonekana kuhatarisha misitu iliyopo na hivyo kuwa tishio kwa mazingira. Kama ilivyo kwa Mwajabu, wananchi wengi wanataja unafuu wa bei ya kuni na mkaa kuwa sababu ya wao kupendelea na matumizi ya nishati hiyo.
Dikson Mlay (45) , mfanyabiashara wa kuku wa kukaanga na baba wa watoto wawili , anasema kwamba anatumia kuni kwenye biashara yake kwa kuwa ni nafuu na inaharakisha upishi wake. Mlay analalamika kwamba mtaji wake ni mdogo hivyo analazimika kubana matumizi kwenye moto ili aweze kupata faida. Anasema: “Ukaangaji wa kuku ni aidha utumie kuni au gesi kwa sababu wanakuwa wengi hivyo wanahitaji moto unaowaka sana ili wasinyonye mafuta mengi. Sasa ukitumia gesi ni hasara mwisho wa siku faida huioni kwa hiyo hapa nikinunua fungu la kuni la Sh.2,000 naongeza na vifuu inatosha kabisa kukaangia kuku wa Sh. 40,000.”
Wanaotumia gesi hutumia mkaa pia
Matumizi ya nishati ya mkaa na kuni katika jiji la Dar es Salaam yametawala sana kiasi ya kwamba hata watu wanaotumia gesi hulazimika kutumia kuni kubana matumizi. Moja kati ya watu hawa ni Desteria Kamugisha 40) ambaye licha ya kutumia gesi ya mtungi au Liquefied Natural Gas (LPG) ya kilo 15 inayouzwa Sh. 50,000 na kudumu kwa miezi miwili na nusu bado analazimika kuwa na mkaa nyumbani kwake. Desteria anatumia gesi kwa sababu anadhani ni salama kwa afya na hurahisisha mapishi lakini anakiri kwamba ili adumu na nishati hiyo kwa muda mrefu inamlazimu kununua mkaa ili kupikia vyakula vinavyochelewa kuiva kama vile maharagwe na makande. Anasema: “Kama ningekuwa napikia hadi maharagwe au kande nadhani ingedumu wiki chache kwa kuwa hapa kwetu tunapika mara tatu kwa siku, inabidi ninunue na gunia la mkaa ili kuchanganya kwa sababu nina familia ya watu 7.”
Mabadiliko hata hivyo yameanza kutokea kwani baadhi ya wananchi wameanza kuacha matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye gesi ya asilia inayosambazwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Moja ya wananchi hao ni Maria Dama (40), mkazi wa Mikocheni, Dar es salaam anayesema kwamba ameona unafuu wa maisha katika kupikia tangu aanze kutumia gesi hiyo ya asilia.
Maria anasema kwamba inamgharimu Sh. 25,000 hadi Sh30,000 kulipia gesi hiyo kwa mwezi kulingana na ugumu wa chakula anachopika tofauti na zamani ambapo alikuwa akitumia gesi ya mtungi wa LPG ambao alikuwa akilipia Sh.50,000 hivyo gharama imepungua karibu nusu. Anaongeza: “Uzuri wa hii gesi [ya asilia] unalipia kadiri ya uwezo wako. Uniti moja Sh1,000, na mimi kwa siku uniti moja inanitosha kupikia milo mitatu na kuchemsha maji ya kunywa.”
TPDC inajenga mitambo ya kusafirisha gesi asilia ambayo imewekwa katika maeneo kadhaa nchini. Marie Mselemu, Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa TPDC, ameiambia The Chanzo wakati wa mahojiano maalum kwamba baadhi ya maeneo yaliyofikiwa na gesi hiyo ni Madimba (Mtwara), Songo Songo (Lindi) pamoja na Bomba la kusafirisha gesi asilia hiyo kutoka Mtwara, kupitia Somanga Fungu mkoani Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam. Kwa jijini Dar es Salaam, wakazi wa maeneo ya  Ubungo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Survey, Makongo Juu, Sam Nujoma, Shekilango, Sinza, Mikocheni – Coca-Cola na  Mwenge wameanza kunufaika na gesi hiyo ambayo imeunganishwa kwenye nyumba zao kwa kutumia mabomba maalum.
“Lengo la Serikali ni kufikisha gesi asilia kwa watu wengi kadiri inavyowezekana ili kupunguza matumizi ya kuni, mkaa na nishati zisizo salama kwa afya na athari za mazingira na gharama,” anasema Mselemu na kuongeza kwamba hatua hiyo itasaidia utunzaji wa mazingira ambayo kwa sasa yapo hatarini kutokana na ukataji miti kwa ajili ya nishati ya kupikia. “Gharama ya gesi hii ni Sh.1,000 kwa uniti ambapo hata mtu wa kipato cha chini anaweza kuimudu. Familia ya watu sita wanatumia uniti moja tu kwa siku sawa na Sh.30,000 mwezi.”
Uhamasishaji washika kasi
Licha ya ukweli kwamba wananchi katika maeneo mengi wameendelea kutumia kuni na mkaa, Serikali haijakata tamaa katika kuwashawishi wananchi waachane na nishati hiyo ambayo inasema siyo salama na kuwafanya kuhamia kwenye matumizi ya gesi. Uhamasishaji huu unafanywa na mamlaka nyingi za Serikali lakini kinara wao ni Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA). The Chanzo ilimuuliza Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA Titus Kaguo wanafanya nini zaidi katika kuwashawishi wananchi waache matumizi ya nishati ya kuni na mkaa mbali na kuwaambia kuwa ni salama kwa afya zao na mazingira?
“Uhamasishaji unafanyika sambamba na kuweka mazingira mazuri na fursa za biashara ili kuweza kupata wafanyabiashara wengi ambao watapeleka gesi ya bei nafuu kwa wananchi,” anasema Kaguo. “Sasa tuna wafanyabiashara wanaotengeneza mitungi midogo ya gesi ya kuanzia kilo mbili inayouzwa Sh6, 000, gharama ambayo hata mtu wa hali ya chini anaweza kuimudu.”
Kaguo anasema juhudi za uhamasishaji wa matumizi ya gesi zinazaa matunda, akitaja ongezeko la matumizi ya gesi ya LPG kutoka lita 6,000 mwaka 2008 hadi kufikia lita 145,000 Juni, 2019. Kaguo anasema hatua hii inatokana na kuwapo gharama ambazo hazimuumizi mtumiaji na muuzaji na pindi wanapoona upande mmoja unaumia wao kama mamlaka husika wanaingilia kati.
Jenifer Gilla ni mwandishi wa kujitegemea wa habari za kijamii, wanawake na vijana anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: jenifergilla2@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatile, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.