The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Simulizi za Mateso Wanayopata Wafanyakazi wa Ndani Mwanza

Yapo matukio ya kuchomwa moto na kubakwa pia

subscribe to our newsletter!

Mwanza. Neema Hamisi* ni binti mwenye umri wa miaka 11 ambaye ni mhanga wa usafirishwaji haramu wa binadamu na ukatili na udhalilishaji dhidi ya watoto. Akiwa na umri wa miaka 10 tu, Neema alisafirishwa bila ya ridhaa yake kutoka mkoani Dodoma alikokuwa anaishi na kusoma, mpaka jijini Mwanza kwa ajili ya kufanya kazi za ndani. Hii ilikuwa ni mwaka 2020 wakati huo Neema akiwa yupo darasa la pili.

Wakati wa mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya, Neema anasimulia kwamba alipofika Mwanza ‘boss’ wake alikuwa ni mama yake mdogo. Neema anadai kwamba alikataa kufanyishwa kazi za ndani lakini mama yake huyo mdogo alimlazimisha. Neema anadai mama yake mdogo alikuwa anamtesa sana, ikiwemo kumlazimisha apikie wanawe chakula, huku yeye mwenyewe akinyimwa kula. Kuna vipigo pia ambavyo Neema huambulia pale ‘boss’ wake alijisikia kumuadhibisha binti huyo.

Kuna siku ilikuwa natakiwa kufanya mtihani shuleni (Neema alikuwa akisoma shule), mama mdogo akanizuia nisiende shule nibaki nyumbani,” Neema anasimulia wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika katika kituo cha WoteSawa, Agosti 23, 2021. “Akaniambia nifue nguo zote za mtoto na za kwake na pamoja na kufanya hivyo alikuja akanipiga na waya mpaka jirani alipokuja kuniokoa.”

Utumikishaji watoto kwa kazi za ndani

Neema, ambaye hakuwa akipokea malipo yoyote kutokana na kazi za ndani alizokuwa akifanya kwa mama yake mdogo, ni mmoja tu kati ya wahanga wengi wa utumikishwaji wanaopatiwa hifadhi katika kituo cha WoteSawa – Sauti ya Wafanyakazi za Ndani Tanzania, shirika lisilo la kiserikali lililopo jijini Mwanza lenye lengo la kuwawezesha kiuchumi watoto wanaofanyishwa kazi za ndani pamoja na kulinda haki zao mbalimbali. 

Tatizo la utimikishaji watoto kwenye kazi za ndani ni kubwa sana jijini Mwanza. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na WoteSawa mwishoni mwa mwaka 2019, katika kata nne za Manispaa ya Ilemela tu ambazo ni Kitangiri, Kawekamo, Nyasaka na Kiseke, watoto zaidi ya 400 walibainika ‘kuajiriwa’ kufanya kazi za nyumbani. Mbali na kupokea malipo finyu yasiyolingana na kazi wanazofanya, watoto hawa pia hukumbana na vitendo vya kikatili vinavyohatarisha ustawi na mustakabali wao wa maisha.

Marry Michael,*16, ni mtoto aliyekuwa akifanya kazi za ndani hapa jijini Mwanza. Mzaliwa huyo wa Ngara, Kagera anaieleza The Chanzo kwamba mnamo Mei 2021 alibakwa na mwajiri wake. Anasema ‘boss’ wake alisubiri siku familia yake imeenda kanisani, siku ambayo yeye Marry hakushiriki ibada kwa sababu zake binafsi, kuweza kutimiza azma yake hiyo ya kumnyanyasa kingono. The Chanzo pia ilikutana na Marry katika kituo cha WoteSawa.

“Akanishika mkono kwa nguvu na kufunga milango yote,” anasimulia Marry kwa sauti iliyojaa simanzi. “Akanipeleka hadi chumbani, akanitupa kitandani na kuanza kunibaka. Nilivyopiga kelele akashika kisu akisema, ‘Ukipiga kelele ninakuchoma kisu.’ Alipomaliza shida zake, akaondoka na kuniacha mwenyewe kitandani nikiwa nalia. Alipokuja mke wake nilimueleza kila kitu na tukaenda polisi kuripoti tukio lenyewe japo sikumbuki limeishaje.”

Achomwa kisu cha moto

Wakati ikiwa inaendelea na shughuli zake za utafiti kuhusu utumikishwaji wa watoto kwenye kazi ndani kituoni hapo WoteSawa, The Chanzo iliweza kukutana na Jamila Nunge,* binti mwenye umri wa miaka 11, mzaliwa wa Bukoba, Kagera. The Chanzo ilimuona Jamila akiwa na makovu sehemu mbali mbali za mwili wake na kutaka kufahamu ilikuwaje mpaka akapata makovu hayo. 

Jamila anaeleza kwamba alikuja Mwanza mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021 kwa mtoto wa shangazi yake kuja kumsaidia kulea mtoto wake. Siku ya tukio, Jamila alichukua Sh1,000 na kwenda kununua vitumbua na kurejesha Sh500. ‘Boss’ wake alichukizwa na hatua hiyo na kuamua kumpa Jamila adhabu iliyomuachia majeraha makubwa mwilini mwake.

“Alishika kisu akakichoma kwenye moto mpaka kikawa chekundu,” anasimulia Jamila huku akiwa anatokwa na machozi. “Akachukua kijiko pia akakiweka kwenye moto na baadae akaleta mwiko. Baadae alianza kunichoma nikawa napiga kelele. Baada ya jirani yetu kusikia makelele akaja kubisha hodi na kuuliza imekuwaje. Mama akajibu amechoka na wizi, kwamba kila siku akiacha pesa mimi naiba kitu ambacho siyo cha kweli.”

Mkoa wa Mwanza unatajwa kuwa moja kati ya mikoa vinara nchini Tanzania kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Mikoa mengine ni Tanga, Arusha, na Mbeya. Ummy Mwalimu, aliyekuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, alisema Juni 2020 kwamba mnamo mwaka 2018, mkoa wa Mwanza ulisajili visa vya ukatili dhidi ya watoto vipatavyo 809 huku jumla ya visa 758 vikisajiliwa mkoani humo kwa mwaka 2019.

Ushirikina, umasikini watajwa kama sababu

Glory Shindika ni afisa wa polisi kutoka dawati la jinsia na watoto, Kituo cha Polisi Igogo kilichopo wilayani Nyamagana, Mwanza. Akiongea na The Chanzo kwa njia ya simu mnamo Agosti 27, 2021, Sindika amezitaja kesi zinazohusiana na ukatili dhidi ya watoto ambazo zimekuwa zikiripotiwa kituoni hapo ambazo ni kuchomwa, kuumizwa na vitu vyenye ncha kali, kulawitiwa, na kubakwa. 

“Sababu kubwa ya kuendelea kwa vitendo hivi [vya ukatili dhidi ya watoto] ni kuendelea kuamini mambo ya kishirikina miongoni mwa wanafamilia na hata wanajamii, kwa sababu kuna watu wanaamini kwamba wakienda kumlawilti au kumbaka mtoto mdogo, watafanikiwa kiuchumi, kitu ambacho sio cha kweli,” anasema Sindika.

Frank Benjamin ni mtetezi wa haki za watoto kutoka shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na upingaji wa ukatili kwa watoto majumbani la Foundation Karibu Tanzania. Benjamin anaiambia The Chanzo kwamba kwa mujibu wa utafiti wa shirika hilo, kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya hali duni za maisha na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. 

“Tuligundua kwamba familia ambazo hazina kipato cha kutosha ndizo zinazoongoza kwa kutenda ukatili,” anasema Benjamin wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Kwa sababu unakuta mzazi amebajeti kipato chake kwa siku husika, mfano ameweka pale Sh2,000. Mtoto na yeye kulingana na hali ya njaa akikuta pale hiyo pesa anaichukua ili akatafute chakula na kupoza njaa. Sasa mzazi anaporudi nyumbani na asiikute hiyo pesa na akaja kubaini mtoto ndiye aliyeichukua, wengi wanawapiga watoto na kuwaumiza.”

Malezi mabaya huchochea ukatili

Benjamini anaongeza kwamba utafiti wao pia umebaini kwamba wapo wazazi wanaotenda vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ambao wao pia walikuwa wahanga wa vitendo hivi wakati wa makuzi yao. Hoja hii inaungwa mkono na Vaileth Chonya, ambaye ni mtaalam wa saikolojia kutoka taasisi ya Tiba Tanzania anayesema kwamba madhara ya ukatili dhidi ya watoto yanaweza yasionekane mara moja lakini siyo kwamba hayapo. 

“Unakuta kwamba ni rahisi kwa mtu aliyefanyiwa ukatili kufanya ukatili huo kwa mtu mwingine,” Chonya anaiambia The Chanzo. “Mara nyingi watoto wanaofanyiwa ukatili wa kingono wasipopata ushauri nasaha wanaweza kuja kufanya ukatili huo kwa watoto wao, au ndugu zao wa karibu pale wanapokuwa wakubwa.” 

Chonya anasema kwamba ni jukumu la mzazi au mlezi kuhakikisha anampatia ushauri sahihi mtoto wake pale anapohisi kuwa mtoto huyo amefanyiwa kitendo chochote cha kikatili, vinginevyo, anaonya Chonya: “Tutakua tunaandaa kizazi kile cha kuja kuwa watu wa kufanya ukatili hata kwa mume wake au mke wake ama watoto wake.” 

Hifadhi na msaada wa kisheria

Amina Adam ni afisa utetezi kutoka shirika la WoteSawa anayebainisha kwamba wao kama shirika wamekuwa wakishirikiana na wadau kadhaa ikiwemo Serikali katika juhudi za kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wanaofanya kazi za ndani jijini Mwanza. 

Mbali na kupinga ukatili kwa wafanyakazi wa majumbali, WoteSawa pia limekuwa likiwachukua wahanga hao na kukaa nao huku taratibu nyingine, zikiwemo za kisheria, zikiendelea ili kuhakikisha watoto hao wanapata haki hiyo.

“Mtoto tunamsaidia kwa kumleta hapa [kituoni] na kumpatia malazi pamoja na mambo mengine,” Adam anasema wakati wa mahojiano na The Chanzo. “Haya ni makazi ya muda, ikimaanisha kwamba anakuwepo hapa wakati kesi yake inafanyiwa kazi. 

Wito wetu ni kwamba ni jukumu la kila mmoja wetu kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Tusikae kimya. Tuchukue hatua stahiki ili watoto wetu waweze kutimiza malengo waliyojiwekea.” 

*Siyo jina lake halisi. 

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts