The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Badala ya Uraia Pacha, Serikali Yaahidi Hadhi Maalum kwa Wanadiaspora

Serikali yasema suala la uraia pacha ni suala lenye mchakato mrefu  wa kikatiba. 

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Serikali imesema kwamba inaendelea kutekeleza mchakato wa mabadiliko ya Sera ya Mambo ya Nje, ambapo moja ya jambo ambalo linategemewa kuwepo kwenye sera mpya baada ya mchakato huo kukamilika ni  uwezo wa Watanzania waishio nje ya nchi kupata “hadhi maalum” itakayowawezesha kupata fursa mbalimbali wanazopoteza pale wanapochukua uraia wa nchi nyingine, ikiwemo umiliki wa mali zisizohamishika, kama vile ardhi. 

Hayo yalibainishwa jana, Agosti 28, 2021, na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula wakati wa kikao rasmi na Watanzania waishio nje ya nchi, maarufu kama wanadiaspora, ikiwa ni mfululizo wa mabadiliko yanayoendelea katika wizara yake. 

“Suala la uraia pacha ni suala lenye mchakato mrefu  wa Katiba,” alisema Balozi Mulamula ambaye kwa sasa yuko nchini Marekani kwa ziara maalumu ya kikazi. Kikao hicho kilifanyika mtandaoni kupitia mtandao wa Zoom. “Lakini tukasema badala ya kuendelea kusubiri, kwa nini tusiangalie milango mingine iliyo wazi kwa sasa?” 

Waziri Mulamula alitolea mfano wa nchi kama ya India ambapo alisema kupitia hadhi maalum, raia wa India wanaoishi nje ya nchi wameweza kupata haki mbalimbali.

Kufuatia hofu iliooneshwa na baadhi ya washiriki hao takriban 700 walioshiriki kikao hicho kwamba “hadhi maalumu” itawapa sehemu tu ya haki, Waziri Mulamula alieleza kwamba ili kuhakikisha hadhi maalum inakuwa na mambo ya kutosha wizara inaendelea kujadiliana na wanadiaspora na wadau wengine, huku wakiwataka wanadiaspora hao kujitokeza kutoa maoni yao kuhusu sera hiyo mpya ya mambo ya nje inayoendelea kutengenezwa, mchakato unaotegemewa kukamilika Disemba 2021.

Kwa Afrika Mashariki, ni Uganda, Kenya na Rwanda tu ndizo zinaruhusu uraia pacha. Nchini Kenya, kwa mfano, mchango wa raia wa nchi hiyo wanaoishi nje ya nchi unakadiriwa kupanda mpaka kufikia dola za kimarekani bilioni tatu kwa mwaka 2020, hii ikiwa ni mara mbili ya fedha zilizotokana na utalii ambazo Tanzania inakadiriwa kuingiza kwa mwaka 2019 kabla ya janga la UVIKO-19. Kwa Tanzania, fedha zinazotokana na wanadiaspora zinakadiriwa kufikia dola za kimarekani milioni 189 kwa mwaka 2020.

Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 unataja Watanzania waishio nje ya nchi kama moja wapo ya mikakati ya Serikali kupata fedha kwa kuwavutia raia hao kuwekeza nchini na kwa kutumia njia bunifu kama bondi ya diaspora. Hata hivyo,  Serikali imekua ikichelea kwa miaka kadhaa kutoa haki mbalimbali kwa wanadiaspora, jambo ambalo Waziri Mulamula aliwahakikishia wanachama wa jumuiya hiyo kulifanyia kazi. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *