The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tamu, Chungu Za Kuagiza Mzigo Kutoka China Kipindi Cha COVID-19

Kupokea bidhaa chini ya kiwango, kuchelewa na kutokufika kabisa kwa mizigo ni baadhi tu ya changamoto ambazo wafanyabiashara wasioweza kwenda China kufuata mizigo wanazilalamikia.

subscribe to our newsletter!

“Nilipokea mzigo ukiwa na viatu 200 vyenye ubora wa chini tofauti na pesa niliyolipia. Ni sawa na ulipie Sh15,000 wakupe kiatu cha Sh5,000. Ilikuwa ni hasara kubwa sana kwangu. Nilichanganyikiwa. Nilipata hasara ya takribani milioni tatu.”

Ni maneno ya Bertha Mmari mkazi wa Kimara, Dar es Salaam anayejishughulisha na biashara ya jumla ya nguo na viatu, akielezea moja ya hasara alizozipata kutokana na kuagiza mzigo kwa njia ya mtandao kutoka nchini China kipindi hiki ambacho dunia inakabiliana na ugonjwa hatari wa COVID-19.

Bertha, 35, hakuwa ni muagizaji wa mizigo. Alikuwa akisafiri mwenyewe mpaka nchini China na kuchagua bidhaa, kuzifunga kwenye maboksi na kisha kuzipeleka sehemu ya kusafirisha kwa ajili ya kuileta nchini Tanzania. Kilichobadilisha utaratibu wake ni COVID-19 ambayo imesababisha mataifa mengi ulimwenguni kufunga mipaka yake ikiwa ni sehemu ya juhudi zao na kupambana na kusambaa kwa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mpaka kufikia saa 10:35 za mchana, Februari 13, 2020,  kulikuwa na jumla ya kesi 107,838,255 za watu walioambukizwa virusi vinavyosababisha COVID-19 huku watu 2,373,398 wakiripotiwa kufariki kutokana na ugonjwa huo duniani. Tangu Machi 28, 2020, China, mwenza mkubwa wa kibiashara wa Tanzania, ilifunga mipaka yake yote na kuzuia uingiaji wa wageni katika taifa hilo. Hatua hii imekuwa na athari kubwa sana kwenye uchumi wa Tanzania huku wafanyabiashara wadogo kama Bertha ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakisafiri kwenda China kuchukua mizigo wakiwa ni waathirika wakubwa wa hatua hiyo.

Mawakala watupiwa lawama

“Unapokuwapo mwenyewe [huko China] unaifunga mizigo yako kwenye maboksi na kuipeleka kwa wakala na kuiacha ikiwa imefungwa,” anaeleza Bertha, mama wa mtoto mmoja, akizungumzia changamoto ya usalama wa mizigo wanayoagiza kutoka China. “Hii ni tofauti na ukiagiza ambapo wakala ndio anakufungia kwenye maboksi. Mawakala wengi siyo waaminifu na hivyo wanakuibia au kukubadilishia mzigo.”

Roda Mwakanele ni mfanyabiashara wa nguo za kike eneo la Sinza, Dar es Salaam, anayezungumzia changamoto ya kuchelewa kwa mizigo na hivyo kusababisha hasara kubwa. Roda, 37, anasema ucheleweshaji wa mizigo husabibishwa na changamoto za usafiri lakini pia kasi ya uzalishaji kwa sasa imezorota nchini China. Kwa maelezo yake, wakati kabla ya ujio wa janga la COVID-19 ilichukua wiki moja hadi mbili tu kutengenezewa aina ya nguo anazotaka sasa inachukua mwezi hadi mwezi na nusu.

Roda anaieleza The Chanzo kwa huzuni: “Niliagiza mzigo tangu Octoba 2020 nikikusudia niuze kipindi cha msimu wa Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya. Lakini mzigo umefika Januari 2021 ambapo hakuna biashara kabisa.”

Kuna wafanyabiashara wengine, kama Frida Mmari, hawakuweza kupokea mizigo yao tangu walipoagiza mwaka jana, 2020. Frida, 45, anasema: “Nlitegemea kuuza mzigo huo wa nguo za watoto kipindi kile cha Sikukuu lakini mpaka leo sijapokea. Nipo tu hapa, sasa sielewi nifanyeje. Na siwezi agiza mwingine hadi huo ufike. Haya mambo kabla ya corona hayakuwapo.”

Mawakala watia neno

Changamoto hizi zinazowakabili wafanyabiashara hawa pia huwaumiza kichwa mawakala wenye dhamana ya kuwasafirishia mizigo yao kutoka nchini China kuja Tanzania, akiwemo Nuru Ezekiel ambaye ni Afisa Huduma kwa Wateja kutoka kampuni ya usafirishaji mizigo ya Choice Shipping Tanzania. Ezekiel anataja sababu kadhaa zinazopelekea mizigo kuchelewa.

Moja ni kwamba kwa sasa meli za mizigo zimekuwa  chache baada ya baadhi ya meli kusitisha huduma ya usafirishaji.

Pili, kwenye ofisi nyingi za uwakala kwa sasa nguvu kazi imepungua kwenye ofisi zao za China ambako ndiko kunakopakiwa mizigo kutokana na wafanyakazi wanaohusika na kupakia na kufunga  mizigo wamerudi nchini Tanzania kupisha maambukizi ya corona.

Sababu nyingine ni viwanda vingi nchini china kufungwa kwa hiyo hivyo vichache vilivyopo vinaelemewa na oda kiasi ya kwamba mteja akitoa oda ya kutengenezewa mzigo inachukua hata wiki mbili kukamilika tofauti na zamani ambapo ilikuwa inachukua siku tatu hadi wiki moja.

Kuhusu malalamiko ya wateja ya kuletewa vitu pungufu au ambavyo havina ubora, Ezekiel anasema mara nyingi hilo linafanyika madukani wanakochukulia mizigo.

“Hilo la kuibiwa na kudhulumiwa sisi hatuhusiki. Sisi tunakwenda kuchukua mzigo tu na wengine tunakuta wameshaufunga tunabeba boksi tunaondoka. Hayo mengine hatujui,” anasema Ezekiel na kuongeza:

“Wateja wengi tunaona wanahama [kwenda kwa mawakala wengine], wakidhani kwamba huko waendako kuna nafuu. Lakini  wengine wanarudi baada ya kuona kuwa kumbe changamoto zinafanana.”

TCRA yatahadharisha

Wafanyabiashara wengi wanaokabiliana na changamoto hizi za kutapeliwa mizigo yao walioagiza kutoka nchini China na kwengineko hupeleka malalamiko yao kwenye Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa sababu shughuli zao nyingi wanafanyia kwenye mitandao eneo ambalo linadhibitiwa na TCRA.

Semu Mwakanjala, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka TCRA, ameithibitishia The Chanzo kwamba TCRA imeshapokea kesi kama hizo nyingi tu na wamekuwa wakishirikiana na polisi kuhakikisha wahalifu wanatiwa nguvuni.

“Lakini kwa utapeli unaohusisha nchi za nje tunafuata taratibu za kisheria kwa nchi hizo mbili tukihusisha Interpol,” Mwakanjala anasema. Anawasihi wafanyabiashara wanaonunua bidhaa mtandaoni kuwa makini kwa kufanya uchunguzi kabla ya kuagiza vitu.

“Sasa hivi mawasiliano yamerahisishwa,” anasema Mwakanjala. “Watu wanaweza kununua na kuuza bidhaa mtandaoni lakini pia kuna watu wanaotumia mitandao vibaya kutapeli wengine hivyo nawasihi Watanzania kuwa makini. Hasa hawa wanaoagiza nje ya nchi inabidi wafanye utafiti na kujiridhisha kabla hawajaagiza bidhaa kwa mtu na kumtumia pesa nyingi.”

Pamoja na changamoto hizi, bado wafanyabiashara wanakiri kwamba kuna faida wanapata kwa kuagiza mizigo kutoka China badala ya kwenda wao wenyewe. Bertha Mmari, kwa mfano, anasema kwamba ukiagiza mzigo nje unaokoa pesa ya nauli ambayo ni zaidi ya shilingi milioni mbili pamoja na pesa ya chakula na malazi kwa siku utakazokaa huko.

“Ukienda mwenyewe kuna gharama kubwa,” Bertha anaiambia The Chanzo.  “Unaweza kutumia hata shilingi milioni nne kwa wiki mbili tu utakazokaa. Lakini ukiagiza mwenyewe unaokoa pesa nyingi.”

Jenifer Gilla ni mwandishi wa kujitegemea wa habari za kijamii, wanawake na vijana anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: jenifergilla2@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatilie, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *