The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Njia Bora ya Kutatua Kero za Muungano ni Kufufua Mchakato wa Katiba Mpya’

"Kero ya msingi ni muundo wenyewe wa Muungano. [Huu] ni muundo ambao haukutupa Muungano ambao una nchi zilizoungana zina hadhi sawa, zina haki sawa, zina wajibu sawa, zinanufaika sawa, [na] zina fursa sawa".

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Kwa siku za hivi karibuni, Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), zimekuwa zikichukua juhudi za pamoja kuhakikisha kile walichokiita, au wanachokiita, kero za muungano zinatatuliwa.

Mnamo Agosti 24, 2021, wakati akiwepo Zanzibar, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango alisema kwamba jumla ya kero 11 za Muungano zimetatuliwa kwa ajili ya kudumisha Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Ili kufahamu changamoto zilizotatuliwa ni zipi na kama je, kweli utatuzi wake unaweza ukaimarisha Muungano huu kati ya Zanzibar na Tanganyika, au Tanzania Bara, The Chanzo imezungumza na mwanasheria mzoefu na mtu ambaye anafuatilia kwa karibu masuala haya kutoka visiwani Zanzibar Awadh Ali Said.

Awadh ni Wakili wa Mahakama Kuu kanda ya Zanzibar na ameshawahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar pamoja kufanya kazi kama Kamishna wa Tume ya Katiba Tanzania.

The Chanzo: Awadh labda kwa kuanzia tu unaweza kutuambia, hususani kwa niaba ya watu ambao hawakuwa wanafuatilia kwa karibu hili suala, hizi kero au masuala 11 ambayo Dk Mpango alisema kwamba yamepatiwa ufumbuzi, ni masuala yenyewe ni yapi haswa?

Awadh Ali Said: Tulichokishuhudia na kukisikia siku za karibuni ndicho hicho ambacho nazungumzia kwamba ni utiaji saini wa makubaliano ya kuondoa hoja takribani 11, na kwa kweli hawakuziita kero kama ambavyo ulitaja. Mara hii tumeshuhudia kwamba hizi ambazo zikiitwa kero za Muungano sasa zimepatiwa istilahi mpya, zinaitwa hoja. 

Kwa sababu kama unakumbuka huko mwanzo, ilianza-, lugha ilikuwa ni-, watu wakizungumza matatizo yanayotokana na Muungano. [majina kama] matatizo ya Muungano, masuala yasiyo na majibu katika Muungano, baadae tukaambiwa sio matatizo ni changamoto. Ikaja kuwa ni kero. Sasa msamiati umebadilika imekuwa ni hoja. 

Kwa kweli neno lililotumika ni hoja na hii isionekane kwamba haina dhamira yake. Dhamira yake ni kupunguza makali ya yale malalamiko kuhusiana na Muungano sasa kwamba sio matatizo, sio kero, sio changamoto bali sasa ni hoja tu. Kwa hiyo, tuliambiwa kwamba kulikuwa na hoja 11 zilizopata ufumbuzi, na waliingia makubaliano ambayo yalisainiwa na mawaziri husika wa pande zote mbili na tuliambiwa kwamba hoja mbili zilikuwa ni za kiutendaji hazikuhitaji kusaini makubaliano. 

Hija [zenyewe zilizopata ufumbuzi] tulitajiwa kwamba ni hoja inayohusiana na misaada, kwamba Zanzibar inastahiki kupata asilimia 4.5 [ya misaada inayotolewa kwa Tanzania]. Hoja ya Wazanzibari kuweza kuwemo katika utumishi ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Tanzania. Hoja ya mambo ya mikopo kuhusiana na Hospitali ya Mnazi Mmoja, barabara ya Chake-Chake na bandari ya Mpiga Duri, hoja ya ukokotoaji wa huduma za simu unaofanywa na [Bodi ya Mapato ya Zanzibar] ZRB.

Kuna hoja ya mapato yatokanayo na uhamiaji kubakia Zanzibar yale yanayokusanywa Zanzibar. Pia, kulikuwa na hoja ya uvuvi wa bahari kuu. Na pia tukaambiwa hoja nyingine pia ni ya maziwa yanayozalishwa na kiwanda cha Zanzibar kuweza kuingia katika soko la Tanzania Bara. Hizo zikawa ndio hoja ambazo zimepatiwa makubaliano tulivyoona katika vyombo vya habari. Na tukaambiwa kwamba kuna hoja nyingine takribani 7 tukaambiwa zimebaki, [yaani] hizo zinafanyiwa kazi.

The Chanzo: Asante, sasa hizi, kwa sababu wanasema ni hoja za Muungano sasa ni kama vile inaonekana mbona hizi hoja zote zinainufaisha Zanzibar, hakuna hoja yoyote ambayo inahusu Tanzania Bara? Kwa sababu tunafahamu Muungano ni Tanzania Bara na Zanzibar, sasa mbona hizi zote zilizowekwa hapa ni kama vile zinainufaisha Zanzibar?

Awadh Ali Said: Kwa sababu katika muundo wa huu Muungano Zanzibar ndio ambayo iko nje katika muundo wa Muungano kwa sababu Serikali Tanzania Bara imo ndani ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inasimamia mambo ya upande wa Tanzania Bara na mambo ya shirika baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. 

Kwa sababu, kama ukitaka uchambuzi wa muundo wetu wa Muungano hapo ulipoundwa, ni kwamba huu muundo wakati Zanzibar na Tanganyika zinaamua kuungana, waliunganisha mambo na yakaitwa Mambo ya Muungano. Kwa hiyo, wakati huo Zanzibar ili kabidhi [kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania]mambo yake 11 na Tanganyika waka kabidhi mambo 11 hayo hayo . 

Yaani, waliyateua [ikiwemo] polisi, uhamiaji, ulinzi yawe 11 wakayakabidhi yote wakayaweka kwamba haya ni mambo shirika kwamba ni Mambo ya Muungano. Lakini baada ya uteuzi ule wa mambo 11 ambayo yaliachiwa kuwa ni Mambo ya Muungano, baadae yale 11 yakachukuliwa yakaitwa upande wa Tanganyika. Kwa hiyo, sasa ikawa Tanganyika, na baadae Tanzania kwa sababu mwanzo hikuwepi katika Muungano hakukuwa na Tanzania, ilikuwa ni Muungano wa Jamhuri ya Tanganyika na Zanzibar. 

Sasa Tanganyika ikawa inasimamia, kwa muundo huu wa Serikali mbili, ikawa inasimamia yale mambo yake ya mwanzo ambayo hawakuyatoa. Kama ambavyo Zanzibar anasimamia yake ambayo hakuyatoa. Halafu ikawa hiyo Tanganyika inasimamia yale 11 ambayo aliyatoa, lakini aliyatoa kama nadharia tu, yalirudi kwake na yale 11 ya Zanzibar yakarudi kwake.

Kwa hiyo, hivi sasa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ile Katiba yao, ile Serikali yao, lile Bunge kule linasimamia mambo ya namna mbili: mambo ya Tanganyika au ya Tanzania Bara, ambayo si ya Muungano, na yale mambo kwa wakati huu yaliyoanza 11, saizi yako 22, ambayo ni ya Muungano. Kwa hiyo, ndio kama unavyosema, Tanzania Bara imevaa koti la Muungano, kwa hiyo Tanzania Bara imo ndani ya muungano. 

Na kwa lugha ya Spika mstaafu katika kitabu chake, [Historia ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar] Mzee Pius Msekwa, alisema [kulingana na] huu muundo wa Muungano, kwa kweli, Muungano ni Tanganyika na Zanzibar ni mgeni mualikwa, [yaani] ni invited guest. Sasa yale ambayo yamefanywa hivi sasa yote ni kwa sababu Zanzibar haina uwezo wakutatua mambo haya bila ya kupata msukumo kutoka kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Sasa ukiangalia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatatua yenyewe kwa upande wa Tanzania Bara. Kwa sababu, chukulia mfano mikopo ile [kwa ajili] ya Hospitali ya Mnazi Mmoja, Bandari ya Mpiga Duri au barabara ya Chake-Chake. Sasa, kama Zanzibar inataka, mfano katika hilo, wanataka fedha, mfano wanataka fedha wanataka kukopa nje. Sasa haya mambo ni ambayo si ya Muungano kwa sababu hospitali ya Mnazi Mmoja, mambo ya afya [na] si ya Muungano, barabara si mambo ya Muungano. Angalau hiyo bandari unaweza ukasema pengine inaingia kwenye jambo la Muungano lakini uendeshaji wake hajafanyika kama wa kimuungano. Sasa haya ni mambo ambayo ni ya Zanzibar nje ya muungano. 

Sasa mambo kama haya upande wa Tanzania Bara unapotaka kujenga barabara yao Lindi kwenda wapi, wapi kwenda wapi, wao wanatumia ile sovereign guarantee [ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania] kukopa. Kwa hiyo, utatue tatizo gani upande wao na halipo? Wao wanatumia, kwa sababu Zanzibar ilitoa mamlaka yake [ya kukopa, kwa mfano] waikaikabidhi kwenye Muungano, lakini Tanganyika mamlaka yake imo mule mule ndani Muungano ambapo na yeye yumo ndani ya Muungano, sasa yeye hana shida hii. Kwa sababu akitaka kujenga bandari, akitaka kujenga nini, akitaka kuchukua mkopo ikitakiwa sovereign guarantee yeye anayo. Kwa hiyo, utamtegemea vipi utatuzi wa matatizo ambayo yeye hakumbani nayo?

The Chanzo: Nikijaribu kujiweka kwenye nafasi ya, unajua, Mtanzania wa kawaida ambaye yupo huku upande wa Tanzania Bara, unadhani kwa tathimini yako, kwa mtazamo wako, wana huo uelewa, kwa mfano, kama huo ulipozungumzia? Kwa sababu kijuu juu umejaribu kuzungumzia haya hizi hoja 11 za Muungano ambazo Serikali imesema imezipatia ufumbuzi. Kwa jicho la mwananchi wa kawaida picha anayoipata ni kwamba haya mambo yote yanaipendelea Zanzibar na hakuna jambo lolote ambalo linahusu Tanzania Bara, unadhani Watanzania Bara wa kawaida wana huo uelewa wa mambo kama uliyoyagusia hapo kiasi ya kwamba hawatoweza kulalamika wakiona maamuzi kama haya ambayo Serikali imeyafanya?

Awadh Ali Said: Uelewa wa usahihi haupo. Uelewa uliopo ni ule uelewa ambao tulitakiwa tuelewa hivyo. Kwanza, tumeshaondoka kwenye uelewa sahihi hasa. Kimsingi, hata hivi sasa watu hawaelewi kwamba Muungano huu ulioundwa mwaka 1964 uliundwa baina ya nchi mbili huru, mataifa mawili huru ambayo taifa la Tanganyika lilipata uhuru 1961 na likawa na kiti chake Umoja wa Mataifa na wakiwa na ofisi zao za Mambo ya Nje na taifa la Zanzibar likiwa na uhuru wake mwaka 1963 na likiwa na kiti chake cha Umoja wa Mataifa na likiwa na ofisi zake za Mambo ya Nje.

[Tanganyika na Zanzibar] zikaungana, zikiwa nchi mbili huru, na katika sheria ya kimataifa hakuna nchi kubwa wala nchi ndogo, nchi yenye watu wengi [na] yenye [watu] kidogo, yenye eneo dogo [na] yenye eneo kubwa. Hapana, nchi ni nchi. Sasa, hata uelewa huo sasa hivi haupo. Sasa hivi uelewa uliopo ni kwamba Zanzibar ni sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini ni sehemu kama nani, kama wilaya, kama mkoa kama nchi, kama nini? 

Sasa suala la uelewa sio kwamba halipo, lipo lile ambalo sio uelewa sahihi. Ni ule uelewa wa kutengenezwa ambao unatakiwa uelewa uwe huu. Hata leo ile Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 baada ya kutokea figusu figisu, unakumbuka siku zile [Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Peter] Pinda alisema Zanzibar siyo nchi na huku Mwanasheria Mkuu katika Baraza la Wawakilishi akamjibu kwa kumwambia kwamba Zanzibar ni nchi. Ilipokuja ile figisu figisu mwaka 2010 Zanzibar ikabadilisha Katiba yake ikasema Zanzibar ni nchi na ni moja kati ya nchi mbili zilizounda Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa ni majibu kwa uelewa ule. 

Lakini lile nalo lilishutumiwa kwa sababu tayari uelewa uliopo sio kwamba Zanzibar ni nchi na hii inatokana na muundo wetu wa Serikali mbili. Kwa sababu, huu muundo wa Serikali mbili ulikuwa ni muundo wa muda kuelekea kwenye Serikali moja. Sasa watu uelewa wao ni kwamba sisi ni taifa moja, ni nchi moja tunaelekea kwenye Serikali moja. Sasa leo ukija ukisema kwamba Zanzibar ni nchi hata huo uelewa huu watu wanauona ni wa ajabu. Kwa hiyo, ni masuala ya uelewa.

Lakini embu huyo anaejenga [hoja hiyo] kwamba Zanzibar ndio imetatuliwa kero zake, embu muulize: Je, Tanganyika ina kero ipi? Kuna lipi ambalo Tanganyika hawalipati kwa sababu ya Muungano? Tanganyika, kwa kutumia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inakopa [ili] kuendesha uchumi wake. Uchumi si jambo la Muungano. Huduma za afya si jambo la Muungano. Elimu [na] mabarabara, yale mambo ya kijamii yote sio ya Muungano. 

Lakini wao hawa kikwazo kwa sababu wao hawajatoa kitu katika muundo wa muungano huu, Zanzibar ndo ina kikwazo. Hata, angalia jambo moja tu, hivi sasa timu, mpira sio suala la Muungano, je, timu ya Tanzania Bara haikujiunga na FIFA? Ni mwanachama wa FIFA na FIFA inatambua timu ya Sovereign State, [taifa huru]. Kwa hiyo, Tanganyika au Tanzania Bara wanatumia sovereignty [Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujiunga [na FIFA] lakini Zanzibar haiwezi [kufanya hivyo].

Kwa hiyo, katika muundo wa Muungano wetu [huu], kero zote, maisha yote, ni kero zinazotoka [upande wa] Zanzibar. Huwezi kusikia kero ya upande wa Tanzania Bara au Tanganyika kwa sababu ndio muundo wetu ulivyo. Ni muundo unaozalisha kero kwa upande wa Zanzibar. Lakini huisikii kero, au mimi nitajie kero moja ambayo inaisibu upande wa Tanzania Bara. Kitu kimoja ambacho Tanzania Bara hawakipati kwa sababu ya muungano huu, embu nitajie kimoja?

The Chanzo: Watakwambia hawaruhusiwi kumiliki ardhi Zanzibar.

Awadh Ali Said: Sasa kumiliki ardhi Zanzibar si suala la Muungano. Kwa mfano, mimi nataka unitajie jambo ambalo kama siyo Muungano Tanganyika ingekuwa [inalipata]. Zanzibar ardhi yake ndani ya Muungano, ingekuwa nje ya Muungano, [yaani kama] ingekuwa hatujaungana je, [wananchi waishio] Tanzania Bara wangekuwa, mfano, wanahaki ya kumiliki ardhi Zanzibar? Kama hatujaungana hakuna hilo au sio? 

Kwa hiyo, ina maana hata tusingeungana jambo hilo lingekuwa halipo. Mimi ninachotaka unitajie kwamba baada ya kuungana [Tanzania Bara] wamekosa kitu gani ambacho wao wamekikosa kutokana na Muungano. Sio jambo gani hawalipati.  Kimsingi, hata hilo suala la ardhi sio sahihi ivo linavosemwa. 

Ardhi Zanzibar kuna umiliki ambao unamruhusu mtu yeyote, kwa mujibu wa sheria, kumiliki ardhi, [mtu] yeyote! Tena sio Mtanzania Bara tu hata Wataliano, Wajerumani wote wanamiliki ardhi hapa. Huku ardhi za fursa [na za] mahoteli unajua wewe zote zinamilikiwa na wageni. Utaratibu ni kwamba Wazanzibari wenyewe wanapomiliki ardhi wanamiliki katika njia ambayo wananunua au wanarithi kupitia freehold. Mwingine anamiliki kupitia leasehold ambayo hata Tanzania Bara ni hivo hivyo na hiyo hata nchi ambayo ingekuwa [haijaungana] kwa sababu hiyo sio suala la kero au unakosa nini? Ni suala la kwamba sisi hatuna fursa hii. 

Mimi ninachozungumzia ni kile ambacho upande wa Tanzania Bara wanakikosa kutokana na Muungano, wao kama nchi ingekuwa si muungano jambo hili tungelipata. Sasa Zanzibar ingekuwa si Muungano wa aina hii wangeweza kukopa nje, wangeweza [kukopa hizo fedha za kujenga bandari ya] Mpiga duri na [za kufanyia shughuli nyengine]. Zingewezekana. Hizi kero zote ni Muungano na ndio maana zinatatuliwa upande wa Zanzibar kwa sababu kule [Tanzania Bara] hazipo.

The Chanzo: Sawa sawa. Sasa, labda kwa sababu wewe umekuwa ni mtu ambaye ukifuatilia kwa karibu sana haya masuala yanayohusiana na iwe kero, masuala, changamoto, matatizo ya Muungano. Nataka kupata tathimini yako kwenye haya masuala yaliyotatuliwa. Unadhani ni kwa kiasi gani au kwa kiwango gani yataenda kuboresha au kuimarisha huu Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika?

Awadh Ali Said: Tumetibu, kwa kweli tumetibu lakini tumetibu ishara, hatujatibu maradhi.

The Chanzo: Sijakuelewa nataka ufafanue.

Awadh Ali Said: Mfano, wewe unaugua malaria. Tatizo lako ni malaria lakini malaria inaleta homa, inaleta kutapika, inaleta kuumwa kichwa, inaleta kutokuweza kula, inaleta vitu vingi [lakini] tatizo ni malaria. Sasa ukimeza Panadol kile kichwa kitashuka kidogo [lakini] badae kitarudi. Kwa sababu hujaitibu malaria. 

Sasa leo wanatibu suala la barabara ya Chake-Chake, kesho [Zanzibar] wakitaka kujenga suala la barabara ya Makunduchi kero ile ile [ya kulazimika kuomba kibali cha kukopa kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania] ya aina ile ile itarudi tena. Leo kuna hili suala la [Hospitali ya] Mnazi Mmoja kesho wakitaka kujenga hospitali ya Chake-Chake halafu wasipewe mkopo kero kama hii itarudi tena kwa sababu umetibu ishara, umetibu matokeo, hujatibu tatizo, tatizo ndio kero hizi ni hoja kweli. Mimi nakubaliana nao wanapoziita hoja hizi kwa sababu hizi ni hoja lakini ile kero ya msingi ni ile malaria. 

Sasa hapa itapozwa saizi imepata ni kama vile kwamba katika Muungano huu ni kama kwamba wewe ulitoa chako na yuke mwenzako katoa chake baadae kile cha shirika kakitia kule kwake anakiendesha wewe huelewi na unaangalia. Lakini ukipata matatizo unamwambia bwana mimi sina kitu, [anakuuliza] kwani tatizo nini? [Unamwambia] mtoto anaumwa ghafla nataka nimpeleke hospitali, [anakwambia] basi chukua hiki!

The Chanzo: Na kero ya msingi kwa hiyo ni ipi kwa mtazamo wako?

Awadh Ali Said: Kero ya msingi ni muundo wenyewe wa Muungano. [Huu] ni muundo ambao haukutupa Muungano ambao una nchi zilizoungana zina hadhi sawa, zina haki sawa, zina wajibu sawa, zinanufaika sawa, [na] zina fursa sawa. Leo ukiutazama Muungano wa Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan ya Kusini, wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wale wote wanaingia pale on equal terms [wakiwa sawa]. [Maana yake ni kwamba] unachonufaika wewe na huyu ananufaika [nacho]. 

Kwa hiyo, muundo wetu ulitegemewa ni muundo wa Serikali mbili kuelekea moja. Sasa wakati Serikali mbili kuelekea moja muundo huo ambao ni wa muda ulikusudiwa, huko Serikali moja hatujafika wakati hilo linaitikisa Zanzibar kero hazitaisha kwa sababu huu [wa sasa] haukuwa muundo wa kudumu. 

Ni kwamba tu haujatimia na hujaungwa mkono kwa upande wa Zanzibar lakini muundo huu ulikuwa ni wa muda wa kuelekea kwenye Serikali moja. Kwa hiyo, kero ya msingi ni ya muundo. Sasa, muufumue muundo muweke muundo ambao utazionesha nchi mbili zilizoungana Zanzibar ile pale, Tanganyika ile pale na tuliyoungana haya hapa ya shirika. Na tunayafanyia kazi kwa manufaa ya pande zote mbili na ni sawa sawa sizungumzii usawa kwa maana ya kwamba usawa wa equality nazungumzia usawa kwa maana ya equity.

Mfano, hata kama manufaa yanakuja, mfano hilo suala la [mapata yatokanayo na] uhamiaji walililolizungumza, suala la uhamiaji ni la Muungano, lakini ukikusanya mapato kutoka uhamiaji, mengi yatatoka upande wa Tanzania Bara kwa sababu kule hata walipa kodi unaweza kukuta kwa mwaka wachukua watu laki tano, Zanzibar ni watu elfu tano. Kwa hiyo, hata ikija katika mgao, equity itahitaji kwamba kule [Tanzania Bara] kwende [mapato] zaidi lakini chini utaratibu maalamu utakaosimamia kwamba na Zanzibar [yanakwenda mapato] stahiki. [Maana yake ni kwamba] kuwe na framework, kuwe na formula maalumu. Lakini leo unawezaje kuja na formula wakati upande mmoja [wa Muungano] upo [yaani] Zanzibar, hiyo Tanganyika ipo wapi? 

Tanganyika imeingia ndani ya Jamhuri ya Muungano na ndio maana wakakwambia imevaa koti la Muungano. Kwa hiyo, kama hamjaenda kwenye tatizo la msingi ni kujibabaisha tu. Leo tutatatua barabara, tutatatua bandari hii, tutatatua hospitali hii, kesho maendeleo yatahitaji tujenge hospitali nyingine mtakuja tena mtasaini hoja nyingine ya hospitali ya Kivunge, [hospitali ya] vitongoji Pemba, barabara ya Makunduchi na barabara ya Nungwi. Mtakuja hivyo hivyo tu kila siku.

The Chanzo: Sasa tunaliendeaje, kwa mfano tukitaka kujibu hiyo kero ya msingi au hilo jambo la msingi, tunaliendeaje, yaani tunafanyaje?

Awadh Ali Said: Tunaliendea kwa namna walivyotaka wananchi kupitia mchakato wa Katiba Mpya uliosimamiwa na Tume ya Kurejebisha Katiba Tanzania iliyosimamiwa na Jaji [mstaafu Joseph] Warioba, maarufu Tume ya Warioba. [Tume hii] ilipendekeza mfumo wa Serikali tatu, iwepo Zanzibar na Serikali yake na mambo yake, iwepo Tanganyika na Serikali yake na mambo yake, na iwepo Serikali ya Jamhuri ya Muungano ambayo itasimamia mambo machache ya Muungano. 

Na hilo lilipendekezwa pia na Tume ya Jaji Nyalali, lilipendekezwa pia na Tume ya Jaji Kisanga. Tume zote zilizoundwa kutatua mambo ya Muungano zilipendekeza hilo na hiyo ndio tiba ya kudumu. Hii kuja sasa hivi mtoto anaumwa, mtoto hana ada ya shule unamsidia unamwambia basi ntakufanyia hiki. Hilo sio suala la kitaifa, sio suala la kudumu ni suala la zima moto tu, pale kuna moto unawaka tunakwenda kuzima. Miungano haiendeshwi [kwa] namna hiyo.

The Chanzo: Awadh mimi nakushukuru sana kwa muda wako na nakutakia majukumu mema.

Awadh Ali Said: Na mimi nakushukuru Khalifa [Said, mwandishi], nakushukuru sana.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 Responses

  1. The Chanzo kwanza pongez Sana kwenu kwa maswali mazuri na ya msingi Sana ktk mahojiano hayo, lkn pia pongez kwa Mwanasheria kwa majibu yake mana kuna vitu wengne sie ndo mara ya kwanza kuvickia imekua darasa zuri Sana kwangu. Lkn pia najiuliza kwanin hadi hii leo ni awam ya sita ya utawala Tz na Zanzibar ni awam ya nane lkn bado muungano wetu unaonekana una uwalakin? Japo nchi imetulia lkn nahisi kuna mivutano isionekana moja kwa moja! Je ni kwamba viongoz wetu hawatilii maanani masuala hayo? Au hayo mambo ni wanasheria ndo wameshindwa kuyashughulikia tangu muungano?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *