The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ripoti za CAG: Wadau Wahimiza Uwazi Matumizi Fedha za Umma

Wasema ubunifu usiwepo kwenye ukusanyaji wa mapato tu bali hata kwenye uwazi wa matumizi yake.

subscribe to our newsletter!

Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, watendaji wastaafu wa Serikali na wadau wengine wa masuala ya uwajibikaji serikalini wamesema kwamba ili Tanzania iweze kufanikiwa katika jitihada zake za kuondosha ubadhirifu wa fedha za umma ni lazima kuwepo na misingi imara itakayolazimisha shughuli zote za Serikali na idara zake kufanyika katika mazingira ya uwazi ili wananchi waweze kufuatilia matumizi ya kodi zao.

Wito huo unaendelea kutolewa ikiwa ni baada ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kicheere kutoa ripoti yake ya mwaka mnamo Aprili 8, 2021, ambayo pamoja na mambo mengine imefichua upotevu mkubwa wa fedha za umma na kuzua mjadala mpana miongoni mwa wananchi juu ya usalama na matumizi sahihi ya kodi zao.

Akiongea leo Jumamosi, Aprili 10, 2021, katika mhadhara uliondaliwa na Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro uliopewa jina la Ufisadi katika Sekta ya Umma: Inavyojidhihirisha, Wawezeshaji Wake na Namna ya Kukabiliana Nayo uliofanyika katika hotel ya New Afrika jijini Dar es Salaam CAG mstaafu Profesa Mussa Assad amesema kwamba kama ambavyo Serikali imeweka mifumo ya imara na ya kisasa, kama vile kutumia teknolojia ya kidijitali, kuboresha ukusanyaji wa mapato, mifumo hiyo hiyo itengenezwe itakayoonesha namna mapato hayo yanavyotumika.

“Sote tunapaswa kuridhika na kiwango cha ubunifu wa kidijitali [katika ukusanyaji wa mapato] ambao Serikali barani Afrika tumeona wakitekeleza siku za hivi karibuni,” alisema Profesa Assad ambaye aliondoka kwenye nafasi hiyo Novemba 5, 2019, katika mazingira yaliyozua mjadala mpana wakati huo. “[Hatua hii] Inaashiria uimara katika utendaji wao wa kazi. Hata hivyo, [ubunifu huu] ni muhimu uende mbali zaidi kuwawezesha wananchi kufahamu miamala ya kiserikali ili waweze kujua namna makusanyo haya yanavyotumika.”

Profesa Assad alisema wakati wa uwasilishaji wa mada yake kwamba kilichopo kwa sasa ni kwamba Serikali zinaonekana kuvutiwa na ubunifu wa kidijitali katika ukusanyaji tu wa mapato na wala siyo katika kuweka uwazi wa namna mapatao hayo yanavyotumika. Aliongeza: “Haitoshi tu [kwa Serikali] kusema tunatekeleza miradi ya kimkakati. Ni lazima miradi hii ipewe uhalali wa kiufundi, kifedha na kimazingira. [Usiri] huwafanya wananchi washuku kwamba kuna kitu wamefichwa na kwamba kuna watu wananufaika kibinafsi katika utekelezaji wa miradi hii.”

Ubadhirifu kila kona

Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2020, CAG Charles Kicheere, pamoja na mambo mengine mengi yaliyoshtua Watanzania, alibainisha kwamba jumla ya Sh2.157 trilioni hazikupita katika mfuko wa hazina, kinyume na Katiba ya nchi na sheria nyengine za nchi zinazoongoza matumizi sahihi ya fedha za Serikali.

CAG Kicheere pia amebaini kwamba kwa mwaka wa fedha 2019/2020, taasisi mbalimbali za umma zimefanya malipo yenye thamani ya Sh29.659 bilioni nje ya bajeti iliyotengwa na zaidi ya Sh15.129 bilioni zilitumika kwa manunuzi ya wizara na baadhi ya taasisi nje ya mpango wa manunuzi. Pia, CAG amebainisha kwamba kiasi cha Sh3.458 bilioni kilitumika kwenye manunuzi ya baadhi ya halmashauri, kiasi ambacho hakikujumuishwa kwenye mipango ya manunuzi ya mwaka husika ya halmashauri.

Ukaguzi maalum wa CAG katika Mamlaka ya Bandari (TPA) umebainisha ubadhirifu wa malipo ya Sh3.76 bilioni ambazo kati ya fedha hizo zaidi ya Sh2 bilioni zilitolewa bila hati ya malipo. Katika ukaguzi maalum uliofanyika katika halmshauri tisa za Nkasi, Buhigwe, Kakonko,  Tabora, Korogwe, Mbinga, Muheza, Longuido na Mvomero, CAG amebainisha kwamba kuna miamala ya thamani ya Sh614.505 milioni yenye viashiria vya udanganyifu. Miamala hii inajumuisha ile inayosababisha upotevu wa fedha za umma kwa njia ya malipo hewa, miamala isiyo ya kweli au ufujaji wa mapato yaliyokusanywa.

Umuhimu wa taasisi imara

Tundu Lissu, mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amesema kwamba kama kuna kitu kimoja ambacho ripoti za CAG zinabainisha ni umuhimu wa demokrasia katika ujenzi wa nchi.

“Tukitaka kudhibiti ufisadi, rushwa na uchafu [ulioibuliwa na ripoti ya CAG], tunahitaji vyama vya siasa imara, maana yake futa haya makatazo ya vyama vya siasa [kufanya kazi zao],” alisema Lissu jana Ijumaa, Aprili 9, 2021, wakati akiongea katika kipindi cha Cyber Lounge kinachoandaliwa na Nadj Media Center kupitia mtandao wa YouTube.

“[Pia], tunahitaji vyombo vya habari imara na vilivyo huru [pamoja na] uhuru wa jumla kwa wananchi tuweze kuzungumza tunapohitajika kufanya hivyo kwenye masuala muhimu ya nchi hii. Ni wakati muhimu sasa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuanzisha tena mchakato wa kutupatia Katiba Mpya ambayo inaweza ikatoa majibu kwa sehemu kubwa ya masuala haya,” alisema Lissu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema.

Rais Samia, hata hivyo, amesikika akisema kwamba wanaotaka Katiba Mpya “wasahau kidogo.

Naye Zitto Kabwe, Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, akiongea katika kipindi hicho hicho cha Cyber Lounge aligusia umuhimu wa ujenzi wa taasisi imara, akisema hatua hiyo ni muhimu kukabiliana na baadhi ya mambo yaliyoibuliwa na ripoti ya CAG kama ubadhirifu wa fedha za umma.

“Mimi naungana na watu wote ambao wanazungumza kuhusiana na suala zima la Katiba [Mpya],” amesema Zitto ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) wakati wa Bunge la 10.  “Kwa sababu Katiba [Mpya] ndiyo mwarobaini wa changamoto zote ambazo tunazo. Katiba Mpya itatuondolea matatizo yote haya [kwa kutuwezesha] kujenga taasisi imara.”

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *