Tanzania inakwenda kuwa na Rais wa kwanza wa kike katika historia yake, hatua ambayo wachambuzi na wafuatiliaji wa masuala ya kisiasa na kijinsia wameitaja kama ni kuandikwa upya kwa historia ya taifa hilo la Afrika Mashariki. Samia Suluhu Hassan ameshakula kiapo kulingana na matakwa ya kikatiba yanayoagiza kwamba baada ya Rais aliyepo madarakani kufariki, makamu wake atachukua nafasi hiyo kwa kipindi kilichobaki cha miaka mitano. Wengi wanaiona hatua hiyo kuwa ni fursa mpya ya ujenzi wa taifa la Tanzania.
Mama Samia, kama watu wengi wanavyomwita, anachukua nafasi iliyoachwa na Rais John Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021, katika Hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salaam, kutokana na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo. Shughuli za kuuga mwili wa Rais Magufuli zinaendelea, huku akitegemewa kuagwa katika maeneo matano tofauti ya Dar es Salaam, Zanzibar, Dodoma, Mwanza na nyumbani kwake Chato, mkoani Geita ambako ndiko atakakozikwa siku ya Ijumaa, Machi 26, 2021. Kwa sasa nchi ipo katika maombolezo ya siku 21, huku baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wakipiga marufuku ufanyaji wa sherehe ya aina yoyote katika maeneo yao husika kupisha maombolezo ya kiongozi huyo aliyedumu madarakani kwa kipindi cha takribani miaka sita.
URais wa Samia Suluhu unakuja huku kukiwa na vuguvugu na harakati nyingi barani Afrika na duniani kwa ujumla zinazolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za maamuzi iwe ni za kisiasa, kibiashara, au kijamii. Rais Samia Suluhu anakuwa ni mwanamke wa tatu katika ukanda wa Afrika Mashariki kushikilia nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Burundi Slyvie Kinigi kukaimu nafasi ya uRais wa taifa hilo kati ya Octoba 27, 1993 na Februari 5, 1994 kufuatia kifo cha Melchior Ndadaye wa kabila la Wahutu ambaye aliuwawa pamoja na watu wengine sita na magaidi wa kabila la Watusi, na hivyo kupelekea mwanzo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Agathe Uwilingiyimana, aliyepata kuwa Waziri Mkuu wa Rwanda, pia aliwahi kukaimu kiti cha uRais cha taifa hilo kuanzia Julai 18, 1993 mpaka alipouwawa Aprili 7, 1994.
Tofauti kubwa kati ya Samia Suluhu na akina Agathe Uwilingiyimana na Slyvie Kinigi ni kwamba Uwilingiyimana na Kinigi hawakuwahi kuapishwa kuwa maRais kamili wa Rwanda na Burundi, wote walikaimu tu, tofauti na ilivyo kwa Mama Samia aliyekula kiapo cha kuwa Rais kamili. Mama Samia pia anaingia kwenye orodha ya wanawake wengine wa bara la Afrika ambao wameshikilia na wanaendelea kushikilia nafasi hiyo ya juu ya uongozi katika nchi zao husika. Hawa wanajumuisha Rais wa zamani wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, Rais mstaafu wa Malawi Joyce Banda na Rais wa sasa wa Ethiopia Sahle-Work Zewde.
Mapokeo chanya
Tathmini ya haraka haraka inaonesha kwamba watu wengi wameupokea uRais wa Mama Samia kwa mtazamo chanya. Hii haimaanishi, hata hivyo, kwamba hakuna watu wanaonesha kuwa na wasi wasi na Mama Samia, kitu ambacho hakishangazi sana ukizingatia ukweli kwamba hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na Rais wa kike. Hata hivyo, hata hao wenye wasi wasi wanaongelea kichini chini tu kwani watu walioupokea uRaisi wa Mama Samia kwa matumaini ni wengi na wamekuwa wakibainisha hisia zao hizo hadharani.
“Miaka 60 baada ya uhuru, Tanzania imejipatia Rais wa kwanza mwanamke, Mheshimiwa Samia Suluhu. Historia imeandikwa,” Dk Victoria Lihiru, wakili na mhadhiri wa sheria kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzana (OUT) na mtafiti wa masuala ya kijinsia aliandika katika ukurasa wake wa Twitter punde tu baada ya Mama Samia kula kiapo. “Binti zetu sasa watajua kuwa hakuna mipaka katika ndoto zao.”
Maria Sarungi-Tsehai, mwanaharakati wa masuala ya kisiasa na muasisi wa vuguvugu la Change Tanzania linalolenga kuhamasisha uwajibikaji wa Serikali, alikuwa na haya ya kusema punde baada ya Mama Samia kuthibitishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania: “Najua kuwa binafsi, wewe ni mtu mkarimu, huna makuu na unapenda majadiliano. Hilo sitabisha. Tuliongea machache wakati wa futari 2017, ikiwemo kuhusu uwezekano wa kufikia ulichofikia leo – Rais wa [Jamhuri ya Muungano wa Tanzania]. Ni siku kubwa kwako na kwa taifa. Nimefarijika.”
“Nilidhani sitaishi kuona mwanamke anaapishwa kuwa Rais wa jamuhuri yetu,” Mwanahamisi Singano, mwanaharakati wa masuala ya kijinsia na Meneja Programu wa shirika la Mtandao wa Maendeleo na Mawasiliano wa Wanawake wa Kiafrika (FEMNET), aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akipongeza ujio wa Samia Suluhu kama Rais wa Tanzania. “Mungu ibariki Tanzania, inaniliza leo.”
Mzanzibari mwenye asili ya Kizimkazi iliyopo kusini mwa kisiwa cha Unguja, Samia Suluhu Hassan amewahi kufanya kazi kama waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya Rais Amani Abeid Karume. Kati ya mwaka 2010 na 2015, alikuwa Mbunge wa jimbo la Makunduchi kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais akishughulikia masuala ya muungano. Mwaka 2014, Samia alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyikiti wa Bunge Maalumu la Katiba lililokuwa na kazi ya kuandaa Katiba Mpya ya Tanzania. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na 2020, Samia alichaguliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Magufuli na hivyo kuwa Makamu wa Rais katika vipindi vyote viwili vya uongozi wa hayati Magufuli.
Mwanzo wa wanawake kujifunza
“Mimi kama mwanamke nimefurahi sana kwa tukio lilitokea, nashindwa kuelezea furaha niliyonayo kwani hatujawahi kuwa na Rais mwanamke katika nchi yetu katika awamu zote lakini sasa tumepata,” Aisha Rashid, mkazi wa Ubungo, Dar es Salaam anayejishughulisha na biashara ya mama lishe, aliileza The Chanzo hisia zake juu ya ujio wa Mama Samia kama Rais mpya wa Tanzania. “Mimi naona tukio hili ni mwanzo wa wanawake kujifunza kuwa kila kitu kinawezekana kama tukiamua. Hivyo, ni muhimu zaidi kusonga mbele [na] kumuombea na kumtia moyo Mama Samia. Naamini anaweza na ataendelea kutungoza kama [Rais] Magufuli.”
Kwa upande Wake Anaeli Thomas amesema kuwa anaamini kasi ya hayati Magufuli kuendelea kutokana na mchango mkubwa na uzoefu alioutoa Rais Samia kwa Rais aliyepita. Wakati wa mahojiano na The Chanzo, Thomas alisema: “Kwanza mpaka Magufuli alimchagua kuwa Makamu wa Rais ni kwamba anamuamini na uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Walishirikiana kwa kipindi kilichopita na wakatuletea maendelea. Hivyo [Rais Samia] ana uzoefu wa kutosha na ni seme tu kuwa tunamuamini na [tunamuomba] Mungu amsaidie. Namshauri Rais Samia kuwa mkali hasa kwa watu wanaofanya uzembe kwa kuchezea mali za umma na wale wanaoshindwa kutekeleza kazi zao wachukuliwe hatua. Mataminio ni kuona kasi ile ile ya hayati Magufuli inaendelea huku akitutazama na sisi wanyonge zaidi.”
Mama Samia anaonekana kutambua matumaini haya ya wananchi wake na uwezekano wa yeye kulinganishwa na Rais Magufuli kiutendaji. Ni katika mazingira haya ndipo Rais Samia aliona umuhimu wa kuwahakikishia Watanzania na dunia kwa ujumla kwamba atajitahidi kadiri ya uwezo wake kuendeleza mema yaliyofanywa na mtangulizi wake na kwamba, “Hakuna kitu kitaharibika chini ya uongozi wangu.”
Katika hotuba yake punde baada ya kuapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania, Mama Samia aliwataka Watanzania kuwa watulivu na kujenga umoja na mshikamano katika kipindi hiki kigumu. “Niwahakikishe kuwa, tuko imara kama taifa, na sisi viongozi wenu tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa tunaanzia pale mwenzetu alipoishia,” Rais Samia alisema kuwatoa hofu Watanzania. “Isitoshe, nchi yetu inayo hazina nzuri ya uongozi na misingi imara ya utaifa, udugu, umoja na ustahamilivu na nidhamu ya vyombo vyetu vya ulinzi na usalama iliyojengwa na viongozi waliotutangulia” ambayo anaitegemea kumuongoza kwenye uongozi wake.
Ameandaliwa na kufunzwa vya kutosha
Kama vile haya hayatoshi kuwahakikishia wananchi wake ambao wanaweza kuwa na wasi wasi na yeye kama kweli anaweza kuliongoza taifa hili, Mama Samia alizungumzia namna anavyomfahamu Rais Magufuli na jinsi alivyovuna mafunzo ya uongozi kutoka kwa kiongozi huyo. Alisema: “Mimi nilipata bahati ya kuwa Makamu [wa Rais Magufuli]. Alikuwa ni kiongozi asiyechoka kufundisha, kuelekeza kwa vitendo vipi anataka nchi hii iwe au nini kifanyike. Amenifundisha mengi, amenilea na kuniandaa vya kutosha. Naweza kusema bila chembe ya shaka kuwa tumepoteza kiongozi shupavu, madhubuti, mzalendo, mwenye maono, mpenda maendeleo, mwana mwema wa bara la Afrika na mwanamapinduzi wa kweli. Mheshimiwa Magufuli alikuwa chachu ya mabadiliko. Kwa kweli, tumepwerea, kwa kuondokewa na kiongozi wetu huyu.”
Wachambuzi wa masuala ya kiutawala wanaamini kwamba hakuna kinachoweza kumkwamisha Mama Samia kuiongoza vizuri Tanzania kama atapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wenzake serikalini, kwenye chama chake cha CCM, wadau wa maendeleo na wananchi kwa ujumla.
Moja kati ya watu wanaoamini hivyo ni Jawadu Mohamed, mchambuzi huru wa masuala ya kisiasa kutokea Dar es Salaam, anayemuelezea Mama Samia kama mtu anayejua nini cha kufanya ili aweze kuendeleza kazi nzuri ya mtangulizi wake na kusahihisha makosa yaliyofanyika huko nyuma.
“Mimi nadhani licha ya kwamba anaweza kukabiliwa na changamoto kama mtangulizi wake, sioni kama ataweza kukwama kwani Rais hufanya kazi na viongozi na wananchi. Hivyo uwezekano wa kufanikiwa ni mkubwa na taifa litakwenda,” Mohamed aliieleza The Chanzo. “Ushirikiano kutoka kwa viongozi wenzake ni jambo la muhimu zaidi katika hili. Mimi sioni hatari kwa sababu watendaji ni wale wale.”
Katika vitu vilivyowafurashisha wengi ni hatua ya Rais Samia kuonesha utayari wa Serikali yake kuliunganisha taifa, kwa kuyaleta pamoja makundi kinzani mbalimbali ili yaunganishe nguvu katika ujenzi wa taifa. Hii ni hatua nzuri ukizingatia majeraha walionayo baadhi ya wananchi ambao wanadhani hawakutendewa haki katika utawala uliopita, wakiwemo viongozi wa vyama vya upinzani wanaodai kudhulumiwa katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Octoba 2020.
“Huu ni wakati wa kuzima tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa. Ni wakati wa kufarijiana, kuoneshana upendo, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na utanzania wetu,” alisema Rais Samia punde tu baada ya kuapishwa. “Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka, bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini. Siyo wakati wa kutazama yaliyopita, bali ni wakati wa kutazama yajayo. Siyo wakati wa kunyoosheana vidole, bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele.”
Aveline Kitomary ni mwandishi wa habari za kisiasa na maendeleo kutokea Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: avekitomary@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatlie, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.