Mara. Wantinku Mashauri, ambaye ni mzaliwa wa kijiji cha Bukabu, kilichopo wilayani Butiama, mkoani Mara, kaskazini-magharibi mwa Tanzania, ni miongoni mwa wasichana waliokimbia ndoa za utotoni kijijini hapo na kukimbilia katika kituo cha kupinga ukeketaji na ndoa za utotoni cha Hope for Girls and and Women Tanzania, au maarufu Nyumba Salama, kilichopo wilayani Butiama.
Mashauri, 15, binti mwenye ndoto kubwa na haiba isiyokifani, alikuwa akiishi na baba yake mzazi tu na anasema kwamba wakati anafikisha umri wa kupelekwa shule kwa ajili ya kuanza masomo katika ngazi ya awali, baba yake alimyima haki hiyo ya msingi ili amuozesha na aweze kujipatia mali kupitia mahari yanayolipwa.
“Baba yangu alisema kwamba hata nikifaulu hanipeleki shuleni,” Mashauri anaieleza The Chanzo wakati wa mahojiano naye ilipomtembelea kituoni hapo. “Nilienda shuleni mwenyewe. Nikajinunulia vifaa mwenyewe. Nilikuwa nakata miti [na kuuza ili kupata pesa]. Nikajinunulia vifaa mwenyewe nikaenda shule. Baba yangu hakushughulika na chochote ili niweze kwenda shuleni.”
Licha ya kujipeleka mwenyewe shuleni, Mashauri alikuwa akiambiwa maneno na baba yake ya kumkatisha tamaa huku akimweleza kuwa hata kama anasoma lakini lazima aolewe punde tu atakapomaliza darasa la saba. Kwa sauti iliyojaa simanzi, Mashauri anasimulia kisa chake:
“Nilipofanya mtihani wa darasa la saba nikarudi nyumbani. Baba yangu akaniambia, ‘Wewe hata kama utafaulu sikupeleki sekondari. Siwezi kumsomesha mototo wa kike halafu aende akabebe mimba shuleni.’
“Nikamwambia basi ninunulie tu vifaa vya shule niende mwenyewe, baba yangu alikataa. Nikakaa nyumbani kumbe alikuwa ameshaongea na kijana mmoja aje anichukue kwa lazima. Watu wakawa wananiambia wewe upo karibu kuolewa. Nakumbuka ilikuwa ni siku ya Alhamisi wakaleta ng’ombe 10 na mbuzi watatu. Mimi nilikuwa ndani sijui kinachoendelea. Baba aliingia ndani akaniambia nijiandae niende kwangu na hataki kuniona.
“Nikamwambia baba mimi nataka kusoma. Alinipiga sana. Alikuwa ananichapia ile mijeredi ya ng’ombe. Muda huo alikuwa amefunga mlango. Baadae alifungua nikakimbia ili kutafuta msaada. Nikaenda kwa Mwenyekiti [wa Serikali ya Mtaa] ambaye aliniandikia barua [iliyonifanya nipokelewe kwenye hiki kituo].
“Ndoto yangu ilikuwa ni kuja kuwa daktari ili nitibu wagonjwa. Lakini baadaye shirika nililokimbilia lilipomfuata baba ili aweke sahihi ya uhamisho alikataa na ndoto yangu ya udaktari ikawa imeishia hapo. Kwa sasa najishughulisha na ufundi stadi ambao nadhani unaweza kunisaidia kuboresha maisha yangu.”
Hali ya ndoa za utotoni
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto ulimwenguni UNICEF za mwaka 2010 na 2017, Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuwa na viwango vya juu vya ndoa za utotoni barani Afrika baada ya Sudani Kusini na Uganda. Sudani Kusini inakadiriwa kuwa idadi ya watoto wa chini ya umri wa miaka 18 wanaoozwa ni asilimia 52, na nchini Uganda ni asilimia 40 na Tanzania ni asilimia 31.
Mnamo June 15, 2021, kuelekea sherehe za Mtoto wa Afrika zinazosherehekewa kila ifikapo June 16, mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayopigania haki za mtoto uliitaka Serikali kuifanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ili iendane na maamuzi ya Mahakama Kuu yaliobainisha kwamba sheria hiyo inakwenda kinyume na Katiba ya nchi na inayowabagua watoto wa kike. Mahakama Kuu iliitaka Serikali ifanye mapitio ya sheria hiyo ili umri wa binti wa kuolewa uongezwe kutoka miaka 14 hadi miaka 18.
Mashauri si sura pekee kwenye takwimu hizi. Annastazia Chacha, 17, ni msichana mwengine aliyejikuta akiwa mhanga wa janga hili lililokosa dawa nchini. Chacha, mzaliwa wa kijiji cha Kitenga, wilayani Tarime, mkoani Mara, alihitimu elimu yake ya msingi mwaka 2020. Anaieleza The Chanzo namna alivyofika katika kituo hiki cha kupokelea wahanga wa ndoa za utotoni na ukeketaji:
“Mwaka 2020, nilimwambia baba natamani kwenda kujifunza ufundi na kuniahidi kunipeleka. Baba alivyoshindwa kutimiza ahadi yake mama mdogo akaja akanichukua akanipeleka kwenye ufundi. Nikasoma miezi mitatu kabla ya baba kuniambia nirudi nyumbani ili niolewe.
“Baba alichukua hatua za kuleta wachumba nyumbani. Wakakubaliana ng’ombe sita [kama mahari]. Wakapanga harusi ifanyike Juni 20, 2021, na baba akaniambia nijiandae niende kwangu. Nilikuwa nikikaa nalia na nikaenda kwa padri nikamweleza. Akanipeleka kituo cha polisi ambako niliandikiwa barua [ya kuniombea ruhusa katika vituo vinavyopinga ndoa za utotoni]. Nikarudi nyumbani nikaificha. Siku moja nikamwambia baba naenda kanisani na nikatumia nafasi hiyo kutoroka mpaka leo sijarudi nyumbani.”
Chacha anasema kwamba nyumba salama inayompatia hifadhi kwa sasa aliifahamu kupitia matembezi viongozi wa nyumba hiyo walikuwa wakiyafanya shuleni na kwenye jamii yenye lengo la kutoa elimu kuhusu ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia na ukeketaji na namna ya kukomesha tabia hizo.
Nyumba salama kwa wahanga wa ndoa za utotoni
Mashauri na Chacha ni wawili tu kati ya wahanga wengi wa ndoa za utotoni wanaopatiwa msaada na shirika lisilo la kiserikali la Hope for Girls and Women Tanzania ambalo linaendesha nyumba salama kwa wahanga wa ndoa za utotoni kama sehemu ya juhudi zake za kukomesha tatizo hilo. Shirika hili limekuwa likipokea kesi mbalimbali za ndoa za utotoni kutoka kila kona ya mkoa wa Mara ambapo kwa mwaka 2021 tu, kati ya Januari na Agosti, jumla ya kesi zipatazo 58 za ndoa za utotoni zimepokelewa kituoni hapo.
Hope for Girls and Women Tanzania ni kituo kinachopinga ndoa za utotoni, ukeketaji na ukatili wa aina mbalimbali kwa wanawake na wasichana katika mkoa wa Mara. Kituo hiki kilianzishwa mnamo mwaka 2017 kufuatia ufadhili wa wadau kadhaa wa ndani na wa nje wenye lengo la kuokoa maisha ya mtoto wa kike na kuhakikisha anapata haki zote za msingi.
Rhobi Samwelly ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hope for Girls and Women Tanzania ambaye anaieleza The Chanzo kwamba mabinti wanaopokelewa kituoni hapo wanafika hapo kutokana na ushirikiano ambao kituo hicho uko nao na polisi ambao kesi nyingi za ndoa za utotoni huripotiwa na kuanzia kwao.
“Tunapowapokea watoto kama hao na kuwapa ushauri wa kisaikolojia pamoja na ushauri nasaha. Baadae tunaenda kwa mzazi kutaka kujua kwa nini alitaka kufanya kitendo kama kile. Lakini kama polisi wanakuwa wameshamkamata mtu huyo basi sheria huwa inafuata mkondo wake.
“[Tatizo ni kubwa kwani] kwa wiki moja tunaweza kupokea kesi tatu za ndoa za utotoni. Nafikiri hii inakupa picha kamili ya jambo zima. Lakini hao ni ambao wamepata fursa ya kutufikia tu. Wapo ambao pia wanakuwa wamelazimishwa huko inawezekana hawakupata fursa ya kufika katika vituo vya nyumba salama. Niwaase wazazi kwamba wawaache watoto wao wa kike wasome. Hawa watoto wana uwezo mkubwa na sisi tumeshawaona.”
Umoja unahitajika kukomesha mimba za utotoni
Clementina Mutakyamirwa ni kaimu Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Butiama ana anaiambia The Chanzo kwamba tatizo la ndoa za utotoni wilayani hapo ni kubwa, akisema kwamba changamoto hiyo inatokana na wazazi wenyewe kutokuwa tayari kuwatimizia watoto wao mahitaji ya msingi.
Mbali na baadhi ya familia kuendelea kushikilia mila na desturi zilizopitwa na wakati, changamoto nyingine inayochochea tatizo la mimba za utotoni wilayani Butiama ni umasikini. Bi Mutakyamirwa anafafanua:
“Mzazi asipoona mwanae ameolewa anaona wanini nyumbani? Lakini nafikiri kitu kikubwa huwa ni uchumi, maana hakuna zao la kibiashara linalowaingizia kipato [wakazi wa Butiama]. Kwa hiyo mzazi anaona ni bora mwanae aolewe tu.
“Kwa nafasi yetu tunajitahidi kukomesha ndoa za utotoni. Ikitokea mtu amepata ujauzito akiwa shuleni, na mwenyemimba akagundulika, huwa tunampeleka polisi. Lakini baadae unakuta wazazi wa binti na wazazi wa mvulana wanayamaliza wao wao. Kesi ikipelekwa tu polisi unaambiwa eti huyo mtu katoroka. Kwa hiyo vitu hivyo vinatukwamisha sana. Lakini naamini tukiungana wote kwa pamoja tunaweza tukalitokomeza tatizo hili.”