Raisi John Magufuli ametangaza leo, Jumatano, Februari 24, 2021, kwamba Serikali inakusudia kulivunja jiji la Dar es Salaam na kupandisha moja kati ya manispaa zake kuwa jiji. Raisi Magufuli alitangaza uamuzi huo wakati wa uzinduzi wa daraja la juu la Kijazi lililopo Ubungo,hafla iliyohudhuriwa na viongozi waandamizi kadhaa wa Serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo ya Tanzania.
“Tunataka manispaa moja katika jiji la Dar es Salaam ndiyo ipandishwe hadhi iwe jiji halafu zingine ziwe manispaa ni kama ilivyo katika majiji mengine,” alisema Raisi Magufuli wakati akihutubia leo. “Jiji la Dar es salaam litaendelea kuwepo lakini tutachukua eneo fulani na nafikiri Ilala inafaa kuwa jiji ndiyo katikati ya jiji la Dar es Salaam.”
Hatua hii ya Serikali inakuja ikiwa inaelekea miaka sitini sasa toka Disemba 10, 1961, ambapo jiji la Dar es Salaam lilitunukiwa hadhi ya kuwa jiji na Malkia wa Uingereza. Lakini hatua hii inamaanisha nini, nini maana ya tamko ili la awali, na jee huu unaweza kuwa mwisho wa uwepo wa jiji la Dar es Salaam?
Historia inaonesha kwamba jiji la Dar es Salaam sio geni katika mabadiliko mbalimbali ya kiutawala na kimuundo. Moja ya mabadiliko ya kwanza ni lile la mwaka 1972 ambapo Serikali ilivunja halmashauri zote nchini na kurudisha nguvu kwa Serikali Kuu (mkoa), mpaka mnamo mwaka 1982 ambapo Serikali ilirudisha tena serikali za mitaa.
Badiliko lingine la kihistoria ni lile lilitokea 1996, ambapo halmashauri ya jiji la Dar es Salaam ilivunjwa na kuundwa tume ya jiji iliyodumu kwa miaka minne, lengo likiwa ni kukabili changamoto za ukuwaji wa kasi wa Dar es Salaam. Kupitia tume hiyo, jiji liliweza kugawanywa katika halmashauri za manispaa tatu, yaani Kinondoni, Ilala na Temeke na hatimaye baadae halmashauri za Kigamboni na Ubungo zikaongezwa.
Kwa kufuatilia historia, pamoja na tamko la awali la Raisi Magufuli na kauli toka kwa wizara ya TAMISEMI juu ya uvunjaji wa jiji la Dar es Salaam ni wazi kwamba mabadiliko ni juu ya halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, jiji kama jiji bado litaendelea kubaki, huku moja ya halmashauri kati ya tano zilizopo ikipandishwa hadhi.
Mfumo wa manispaa na jiji ni mfumo unaojaribu kurudisha madaraka kwa wananchi kwa kufanya viongozi wa kuchaguliwa na wananchi kuwa na mamlaka moja kwa moja juu ya maendeleo katika maeneo yao. Halmashauri ya jiji inaongozwa na Meya anayechaguliwa katikati ya madiwani, vivyo hivyo katika manispaa Meya huongoza ingawa chombo cha juu chenye mamlaka kiutawala ni Baraza la madiwani.
Halamashauri ya jiji la Dar imekuwa ikifanya kazi kama kiunganishi (coordination) kati ya manispaa zote zilizoko ndani ya Dar es Salaam, hii ikimaanisha kazi zinazoingiliana lakini ziko nje ya manispaa husika hufanywa na halamshauri ya jiji hasa kwenye upande wa miundombinu, mazingira, taka, maegesho ya magari. Mfumo huu pia unaonekana kwenye majiji mengine kama Arusha, Dodoma na Mwanza.Kwa kupandishwa hadhi manispaa ya ilala, hii inamaanisha sehemu kubwa ya kazi za uunganishi (coordination) kwa sasa zitafanywa ndani ya iliyokuwa manispaa ya ilala, hapo hapo kazi zote za awali za manispaa ambazo ni nyingi zaidi, zitaendelea kama mwanzo. Kiutendaji kuna uwezekano mkubwa wa kuanzishwa idara ya jiji itakayokuwa ikishughulikia mambo yote ya jiji.
Toka kurudishwa kwa mfumo wa manispaa na jiji kumekuwa na maendeleo dhahiri ndani ya Dar es Salaam.Hata hivyo, kuna maswali juu ya changamoto mfano mipango miji, changamoto za tabia ya nchi zinazosababisha kuharibika kwa miundombinu mara kwa mara, pamoja na mfumo wa usafiri usiokidhi mahitaji yaliyopo, mambo yote haya yanaangukia katika sehemu ya utendaji wa jiji.
Kimfumo kati ya mwaka 2015-2020 kulionekana kuwepo na mwingiliano mkubwa wa kimamlaka kati ya halmashauri ya jiji pamoja na manispaa na viongozi wa mkoa na wilaya. Hii ni kwa sababu maeneo mengi ya Dar es Salaam yalikuwa chini ya mameya toka kwenye vyama vya upinzani. Kimuundo shughuli za kimaendeleo hufanyika na halmashauri wakati mkoa na wilaya wakihusika zaidi na shughuli za kisiasa na usalama, pamoja na kukukutanisha wadau wote katika mkoa husika.
Tayari waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo ameshatoa taarifa ya kupandishwa hadhi halmashauri ya manispaa ya Ilala kuwa halmashauri ya jiji la Dar es Salaam kuanzia Februari 24, 2021. Huku akieleza kuwa watumishi wa iliyokuwa halmashauri ya jiji la Dar es Salaam watapangiwa vituo vipya vya kazi, vilevile amefafanua taratibu za mgawanyo wa mali na madeni zitaendelea kwa mujibu wa sheria ya Serikali za Mtaa. Bado ni mapema kuweza kutabiri ufanisi au udhaifu wa mfumo huu mpya, katika majuma yajayo tutaweza kuona zaidi namna serikali itakavyoisuka halmashauri mpya ya jiji. Je, mfumo huu mpya utaweza kutimiza ndoto za kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji la kisasa (smart city)?