Dar es Salaam. Siku ya Alhamisi, Oktoba 7, 2021, itakumbukwa katika historia ya dunia kama moja ya siku ambayo Watanzania wengi ulimwenguni kote waliunganishwa na kufurahishwa na hatua ya Mtanzania mwenzao anayeishi nchini Uingereza Abdulrazak Gurnah kutangazwa kama mshindi wa Tuzo za Nobeli katika kipengele cha Fasihi.
Kwa hatua hiyo, Gurnah, 73, anakuwa mshindi wa 118 katika kipengele cha fasihi toka mwaka 1901. Gurnah ni mwandishi wa riwaya 10, ikiwemo riwaya zake mbili mashuhuri za Paradise na Desertion. Tuzo hiyo ya Nobeli ina thamani ya dola milioni 1.14 za kimarekani.
Kihistoria, Gurnah alizaliwa na kukulia Zanzibar mpaka alipofikisha miaka 18 na kuhamia nchini Uingereza mwishoni wa miaka ya sitini. Amekuwa akifundisha Chuo Kikuu cha Kent nchini Uingereza na mara nyingi amekuwa akielezea hadithi na shuhuda nyingi kuhusu Zanzibar kupitia mihadhara na maandishi yake mengi.
Watanzania wengi wamepokea habari za Gurnah kushinda tuzo hiyo kwa furaha kubwa, wengi wakionesha kushangilia katika mitandao ya kijamii. “Habari njema, Mtanzania wa kwanza (Mzanzibari) kushinda tuzo za Nobel,” anaandika Zitto Kabwe kwenye ukurasa wake wa Twitter. “Abdulrazak Gurnah ameshinda tuzo za Nobeli katiika fasihi.”
Tuzo hii imeenda kwa Abdulrazak Gurnah kwa sababu ya kazi zake hasa zinazoangazia swala la ukoloni na wakimbizi, huku Zanzibar ikitajwa katika kazi zake nyingi. Ni mwana halisi wa Zanzibar na Zanzibar haijawahi kutoka moyoni mwake.
Hata hivyo, wakati Gurnah na Watanzania wengine waishio ughaibuni wakijivunia Utanzania wao, sheria za Tanzania haziwatambui pale wanapochukua uraia wa nchi nyingine. Raia hao huonekana ni wageni wasiostahili haki za utaifa. Sheria za Tanzania hazina nafasi kwa uraia pacha na hiki kimekua kilio cha Watanzania wengi waishio ughaibuni.
Tanzania haijawahi kuchoka kujivunia watu wake wanaoishi nje za nchi pale wanapofanya vizuri, hata kama ni kupitia bendera ya taifa jengine. Hii ilionekana katika kombe la dunia kwa mchezaji wa Denmark, Yussuf Poulsen na hata katika mashindano ya Olympiki kupitia mwanamichezo wa Ujerumani, Malaika Mihambo, wote wakiwa na asili ya Tanzania. Lakini linapokuja suala la kuwatambua kisheria, kumekua na mzunguko wa muda mrefu usioisha.
Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje Liberata Mulamula wakati akiongea na raia wa Tanzania waishio ughaibuni alizungumzia juu ya kuja na hadhi maalumu, akielezea kuwa suala la uraia pacha lina mlolongo mrefu wa Kikatiba. Inategemewa mpaka mwishoni wa mwaka huu baada ya kukamilika kwa mapitio ya sera ya mambo ya nje jambo hili la hadhi maalum litafanyika.
Hata hivyo, kwa wanadispora wengi kilio chao kikubwa kimekuwa kupata uraia pacha, huku wakiamini hatua hiyo itawawezesha zaidi katika kuwekeza na kutumika moja kwa moja katika kuchangia uchumi wa taifa lao kama ilivyo kwa wenzao wa nchi za Afrika, kama vile Kenya.