The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Walalamikia Katazo la Kufanya Sherehe kwa Siku 21

Ingawa wameguswa na msiba wa Rais Magufuli, wakazi wa Dar es Salaam wanalalamikia athari zitokanazo na katazo la kufanya sherehe, wakisema linaathiri ratiba na uchumi wao. 

subscribe to our newsletter!

Stella Kasobe alitarajia kufunga ndoa Aprili 3, 2021, lakini shughuli hiyo haitafayika tena siku hiyo kutokana na amri ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Aboubakar Kunenge ya kukataza ufanyikaji wa sherehe za aina yoyote katika jiji hilo kuu la kibiashara nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya kuomboleza kifo cha aliyekuwa Rais wa tano wa Tanzania John Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena kutokana na matatizo ya moyo.

Akiongea na waandishi wa habari Machi 19, 2021, siku ambayo Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania, ikiwa ni siku mbili baada ya kifo cha Rais Magufuli, na kutangaza siku 21 za maombelezo — kuanzia Machi 17 hadi Aprili 7 — Kunenge alisema: “Nitoe agizo, katika siku 21 hizo [za maombolezo] hakuna sherehe yoyote itakayoruhusiwa kufanyika [ndani ya Dar es Salaam]. Sisi ni waungwana, tuheshimu mila na desturi zetu za Watanzania. Huu ni msiba mkubwa, hatuwezi kuona sherehe zikiendelea.”

Wakati wa mahojiano na The Chanzo, Stella, 28, amesema kwamba hatua hii imemuharibia mipango yake kwa kiwango kikubwa kwani kamati yake ya harusi ilishaandaa kila kitu, ikiwemo kulipia ukumbi, wapiga picha, mshereheshaji na mambo mengine.

“Na tukitaka kubadilisha tarehe tunaona kila tarehe inatukio na watu tuliowalipa wanaratiba zao,” anasema Stella kwa sauti inayoonesha kuchanganyikiwa. “Pia na sisi ni Waislamu, tulitaka tufunge ndoa kabla ya mfungo wa Ramadhani ambao unategemewa kuanza Aprili 13 au 14. Kusema kweli mpaka sasa sijajua hatima ya harusi yangu.”

Mkazi huyo wa Sinza Mori, Dar es Salaam, hajui ni lini ndoa yake itafungwa baada ya tarehe ya awali kughairishwa, huku akibainisha kwamba familia yake inaangalia taratibu zingine za kushughulika na kadhia hiyo.

Sherehe kukatishwa

Stella ni mmoja tu kati ya wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam ambao wameona shughuli zao za sherehe zikikatishwa kufuatia kifo cha hayati Rais Magufuli ambaye anatarajiwa kuzikwa Machi 26, 2021, nyumbani kwao Chato, mkoani Geita. Mbali na sherehe za harusi, minong’ono pia inasikika ikihoji hatma ya sherehe za Sikukuu ya Pasaka inayotarajiwa kufanyika Aprili 4, 2021.

“Hapana, nina uhakika [Kunenge] anazugumzia sherehe kubwa kama harusi nakadhalika,” alisema mkazi mmoja wa Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe na ambaye amepania kusherehekea Sikukuu ya Pasaka. “Watu watasali na kurudi nyumbani baada ya hapo hakurusiwi muziki, ni kula tu basii? Au nimeelewa vibaya? Kwenda beach hatuwezi kwenda? Au itakuwa nyumbani tu?”

Upendo Michael, pia mkazi wa Dar es Salaam aliyefunga kwa siku 40, alikuwa na haya ya kusema kuhusiana na katazo la Mkuu wa Mkoa Kunenge: “Ni muhimu kusherekea Pasaka kwa sababu tumefunga kwa siku 40 na siku hiyo Yesu anafufuka kwa hiyo hiyo ni sherehe kubwa ya furaha. Mimi naona turuhusiwe tu.”

Mmoja wa washereheshaji maarufa jijini Mickson Pettit, maarufu kama MC Pettit, amesema ameathiriwa sana kiuchumi na agizo la Mkuu wa Mkoa. MC Pettit ameileza The Chanzo kwamba kulikuwa na sherehe ambazo alipaswa kuhudhuria kama MC lakini imeshindikana kutokana na zuio hilo la sherehe. Kwa tarehe za sherehe hizo kupelekwa mbele, kumetokezea muingiliano wa sherehe kitu ambacho kinaathiri moja kwa moja kazi yake kwani kuna baadhi ya sherehe inabidi aachane nazo.

“Mfano mimi ninakuwa na sherehe moja kwa siku moja hivyo zinapokuja kuwa sherehe mbili kwa siku moja napata hasara na kwa sherehe nyingi nimeshapata malipo ya awali,” analalamika MC Pettit. “Mkuu wa Mkoa [Kunenge] angeruhusu sherehe ziendelee lakini kwa mfumo tofauti, kama vile kunyamaza kwa dakika kadhaa katikati ya sherehe kama ishara ya kuonesha heshima kwa hayati Rais Magufuli.”

Naye Haika Lawere ambaye ni msimamizi wa ukumbi wa sherehe wa Mbezi Garden, Dar es Salaam, amesema wamelazika kukosa mapato kutokana na siku za maombolezo. Anasema: “Kuna sherehe kama sita zimeahirishwa hapa na tayari tulishapokea fedha za awali wakisema wasogezewe mbele na hizo tarehe za mbele zina watu. Hivyo, mipango tayari imeharibika na hatuna la kufanya kwa sababu huu ni msiba wa kitaifa.”

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts