The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Miruzi Mingi Yamuweka Rais Samia Katika Njia Panda

Rais Samia anakabiliwa na changamoto za kukidhi matakwa ya makundi mbali mbali ya kijamii, kisiasa na kiraia. Wakati hawezi kukidhi matakwa ya kila kundi kwa kasi inayotakiwa na kundi husika, Rais Samia ana nafasi ya kuandika historia tofauti na ile ya mtangulizi wake.

subscribe to our newsletter!

Ukiacha tamaa za kibinadamu, sidhani kama kazi ya urais wa awamu ya sita, anayohudumu Mama Samia Suluhu Hassan ni ya kuonea wivu. Ni kazi ngumu inayokuja na changamoto nyingi hasa katika muktadha wa namna alivyoingia madarakani. Hivi sasa, Rais Samia anasikia miruzi  mingi ikiita na kumtaka afanye hili au lile. Miruzi yote hii inaakisi matarajio na matakwa ya makundi mbalimbali ya kijamii. Hata hivyo, hii si miruzi  ya kawaida inayosikika kila Rais aingiapo madarakani. Miruzi anayopigiwa Rais Samia, kwa mtazamo wangu,  inaakisi udharura wa urais wake na urithi wa taifa lililogawanyika aliloachiwa na mtangulizi wake, hayati John Magufuli.

Aina moja ya miruzi inayosikika kutoka kwenye mabaki ya kundi la hayati Magufuli lililomo ndani ya chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) ambalo lingependa kuona Rais Samia akikazia palepale alipoachia kiongozi huyo aliyefariki Machi 17, 2021, kutokana na changamoto za mfumo wa umeme wa moyo. Hawa wanataka urithi wa sera, mitazamo, na mbinu za kiutawala wa Magufuli zidumishwe – COVID-19 ipuuzwe, vyombo vya habari vibanwe, vyama vya siasa vikandamizwe, wanyonge washerehekewe, mabeberu wachuniwe na kadhalika. Kundi hili linaonekana kumchunga Rais Samia kwa ukaribu sana kuhakikisha kwamba hawi na huruma sana na hivyo kushindwa kufikia ndoto za hayati Magufuli aliyetawala kwa mkono wa chuma.

Humo humo ndani ya CCM, hata hivyo, kuna wakora waliotengwa na utawala wa Rais Magufuli, kitu kilichowafanya waonekane kama watoto wa kambo. Kundi hili linajumuisha wale waliofumwa wakimbagaza Rais Magufuli kwenye maongezi yao ya simu na kulazimika kutambaa hadi Ikulu kwenda kuomba msamaha. Walisamehewa lakini mustakbali wao kisiasa kwa miaka ya utawala wa Rais Magufuli ulishaandikwa kuwa watasota kwenye viti vya nyuma bungeni. Hawa, ambao wengi wao walikuwa karibu na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete, bila shaka wanataka Rais Samia aweke mazingira yatakayowawezesha kupata fursa ya kukua kisiasa kutokana na sifa na utendaji wao.

Kwa upande mwengine kuna vyama vya upinzani, ambavyo vimepata matumaini mapya vikiwa na madai lukuki – Katiba Mpya,  haki ya kufanya shughuli zao za kisiasa, uhuru wa vyombo vya habari, bunge lionyeswe moja kwa moja, kukoma mashambulizi ya watu wasiojulikana na uchunguzi wa matukio ya kupotea watu huko nyuma, kukomeshwa kwa vikosi kazi vinavyokusanya kodi kibabe pamoja na madai mengine mengi.

Wanaharakati nao, wengi wao wakiwa wamejikita mitandaoni, wana madai mengi mno yanayoakisi misimamo mikali, ikiwemo kutamani kuona anguko la wafuasi muhimu na wa karibu wa adui yao mkubwa Rais John Magufuli. Tayari wanaharakati hao, baadhi wanajulikana na wengine wasiojulikana, walishaanza kufurahia kuondolewa kwa Dk Bashiru Ali na Profesa Palamagamba Kabudi kutoka kwenye nafasi zenye ushawishi za Ukatibu Mkuu Kiongozi na Uwaziri wa Mambo ya Nje, sasa wanataka kichwa cha Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dotto James na wengine kadhaa! Kuna wanaharakati wa jinsia, au mafenisti kama wanavyojiita, ambao wamepinga kumuita Rais Samia ‘mama’ wakidai huko ni kudogosha ukuu wake na ni njama za kujenga na kumtundikia matarajio yasiyo sawa na yaliyowekwa kwa marais wanaume!

Urais Katika Nyakati za Kipekee

Wakati akieleemewa na matarajio haya makubwa, ikumbukwe kuwa urais wa Mama Samia sio wa kawaida. Ni madaraka yaliyomjia kidharura, ambayo wengine hawakutarajia kumdondokea. Rais Samia hakuchaguliwa kama rais katika Uchaguzi Mkuu.  Pia, kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe hakuwa na hata msukumo wa kutafuta umakamu urais, achilia mbali urais. Katika hotuba yake moja, Rais Samia anaelezea namna mwaka 2015 alivyoshtukizwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM na kuambiwa kuwa atakuwa mgombea mwenza, akakataa hadi akaangua kilio! Leo, mwanamama huyu ambaye bila shaka angetamani amalize tu miaka yake 10 ya umakamu, kisha akapumzike, anajikuta Ikulu!

Lakini kama hiyo haitoshi, Samia ni mwanamke, jambo ambalo linaleta shaka kwa wahafidhina wa mfumo dume. Wakati kuwa kwake makamu wa rais, ilionekana kama jaribio la ‘Je wataweza?’ sasa mara huyo yuko Ikulu akiwa na mamlaka ya juu kabisa! Kwa hiyo, Rais Samia ana kazi kubwa ya kukidhi matarajio ya makundi mbalimbali huku akijaribu kutengeneza urithi wake wa namna atakavyokumbukwa. Hii ni kutokana na ukweli kwamba njia aliyopitiaa kisiasa hadi kufika hapo, jinsia na asili yake, vyote vinaweka kiwingu cha shaka. Hata hivyo, kuna mambo mengi yanayombeba Rais Samia. Kwanza, ni uungwaji mkono mkubwa katika siku zake za mwanzo kutoka kwa makundi karibu yote  – ikiwemo vyama vya upinzani na wanaharakati, uungwaji mkono huo ni mtaji mkubwa sana kisiasa.

Lakini pengine faida kubwa aliyonayo Rais Samia ni kutanguliwa na kiongozi ambaye licha ya sifa nyingi anazopewa kwa miradi mikubwa mikubwa aliyoiacha kuna makosa makubwa pia ya kimkakati aliyafanya yaliyobomoa umoja wa kitaifa, kuchochea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kiraia na ustawi wa wananchi kwa ujumla. Kwa ufupi, ni rahisi mno kwa Rais Samia, kama atataka kufanya hivyo, kuvuna alama dhidi ya mtangulizi wake, hayati Rais Magufuli. Katika mambo ambayo angeweza kuyarekebisha haraka ni kutengua amri ambazo baadhi zilikuwa kinyume cha sheria na Katiba zilizozuia uhuru wa kufanya shughuli za siasa na uhuru wa vyombo vya habari. Mabadiliko pia yanahitajika katika mikakati ya mapambano dhidi ya janga la COVID-19 na katika marekebisho ya mifumo wa kodi na ukusanyaji wake. Kusema ukweli, linahitajika neno tu la Rais Samia kuweza kurekebisha kasoro hizi na kumfanya mwanamama huyo aonekane kama shujaa.

Mambo mawili ya jumla naweza kumshauri Rais Samia. Kwanza, asikubali kurithi ugomvi wa mtangulizi wake ili kuridhisha wahafidhina, wafuasi wa Umagufuli katika chama chake na wala asiegemee katika moja ya makundi niliyoyataja. Kama ambavyo ameleta salamu mpya za kitaifa, akiwasalimia wananchi wake kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vile vile Rais Samia ana nafasi ya kuleta mabadiliko muhimu ya kiuchumi na kisiasa huku akilinda na kuendeleza mema yaliyofanywa na mtangulizi wake kwa kuongozwa na maslahi mapana ya kitaifa badala na kikundi fulani. Hata hivyo, ni muhimu pia kuonya kwamba katika kufanya hayo, ni muhimu Rais Samia aende taratibu. Mifumo isiyo ya haki iliyojengwa kwa miaka mingi, haiondolewi kwa siku moja, labda kama Mama Samia anataka kufanya mapinduzi ambayo yenyewe yana gharama zake na ni kubwa sana.

Njonjo Mfaume ni mwandishi wa habari na mchambuzi wa masuala ya kisiasa. Kwa mrejesho, wasiliana naye kwa meseji kupitia 0735420780 au mfuatilie Twitter kupitia @njonjoOKAY. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelekezo zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *