The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tafakuri Juu ya Mtoto wa Tanzania

Jitihada zaidi zinahitajika kujenga Tanzania inayomlinda mtoto dhidi ya ukatili na unyanyasaji.

subscribe to our newsletter!

Siku ya mtoto wa Afrika huazimishwa Juni 16 kila mwaka tangu ilipotangazwa rasmi na uliokuwa Umoja wa Afrika (OAU) mwaka 1991 kwa lengo la kuenzi mapambano ya wanafunzi watoto wadogo walioandamana katika kitongoji cha Soweto, nchini Afrika Kusini, mnamo Juni 16, 1976, kupinga aina ya elimu duni na ya kibaguzi iliyokuwa ikitolewa na Serikali ya kikaburu iliyokuwa ikitawala nchi hiyo. Maandamo hayo yaliyopelekea vifo ya watoto kati ya 120 na 700, yameacha alama muhimu kwa jamii ya kibinadamu juu ya umuhimu wa kuhakikisha haki za watoto zinazingatiwa na Serikali, wazazi na jamii kwa ujumla.

Katika maazimisho ya mwaka huu 2021, kauli mbiu ya siku hiyo inahimiza kutekeleza kwa Agenda ya Afrika ya 2040 ambayo inalenga uwepo wa jamii ambayo inalinda  haki zote za mtoto. Katika agenda hii ambayo inapaswa kutekelezwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), baadhi ya malengo yake yanahimiza kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2040 kila mtoto wa Kiafrika awe amelindwa dhidi ya ukatili, unyanyasaji, unyonyaji na kuhakikisha mtoto anapata mahitaji yake yote muhimu ikiwemo elimu bora na afya bora itakayomwezesha kuishi vema. Pia, agenda inasisitiza nchi zote wananchama kuhakikisha sio tu zinatekeleza kikamilifu sheria na sera zinazohusu watoto bali pia zinakuwa na sheria, sera na mifumo yote ya kitaasisi ambayo ni rafiki kwa watoto.

Nchini Tanzania, ipo sheria ya mtoto ambayo imeelezea haki za msingi za mtoto kama zilivyotajwa kwenye mikataba ya kimataifa kama vile Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (CHC) wa mwaka 1989 na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) wa mwaka 1990 ambayo yote Tanzania kama mwanachama wa jumuiya za kimataifa iliiridhia. Kwa ujumla, sheria hiyo ya mtoto ya mwaka 2009 pamoja na hiyo mikataba ya kimataifa yote kwa pamoja imeipa wajibu Serikali, wazazi na jamii kuwalinda watoto dhidi ya aina yoyote ile ya ukatili na ubaguzi, na kuhakikisha watoto wanapatiwa mahitaji yote ya msingi.

Licha ya kuwepo kwa sheria na kuridhia kwa mikataba hiyo ya kimataifa inayolenga kulinda haki za mtoto, bado Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za watoto kama vile ukatili wa kingono, ukatili wa kimwili na kisaikolojia, utumikishwaji wa watoto, mimba za utotoni, ndoa za utotoni na ukosefu wa lishe na huduma bora za afya kwa watoto wote.

Ukatili dhidi ya watoto

Kwa mfano, ripoti ya haki za binadamu ya mwaka 2020 iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) mwezi Aprili mwaka huu, inaonesha katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2019 matukio ya ukatili dhidi ya watoto yameongezeka kwa asilimia 49 kutoka 10,551 hadi 15,680, huku matukio kama ulawiti na ubakaji wa watoto kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita yakiendelea kuripotiwa polisi kufikia wastani wa matukio 7,388 kwa mwaka, mengi yakiwa ni dhidi ya watoto. Hii ni dalili mbaya sana katika kuhakikisha tunaifikia Afrika inayojali haki za watoto.

Ndoa za utotoni na mimba za utotoni bado zimeendelea kushika kasi nchini. Kwa mfano, kwa miaka mitatu kati ya 2016 na 2018, LHRC ilikusanya matukio zaidi ya 2,991 ya mimba za utotoni yaliyoripotiwa katika mikoa mbalimbali yakiwahusu watoto wenye umri kati ya miaka 13 na 17 hivyo kupelekea watoto hao kushindwa kuendelea na shule sambamba na kufanyiwa vitendo vya kibaguzi. Tatizo la ndoa za utotoni linafanywa kuwa kubwa zaidi na kitendo cha Serikali kushindwa kufanya marekebisho ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayoruhusu wasichana wa miaka 14 na 15 kuolewa licha ya Serikali kuridhia mikataba ya kimataifa inayopinga ndoa za utotoni pamoja na hukumu iliyotolewa na Mahakama dhidi ya ndoa za utotoni. Hii yote inatia shaka kama kweli Tanzania itaifikia Afrika inayojali haki za watoto kufika mwaka 2041.

Shuleni ambako inategemewa kuwa ndiko mahali watoto wanapatiwa haki yao ya elimu nako kumeonekana kuna changamoto kubwa kwa watoto wengi. Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la HakiElimu inayohusu hali ya ukatili wa watoto wa shule Tanzania Bara iliyotolewa Februari 2021, inaonesha asilimia 87.9 ya watoto wa shule za sekondari na msingi wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili kwa namna moja au nyingine hasa kupitia adhabu ya viboko. Ripoti hiyo pia inataja takribani asilimia 34.3 ya watoto wa shule walinyanyaswa kisaikolojia hususan na wazazi wa walezi wao.

Lishe ya mgogoro

Kwa upande mwingine, kutokana na hali mbaya ya lishe licha ya Tanzania kuwa mojawapo ya wazalishaji wakubwa wa chakula na kuwa na mifugo mingi barani Afrika ukiiacha Ethiopia, hali duni ya lishe imeendelea kuathiri zaidi watoto. Lishe duni kwa watoto imepelekea udumavu wa watoto na magonjwa hasa kwa wale walio chini ya miaka mitano. Hii imepelekea Tanzania kuwa nchi inayopoteza takribani watoto 100 kila siku kutokana na lishe duni. Hivyo bado watoto wengi  wanaikosa haki yao ya kuishi na kuwa na afya njema kama haki zao za msingi ambazo zilipaswa kulindwa na kutekelezwa na serikali, wazazi na jamii kwa ujumla.

Kutokana na changamoto hizi ni muhimu sana kwa wadau ikiwemo Serikali, wazazi, vyama vya kisiasa, taasisi za kidini, jumuiya za wananchi, asasi za kiraia na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanashikamana kukabiliana na changmoto hizi ili kuhakikisha tunaifikia Afrika inayojali haki za watoto. Pia, siku hii ya mtoto wa Afrika inapaswa kutukumbusha kuwa umri au rika sio kigezo cha binadamu kudai haki zake au kuleta mabadiliko. Kwa mantiki hiyo basi Juni 16 iwakumbushe watoto wa Afrika ya leo kwamba nao wana wajibu mkubwa wa kutetea haki zao bila ya kujali jamii inayowazunguka ipo mbali kiasi gani katika kuwatimizia mahitaji yao au kuwapigania haki zao.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts