The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Haiti: Taifa Lililojaa Visa vya Mapinduzi, Udikteta

Hali duni za maisha ya watu zimekuwa chanzo kikuu cha sintofahamu za kisisasa ambazo zimekuwa zikiikumba nchi hiyo tangu karne ya kumi na tisa. 

subscribe to our newsletter!

Mnamo Julai 7, 2021, picha zilianza kuzunguka mitandaoni zikionesha kikundi cha watu wakiwa na silaha kali kana kwamba wako kwenye operesheni ya kijeshi. Hapo hapo habari zikasikika kuwa Rais wa Haiti Jovenel Moïse aliuwawa kwa kupigwa risasi. Ripoti kutoka kwa viongozi waandamizi wa Haiti zilieleza kwamba Rais Moïse alipigwa risasi 12 kwa kutumia silaha za kivita na bastola. Katika shambulio hilo, mke wa Moïse pia alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya.

Mamlaka za taifa hilo la Karibian tayari zinamshikilia mmoja wa raia wake aliyekuwa anaishi katika jiji la Florida, nchini Marekani kwa madai ya kuhusika na mauwaji ya Rais Moise. Christian Emmanuel Sanon, 63, anashutumiwa na Jeshi la Polisi la Haiti kukodi mamluki 28 kwa ajili ya kuendesha operesheni hiyo iliyozua gumzo ulimwenguni kote. Kati ya mamluki hao, 26 wanasemekana kuwa wanajeshi wastaafu toka Colombia na wawili kuwa raia wa marekani wenye asili ya Haiti . Mpaka sasa 17 tu ndio ambao wamekamatwa huku watatu wakiuwawa na polisi

Baadhi ya Mamluki waliokamatwa wakihusishwa na tukio hilo la mauaji ya Rais wa Haiti

Lakini Haiti, taifa la takribani watu milioni 11 kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia (WB), lina historia ndefu ya machafuko ya kisiasa na utawala wa Rais Moise haukuwa na utofauti. Machafuko haya ya kisiasa, yanayoenda sambamba na uchumi dhaifu, yanadaiwa kusababisha uhamaji wa takribani watu milioni tatu kutoka nchi hiyo kwenda nchi nyingine mbalimbali ulimwenguni.

Jamhuri ya kwanza ya watu weusi

Historia ya kisiasa ya Haiti ndiyo iliyoijenga Haiti ya leo. Kufuatia vita kali kati ya watumwa dhidi ya majeshi ya Ufaransa, Hispania na Uingereza, iliyopiganwa kati ya mwaka 1791 na 1804, Haiti ilikuwa nchi ya kwanza kuongozwa na watu waliokuwa watumwa. Mapinduzi ya Haiti yaliongozwa na Jean-Jacques Dessalines, ambaye hata hivyo aliuwawa na wasaidizi wake baada ya kulitumikia taifa hilo kwa kipindi cha miaka miwili tu.

Historia hii ya kuua watawala ilijirudia mwaka 1869 alipouliwa Sylvain Salnave; ikajirudia tena mwaka 1912 alipouliwa Michel Cincinnatus Leconte, ambaye ni mjukuu wa mtawala wa kwanza wa Jamhuri ya Haiti na Jean Vilbrun Guillaume Sam aliyeuliwa mwaka 1915.

Mpaka hapa unaweza kuona ni kwa namna gani historia ya taifa hili ilivyojaa mazonge. Udumavu, mapinduzi ya kijeshi, uchawi, rushwa na udikteta ndiyo Haiti ya jana na leo. Kati ya 1843 mpaka 1915, Haiti imehudumiwa na jumla ya viongozi 22, ila ni mmoja tu aliyeweza kudumu madarakani na kumaliza awamu yake yote.

Kati ya 1986 na 2004 kumekua na mapinduzi ya kijeshi matano, kumekuwa na marais wa mpito wasiohesabika, mpaka kuna kiongozi aliyekaa siku tatu tu. Hii historia ndio inayotuleta karibu zaidi kuelewa kuuwawa kwa Rais wa Haiti.

Hata hivyo, kuna historia muhimu zaidi itakayotupa mwangaza; kipindi cha udikteta mwaka 1957 mpaka mwaka 1986.

Uchawi waondosha taasisi za nchi

Wasomi na wadadisi wamejadili kwa mapana na marefu kiini cha matatizo ya taifa hili la Haiti. Moja kati ya hoja zinazotolewa ni kwamba hali za sintofahamu za kisiasa na kiuchumi za taifa la Haiti zinatokana na uwepo wa taasisi imara za kidemokrasia na utawala katika nchi hiyo. Taasisi hizi muhimu katika uongozi wa nchi inasemekana ziliharibiwa kabisa chini ya utawala wa Rais Francois “Papa Doc” Duvalier aliyeiongoza Haiti kwa mkono wa chuma kati ya 1957 na 1971.

Katika kipindi cha utawala wake, Papa Doc, daktari wa binadamu aliyegusa hisia za wananchi wengi wa Haiti na kupata imani kutoka kwa jeshi la nchi hiyo, alibadilisha maafisa wote waandamizi wa jeshi na kisha kuunda kikosi chake cha kujihami maaarufu kama Tonton Macoutes ambacho wanachama wake wengi walikuwa ni wafungwa waliokua na hatia mbalimbali zikiwemo za mauaji na wizi. Kazi kuu ya kikosi hiki ilikua ni kuteka, kuua na kuharibu. Tonton Macoutes ilifikia kipindi kikawa na nguvu kuliko jeshi la Haiti, huku kikosi hiki kikifanya kazi nje ya mfumo wa sheria.

Papa Doc Duvalier alivyoingia madarakani mwaka 1957

Moja kati ya mambo ya ajabu aliyofanya Papa Doc, ambaye mwaka 1968 alijitangaza kuwa rais wa maisha, ni kuwaaminisha wananchi wake kwamba yeye alikua ni mojawapo ya mzimu wa kifo maarufu kama Baron Samedi. Inadaiwa kwamba Papa Doc alikunywa damu za watoto wa mahasimu wake wa kisiasa. Kupitia vitisho, kuteka, kutesa, kupoteza na kuua Papa Doc aliweza kuwatiisha watu wa Haiti, ila kupitia uchawi Papa Doc alihakikisha Haiti wanaogopa hata kumuwazia vibaya wakiwa peke yao. Kama hii haitoshi, Papa Doc alihakikisha anajenga picha kwamba yeye ni kiongozi anayependwa na watu wake, alifanya hivi kwa kuzunguka mtaani na kugawa hela kama inavyompendeza, Papa Doc mtoa riziki.

Matukio yote haya yalipelekea jaribio la mapinduzi dhidi ya Papa Doc mnamo mwaka 1964 ambapo hata hivyo halikufanikiwa. Vijana 13 wenye asili ya Haiti waliorudi nchini kutokea nchini Marekani ambao walitajwa kuhusika na tukio hilo walisakwa na kuuwawa, wawili kati ya vijana hawa waliuwawa nchi nzima ikishuhudia. Mmoja kati ya vijana hao wawili aliwekwa uwanja wa ndege wa nchi  hiyo kuhakikisha kila anayeingia Haiti anamuona, hata maiti ilivyonuka na kuharibika vibaya haikuondolewa.

Hata hivyo, Papa Doc alifariki mwaka 1971 na kurithiwa na mtoto wake Jean-Claude ‘Baby Doc’ Duvalier ambaye naye aliendeleza ukatili na mauaji ya baba yake mpaka 1986 alipofurumishwa kwa mapinduzi ya kijeshi.

Moise akosa uungwaji mkono

Haiti baada ya tawala za viongozi hawa wa kiimla ilianza kubeba jina la nchi iliyoshindwa. Toka utawala wa akina Duvalier, Haiti imeshuhudia mapinduzi ya kijeshi matano. Maandamano ya wananchi wasioridhishwa na hali zao za kimaisha yamekuwa ni desturi ya watu wa taifa hilo. Ni katika muktadha huu ambapo Rais Jovenel Moïse, aliyeuwawa Julai 7 mwaka huu, aliingia madarakani.

Moise si Rais aliyekuwa na uungwaji mkubwa kutoka kwenye makundi mbalimbali ya nchi yake, ikiwemo vyama vya upinzani. Kutokana na hali ngumu ya maisha, maandamano yalitawala nchini humo kipindi cha mwaka 2019 na 2020 huku wananchi wakishinikiza kujiuzulu wa Moïse kwa kushindwa kuboresha hali zao za maisha. Ubadhirifu wa mali za Serikali na jamii iliyogawanyika katika mrengo wa rangi kati ya watu weusi na wale wenye weupe (light skin) vyote vilichagiza vuguvugu hili kuendelea.

Mitaa ya Haiti baada ya kifo cha Moise

Akiwa anakabiliwa na upinzani wa aina hii, Moïse, ambaye amewahi kunukuliwa akisema kwamba baada ya Mungu hakuna mtu mwenye nguvu zaidi yake nchini humo, aliendesha mpango wa kung’ang’ania madaraka kwa kufanya mabadiliko ya Katiba ya Haiti yenye kukidhi matakwa yake ya kisiasa na yale ya washirika wake. Tayari Katiba pendekezwa ilishatoka na kura ya maoni ilitegemewa kufanyika Juni 2021 lakini ikaahirishwa mpaka Septemba 2021 kwa sababu ya janga la UVIKO-19.

Hali ilikuwa mbaya sana kwa Moise kiasi ya kushirikiana na makundi ya kihalifu ili kuimarisha uwepo wake madarakani. Halii hii ilipelekea makundi haya kufanya uhalifu katika jamii bila kuwepo uwajibikaji wowote kutoka serikalini na pale waziri anayehusika na masuala ya kipolisi alipotishia kuondosha uhusiano kati ya makundi hayo na Serikali Moise  alimtoa haraka madarakani.

Nini Haiti inaifundisha Afrika?

Miaka 29 ya udikteta wa Papa Duvalier na mtoto wake ndio kama ulikua msingi mkubwa wa anguko la Haiti. Kitu cha kwanza Haiti ilipotea baada ya watawala kutukuzwa juu ya wananchi, hakuna kitu ambacho hakikuitwa kwa jina la Duvalier Haiti, alijaribu mpaka kuujenga mji wake kupitia pesa za walipa kodi. Inapofikia mahali viongozi wa nchi wanakuwa muhimu kuliko wale waliowapa dhamana, hiyo ni njia ya uhakika kuelekea kwenye taifa lililoshindwa.

Nchi zetu zina kitu cha kujifunza kutoka kwenye uzoefu wote huu wa taifa la Haiti. Taasisi imara ni kila kitu kwenye kujenga taifa endelevu. Kumekuwa na maoni kutoka kwa baadhi ya wadau katika bara la Afrika, ikiwemo hata hapa Tanzania, wakitoa hoja kuwa  kuendesha nchi kwa misingi ya utawala wa sheria kunachelewesha maendeleo. Tumeona Haiti, kunapokosekana taasisi imara zilizojengwa kwenye misingi ya sheria na utawala bora, hakuna kinachoweza kuendelea.

Uzoefu wa Haiti unatuonesha kwamba huwezi kumpa binadamu mwenye damu na nyama mamlaka ya Mungu na utegemee atende haki. Haiti kipindi cha Papa Doc haikua na Rais bali mungu aliyeweza kuagiza nani aishi nani afe. Nani ale nani asile. Nguvu yoyote inayotolewa kwa mtu yoyote kuna umuhimu wa kuweka mizania ya kuhakikisha hakuna aliye juu ya mstari wa watu, wananchi kwa ujumla wao. Unapotenda kosa la kumfanya mtawala Mungu, ni ngumu kurudi na kuwa na taifa tena.

Lakini uzoefu huu wa Haiti pia unatukumbusha umuhimu wa kuwa na matumaini. Pamoja na kupoteza taifa lao na mifumo ya uongozi, wananchi wa Haiti bado wanaamini hatma ya taifa lao ipo mikononi mwao na wamekuwa wakifanya kila linalowezekana kubadilisha hali ya mambo katika nchi yao. Maandamano na harakati nyengine za mageuzi zinazoendelea nchini Haiti kwa sasa zinalenga kutuma ujumbe kwa watawala wao na dunia kwa ujumla kwamba: hatutaki mapinduzi tena, tunataka Katiba, tunataka demokrasia. Hapa Tanzania, na Afrika kwa ujumla, tunajukumu la kuamini, kutumaini na kutenda na kuhakikisha kwamba ya Haiti hayatokei kwenye nchi zetu. Ili kufanikisha hilo, ni muhimu kuung’oa mzizi wa uovu kabla haujachipukia, kujihusisha na mambo ya taifa na nchi kwa wivu na mapenzi makubwa kwa mataifa yetu.

Tony Alfred ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa anayepatikana Dar es Salaam, Tanzania. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tonyalfredk@gmail.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 Responses

  1. the story is too lit, it motivate to go extra mile for more details. I can do a voice over for it

  2. The story is too lit, it motivate to go extra mile for more details. I can do a voice over for it

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *