Mheshimiwa Rais, licha ya uwepo wa misingi ya kitaasisi na kisheria katika uwanda wa haki jinai, bado kuna changamoto zinazotia doa suala la utoaji haki nchini. Barua hii inabainisha masuala machache ambayo kama yakifanyiwa kazi tutapunguza vilio vya haki na kuleta unafuu na ufanisi. Kwa hali ya sasa, kama alivyowahi kusema Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwamba: “hatuwezi kutatua matatizo yetu kwa kujidanganya kuwa hayapo,” nami nasema, matatizo yapo kama ambavyo nitafafanua hapa chini. Wito wangu ni kwamba tuyakubali na tujisahihishe.
Mheshimiwa Rais, katika uendeshaji wa mashitaka ya jinai, husuani makosa yasiyo na dhamana, Mahakama haina sauti yoyote zaidi ya kusikiliza upande wa mashitaka (Serikali) wanasema nini. Utamaduni huu umebarikiwa na sheria, husuani Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya Jinai (CPA). Lakini je, inapaswa kuwa hivi? Kwamba, pasi na mwongozo wa Serikali, Mahakama haiwezi kufanya lolote? Ukifungua kesi kukosoa mwenendo wa shauri lako, kwa mfano; tegemea ugumu katika shauri hilo. Kesi itaondolewa mahakamani, utakamatwa papo hapo na kushitakiwa kwa kesi hiyo hiyo. Kama ulishakaa miaka minne jela, utaanza upya kwa kuwa shauri ni jipya. Hivi ndivyo Mahakama inavyopokwa mamlaka na Serikali ambayo ni upande katika kesi. Kwa ujumla, kuna matumizi mabaya ya kanuni ya nolle prosequi.
Mahabusu mmoja aliyekaa gerezani kwa miaka 10 amekumbana na kadhia hii. Akiwa ameongea na mashahidi 19 wa Jamhuri, tayari kwa utetezi, kesi ikaondolewa mahakamani (nolle prosequi), akakamatwa papo hapo, akashitakiwa upya kwa kosa hilo hilo, Mahakama hiyo hiyo. Hadi sasa bado yupo gerezani akiambiwa upelelezi haujakamilika. Ukijiuliza upelelezi upi tena? Hupati jibu. Lakini hii ndiyo taswira ya jinsi mambo yanavyofanyika katika mnyororo wa haki jinai. Nafasi ya Mahakama? Sio kwa ubaya, ila ni sahihi kusema kwamba Mahakama haina mamlaka. Ni mgogoro wa kisheria? Labda! Lakini endapo Jamhuri ingetekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kusingekuwa na mateso kupitia Mahakama kwa watu wasio na hatia kama inavyofanyika sasa. Na kwa kuwa Mahakama ni chombo cha utoaji haki, inategemewa ifanye zaidi ya hiki kinachofanyika sasa hivi. Mahakama na taratibu za haki jinai zisitumike kama mhuri wa kuhalalisha mateso kwa watu wasio na hatia.
Mheshimiwa Rais, katika makosa yasiyo na dhamana, kazi pekee ya Mahakama ni kujiridhisha kama dhamana imezuiwa, kisha kuahirisha kesi kwa maelekezo ya Jamhuri. Wimbo huu unaweza kuimbwa kwa miaka mingi, kwa kadri Serikali itakavyoona vema. Kama kesi ni ya kubumba au yenye nia ovu, mtuhumiwa atakaa gerezani kwa muda unaowapendeza walioamuru iwe hivyo. Ni ajabu kwamba mateso haya kwa binadamu wenzetu yanahalalishwa na ukimya wa viongozi na wananchi.
Kuna vijana walishitakiwa wakiwa na umri kati ya miaka 12 na 14 (watoto wadogo). Kesi yao ilijaa danadana. Ilianzia Mahakama ya Watoto. Baadaye Mahakama Kuu. Iliondolewa mahakamani wakakamatwa na kushitakiwa upya zaidi ya mara mbili. Baadaye, wakiwa hatua ya kujitetea, Jamhuri ikakatia rufaa uamuzi mdogo wa kupokea nyaraka. Wakakaa mwaka na nusu bila kwenda Mahakamani wakisubiri kikao kusikiliza hiyo rufaa katika Mahakama ya Rufani. Baadaye, wakaletewa wito wa kwenda Mahakama Kuu tena. Kwahiyo, kikao cha Mahakama ya Rufani hakikufanyika. Muda ulipotea bure. Walipoitwa Mahakama Kuu katikati ya mwaka 2020, Serikali ikawasilisha ombi la kuondoa kesi Mahakamani (nolle prosequi) – baada ya miaka kumi ya kukaa gerezani bila hatia. Ikumbukwe kwamba, walishitakiwa wakiwa watoto wadogo. Wametumia utoto wao wote gerezani. Wamekosa huduma stahiki kwa mtoto: elimu na malezi. Wamepoteza malengo na matarajio yao. Wametumikia adhabu bila kutiwa hatiani. Jambo hili ni baya sana. Hakuna aliyenufaika na mateso hayo. Hata polisi na waendesha mashitaka hawanufaiki kwa vyovyote vile. Mfano huu ni mmoja kati ya mingi. Kwanini inashindikana kuchora mstari kati ya wahalifu na wasio na hatia, kila mtu apate stahiki yake?
Mheshimiwa Rais, ukiwauliza watu walioko magerezani leo wachague kati ya kuishi na kufa, kati ya kumi utapata angalau mmoja ambaye yuko tayari kupoteza maisha kwa kuwa haoni maana ya kuwa hai huku akipata mateso. Huu ndio uhalisia. Mateso wanayopitia hayamithiliki. Sababu ya mateso haya iko bayana. Kuna watumishi wa umma hawatimizi wajibu wao na hakuna anayejali, labda wewe utaliona hili. Mimi najiuliza, hivi kweli tuna utawala wa sheria nchini Tanzania? Ukiwa kizuizini ukauona upande wa pili wa sheria, utaona jinsi suala la haki za binadamu linavyopigwa danadana Tanzania. Kuna dhana miongoni mwa watumishi wa umma kwamba wimbo wa haki za binadamu tumeletewa. Hawako tayari kuuimba. Lakini je, ni kweli kwamba hatupaswi kuheshimu utu wa mtu? Unapojenga barabara, usipoitumia wewe, itawafaa hata majirani zako. Tendo lolote jema, kwa vyovyote vile, litamfaa mtu. Mfumo imara wa haki jinai utaleta unafuu na faida kwa taifa letu. Tuchukue hatua. Tutajikwamua kutoka hapa tulipo kwa kuwa na mgawanyo rasmi wa mamlaka. Serikali itimize wajibu wake. Kusiwe na upendeleo na uonevu. Mtu ashitakiwe kwa haki na kwa wakati. Mwenendo wa mashitaka udhibitiwe. Mahakama irejeshe(we) mamlaka yake kama chombo cha utoaji haki. Sheria zote zinazoleta ukakasi katika mnyororo wa haki jinai zifutwe. Hii ni kwa ajili yetu na vizazi vijavyo. Tunaweza kufanya vizuri zaidi ya sasa.
Kuhusu upelelezi usio na kikomo
Mheshimiwa Rais, upelelezi usio na kikomo kwa baadhi ya makosa ya jinai ni kero kubwa sana. Hata katika makosa yenye ukomo wa upelelezi, bado ni changamoto kutekeleza matakwa ya kisheria. Mahakama haifanyi vizuri katika hili. Kuna ukomo ila mtuhumiwa haachiwi kwa kuwa eti atakamatwa hapo hapo na kurudishwa upya mahakamani. Aibu gani hii? Hali ilivyo, ukamilishwaji wa upelelezi katika makosa yasiyodhaminika limeachwa mikononi mwa Serikali. Kwamba, ni hiyari yao kufanya upelelezi kwa muda watakaohitaji. Japo hii ni sawa kama mshukiwa hayuko kizuizini au hajashitakiwa, lakini mtu anaposhitakiwa, akatupwa gerezani kusubiri hatma yake, ukomo na udhibiti wa kimahakama katika upelelezi ulipaswa kuwa lazima. Sheria zetu zimeruhusu watu wachezee maisha ya binadamu wenzao kadri wanavyotaka.
Mheshimiwa Rais, ukiniuliza mimi kama tuna sababu ya kujikosoa kama taifa nitajibu ndio. Kushitaki kabla ya uchunguzi, au kuchelewesha upelelezi, ni jambo lisilokubalika katika jamii ya wastaarabu. Jamii zilizostaraabika huzingatia utu, haki na maslahi ya mtu wakati wa kushughulikia tuhuma dhidi yake. Mashitaka huja baada ya upelelezi. Kama ni uchunguzi, mshukiwa anahakikishiwa haki zote ikiwemo haki ya dhamana. Jambo hili yafaa lijumuishwe kwa vitendo katika mnyororo wa haki jinai nchini.
Mheshimiwa Rais, usikubali kila unachoambiwa, kwamba tunakwenda vizuri. Washukiwa wanakaa vituo vya polisi kwa zaidi ya mwezi mmoja na hili hautalikuta kwenye taarifa za mahabusu wanaolala vituo vya Polisi (occurence book). Wanajua wanavyofanya ili kupoteza kumbukumbu. Wapo watu waliokaa vituo vya polisi zaidi ya mwezi. Baadaye tena wakae gerezani miaka na miaka wakisubiri upelelezi ukamilike. Mtu aliyedaiwa kumteka tajiri Mohamed Dewij, alikaa Kituo cha Polisi zaidi ya mwezi mmoja. Na sasa yuko gerezani zaidi ya miaka miwili na upelelezi wa kesi yake haujakamilika. Ni hatari kuona haya yakifanyika chini ya uangalizi (na ukimya/idhini) wa viongozi wetu.
Mheshimiwa Rais, wapo ambao kesi zao zinasikilizwa. Lakini hawawezi kujihakikishia kupata haki kwa wakati. Mwenendo wa kesi nyingi hauridhishi. Kuna maahirisho yasiyo na msingi japo sheria inakataza. Mashahidi hupelekwa kwa kusuasua. Upande wa pili wa sheria (unaotokana na utashi wa Serikali) ni mchungu sana kuufahamu licha ya kuuishi. Upelelezi bila kikomo wala udhibiti wa mahakama ni hatari kwa mustakabali wa haki zetu. Mfumo wa “peleleza-kamata-shitaki” utasaidia kudhibiti matumizi mabaya ya mamlaka. Mifumo ya haki jinai, kwa sasa, inatumika kurasimisha mateso kwa watu wasio na hatia. Ikiamuriwa ushughulikiwe, ni moja kwa moja, hadi watesi wako watakapoona imetosha. Serikali inafaa ijikosoe, ifanye kwa ajili ya watu. Tubadilishe sheria zibebe dhana ya haki zaidi. Serikali ilenge kutenda haki, haki tu. Vilio vya haki visiposikilizwa ni hatari kwa ustawi wa Taifa. Umoja wa kitaifa ni kitendawili kama baadhi yetu wanafanywa mateka katika ardhi yao.
Kesi za kubumba, mashitaka ya hila
Mheshimiwa Rais, waathirika wa huu uonevu ni wengi zaidi ya wanaosikika. Katika kilichotajwa kuwa vita ya kiuchumi, vita ya madawa ya kulevya, vita dhidi ya wakosoaji wa Serikali ya awamu ya tano na wakati mwingine, chuki za wenye mamlaka dhidi ya watu wenye uhuru wa kiuchumi, wasomi na wenye fikra huru, yote kwa ujumla, yamesababisha lundo la mahabusu wenye kesi za kubumba wasio stahili kuwa gerezani. Wapo walioko uraiani kwa dhamana huku kesi zao zinaendelea.
Sipendi kumnyooshea mtu kidole. Lakini kwa nafasi yako una uwezo wa kutambua nani aliasisi na anaendeleza tabia hii chafu. Ofisi ya Mashitaka ya Taifa (NPS) na Jeshi la Polisi na idara nyingine ni washirika katika hili. Kuna task force ambazo zimeshamiri sana. Kukosekana kwa mgawanyo sahihi wa mamlaka na uendeshwaji wa ofisi hizi muhimu bila kujali taaluma, utu wala hofu kwa Mwenyezi Mungu kumechangia ongezeko la kesi za namna hii kwa miaka mitano iliyopita.
Mheshimiwa Rais, watu wa kada zote ikiwemo watumishi wa umma, wafanyabiashara, wasomi, wanaharakati na wanasiasa, wamekuwa waathirika wa mchezo huu mchafu dhidi ya ubinadamu na utu. Ninadhani kwamba kuna haja ya kurejea malalamiko lukuki yaliyowasilishwa na hawa watu – wao binafsi ama kupitia kwa Mawakili wao – katika ofisi mbalimbali ili kupata mwafaka. Ninashauri wapewe kipaumbele watu walioko magerezani na vizuizini kwa kuwa kukosa uhuru hata kwa dakika moja, ukijua huna hatia, ni mateso makubwa sana. Pia, kesi zote za kubumba na rekodi za jinai zenye mrengo huu zifutwe. Nafuu itolewe kwa wote walioporwa mali zao.
Mateso katika vituo vya polisi
Mheshimiwa Rais, watu wa Mungu wameteswa sana. Mateso yasiyomithilika. Sio lazima ikutokee ndio ukubaliane na mimi kwamba watu wanateswa. Mshirika wangu Mdude Nyagali, ambaye sasa analipa gharama ya kuikosoa Serikali yake, aliwahi kutoa ushuhuda wa mateso aliyopata akiwa mateka kizuizini mikononi mwa dola la awamu ya tano. Licha ya kwamba Mdude aliwataja watu na taasisi zilizoshiriki kumtesa, hakuna aliyechukuliwa hatua hadi sasa. Mateso yapo ni wakati mwafaka wa kujisahihisha.
Wapo watu wana ulemavu wa kudumu kutokana na vipigo wakiwa chini ya polisi. Idadi kubwa ya mahabusu walioko magerezani walikiri makosa yao wakiwa vituo vya polisi. Ilikuwaje? Walishughulikiwa. Polisi huwa wanahitaji uwape ushirikiano ambao kwao ni kusema kile wanachotaka kusikia, sio kile unachotakiwa kusema. Kazi ya uchunguzi haifanyiki kisayansi wala kitaalamu. Inafanyika kwa nyenzo za mateso. Unamminya mtu makende ili akiri kosa, halafu iweje? Wapo waliolazimika kukatwa uume kwa kuwa wakati wa mateso waliingiziwa “spoku” kwenye mrija wa mkojo katika uume, ikasababisha kansa ambayo hutegemei itibiwe kizuizini au gerezani.
Mheshimiwa Rais, zipo task force. Zimeundwaje, na kwa nini zinafanya majukumu ya kipolisi? Kwa wanaofahamu, maana ya task force ni mateso, mateso, mateso. Watu wameteswa sana na hivi vikundi. Hakuna sababu ya kuukimbia ukweli. Mjadala kuhusu task force upo tangu enzi wa Bunge la kumi na moja Mhe. Godbless Lema, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (CDM), aliwahi kuligusia na hivi karibuni katika Bunge la kumi na mbili, Mhe. Nape Nnauye, mbunge wa Mtama (CCM), amerudia suala hili. Ni mabavu, mabavu, mabavu. Usiingie kwenye 18 zao.
Mheshimiwa Rais, ili kuona ukubwa wa tatizo, na kwa minajili ya kujali, ni vema kuangalia upya suala la haki za mshukiwa chini ya polisi au mamlaka flani. Maandishi katika sheria zetu kuhusu taratibu za haki jinai kwa sasa ni sawa na gheresha tu. Kwamba na sisi tuna sheria. Ila utekelezaji wake, japo zote sio sheria nzuri, unategemeana na utashi. Kuna wakati Tanzania iliongozwa kwa kadri kiongozi anavyoamka. Haya mambo yalishuka hadi kwa watendaji wa chini. Ukiwa chini ya polisi au task force wenye nia ovu utaona kuwa uko mbali sana na sheria, mbali na dunia wanakoishi binadamu. Tujikosoe!
Makubaliano ya kukiri kosa, au plea bargain
Mheshimiwa Rais, kabla ya kutungwa kanuni za utekelezaji wa sheria ya “makubaliano ya kukiri kosa,” ilikuwa vigumu sana kuona utekelezaji wa sheria hiyo katika jicho la haki. Licha ya shabaha nzuri ya sheria hii, utekelezaji wake unaleta walakini. Sheria hii imekuwa mbadala wa upelelezi katika makosa ya uhujumu uchumi. Kwamba, ili umalize kesi, lipa fedha ondoka ukaendelee na shughuli nyingine. Wangapi wanamudu nafuu hii ya kinyonyaji?
Mheshimiwa Rais, pamoja na mambo mengine, ni muhimu kubainisha kwamba makubaliano hayafanyiki kwa hiari ya pande zote, hususani upande wa mshitakiwa ambaye anakuwa na njia moja tu ya kumaliza kesi yake – yaani kukiri kosa. Wakati mwingine, hakuna majadiliano na kama yatafanyika, basi ni geresha kwa kuwa mshitakiwa hupewa chaguo moja ambalo, hata hivyo, ataliafiki kutokana na mazingira aliyopo. Mawasiliano yanafanyika gizani. Hakuna vikao (rasmi) wala kumbukumbu za majadiliano kwa ajili ya rejea. Nafuu hii inategemea utashi wa waendesha mashitaka. Utatembea umbali mrefu kuipata. Rushwa katika zoezi hili haitajwi hadharani kwakuwa haupo ushahidi wa moja kwa moja, lakini je, hatuna sababu ya kuchunguza?
Mheshimiwa Rais, tunaweza kuboresha; zoezi lifanyike kwa uwazi na bila shuruti – angalau chini ya usimamizi wa taasisi huru kama Mahakama. Makubaliano yanayofanyika nje ya Mahakama na kusajiliwa Mahakamani upo uwezekano kuwa hayamaanishi kauli moja! Tujikosoe!
Makosa yote yawe na dhamana
Mheshimiwa Rais, ninaheshimu maamuzi ya Mahakama ya Rufani ya hivi karibuni kuhusu suala la dhamana, kwamba zuio la dhamana liendelee kuwepo kwa baadhi ya makosa. Lakini ni maoni yangu kwamba bado tunahitaji mjadala na mwafaka juu ya suala hili. Kuna haja ya kuwekeza jitihada kung’amua namna ya kudhibiti utolewaji dhamana kuliko kujielekeza kuzuia dhamana. Mahabusu ni wengi magerezani kuliko wafungwa. Kwa nini? Wamenyimwa dhamana, upelelezi na uendeshaji wa kesi unachukua muda mrefu, miaka hadi miaka. Ninapendekeza kwamba uamuzi wa kuruhusu ama kuzuia dhamana uwe wa Mahakama kuingana na mazingira ya kesi husika. Tuondokane na sheria inayozuia dhamana na kuondoa nafasi ya Mahakama. Kuamua haki, wajibu na maslahi ya mtu iwe kazi ya Mahakama sawa na Ibara ya 13(3) na 107 A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ukuu wa Katiba unabakia kwenye maandishi kama kuna sheria zinazokinzana na Katiba – kama hii ya kuzuia dhamana kwa nasibu bila utaratibu na bado zinatumika. Majirani zetu Zanzibar, Kenya, Uganda wameondokana na utaratibu huu usiofaa.
Mheshimiwa Rais, kwa upande mwingine, ruksa ya dhamana kwa watuhumiwa itaondoa mashitaka ya hila, kama yale ya “mchagulieni kosa lisilo na dhamana akakae jela.” Itadhibiti rushwa na urasimu, itapunguza msongamano magerezani, itatilia mkazo dhana ya ukuu wa Katiba na Kanuni zake, mathalani: “mtuhumiwa kutokuwa na hatia hadi ithibitishwe, mgawanyo wa mamlaka na uhuru wa mahakama,” na kudhibiti upelelezi.
Mheshimiwa Rais, kwa sasa, idadi ya mahabusu inatumika kama kiashiria kuonesha utendaji kazi wa watu flani. Lakini je, idadi ya mahabusu inaendana na idadi ya kesi zinazokamilika kwa mwaka? Wangapi wanakutwa na hatia? Wangapi wanaachiwa? Majibu ya maswali haya yanachukiza! Kiwango cha watu wanaoteswa bila hatia kiko juu sana. Watu waliokaa mwaka na zaidi gerezani ni wengi kuliko wenye siku moja hadi miezi sita. Hii sio sawa.
Mheshimiwa Rais, kauli za hivi karibuni za Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma na wadau wa haki jinai kuhusu dhamana zinaashiria hitaji la mwafaka mpya. Kwa kuwa, kwa sababu zinazotabirika, imeshindikana kutengua sheria kandamizi inayozuia dhamana kupitia Mahakama, ninaishauri Serikali kuiangalia upya kwa manufaa yetu sote. Ninaamini kwamba inawezekana watuhumiwa kupewa dhamana kwa udhibiti na uangalizi wa mahakama – kama inavyofanyika Zanzibar, Kenya na Uganda. Tubadili sheria hii.
Mahakama mtandao
Mheshimiwa Rais, Mahakama ya Tanzania imeanza kutoa huduma kwa kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Mfumo huu uliokuwa katika majaribio, umetumika zaidi wakati wa janga la COVID-19, tangu Machi, 2020. Shabaha ni kurahisisha ufikiwaji wa huduma za kimahakama. Mahakama, kwa bahati mbaya, imerasimisha matumizi ya TEHAMA bila maandalizi stahiki. Mahakama (na Wizara ya Sheria), kwa ujivuni, imetaja mfumo huu kama sehemu ya mafanikio yake.
Wakati Mahakama ikijipongeza kuendesha mashauri kupitia mtandao, wapo wanaoihesabu hatua hiyo kuwa ni uongo, dharau na kutokuheshimiana. Uongo kwa umma, dharau na kukosewa heshima kwa mahabusu. Kwa nini? Kwa sababu Mahakama Mtandao inafanya kazi ya kuahirisha kesi – mara nyingine kwa Hakimu mmoja au karani, ajabu! Hakuna uhakika wa kuonana na hakimu au mwendesha mashitaka wako. Umeme au mtandao vikifeli, siku imeisha, rudi baada ya siku 14. Siku 14 baadaye, una uhakika wa kukutana na hali ileile uliyoiacha.
Mheshimiwa Rais, maboresho – utayari, fedha na maarifa – yanahitajika ili mfumo huu ulete nafuu na ufanisi uliokusudiwa. Miundombinu (majengo na vifaa) ya Mahakama na Magereza iboreshwa kukidhi mahitaji ya teknolojia. Magereza wana unafuu hawapeleki mahabusu mahakamani hususan Mahakama ya Mkoa wa Dar, Kisutu. Lakini athari za mfumo huu kwa mahabusu ni kubwa. Wanakaa gerezani bila mawasiliano na Mahakama kwa muda mrefu. Ikitokea mahabusu akateswa, hana mahali pa kukimbilia. Ufuatiliaji wa kesi pia unakuwa mgumu. Kurasimisha mfumo sio jambo baya. Lakini urasimishaji uendane na mahitaji ya walaji.
Watoto, watu wenye ulemavu na wageni
Mheshimiwa Rais, licha ya uwepo wa mahabusu na mahakama za watoto, si ajabu kukuta watoto wadogo katika magereza ya watu wazima. Tabia wanazojifunza haziwasaidii. Wanakosa elimu, malezi na hifadhi ya jamii. Chakula na matibabu duni ni hatari kwao. Watoto ni waathirika wa ulawiti magerezani – japo haitatokea upewe taarifa rasmi. Ninakusihi, mulika eneo hili, tujali watoto wetu.
Mheshimiwa Rais, mahabusu wenye matatizo ya afya ya akili wapo wengi magerezani japo wanapaswa kuwa hospitali. Mtu anayekula magazeti, au kinyesi, au kula jalalani, anakaa gerezani ili iweje, kwa faida ya nani? Wanateseka na kuathirika zaidi. Wanafungiwa vyumba vya peke yao bila uangalizi makhsusi. Wanalazimika kusubiri upelelezi ukamilike mwaka hadi mwaka. Uelewa wa kawaida ni kwamba wanahitaji huduma kabla ya kushitakiwa. Polisi na Ofisi ya Mashitaka warejee mashauri ya watu hawa, hatua stahiki zichukuliwe. Heshima na utu wao ni vema vikalindwa.
Wageni, tabaka la wakimbizi na watafuta hifadhi, japo miongoni mwao kuna wenye sifa za kutamkwa kuwa wahalifu, wapo pia wasio na hatia. watu hawa, kwa ujumla, wanapokamatwa hutupwa vituo vya polisi (mbele ya kamera) na kuitwa wahamiaji haramu, kisha katika mazingira ya hofu na ugeni, wasiweze kujitetea, hutupwa gerezani. Ni vema kuchunguza kesi za namna hii ili watafuta hifadhi, wasiostahili mateso na adhabu, wabainike na wapewe nafuu wanayostahili.
Mheshimiwa Rais, wanawake magerezani wana mahitaji makhsusi ambayo hawaruhusiwi kuyapata. Marufuku ya taulo za kike, kwa mfano, ni kitendo cha kikoloni na kikatili sana dhidi ya utu wa mwanamke. Wenye ulemavu, watoto au ujauzito, wako hatarini kwa kuwa, kwa vyovyote vile, mazingira ya gerezani hayawezi kumfaa mtu wa hali hiyo. Miundombinu na huduma za jamii ziboreshwe kukidhi mahitaji makhsusi ya wanawake.
Hali ya magereza yetu
Mheshimiwa Rais, zipo sheria za kikoloni zinazoninyima haki ya kukuambia yafuatayo. Lakini nalazimika kukusimulia, na moja ya ombi langu ni kufutwa sheria hizo. Ni imani yangu kwamba mazungumzo haya hayatahesabika kama uchochezi kwakuwa sina nia ovu. Mahabusu magerezani kwa sehemu kubwa hawaishi kwa kufuata sheria bali amri na maelekezo ya siku kwa siku ya askari magereza – hata kama hayatokani na sheria, na si ya haki. Ukipata nafasi ya kuwasikiliza mahabusu ambao sasa ni zaidi ya elfu kumi magerezani, utasikia mengi. Ukaguzi magerezani ni zoezi linaoacha maumivu makubwa kwa mahabusu. Licha ya shabaha njema, kubaini vitu visivyohitajika, askari magereza hugeuza zoezi hili kama nyenzo ya mateso kwa watu wasio na silaha, na hawawezi kupambana. Ukaguzi upo wa aina mbili. Mosi, mahabusu wanaporudi kutoka mahakamani ama kushukiwa kuwa na kitu visivyohitajika – kilevi, fedha au silaha – hukaguliwa. Pili, kaguzi maalum chini ya askari magereza (wa kikosi maalum).
Mheshimiwa Rais, upekuzi si hoja lakini utekelezaji wake ndio tatizo. Ni ukoloni, ukatili, na tishio dhidi ya utu wa mtu. Mahabusu, bila kujali umri, wanavuliwa nguo ili wapekuliwe. “Vua nguo, ruka kichura, kohoa, chuchumaa, simama juu.. chini,” ni maelekezo yanayozingatiwa katika upekuzi. Ukisikia “niletee kinyesi chako,” utatakiwa ukajisaide kwenye ndoo ulete ushahidi kuonesha hujabeba kitu tumboni. Ndoo moja inatumiwa na mahabusu wangapi? Ni aibu! Udhalilishaji katika zoezi hili haumithiliki. Hakuna faragha. Ni wapi, duniani, penye wastaarabu, ambapo huu mfumo wa kifedhuli bado unatumika? Heshima kwa utu wa mtu imekuwa hiyari badala ya sheria.
Mheshimiwa Rais, askari magereza wa kikosi maalum, hawa usiombe wafanye ukaguzi. Ni kama nyuki wamekuvaa. Ukisikia filimbi, lala chini subiri kuvua nguo, kipigo, matusi na kila aina ya mateso watakayokuchagulia, kwa nyenzo wanazotaka. Hufuatiwa na uharibifu wa vyakula, nyaraka na mali za mahabusu. Wasipokunywa, basi kwa nadra sana watamwaga soda, maji, au maziwa – mali za mahabusu, bila sababu. CCTV camera za magerezani zina kumbukumbu ya matukio haya ya kinyama.
Lakini je, upekuzi huu ni sahihi? Tumepita hapa au pale penye ukaguzi wa hali ya juu. Lakini sikumbuki ulazima wa kuvua nguo, kupigwa, kuteswa na kuharibiwa mali katika upekuzi. Wanachofanya askari kwa mahabusu ni ukatili na jinai. Kero hii itatuliwe haraka. Askari magereza wakumbushwe kwamba mahabusu sio wahalifu na kwamba hata wahalifu wanatekeleza adhabu kwa mujibu wa sheria. Kiwango cha uvunjifu wa sheria magerezani kiko juu sana.
Mheshimiwa Rais, huduma duni za afya ni tatizo sugu. Ninakushauri uweke kipaumbele cha huduma za afya kwa mahabusu. Ni binadamu wenzetu ambao hawajatamkwa kuwa wahalifu. Na hata kama wangekuwa wafungwa, bado wana stahiki zao kama binadamu. Huduma duni na mazingira yasiyoakisi afya ni hatari kwa maisha ya binadamu. Dawa na vipimo ni lazima viwepo wakati wote. Malazi duni yanayosababishwa na msongamano wa mahabusu magerezani ni kero isiyo ngeni masikioni na midomoni mwa viongozi wa juu zaidi wa nchi hii. Kama gereza lililokusudiwa kuhifadhi mahabusu 800 linabeba mahabusu zaidi ya 2000, jiulize hali ikoje. Msongamano unatisha. Kwenye magereza mengi, godoro jembamba la futi tatu kwa sita linalaliwa na mahabusu zaidi ya wawili. Wanalalaje? Ndio maisha tuliowachagulia, na bado sio wahalifu. Msongamano utapungua kwa kuruhusu dhamana, kufuta kesi za hila, na kupeleleza na kusikiliza kesi kwa wakati. Haya yote yako ndani ya uwezo wa Serikali unayoiongoza.
Wito
Mheshimiwa Rais, kwa kuwa tulikubaliana kuwa jamii ya watu wastaarabu, tunalazimika kutumia mifumo rasmi kuendesha maisha yetu ya siku kwa siku. Ni kwa mantiki hii hii, utendaji usioridhisha wa mamlaka za Serikali unaathiri haki, wajibu na maslahi ya watu. Katika barua hii, angalau kwa kila hoja, nimebainisha nini kifanyike. Kwa kuwa unaweza kuona mbali, ninakusihi uitikie wito wangu kwa haraka ili kunusuru hali za mahabusu wa sasa na watarajiwa.
Katika kushughulikia tuhuma zozote za jinai, sheria zizingatiwe. Aidha, zipo sheria mbovu. Ninashauri zifanyiwe marekebisho kwa manufaa yetu sote kama taifa. Ondoa mamlaka mikononi mwa watu kwa kuwezesha taasisi zifanye kazi kwa ufanisi, zitathminiwe na kufuatiliwa. Utendaji kazi wa polisi, katika eneo hili hauridhishi. Polisi (DCI) wakikwama usitarajie ufanisi kwa Ofisi ya Mashitaka ya Umma (DPP). Dhibiti rushwa katika mnyororo wa haki jinai. Ondoa muingiliano wa kimamlaka unaojitokeza kati ya Mahakama na Serikali. Zuia maelekezo ya Serikali kwa Mahakama. Mahakama huru ni muarobaini wa mambo mengi.
Mungu ibariki Tanzania.
Tito Magoti ni mwanaharakati wa haki za binadamu, anayeishi Dar es Salaam, Tanzania. Kwa maoni, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni titomagoti@gmail.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupitia @TitoMagoti. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa masuali zaidi.
30 responses
Mfumo wa haki tanzania bado una element za enzi za ukoloni zenye lengi moja tu la kuutweza utu wa mwafrika, tusipoamua kwa makusudi kuubadili mfumo wote tutabaki nyuma tukifanya kazin za mabeberu bila wenyewe kujua.
Jambo la msingi la kufanya ili kuubadili mfumo wetu ni kuanza na kuubadili katiba yeti ya sasa.
Mungu akutunze rafiki yangu, pia pole sana kwa mikiki uliyoipitia ndani ya miaka 6 iliyopita. Nikutie moyo kuwa Mungu hawezi kumwacha mwenye haki wake ateseke
Mfumo wa Haki Tanzania hakika unahitaji reformation kubwa. Haki za watu zinaminywa Sana kupitia sheria na kanuni kandamizi. Utu wa mtu kwa sasa hauna thamani. Ni aibu mshukiwa kutumikia adhabu kabla ya mahakama kuhukumu.
Kaka pole kwa uliyopitia pamoja na watanzania wengine, sauti hii ni ishara ya ukumbozi kwa jambo fulani, lakin mengi umesema na naamin wewe sio wa kwanza kushuhudia hya wapo na wengne, tusubiri tuone kama sikio la kufa litasikia dawa!
Tafadhali MAMA tunakuomba usome barua hii😭😭😭😭😭
Asante Tito kwa kujitoa kutetea haki za binadamu. Nimependa umegusia mengi ninayoyafahamu kuhusu mahabusu. Naamini mheshimiwa Raisi kama mama atayasikiliza na kuyafanyia kazi. Hii ni njia kubwa sana ya kupata thawabu hapa duniani na mbinguni pia.
Maana kama familia za mahabusu tumepitia na tumeona mengi. Mama naamini umekuja kutukomboa katika hili. Watoto wangu hasa yule aliyezaliwa baba yake akiwa gerezani huniuliza mama kwanini baba alituacha. Naishia kugubikwa na machozi. Miaka mitano na mwezi mmoja sasa.Mtoto amezaliwa ameanza shule hadi anajua kusoma sasa baba yake yuko gerezani. Eti ni mahabusu, hata kosa sijawahi kuliona mpaka leo. Mungu ibariki Tanzania
Sioni mtu ambae ana utu, huruma na anae heshimu haki za wengine kuona kilichoandikwa humo hakina maana. Ni uchungu uliopitiliza kuona yanayofanyika yanafanywa na watu wale wale tunaoishi pamoja kama ndugu. Matumizi mabaya ya ofisi, rushwa na ukomoaji vinaua haki msingi za watu wengi na kwa jinsi hiyo chuki, huzuni na msongo wa mawazo unaozalishwa kwenye maisha ya WATANZANIA hawa au pengine mimi mwenyewe hayana afya na lengo la kuijenga jamii bora yenye kuheshimu sheria na kuzilinda.
Kama hujawahi Kukaa huko maabusu unaweza kudhani yanayoandikwa ni uzushi… .nimekaa miezi minne maabusu, hao task force ni wanyama sio watu……
Huu ndio ukweli na Uhalisia wa nchi inavyopelekwa na wenye SAUTI badala ya kufuata SHERIA na KANUNI.
Ahsante sana Tito kwa kuyaanika haya ambayo yamkini wengi wanayapitia lakini wanakosa pakuyasemea. Kwa barua hii imedhirisha ni kwa kiasi gani utawala wa sheria na haki za binadamu hauzingatiwi na cha kusikitisha zaidi kuna watu wako juu ya sheria wakitumia vyeo na nyadhifa walizo nazo kukandamiza na kudhalilisha watu wasio na hatia.
Mungu akuongezee hekima zaidi na zaidi, kama mtanzania najivunia uwepo wako kaka. Asante kwa kuipaza sauti yako juu ya mfumo wa haki👏
Barua imejaa vilio vya kudai haki za watuhumiwa, mahabusu na wafungwa ninaimani vilio hivi vitamfikia Mhe.Rais na atachukua hatua “Haki huinua taifa” Mithali 14:34
I have read word to word and my head is still spinning. The scope of the problem goes deeper beyond my imagination and i think you are the most accurate and capable voice to speak on this matter and i pray this message does not land on deaf ears for the sake of our nation. Be blessed brother
Dah nimesoma nimesoma nimesononeka sana ahsante kwa barua hii najua vile watu wanavyoumia mungu awafanyie wepesi
Tito pole kwa yaliyokukuta Mungu wetu yu mwema sana unaandika kutoka kwenye eneo la mapambano sio hadithi umeyaishi,napata hisia kwamba ilibidi upitishwe njia hiyo ili dunia ijue kilichopo chini ya carpet,wewe ni mshindi kalamu yako itaokoa wengi,Naiona siku mpya haya nayo yatapita..
Tunahitaji watetezi, Activists kama were Tito come on brother
kweli ukitaka kujua utamu wa ngoma ingia kati ucheze, niliwahi kukamatwa na polisi wa doria bila kujua kosa langu waliomba rushwa waniachie, sikuwapa niliwaambia nazijua haki zangu wakachukia tukiwa njiani kuelekea kituoni wakawa wanaulizana wanipe kosa gani, wakaambizana huyu tutampiga pesa ya dhamana hachomoki, nakumbuka tulivofika kituoni nilikula kichapo kama jambazi, kile kichapo nilishindwa kutembea wiki nzima damu iliganda baadhi ya sehemu za mwili, nina makovu hadi leo, yaani hua najiuliza ningekua nakosa kweli sijui ingekuaje, hua nasema wale jamaa wasipoenda jehanamu lazima kuni zitakua zimeisha au moto umezimwa huko kwenye haki, sheria zimewapa mpenyo wakubabimbikiza watu kesi na kunyanyasa watu huru,haiwezekani polisi wakamate watu na wafanye upelelezi wao wenyewe, kweli Mh. Samia Suluhu hassan tusaidie, usije ukaulizwa mbele za haki ulifanya nini kuondoa mateso kwenye huu mfumo wetu wa hovyo kweli kweli wa utoaji haki.
Pole mzee
😢😢😢 Kuna Watu mbele ya Mungu sijui watajibu nini, Mungu Ilegeze mioyo yao migumu Amina
Daah! Maandishi kutoka moyoni kabisa.
Mungu mwema wakati wote, kwa pamoja tuendelee kupaza sauti.
Hongera tito nimesoma hili andiko hakika kuna uozo mkubwa sana unafanyika ktk magereza as if c binadamu wenzao wanaowafanyia hayo cc sote ni waja na hakika kwake tutarejea ya nn kufanya ushenzi km huo kwa mwanadamu mwenzako?
MWENYEZI MUNGU HALALI WALA HASINZII TUENDELEE KUOMBA HAYA YOTE YANA MWISHO.
Hi Tito
Hsante kwa kuwa sauti ya Watanzania na Wageni wanao onewa,na kunyimwa haki zao
Inaumiza Sana .
( Mtendee binadamu mwenzako kama unavyo taka kutendewa wewe )
Mungu anaona,anasikia,anajua kilakitu ambacho kiko chini ya jua.
Habakkuk 1 : 13 Why are you silent while the wicked swallow up those more righteous than themselves.
Mika 7 : 3 Wote ni mabingwa wa kutenda maovu, viongozi na mahakimu hutaka rushwa, wakubwa huonyesha wazi wazi nia zao mbaya na kufanya hila kuzitekeleza.
Hosea 4 : 6 Mungu anasema hivi watu wangu wanaangamia Kwa kukosa maarifa / kukosa viongozi waadilifu, na wenyekuheshimu Utu wa watu,kukosa hurumu,na Zaidi ya yote kutokuwa na hofu ya Mungu.
Haya yote yanafanyika kwa maslahi ya nani? Inasikitisha sana kuishi katika unyama wa hali hii.
Umenena hakika! Ujumbe utasomwa na kufika kunako stahili!
Ahsante sana Tito kwa kuyaanika haya ambayo yamkini wengi wanayapitia lakini wanakosa pakuyasemea. Kwa barua hii imedhirisha ni kwa kiasi gani utawala wa sheria na haki za binadamu hauzingatiwi na cha kusikitisha zaidi kuna watu wako juu ya sheria wakitumia vyeo na nyadhifa walizo nazo kukandamiza na kudhalilisha watu wasio na hatia.
Katiba mpya na bora ni sasa mifumo yote imeoza ni kufumua na kuanza upya
Hii barua ningeiona kabla ya submission za vielelezo tungeiweka kama kielelezo.
So narrative and composed. Big up folk.
Kongole sana Ndugu Yangu Tito Barua hii it Marked the Point in our struggle history for Katiba Mpya na ustawi wa sheria na haki nchini.História itakukumbuka.