The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tozo za Laini na Miamala ya Fedha Zinafuta Maana ya Tanzania ya Kidigitali

Katika nyakati hizi ambazo watu wanahitaji kuwasiliana zaidi, kazi nyingi zinafanyikia kwenye mtandao, kuongeza tozo tena juu ya gharama za mawasiliano ni kuendelea kudidimiza Tanzania ya kidigitali.

subscribe to our newsletter!

Jioni ya leo, Juni 10, 2021, Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba ameweza kuwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022. Bajeti hii imetengewa jumla ya shilingi trilioni 36.33, ambapo  matumizi ya kawaida yatakuwa ni shilingi trilioni 23 na  bajeti ya maendeleo itakuwa  ni shilingi trilioni 13.3. Bajeti hii inakuja katika kipindi ambacho hali ya kiuchumi nchini Tanzania na ulimwenguni kwa ujumla imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na janga la UVIKO-19, ambapo ukuaji wa uchumi wa Tanzania unaripotiwa kushuka mpaka  asilimia 4.8, huku sekta kama utalii zikiwa zimepoteza sehemu kubwa ya mapato, zaidi ya asilimia 70.

Katika hali ya kutafuta vyanzo vipya vya mapato, Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa pendekezo la kutoza shilingi 10 hadi shilingi 200 kwa kila laini ya simu kulingana na uwezo wa kuongeza salio. Pia, bajeti hio imependekeza kutoza tozo ya Sh10 hadi Sh10,000 katika kila muamala wa kifedha unaofanywa kwa njia ya simu. Pia, katika hotuba hiyo hiyo iliyosomwa leo na Dk Mwigulu Nchemba, Serikali ilieleza kuwa inaenda kufuta kodi ya ongezeko la thamani katika simu janja, modemu na vishkwambi (tablets) katika adhma yake ya kufikia Tanzania ya kidigitali. Hata hivyo, inaonekana kuna ukinzani mkubwa katika mipango hii miwili ya Serikali.

Ujumuishi katika huduma za kifedha

Ripoti ya hali ya uchumi Tanzania toleo la Juni 2020 kutoka Benki ya Dunia (WB) inaonesha ni asilimia 23.4 tu ya watu kwenye sehemu za mijini wenye akaunti za benki, na asilimia 5.1  ya watu vijijini wana akaunti za benki. Ripoti hiyo inaeleza kwamba namna pekee Watanzania wengi hujumuishwa katika huduma za kifedha ni kupitia huduma za kifedha za simu (mfano, M-Pesa, Tigopesa, Halopesa na zinginezo). Huduma hizi zimeendelea kuwa na watumiaji wengi ambapo mpaka kufikia Aprili 2021 kulikua na watumiaji  milioni 32 wa huduma za fedha kwa njia ya simu. Hata hivyo, idadi hii bado hailingani na idadi ya watumiaji wote wa simu ambapo mpaka Aprili 2021, kulikua na watumiaji milioni  53.

Moja ya sababu kubwa inayotajwa za watu kutokutumia huduma ya kutuma  fedha kwa simu kwa uwezo uliopo, ni gharama katika kutumia huduma hizo, hususani kwa miamala midogo midogo inayotumiwa na watu wengi. Kwa kutoa, kuweka au kuhamisha  fedha kuanzia Sh20,000 na kushuka, inahusisha makato ya kuanzia asilimia 9.5 mpaka asilimia 35 kwa muamala mdogo wa Sh1,000, hii ikiwa ni pale unapotaka kutoa kwa wakala. Tozo ya Sh10 mpaka Sh10,000 kwa kila muamala sio tu itageuka kikwazo bali inaweza kuzuia sehemu kubwa ya watu ambao hawajajiunga na huduma hizi kushindwa kutumia au kwa wanaoutumia kukimbia. Na hata kwa miamala mikubwa  kuanzia milioni tatu na kuendelea ambayo kwa sasa inaweza kuhusisha gharama za utoaji wa Sh10,000, kwa kuongeza 10,000 zaidi inaweza kuondoa umaana mzima wa kutuma fedha kidigitali.

Pamoja na kuwa na zaidi ya watu milioni tatu ambao hawajaunganishwa na mtandao na zaidi ya milioni 18 ambao hawapati mtandao wa intaneti bado gharama za vifurushi ni mwiba mkubwa kwa wananchi walio wengi. Mfano, gharama za intaneti kwa kifurushi cha MB 500 kwa mwezi ni mara mbili ya kiwango kinachoshauriwa na Umoja wa Mataifa (UN Broadband Commission). Mara kadhaa kumekuwa na malalamiko kedekede pale gharama za vifurushi zinapoongezeka. Katika nyakati hizi ambazo watu wanahitaji kuwasiliana zaidi, kazi nyingi zinafanyikia kwenye mtandao, kuongeza tozo tena juu ya gharama za mawasiliano ni kuendelea kudidimiza Tanzania ya kidigitali.

Nini kifanyike?

Serikali kupunguza kodi kwenye kuingiza simu nchini haiwezi kuleta tija iliyotakiwa kama gharama za matumizi zitaendelea kupaa. Ni hivi karibuni tu Serikali imepokea mkopo wa shilingi bilioni 347 kutoka kwa Benki ya Dunia kwa ajili ya Tanzania ya kidigitali, malengo yaliyowekwa katika mradi huu yanaweza yasitimie kama wananchi wakiwekewa ukuta wa gharama katika kuifikia Tanzania ya kidigitali.

Lakini nini kifanyike hasa ukizingatia uzorotaji wa uchumi kutokana na athari zitokanazo na janga la UVIKO-19? Kwanza, ni muhimu kwa Serikali kuiangalia sekta ya mawasiliano nchini na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa ujumla kwa jicho la muda mrefu, badala ya kila wakati kufikiria kumtoza mwananchi ambaye tayari yuko kwenye dimbwi la umasikini. Ni muhimu kwa Serikali kuangalia vyanzo vingine vya mapato. Kwa mfano, kuna makampuni makubwa kama Netflix, Youtube na kadhalika ambayo tayari wanatengeneza fedha kwa kutoa huduma zao hapa nchini. Serikali inaweza kuangalia namna ya  kuzifikia na kuzitoza kodi kampuni hizi. Bahati nzuri ni kwamba jambo hili limeweza kufanyika hata katika nchi nyingi duniani, ikiwemo jirani yetu Kenya ambapo makampuni kama Netflix tayari wameweka kwenye miundombinu yao kodi kwa ajili ya Serikali ya nchi hiyo. Serikali ya Tanzania inaweza kuangalia namna wanavyoweza kutekeleza hatua kama hiyo.

Pia ni muhimu serikali kuzingatia matumizi bora ya fedha za umma kwani bado kuna sehemu kubwa fedha hizo zinazotumika kwa namna ambayo siyo bora. Kwa mfano, ujenzi wa nyumba za wakuu wa mikoa uliotengewa fedha kuanzia shilingi milioni 150 mpaka milioni 800 kwa nyumba moja siyo matumizi bora ya fedha za umma au shilingi bilioni 11 zilizotengwa na Wizara ya Miundombinu kujenga nyumba 20 za viongozi. Hivyo, kufanya wastani wa kujenga nyumba moja kuwa shilingi milioni 559, haya siyo matumizi mazuri katika nyakati hizi. Pia, kwa kuzingatia athari za ugonjwa wa UVIKO-19, sio sahihi kwa Serikali kutenga shilingi bilioni 506 kwa ajili ya kununua ndege za ziada tatu, ilhali ndege 12 zilizopo bado hazijaweza kuleta tija. Sio kila mradi uliosemwa utafanywa una mantiki, na mradi wa kununua ndege kwa sasa ni mzigo mkubwa hasa ukizingatia watumiaji wa ndege hawafiki hata asilimia moja ya Watanzania na kwa kuzingatia anguko la biashara ya ndege sababu ya UVIKO-19.

Tony Alfred ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tonyalfredk@gmail.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts