Hoja za kupigania uhuru wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), maslahi ya mawakili pamoja na kutafsiri upya uhusiano wa taasisi hiyo na Serikali zimetawala ahadi za wagombea watano wa nafasi ya urais wa chama hicho ambao wanategemewa kupigiwa kura katika uchaguzi utakaofanyika siku ya Ijumaa, Aprili 16, 2021, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), jijini Arusha.
Huu utakuwa ni uchaguzi wa kwanza wa TLS tangu Bunge lipitishe mabadiliko kwenye Sheria ya TLS ambapo, pamoja na mambo mengine, yaliweka vikwazo kwa sifa ya uanachama wa Baraza la TLS; kuanzishwa kwa ukomo wa wajumbe wa baraza ambao utakuwa ni mihula miwili kila mwaka; kuanzishwa kwa utoaji wa hesabu na ripoti kuhusu TLS ambapo ripoti za ukaguzi, ripoti za mwaka na taarifa za mikutano mikuu zitatakiwa kupelekwa kwa waziri anayehusika na masuala ya sheria; pamoja na kuanzishwa kanuni zitakazotawala kazi za mkutano mkuu wa TLS ambao sasa hautajumuisha wanachama wote bali mahudhurio yatakuwa ya uwakilishi.
Wagombea watano waliojitojeza kuwania nafasi hiyo ya urais wa TLS ni Flaviana Charles aliyewahi kuwa makamu wa rais wa TLS 2014-2015, Dk Edward Hoseah aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Fransis Stolla aliyewahi kuwa Rais wa chama hicho mwaka 2012, Albert Msando na Shehzada Walli, wote wakiwa ni mawakili maarufu nchini.
Ikiwa ni siku nane tu zimebaki kuelekea uchaguzi, kampeni za kila mgombea zimepamba moto huku kila mgombea akieneza sera zake za nini ataifanyia TLS endapo kama atachaguliwa kuwa rais wa chama hicho cha kitaaluma. Wagombea hawa wamekuwa wakitumia njia mbali mbali za kusambaza ahadi zao ikiwemo matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii, hususan Twitter, ambako wanaamini wapiga kura wao wengi ndiko waliko.
Licha ya kwamba wagombea wako watano, uchaguzi wa mwaka huu wa TLS unaonesha kinyang’anyiro kipo baina ya mwanamama Flaviana Charles na Edward Hoseah, wagombea wawili ambao mpaka sasa kampeni zao zinaonekana kutawala majukwaa ya mitandao ya kijamii. Wawili hawa mpaka sasa ndiyo wagombea ambao wana uungwaji mkubwa sana hususani kutoka kwa watu wanaotumia mtandao wa kijamii wa Twitter.
Mazingira bora na salama kwa mawakili
Katika mahojiano maalumu na The Chanzo, mmoja wa washiriki katika kinyang’anyiro hicho cha urais wa TLS Flaviana Charles alibainisha kwamba moja kati ya ajenda zake kuu ni kuhakikisha wanasheria nchini Tanzania wanafanya kazi katika mazingira bora na salama pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha kwamba matawi ya TLS yaliyoanzishwa nchi nzima yanakuwa imara.
“Nilishawahi kuwa makamu wa Rais, hivyo naelewa vitu vingi,” Flaviana, mwenye Shahada ya Uzamili ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Conventry, Uingereza, anaiambia The Chanzo. “Kwanza, nitaunganisha wanasheria kushikamana kutatua changamoto zao, kusimamia ustawi wa sheria na natamani kuona wadau mbalimbali kushirikiana kuhakikisha utawala wa sheria [nchini Tanzania]. Nitaibua fursa kwa wanasheria ili waweze kunufaika na taaluma zao. Kuna wanasheria wachanga watapata watu wa kuwasaidia kuwaongoza na pia nitawahamasisha kujiunga na mifuko ya kijamii kama [Mfuko wa Bima ya] Afya.”
Endapo kama Flaviana Charles atachaguliwa kuwa Rais wa TLS, hatua hiyo itakifanya chama hicho kuwa na historia ya kuwahi kuwa na marais watatu wanawake tangu kuazishwa kwake mwaka 1954 na sheria ya Bunge, Sheria ya Jumuiya ya Wanasheria ya Tanganyika. Mpaka sasa Jaji Joaquine De Mello na wakili na mwanaharakati mashuhuri nchini Tanzania Fatma Karume ndiyo wanawake pekee waliowahi kuwa marais wa TLS. Jaji Joaquine aliiongoza TLS kati ya mwaka 2007 na 2008 wakati mwenzake Fatma akiwa rais wa chama hicho kati ya mwaka 2018 na 2019.
The Chanzo ilimuuliza Flaviana Charles anajisikiaje kuwa mgombea pekee mwanamke kwenye kinyang’anyiro cha urais wa TLS na anadhani ni changamoto gani atakabiliano nazo endapo kama atashinda kinyang’anyiro hicho.
“Inahitajika ujasiri na kujitoa kuona ni namna gani unaweza kuongoza wanasheria ambao ni zaidi ya 10,000,” alijibu Flaviana mwenye Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. “Hata hivyo, ni muhimu wanawake kuchukua hatua. Unajua nafasi ya urais ina changamoto zaidi kwa sababu ni nafasi ya juu zaidi katika taaluma ya sheria. Hivyo, kwa uthubutu wangu naweza kuwa na nafasi ya kutatua changamoto zilizopo kirahisi. Kikubwa ni kuchukua hatua na kutokuogopa kukosolewa unavyo take risk. Hivi ndivyo unavyokuwa na nafasi ya kufanikiwa. Naamini naweza kushinda, uwezo ninao na ushawishi pia.”
Kutoka TAKUKURU mpaka kugombea urais TLS
Kama wewe ni mtumiaji wa mtandao wa Twitter basi kuna uwezekano mkubwa sana kwamba tayari unamfahamu Dk Edward Hoseah, mgombea mwengine wa urais wa TLS, ambaye matangazo ya kumpigia kampeni bosi huyo wa zamani wa TAKUKURU yameenea katika mtandao huo. Ni mgombea aliyepata uungwaji muhimu mkono kutoka kwa aliyepata kuwa rais wa TLS kwa mwaka 2017 – 2018 Tundu Lissu, aliyemuelezea Dk Hoseah kama mtu “anayeweza kupaza sauti kuhusu taaluma [ya sheria] na utawala wa sheria.”
The Chanzo haikubahatika kumpata Dk Hoseah akisema amebanwa sana na ratiba za kampeni. Hata hivyo, akiongea na mwandishi Said Kubenea wa Mwanahalisi TV, Dk Hoseah, Daktari wa Falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kwamba anaamini anaweza kuwa rais bora wa TLS kuliko wapinzani wake kutokana na uzoefu mkubwa wa shughuli za utawala na masuala mengine ya usimamizi.
“Nagombea kwa sababu tatu,” Dk Hoseah alimwambia Kubenea. “Kwanza, ni haki yangu ya kidemokrasia, pili ninawiwa chama kinahitaji mtu mzoefu katika sehemu mbalimbali. Nimefanya kazi mahakamani lakini pia nimeshiriki katika shughuli nyingi za Bunge. Nina uzoefu wa kujua Bunge linafanyaje kazi. Hivyo, kwa nini nione vibaya kusaidia chama [cha TLS]?”
Mwandishi huyo wa Corruption in Tanzania: The Case for Circumstantial Evidence, kitabu kinachozungumzia nafasi ya ushahidi wa kimazingira katika uchunguzi na uendeshaji mashtaka wa kesi zinazohusiana na rushwa nchini Tanzania, anabainisha kwamba endapo kama atapewa ridhaa ya kuwa Rais wa TLS kitu cha kwanza ni kwamba atazingatia utawala wa sheria, kutetea wananchi na kushirikiana na Serikali. Anafafanua: “Pia, TLS inaangalia namna ya kuwekeza ili kujiendesha kiuchumi. Napendekeza, tayari tuna jengo la Wakili House, tunahitaji kujenga ukumbi mkubwa na pembeni mwake tuweke [nyumba za wageni] ambapo watu watalala tunaweza kukopa benki na tukawekeza.”
‘Uanaharakati’ wa TLS, uhuru wake na umoja wa mawakili
Naye Albert Msando, wakili maarufu nchini Tanzania anayeshiriki katika kinyang’anyiro hicho ameileza The Chanzo kwamba changamoto kubwa kwa sasa inayoikabili taasisi ya TLS ni uhusiano wake na Serikali, akisema kwamba uongozi wake, kama atapata nafasi ya kuiongoza taasisi hiyo, utalenga kuuboresha uhusiano huo kwa faida za chama na Serikali pia.
“Lazima tuliangalie hili suala la TLS kubaki kuwa chama cha kitaaluma na sio chama cha wanaharakati,” anasema Msando ambaye pia analenga kusimamia matumizi mazuri na yenye faida kwa wanasheria wachanga na wenye matatizo mbalimbali ambapo riba itakuwa nafuu. “Ni lazima itambulike kuwa TLS ipo kwa ajili ya kusaidia na kushauri na hata pale inapokosoa lengo lionekane kuwa ni jema na sio kuonekana kutumika. Hili nitalifanyia kazi endapo nitachangualiwa.”
Fransis Stolla, aliyewahi kuwa Rais wa chama hicho, ameieleza The Chanzo kwamba kinachohitajika kwa sasa ni kuifanya TLS kuwa huru akilenga kulifanikisha hilo kama atapata ridhaa ya wanachama wa TLS kuiongoza taasisi hiyo.
“Chama cha wanasheria ni nguzo muhimu katika [kuifanya] Mahakama kutenda haki. Mifumo iliyopo sasa inafifisha uhuru wa chama,” anasema Stolla. “Nitashawishi [pia] kuongeza kipindi cha uongozi angalu miaka miwili kuliko mmoja. [Miaka miwili] inatosha kwa utekelezaji na maboresho ya kanuni ndani ya chama kama fedha, rasilimali watu na kadhalika na kukusanya fedha chama kiweze kujimudu.”
Mgombea mwengine anayeshiriki katika kinyang’anyiro hicho ni Shehzada Walli, moja kati ya mawakili maarufu nchini Tanzania, ambaye kipaumbele chake kikubwa ni kuzingatia utawala wa sheria kwa kuleta mahasiano ya karibu kati ya TLS na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuleta chachu ya kuboresha sheria zinazoongoza nchi.
“Kingine ni kujenga umoja na ushirikiano kati yetu [mawakili]. Nitaondoa pengo kati ya mawakili wakongwe na mawakili wachanga, kuwezesha kanda za TLS kwa kuwainua mawakili kiutendaji na kupewa vifaa stahiki,” anasema Walli. “Nitatengeneza nafasi za uwekezaji kwa maendeleo ya TLS pamoja na fursa za uwekezaji ili kupunguza utitiri na mzigo wa ada kwa wanachama. Nikichaguliwa nitarejesha heshima ya TLS kwa kuangalia ajira za mawakili na viwango vya malipo ili mawakili wasiishi katika hali duni. Tutaweka utaratibu wa kufuatilia malipo stahiki, kutoa mikopo nafuu, kusaidia ofisi za mawakili wenye shida ya kifedha, na kuunda mfuko wa maafa.”
Utetezi maslahi ya wanasheria
Hardson Mchau ni mchambuzi wa masuala ya kisheria ambaye pia ni mwanachama wa TLS anayesema kwamba msimamo wa wanasheria kwa miaka 10 iliyopita ni kupata kiongozi ambaye anaweza kutetea maslahi ya wanasheria mbele ya Serikali. Mchau anadai kumekuwepo na migogoro pale ambapo haki za wakili zinakiukwa kwa maslahi ya Serikali hasa pale wakili anaposimamia kesi ambayo Serikali inamaslahi nayo.
“[Wakili] anakamatwa, anashtakiwa, anafanyiwa vitu visivyofaa [na] wengine wanazushiwa baada ya kutofautiana na kiongozi [wa Serikali],” Mchau anaieleza The Chanzo. “Pia kuna shida Serikali kuingilia baadhi ya mfumo wa uendeshaji wa chama cha wanasheria, kwa hiyo bado tunataka mtu mwenye uwezo wa kuiwekea Serikali mipaka. [Tunataka] kiongozi atakayetengeneza mfumo wa kuwasaidia mawakili pia. Katika kipindi cha miaka miwili na mitatu, kuna baadhi ya mawakili walishtakiwa kwa makosa yasiyo na dhamana na hawakuweza kutetewa.”
Aveline Kitomary ni mwandishi wa habari za kisiasa kutokea Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe: avekitomary@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii, au una wazo la habari ambalo ungependa tulifuatilie, au ni mwandishi wa habari wa kujitegemea unayetaka kuandikia The Chanzo, unaweza kuwasiliana na mhrariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maswali zaidi.