The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nimeishi na Virusi vya UKIMWI kwa Miaka 27 Bila Mwenyewe Kujijua

Baada ya kumpoteza mpenzi wangu, hali yangu imenifanya nisite kuwaambia watu wangu wengine wa karibu ukweli kwani nahofia kuwapoteza na wao pia.

subscribe to our newsletter!

Kwa majina naitwa Atuganile Dominick ni mzaliwa wa Tukuyu, Mbeya na sasa naishi jijini Dodoma. Mimi nilizaliwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi bila mimi mwenyewe kugundua. Nilipofikisha umri wa miaka 11 nilianza kupata homa za mara kwa mara,  ikiwemo kutokwa  na vipele sehemu za siri. Kutokana utoto niliokuwa nao sikuweza kufanya lolote. Nilikuwa nikiugua sana na sikuwahi kuambiwa chochote kuhusu hali yangu.

Ilipofika mwaka 2000, mama yangu alifariki dunia. Kwa wakati huo sikujua sababu ya kifo cha mama yangu. Miaka tisa baadae, yaani mnamo mwaka 2009, nilipata pigo jingine la kuondokewa na baba yangu mzazi. Baba nilijua amefariki na nini lakini mama sikujua. Kwa baba nilijua sababu alikuwa akichukua dawa hospitali na kuzitumia.

Baada ya wazazi wangu kufariki mimi niliendelea kuumwa na bado sikuwa najua naumwa na nini. Nilikuwa nikiuliza wananiambia naumwa uti wa mgongo. Wakati mwingine unashangaa shingo inakakamaa na huwezi kugeuka. Utashangaa nakata kauli siongei. Mkono unajikunja na haukunjuki na vipele vinatoka na kupotea.

Nilipofika darasa la saba, hiyo ilikuwa mwaka 2009, hali yangu ya kuugua mara kwa mara ilipungua. Mwaka 2011, nikiwa na umri wa miaka 17, nilipata ujauzito. Mwanamke anapokuwa mjamzito hupimwa magonjwa mbalimbali kuhakikisha kuwa afya ya mama na mtoto inakuwa salama. Lakini baada ya mimi kupimwa sikuambiwa lolote kuhusu afya yangu.

Lakini kwenye kadi yangu ya kliniki niliwekewa alama nyekundu bila ya kujua ina maana gani. Nilipofika nyumbani dada yangu aliniuliza, “Mbona wamekuzungushia alama hii kwenye kadi,  hujaambiwa kitu chochote?” Nikamwambia kuwa hawajaniambia kitu chochote. Nilipo jifungua mwanangu nilimnyonyesha kwa muda wa mwaka mmoja na miezi sita.

Mwaka 2016, niliamua kuja Dodoma kufanya kazi za ndani ili kupata pesa kwa ajili ya kumuhudumia mtoto wangu ambaye nilimuacha na dada yake jijini Mbeya. Kuna dada alinichukua kuja Dodoma kufanya kazi za ndani. Aliniambia twende Dodoma ukafanye kazi za ndani.

Maisha yangu ya kazi yalikuwa mazuri na hakukuwa na changamoto yeyote lakini nilianza kuona dalili ya kutokwa na vipele na ngozi kusinyaa. Nakumbuka hata wakati niko nyumbani Mbeya ngozi ilikuwa inasinyaa. Naweza kukaa siku tatu mbili halafu ngozi inarudi kwenye hali yake ya kawaida.

Hali ya mwili ilianza kubadilika na hivyo nishauriwa kwenda kupima maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Machi 3, 2021, nilienda katika moja ya vituo vya afya hapa Dodoma kupima afya yangu. Nilikuwa natokewa na vipele mwili mzima. Nikashauriwa kwenda kupima. Nilivyokwenda kupima baada ya kuwaelezea nimekua nikitokewa na hali hii toka nikiwa mtoto wakaniuliza “Mama yako yuko wapi?” Nikasema amefariki. Wakaulizia kuhusu baba yangu pia nikawaambia amefariki pia.

Hospitalini nikaulizwa kwamba wazazi wangu walikuwa wanaumwa na nini. Mimi nikasema sijui licha ya kuwa baba nilikuwa najua amefariki na nini. Lakini nikasema sijui. Wakaniuliza, “Ulivyokuwa mtoto hukuwahi kupewa dawa yeyote ile ya kila siku?” Nikawaambia kuwa sijawahi.

Baada ya kuulizwa maswali hatimaye madaktari wakanieleza ukweli kuhusu hali yangu. Daktari akaniambia, “Hivi ninavyo zungumza na wewe, wewe tayari ni muathirika wa virusi vya UKIMWI. Nenda kaulize ndugu yako yeyote yule kwamba wazazi wako wamefariki kwa ugonjwa gani.” Nilipomuuliza dada yangu akanimbia kuwa aliwahi muuliza baba wakati wa uhai wake kuwa hali yake ya kuumwa ilianza mwaka gani. Ndipo baba akasema ilianza mwaka 1992 kabla ya mimi kuzaliwa.

Taarifa kwamba mimi nilikuwa muathirika wa virusi vya UKIMWI ziliniumiza moyo sana. Sikujua cha kufanya zaidi ya kuanza kuishi kwa wasiwasi kwa kuhofia kuwa jamii itanitenga endapo nikieleza hali yangu ya kuishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi. Nilijisikia vibaya sana. Hata chakula kilikuwa hakipiti baada ya kupokea majibu hayo. Lakini namshukuru Mungu mwanangu hana maambukizi. Niliomba wampime na alikutwa mzima.

Baada ya mimi kupokea majibu nilimueleza ukweli mpenzi wangu na ndipo na yeye aliongozana na mimi kwenda kupima afya yake na baada ya kupima yeye na hakukutwa na maambukizi ya virusi vya ukimwi, hapo ndipo mahusiano yetu yalivunjika. Hatukuweza kuendelea tena. Hii imenifanya nisite kuwaambia watu wangu wengine wa karibu kwani nahofia kuwapoteza.

Ushauri wangu kwa kila mmoja wetu ni kujenga utamaduni wa kupenda kupima afya zao mara kwa mara ili kujua hali zao. Serikali na wadau wengine ni muhimu wakaendelea kuwashika mkono watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya UKIMWI. Jamii pia inapaswa ifahamu kwamba sisi ni kama walivyo tu watu wengine na hivyo wasitanyanyapae.

Mipango yangu ya maisha kwa sasa ni kwamba napambana kuwa na duka ambapo nitakuwa nauza bidhaa mbalimbali. Kwa sasa najishughulisha na shughuli ndogondogo kama vile ufuaji wa nguo kwa watu kwa ajii ya kujipatia kipato. Nina amini kwamba juhudi zangu hizi zitaniwezesha kufanikisha azma yangu hii pamoja na kujenga nyumba kwa ajili ya kuishi na mwanangu.

Atuganile Dominick amesimulia kisa hiki kwa mwandishi wa The Chanzo mkoani Dodoma Jackline Kuwanda. Unaweza kumfikia Jackline kupitia jaquelinevictor88@gmail.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na simulizi hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *