The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Rais Samia Ingilia Kati Uvunjifu wa Katiba Unaofanywa na Spika Ndugai

Ni kuhusu hatua ya Spika Ndugai kuruhusu uwepo wa wabunge waliotokana na CHADEMA licha ya chama hicho kutangaza kuwavua uanachama wawakilishi hao.

subscribe to our newsletter!

Mheshimiwa Rais, mimi Ponsian Baitatafe,  mkazi wa kijiji cha Kasharunga, Kata ya Kasharunga, Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera, nakuandikia rasmi kueleza duku duku langu juu ya Spika wa Bunge Job Ndugai ambaye licha ya kula kiapo cha uaminifu cha kuilinda, kuihifadhi, na kuitetea Katiba ya Tanzania ameshindwa kutimiza jukumu hilo kwa kuwaacha wabunge 19 wasio na chama kilichowapeleka bungeni kuendelea kushiriki shughuli za mhimili huo unaohusika na utungaji wa sheria za nchi.

Mheshimiwa Rais, mimi raia wa kawaida na raia wengine tutawaelewa vipi tunapoona Katiba ya nchi  inakanyagwa kanyagwa mbele ya macho ya viongozi ambao licha ya kuiona hali hiyo wanashindwa kuchukua hatua yoyote?  Je, mliapa kuilinda Katiba isinyeshewe na mvua au isiliwe na mchwa? Vijana na watu wengine watajifunza nini kupitia kitendo hiki cha Spika Ndugai ambaye ameamua kwa makusudi kuvunja Katiba ya nchi na sheria nyengine za nchi, huku kukiwa hakuna yoyote anayemkemea, hata chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM), kikimuangalia tu?

Mheshimiwa Rais, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, mnamo Mei, 11, 2020, Spika wa Bunge la 12 Job Ndugai, alivunja na kukanyaga  Katiba ya nchi yetu kwa kuamua kuwarejesha bungeni wabunge walioadhibiwa na chama cha upinzani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kile chama hicho kiliita ‘utovu wa maadili’ na kupelekea kuvuliwa nafasi zao za uongozi na uanachama wao pia ndani ya chama hicho. CHADEMA kilimjulisha Spika Ndugai kwamba David Silinde, Peter Lijualikali, Joseph Selasini na Wilfred Rwakatare kuwa siyo wanachama wa chama hicho tena. Lakini Spika Ndugai akadharau hatua hiyo ya CHADEMA na kuwarejesha watu hao bungeni.

Mheshimiwa Rais, CHADEMA siyo chama cha kwanza cha siasa kuvua wanachama wake uanachama na hatua hiyo kuathiri nafasi za watu hao waliokua bungeni. Kitendo kama hiki kilifanywa na CCM mnamo Machi 17, 2017, pale kilipomvua uanachama aliyekuwa mbunge wa viti maalumu Sofia  Iddi Simba na kupeleka taarifa kwa Spika Ndugai ambaye haraka hara alisoma barua hiyo bungeni, akisema kwamba kwa mjibu wa ibara ya 71(1)(f) ya Katiba, Sofia Iddi Simba hakuwa mbunge tena kufuatia hatua hiyo iliyochukuliwa na chama chake.

Halima Mdee na wenzake

Mheshimiwa Rais, lakini suala jengine linalomwonesha Spika Ndugai kama mtu ambaye hayuko tayari kuongoza kwa kufuata Katiba linahusu hawa wanaoitwa Wabunge wa Viti Maalumu 19 wakiongozwa na  Halima Mdee. Kama utakuwa umefuatilia kwa karibu sakata hili, utakuwa unafahamu kwamba kupatikana kwa wawikilishi hawa kulileta utata, ambapo chama chao cha CHADEMA kilikanusha kuwa hakijawahi kuteua Wabunge Viti Maalumu. CHADEMA ikaenda mbali zaidi kwa kusema kwamba baadhi ya hao wanachama 19 ni wajumbe katika vikao na kutakiwa waseme ni lini chama kiliitisha mkutano wa kupitisha majina yao. CHADEMA ikasema kuna uwezekano mkubwa wa wanachama hao kushirikiana na watu wengine kughushi barua ya chama, sahihi na muhuri pia. Kufuatia hatua hiyo, CHADEMA kiliwafuta uanachama washukiwa kwa kukosa sifa ya uaminifu, na kumwandikia Spika Ndugai kumtaarifu kwamba Halima Mdee na wenzake hao 18 sio wanachama wa CHADEMA. Spika Ndugai, hata hivyo, akasema ‘Wabunge’ hao watabaki bungeni na hakuna wa kuwafanya lolote!

Mheshimiwa Rais, kwa mujibu wa Katiba, wewe ni sehemu ya Bunge na ndiyo msingi wa kuielekeza kero hii kwako kwani naamini kwa namna unayoiona ni bora kwako na taifa unaweza kulishughulikia suala hili. Kwa maoni yangu, ukiliacha jambo hili libaki kama lilivyo sisi wananchi tutaona kwamba wewe pia ni miongoni mwa wanaokiuka kiapo cha uaminifu cha kulinda na kuitetea Katiba. Hii inaweza kukuharibia kwenye ‘rekodi’ unayotaka kujiwekea kama kiongozi unayeoongoza kwa kufuata misingi ya kisheria na kikatiba, usiyekubali dhulma ya aina yoyote.

Mheshimiwa Rais, ulitahadharisha kwa maneno yako mwenyewe kwamba kero zimalizikie wilayani na mkoani na kwamba hutaki kuona bango la malalamiko ya wananchi wakati ukienda kwenye ziara zako kwenye maeneo mbali mbali ya nchi. Lakini, kero yangu mimi haimuhusu Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa au Mkurugenzi wa Halmashauri. Kero yangu mimi ni kuhusu ukuu wa Katiba ambao Spika Ndugai kwa makusudi na kwa maslahi anayoyajua mwenyewe ameonesha kuudharau kwa kuwaruhusu akina Halima Mdee na wenzake kuendelea kubaki bungeni licha ya kutokidhi vigezo vya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Rais, naomba nitahadharishe kwamba kulalamikia kwangu uwepo wa akina Halima Mdee na wenzake na akina Joseph Selasini na wenzake ndani ya Bunge hakutokani na nongwa au choyo kwa akina mama na baba hao ambao pamoja na mambo mengine naendelea kuwaheshimu sana kama binadamu na Watazania wenzangu. Wala wito huu haukutokana na chuki binafsi dhidi ya Spika Ndugai. Isipokuwa, mimi kama raia wa nchi hii na mwanachama hai wa chama chetu cha CCM nakosa uvumilivu ndani ya nafsi yangu ninapoona Katiba ya nchi inapovunjwa, kukanyagwa na kupuuzwa mbele ya macho ya viongozi wanaotokana na CCM, kitu ambacho nahofia kinakidhoofisha chama na kutoa picha mbaya kwa vizazi vijavyo pamoja na kuwapa ajenda vyama vya upinzani ya kutushambulia.

Uwepo wa Katiba na sheria nyengine ni vielelezo vya ustaarabu ambao kama taifa tumeufikia na haina maana ya kuwa na Katiba na sheria lakini tukaacha kuzifuata. Hali hii inatia dosari ustaarabu wetu na sitegemei kwamba  unaweza kulivumilia hilo. Unaweza kufanya kitu.

Ponsian Baitatafe ni diwani mstaafu wa Kata ya Kasharunga, iliyopo wilayani Muleba, mkoani Kagera kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Kwa maoni na ushauri unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni Pbaitatafe@gmai.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Unataka kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.  

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *