The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kwa Nini Othman Masoud Ni Chaguo Sahihi Kwa Nafasi Ya Makamo Wa Kwanza Wa Raisi

Uzoefu wake kwenye masuala ya kiserikali na uthubutu wake wa kusema na kufanya anachokiamini bila woga unamfanya Othman Masoud kuwa chaguo sahihi kwa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Raisi wa Zanzibar. 

subscribe to our newsletter!

Ukisoma wasifu wa maisha ya Othman Masoud Othman, ambaye leo ameteuliwa na Raisi Hussein Mwinyi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, akiwa mrithi wa Maalim Seif Sharif Hamad aliyeaga dunia hivi karibuni, utagundua namna ambavyo gwiji hilo la sheria limekuwa likiaminiwa na Marais wa awamu mbalimbali wa Zanzibar — kutoka Rais Salmin Amour mpaka sasa Rais Hussein Mwinyi —  kufanya kazi muhimu na nyeti za kitaifa, kazi ambazo watu waliowahi kufanya naye kazi kwa karibu wanakiri kwamba alizifanya kwa ufanisi na uadilifu mkubwa.

Salmini Amour, Rais wa awamu ya tano aliyeongoza Zanzibar kuanzia Oktoba 25, 1990 mpaka Novemba 8, 2000, alimteua Othman kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais aliyehusika na masuala ya kisheria na hatimaye kumpandisha cheo kwa kumteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu mwaka 1993 wakati huo Othman akiwa na umri wa miaka 30 na miaka nne tu tokea kuajiriwa serikalini.  Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Raisi Salmin Amour aliamua kumbakisha Othman katika nafasi hiyo ya Katibu Mkuu na Naibu Mwanasheria Mkuu.

Mwaka 1997, Othman akiwa na miaka 34, Raisi Salmin Amour alimteua kuwa Mwenyekiti wa mwanzo wa Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB).  Miongoni mwa wanasheria ambao Othman aliwatafuta na kuajiriwa na Bodi ya Mapato kama Katibu wa Bodi na Msaidizi Katibu wa Bodi ni Bwana Asaa Ahmad Rashid, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Maadili Zanzibar na ambaye alikuwa Katibu wa Tume ya Maoni ya Katiba, au maarufu kama Tume ya Warioba, na Bi Khadija Shamte ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria. Othman aliitumikia nafasi hiyo ya uenyekiti wa Bodi kwa vipindi vyote viwili vya miaka mitatu mitatu hadi mwaka 2003.

Kazi nyengine muhimu ambayo Othman Masoud aliaminiwa na Serikali ilikuwa ni kuongoza mapatano ya kuanzisha mradi wa Kampuni ya simu ya Zantel kuanzia kwenye ubia na Etisalat hadi kupatiwa leseni ya Njia za Simu za Kimataifa yaani International Gateway License kutoka Kamisheni ya Mawasiliano Tanzania (TCC).  Mafanikio muhimu katika kazi hii yalikuwa ni kuiwezesha Serikali ya Zanzibar kupata hisa 18 kutoka tisa zilizokuwa zimeshaamuliwa na wabia wa mradi huo.

Rais Amani Abeid Karume alimuamini Othman kwa kumteua kuwa Katibu Mkuu muanzilishi wa Wizara ya Katiba na Utawala Bora na Naibu Mwanasheria Mkuu mwaka 2000.  Miongoni mwa mafanikio yake yanayotajwa na wengi ni kufanya marekebisho ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali [CAG] na pia kuifanyia marekebisho Kamisheni ya Wakf na Mali ya Amana kwa kuunda Kamati ya Wataalamu ya Uchunguzi na kupendekeza Sheria mpya ya Wakf.

Mwaka 2002, Rais Karume alimteua Othman kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka wa Mwanzo wa Zanzibar. Miongoni mwa mafanikio makubwa aliyoyapata ni kuanzisha ofisi hiyo kitaasisi na kiutendaji ambayo hapo mwanzo haikuwepo. Baadhi ya hatua muhimu na za kipekee alizochukua ilikuwa ni pamoja na kuanzisha mfumo wa wanasheria kuendesha mashtaka badala ya polisi, ambao kwa kitaalamu unajulikana kama civilianization of prosecution ambao ulitekelezwa kwa awamu. Hata Tanzania Bara chini ya DPP Dk Eliezer Feleshi, walikuja Zanzibar kujifunza mfumo huo na wao kuuanzisha nchini kwao.

Mafanikio mengine makubwa ni kuwajengea uwezo wanasheria wa Serikali wa Ofisi ya DPP kwa kuanza kuwaajiri kwa mfumo unaozingatia sifa na umahiri, yaani strict meritocracy.  Aidha kuwapatia wanasheria hao mafunzo ya uendeshaji mashtaka ndani na nje ya Tanzania ikiwemo mafunzo ya miezi mitatu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya Rwanda (ICTR- Arusha).  Matokeo ya kuwajengea uwezo huo, wengi wa wanasheria katika Ofisi hiyo wameteuliwa katika nafasi muhimu serikalini.  Miongoni mwao ni Bwana Suleiman Masoud, Waziri wa Maji na Nishati; Bi Raya Msellem, Katibu wa Baraza la Wawakilishi; Bwana Shaaban Ramadhan, Naibu Mwanasheria Mkuu; Bi Aziza Idi Suwedi, Jaji wa Mahkama Kuu; Bwana Muumin Khamis, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka; Bi Mwanamkaa Abrahman, Mkurugenzi Mkuu, Kampuni ya Mafuta ya Zanzibar; na Bwana Mohammed Khamis, Makamo Mwenyekiti, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Rais Karume pia alimteua Othman kuwa Mwenyekiti muanzilishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar (IPA).

Rais Ali Mohammed Shein naye alianza kwa kumteua Othman Masoud kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar mwaka 2011.  Miongoni mwa yanayotajwa kuwa mafanikio yake ni mageuzi ya Ofisi hiyo nyeti kwa kuibadili kimuundo kwa kuanzisha Vitengo (specialised Units), kupendekeza sheria ya kuendesha Ofisi na Maktaba ya kisasa.  Katika muda mfupi aliotumikia Ofisi hiyo, aliweza kusimamia ujenzi wa jengo jipya la Ofisi hiyo. Mwaka 2014, wakati wa mchakato wa mabadiliko ya katiba, Rais Shein alitengua uteuzi wa Othman Masoud kama Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, hatua ambayo wengi wanaona ilitokana na misimamo ya Othman iliyokuwa inakinzana na misimamo ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye suala la maslahi ya Zanzibar kwenye muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Kisiasa, Chama cha ACT-Wazalendo kiliwahi kumtumia Othman baada ya kumuomba achangie utaalamu wa Othman wake katika kuandaa ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 na kumteua katika Kamati yake ya Ilani.  Hatimaye alipewa kazi ya kuiwasilisha rasmi siku ya uzinduzi, kazi ambayo aliifanya kwa weledi. Aidha, alikuwa mmoja wa walioinadi Ilani hiyo katika vyombo mbali mbali vya Habari.

Katika medali za kimataifa, mnamo mwaka 2017, Othman aliaminiwa na Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia tasnia ya ubunifu na uvumbuzi (World Intellectual Property Organisation) lenye makao yake makuu Geneva, Uswiss.  Othman aliteuliwa na mkutano huo kuziwakilisha nchi 54 za Bara la Afrika katika Bodi ya Usimamizi yaani Independent Advisory Oversight Committee wa Shirika hilo baada ya kushinda kinyang’anyiro cha wagombea 119 kutoka nchi kadhaa za Afrika.  Kazi za Bodi hiyo ni kuhakikisha kwamba sheria, taratibu, maadili, matumizi ya fedha, hatua za kinidhamu kwa wafanyakazi na utendaji wa Mkurugenzi Mkuu na Sekretariat vinafuata viwango vya uwajibikaji vilivyowekwa katika miongozo mbali mbali ya Shirika hilo na Umoja wa Mataifa.  Aliteuliwa kwa mkataba wa miaka mitatu ambayo iliongezwa tena kwa miaka 3 hadi December 2022.

Uzoefu wake kwenye masuala ya kiserikali na uthubutu wake wa kusema na kufanya anachokiamini bila woga unamfanya Othman Masoud, mbobezi wa tasnia ya sheria akishikilia shahada tatu za sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha London, Uingereza (SOAS) na Chuo Kikuu cha Turin, Italy, kuwa chaguo sahihi la mrithi wa Maalim Seif Sharif Hamad kwa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Raisi wa Zanzibar. Raisi Mwinyi amedhihirisha nia ya dhati ya kuwaunganisha Wazanzibari na kuboresha ustawi wao, bila shaka Othman Masoud atakuwa msaada mkubwa katika juhudi hizo.

 

Khaleed Said Suleiman ni Mzanzibar anayeishi Toronto, Canada. Unaweza kuwasiliana naye kupitia  khaleed_ihaab@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unaweza kuchapisha kwenye safu hii kwa kuwasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *