The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Catherine Ruge: Mambo Niliyopitia Kwenye Maisha Yamenifanya Niwe Imara Zaidi

Nje ya siasa na harakati, Catherine anatumia muda mwingi na watoto wake, anasema pia anakipenda sana kitanda chake.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Leo kwa bahati nzuri tumepata fursa ya kuzungumza na Catherine Ruge, Katibu wa Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA), lakini pia mbunge mstaafu wa viti maalumu kupitia tiketi ya CHADEMA kwa Jimbo la Serengeti. Mnamo mwaka 2020, Ruge aligombea ubunge wa jimbo la Serengeti kupitia tiketi ya CHADEMA. Na leo, kwa bahati nzuri, tumebahatika kumualika kwenye Podcast yetu hii kuzungumzia, sana sana, harakati zake za kisiasa na mustakabali mzima wa BAWACHA na CHADEMA kwa ujumla na hali ya siasa zetu za nchi kwa sasa. Endelea … 

The Chanzo: Dada Catherine, karibu sana kwenye Podcast hii ya The Chanzo.

Catherine Ruge: Asante sana. Nashukuru leo kupata fursa ya kuwa sehemu ya Podcast za The Chanzo. Nashukuru sana, Khalifa [Said, mwandishi]. 

The Chanzo: Nashukuru sana. Labda kwa kuanzia, nataka unisaidie, hili linaweza likawa ni suala binafsi kusema kweli, Msubhati maana yake ni nini? Kwa nini unajiita Catherine Ruge Msubhati, na ndivyo inavyotamkwa hivyo kabisa au nakosea? 

Catherine Ruge: Kwa Kiswahili, hiyo ndiyo njia sahihi ya kuitamka Msubhati, lakini kwa kule [kwetu], kwa kilugha wanasema Msuvati, unaelewa? 

The Chanzo: Yaani hii bh inatamkwa kama v?

Catherine Ruge: Ndiyo. Msuvati. Lakini kwa kuiandika lazima utaandika Msubhati na mtu atasoma kwa jinsi ambavyo, si unajua kuna zile lugha za makabila, [kwa hiyo] linaandikwa hivyo lakini hauwezi kulitamka hivyo. Lakini wale wenyewe, wenye lugha yao ndio wanatamka hivyo. Kwa hiyo, njia sahihi ya kutamka ni Msuvati au Omosuvati. Msuvati au Omosuvati kwa sababu kule kuna makabila [mawili]. Kuna Wakurya [na] kuna Wangoreme. Kwa hiyo, Wakurya wanasema Msuvati, Wangoreme wanasema Omosuvati lakini ni makabila yanayoingiliana. Kwa hiyo maana yake ni dada [au] binti anayeheshimika katika jamii. 

The Chanzo: Hiyo inavutia sana.

Catherine Ruge: Ni kweli.

The Chanzo: Asante sana. Na bila shaka historia yako itakuwa imeshaandikwa sehemu fulani na nafahamu pia kwamba wewe ni moja kati ya wanasiasa wachache Tanzania wanawake ambao wanakurasa kwenye mtandao wa Wikipedia ambao unaelezea wewe ni nani, maisha yako na vitu kama hivyo. Lakini pengine kwa niaba ya watu ambao hawafahamu majukwaa hayo, kama hizo za Wikipedia, nilikuwa nataka uelezee kwa ufupi labda hivi safari yako ya kisiasa ilianzia wapi? 

Catherine Ruge: Sawa. Labda niseme kuna vitu vinaweza vikakutokea kwenye maisha na ukawa unahisi labda ni curse, curse sijui kwa Kiswahili mnaitaje? 

The Chanzo: Laana. 

Catherine Ruge: Ni laana, lakini kumbe kupitia hiyo laana, ukaja ukawa [sehemu ya] suluhu katika jamii unayotoka. Sasa mimi katika maisha yangu nina safari ambayo sio, ni safari ambayo ina taabu yaani. Sio safari ambayo imenyooka. Nimepita kwenye mabonde [na] milima lakini njia yote niliyopita, safari yote ambayo nimetembea, imenifanya nimekuwa imara sana. Kwa hiyo, nasema yale yote niliyoyapitia yamenijenga sasa hivi [na] yamenijenga sana. 

Kwa hiyo, mimi nikiwa katika umri wa miaka 11 nilitakiwa nikeketwe. Nadhani unafahamu mila na desturi za makabila hasa ya Mara, [kabila la] Wamasai, [mkoa wa] Singida [na kwengineko] mtoto wa kike miaka hiyo ilikuwa ni lazima akeketwe na kama hajakeketwa basi wewe kwanza sio Msubhati na wala huonekani kama ni mtu kwenye jamii. Kwa hiyo, nikiwa na umri wa miaka 11 tu nilitakiwa nikeketwe. Kwa sababu familia niliyokuwa natoka ilikuwa inaamini kwenye hilo jambo. 

Kwa hiyo mimi nilinusurika na ukeketaji. Nilinusurika ukeketaji na nisingependa nizungumzie nimenusurika vipi. Kwa sababu inagusa familia yangu na hawafurahii [mimi kuzungumzia jinsi nilivyonusurika]. Kwa sababu ni kitu ambacho walikifanya bila kujua. Kwa hiyo, nilishafanya mahojiano huko nyuma [kuhusiana na mada hii na kueleza] yale ambayo yalitokea lakini familia yangu iliumia. Hiyo ilikuwa nafikiria mwaka 2018 kwa hiyo familia yangu iliniumiza. Kwa hiyo naomba tuushie hapo hapo kwa nilinusurika ukeketaji na jamii niliyokuwa natoka na familia niliyokuwa natoka ilikuwa inaamini hivyo kwamba ni lazima mtoto wa kike ili awe mtoto wa kike ni lazima apitie hatua hiyo [ya ukeketaji] kwenda kwenye hatua nyingine [ya makuzi]. 

Na [jamii ninayotokea] ilikuwa inaamini ni heshima na ili uweze kuolewa ili uonekane wewe ni Msubhati ni lazima ukeketwe. Kwa hiyo, mimi nilinusurika. Kwa hiyo, kwa kipindi hicho sikuwa najua madhara ya ukeketaji lakini niliogopa. Kimsingi [ni] kwa sababu nilishuhudia binti wa baba yangu mkubwa wakati anakeketwa alizimia na akatokwa na damu nyingi sana. Sasa, kwa sababu nilikuwa na umri kama wa miaka mitano hivi, nafikiri nilikuwa na umri wa miaka mitano, nilijua amefariki kwa sababu mpaka naondoka kwenye ile sherehe jioni saa 12 hakuwa ameamka. Kwa hiyo, nikawa nimepata woga. Kwa hiyo, na mimi nikawa naogopa. Nikawa sitaki na hivyo ndivyo nilivyonusurika na ukeketaji. 

Kwa hiyo baadae, katika kusoma, umeelewa? Katika kusoma, katika safari yangu ya maisha, nikaelewa madhara sahihi, na kwa sababu baada ya kuwa nimenusurika nilitengwa, nikaonekana sio mtu kawaida. Kwa hiyo, dawa pekee [ya kupambana na hali hii ya kutengwa] mimi niliiona ni kusoma, [yaani] ni kupata elimu. Sifahamu [ni lini] mimi nimepata akili [ya maisha]. [Labda] nikiwa darasa la nne, yaani ile akili kabisa kwamba yaani akili ya maisha. Kwa hiyo, nilikuwa nikikua vyema sana kiakili, unaona? Akili yangu wakati nipo darasa la nne nadhani labda ilikuwa ya mtu wa kidato cha pili. 

Kwa hiyo, nikasema lazima nishike elimu, [lazima] nimkamate huyo [mtu anayeitwa] elimu. Kwa hiyo, nilisoma na mimi nimesoma shule zote za Serikali. Kwa hiyo, nilipomaliza darasa la saba, nikaenda Shule ya Sekondari ya Wasichana Msalato. Nikamaliza nikachaguliwa [kwenda] Shule ya Sekondari ya Kilakala. [Baadaye] nikaenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Baada ya hapo nikafanya CPA [mafunzo maalumu ya kiuhasibu]. Nikaajiriwa nikiwa chuo kwa sababu nilikuwa mwanafunzi wa kwanza [kwenye darasa langu]. Kwa hiyo, hivyo ndio ikaenda hivyo safari yangu. 

Sasa, ngoja nirudi kwa nini niliingia kwenye siasa. Kwa hiyo, nilivyomaliza kidato cha sita, wakati nimerudi sasa kijijini, msomi sasa, naonekana mtoto msomi mtukutu [anacheka], kwa hiyo nikaanza kuongea na familia yangu [kuhusu ukeketaji], unaona, kwamba madhara ya hivi vitu na nini. Lakini pia, katika kipindi hicho mimi namaliza kidato cha sita, nikawa nimeweka mfano kwa kuigwa [kwenye eneo la kukataa kukeketwa]. Kuna wadogo zangu ambao walikuwa wanakataa kukeketwa. 

The Chanzo: Hiyo ilikuwa ni mwaka gani? 

Catherine Ruge: Wakati namaliza kidato cha sita? Ilikuwa [mwaka] 2004 nafikiri. Nafikiri [ilikuwa ni] 2004. Kwa hiyo wakati ule kulikuwa na watu tayari, ndugu zangu wengine, watoto wa baba mkubwa, wadogo, mashangazi [wote] walikuwa wanakataa wanasema, “Mbona Dada Catherine amekataa [kukeketwa]?” Kipindi hicho jina la nyumbani naitwa Nyakao. 

The Chanzo: Unaitwa? 

Catherine Ruge: Nyakao, jina langu la nyumbani. Ndiyo hivyo. [Wale mabinti wakawa wanasema]: “Mbona dada Nyakao amekataa? Mbona ameendelea kufaulu [shuleni na vyuoni]? [Dada Nyakao] aliambiwa hatakuwa mtu yeyote kwenye maisha.” Wakati huo nilikuwa bado sijaolewa lakini baadae nilivyoolewa [hawa mabinti wakaendelea kuhoji] wakasema, “Mbona ameolewa? Mbona vitu vyote aliambiwa atakuwa hajawa?”

Kwa hiyo, kuna vitu mimi niliisaidia familia yangu kuvunja ile desturi au utaratibu uliokuwepo. Kwa hiyo, watu walikuwa wana uwezo wa kukataa [hivi vitendo vya ukeketaji]. Tena wao walikuwa hata hawakimbii. Walikuwa wanakataa na hawafanywi jambo lolote, umeelewa? Kwa sababu walikuwa wananitolea mimi mfano. Kwa hiyo, mimi nashukuru Mungu kwamba niliweza kuweka huo mfano ambao ni chanya katika familia yangu na katika jamii [yangu] na watu wakaanza kukataa kukeketwa kupitia mimi. 

Kwa hiyo, nikawa natoa elimu, naongea na wadogo zangu, naongea na dada zangu, naongea na mashangazi, bibi, na nani na nani. Wakati nimeanza kufanya hivyo, kwa hiyo ikawa kila nikienda likizo ilikuwa ni lazima nizungumzie hilo jambo. Kwa hiyo, nikaanza kutoa elimu kwenye jamii inayonizunguka na baadae nilipoanza kufanya kazi nikaamua kuendelea sio tu kwenye jamii yangu, nikawa naenda kwenye kijiji kingine [ambacho] kuna sherehe [inafanyika], nitawaita watu nitazungumza nao. Yaani, [kwenye sherehe] nitaanzisha mada ya [ukeketaji]. 

Baadaye, nikaanzisha [shirika lisilo la kiserikali] NGO, unaona, kwa hiyo nikaanza kufanya harakati za kukomesha vitendo vya ukeketaji. Hiyo ilikuwa ni [mwaka] 2013 nafikiri. Nikaanza kufanya utetezi shuleni, kwenye jamii, shule za sekondari [ambako nilikuwa] nakutana na wale mabinti wanaotakiwa wakeketwe maaana mara nyingi wanakeketwa aidha wakiwa wamemaliza darasa la saba au wakiwa kidato cha pili. 

Kwa hiyo, nazungumza nao [mabinti], nazungumza na walimu, nazungumza na wazazi, nazungumza na wazee, unaona? Ingawa walikuwa wananiita mtoto mtukutu, [wakisema]: “Yaani, yule dada anatuharibia watoto” na nini. Sasa hapo sikuwa mtoto tena. Hapo tayari nimeolewa na nina mtoto mmoja tayari. Nilikuwa mama. Kwa hiyo, wakawa wanasema “Anatuharibia watoto wetu, anatuharibia watoto wetu.”

Sasa ule utetezi niliokuwa nafanya, watu wakahisi kwamba labda mimi nataka kuwa mtu fulani kwenye jamii, unaona, umeelewa? Kwa hiyo, watu wakawa wanasema, “Yule dada anatakiwa awe mbunge.” Kwa hiyo, ulivyofika [mwaka] 2014 wakati heka heka za uchaguzi zinaanza wakaanza kusema, “Yule dada tumtafute, tumtafute.” kwa hiyo, watu wakaanza kunitafuta kwamba nigombee ubunge na nini na nini lakini mimi sikuwa nimevutiwa sana na siasa. Mimi nilikuwa nimevutiwa na masuala ya kijamii. Tena jamii ninayotoka [ili niisaidie] kuondokana na zile mila potofu. 

Lakini pia nilikuwa nafanya utetezi watoto wa kike wapelekwe shuleni kwa sababu wazazi walikuwa hawataki kupeleka watoto wa kike shuleni hata kama amefaulu anaambiwa aolewe. Kwa hiyo, nilikuwa napambana kweli kweli. Kwa hiyo, watu wakaona mimi nafaa kuwa mwakilishi wao, unaona? Kwa hiyo, mimi nilikuwa tayari nimejiunga na CHADEMA toka nipo chuo. [Tangu kipindi hicho] nilikuwa niko CHADEMA lakini sikuwa active kwenye siasa. Kwa hiyo, baada ya kushawishiwa nikarudi Serengeti nikaanza kujihusisha na  CHADEMA na nini na nini na baadae nikaingia kwenye siasa. 

Kwa hiyo hivyo ndivyo nilivyoingia kwenye siasa. Bahati nzuri mimi ni mwanamke ninayejituma sana. Ni lazima utanitambua tu. Hata nikiwa sehemu nisiongee jambo, utanitambua tu. Kwa hiyo, nikaingia kwenye chama [na] kwa sababu ya juhudi zangu na uwezo wangu nitambulika, unaona? Kwa hiyo, nikagombea [kwenye Uchaguzi Mkuu wa] 2015 sikushinda. Lakini nilifanya kampeni kwenye jimbo langu [na] kwa mara ya kwanza tukapata mbunge wa upinzani kwa sababu [Marwa Ryoba Chacha, aliyehamia Chama cha Mapinduzi – CCM, 2018] nilikaa siku 72 jimboni nikifanya kampeni bega kwa bega na yule mgombea ambaye alikuwa ni mgombea wa jimbo. [Mimi] nilikuwa mgombea wa viti maalumu. 

The Chanzo: Sawa, maana yake ni kwamba ulijaribu kutafuta ridhaa ya chama chako kugombea lakini kura hazikutosha kwenye kura za maoni, sivyo?

Catherine Ruge: Hapana, ngoja nifafanue.

The Chanzo: Sawa.

Catherine Ruge: Ni kwamba sikugombea jimbo 2015. 

The Chanzo: Sawa. 

Catherine Ruge: Niligombea viti maalumu.

The Chanzo: Nimekuelewa.

Catherine Ruge: Lakini ili upate [ubunge wa viti maalum] lazima kuwe na kura za mbunge, za wabunge wa majimbo. Kwa hiyo, ili upate nafasi ya kuteuliwa mbunge wa jimbo unalotoka akishinda unakuwa na nafasi nzuri ya kuteuliwa kwenye nafasi ya viti maalumu. Kwa hiyo, mimi nilishiriki kwenye kampeni za mbunge wa jimbo langu asilimia 100 hususan kutoka kwenye upande wangu kwa sababu kule [mkoani Mara] kuna siasa za makabila. Na mimi natoka kwenye familia kubwa sana kwa ukanda ambao natoka, familia yetu ni kubwa sana ni familia ya wasomi, yaani kwenye ukanda ninaotoka familia yetu ndio familia ambayo imesomesha watu wengi, yaani sisi tuna wahitimu zaidi ya 40 ambao ni vijana. 

The Chanzo: Kwenye familia yenu? 

Catherine Ruge: Kwenye familia yetu.

The Chanzo: Sawa sawa. 

Catherine Ruge: Waalimu, wanasheria, madaktari, wauguzi nakadhalika. Hususan vijana wakiume, tuseme vijana wa kiume wengi ndio wamesoma. Kimsingi, juzi ndio tumepata msichana wa pili aliye na shahada kwenye familia yetu, mimi ndiyo nilikuwa wa kwanza. Mimi ndio nilikuwa mwanamke wa kwanza kabisa kwenye familia yetu ya Ruge kuwa na shahada. 

The Chanzo: Waooo! 

Catherine Ruge: Yaani shahada. Wapo wenye stashahada na nini hizo ngazi za chini, kama vile astashahada. Na baadae juzi ndio tulimpata mhandisi. Tumepata mhandisi, kwa hiyo kwa sasa [familia yetu] tuna mhasibu mwanamke na tuna na mhandisi [mwanamke]. Lakini tunao wahasibu kibao karibia saba.

The Chanzo: Wanaume? 

Catherine Ruge: Wanaume. Kwa hiyo, bado hata familia yangu na yenyewe ilikuwa inaamini kwenye kuwapa fursa vijana wa kiume zaidi ya vijana wa kike au mabinti, unaona? Kwa hiyo, bado hicho kitu kilikuwepo pia kwenye familia yetu, unaelewa? Lakini [hali] kwa sasa haiku hivyo. Sasa hivi wote tunapata fursa sawa na ndio maana juzi tumepata binti wa pili ambaye amekuwa mhandisi. Lakini tunao hawa wa chini wenye stashada za pharmacy, astashahada za uuguzi na kadhalika, waalimu nakadhalika.

Hivyo ndivyo ingia kwenye siasa. Kwa hiyo 2015 sikuweza kufanikiwa kuingia [bungeni kama mbunge wa viti maalum] kwa awamu ya kwanza kwa sababu yale majina huwa yanapangiliwa. Mimi nilikuwa namba 38 na [na CHADEMA] tukapata nafasi za watu 36. Baadae yakaenda kwenye uchaguzi mdogo, akaenda mtu wa 37. Lakini [ni kama vile] kulikuwa na baraka iliyojificha [kwani] kuna mbunge alifariki [Dk Elly Macha, aliyefariki Machi 2017], Mungu amrehemu, mimi nikaenda kuchukua nafasi yake kwa sababu nilikuwa namba 38 kwenye ile orodha ya [Tume ya Taifa ya Uchaguzi] NEC.

Kwa hiyo mimi niliingia bungeni kati kati ya mwaka 2017 [na] nimekaa miaka mitatu, au miezi 31. Kwa hiyo, baadae nikaona nimejengewa uwezo nikaenda jimboni, nikaenda kugombea jimboni na kuandika historia kwani nilikuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya jimbo letu [kwa mwanamke] kugombea ubunge, yaani kwa hiyo kulikuwa na hamasa kubwa hasa miongoni [mwa] wanawake na vijana.

Kwa hiyo, wakaniita Msubhati. Hilo jina sio kwamba mimi nilijipa. Wao [wananchi] wenyewe [ndo walinipa] kwa sababu ya ile heshima ambayo nimewapa [kwa kuwa] mwanamke wa kwanza katika historia kwenda kusimama jimboni wakaniita Msubhati. Kwa hiyo, [ikawa] ni Msubhati [na] Msubhati ndio anagombea. Yaani [wananchi walikuwa] wanasema hii ni zamu ya Msubhati kwamba hii ni zamu ya mwanamke, ni zamu ya dada, ni zamu ya binti. Ndio ilikuwa hivyo mpaka kuna wimbo walinitungia wakasema hii ni zamu ya Msubhati.

The Chanzo: Nadhani huko tutakuja. Bila shaka ningependa sana kufahamu mtazamo wako kama mgombea mwanamke. Lakini kwa mfano tukirudi nyuma kidogo tu kwenye-, na kwa sababu una historia hiyo, unajua kufanya uchechemuzi au uwanaharakati dhidi ya masuala ya ukeketaji, nilikuwa nataka nifahamu pengine kwa mtazamo wako kwa nini, kwa mfano, hivi vitendo vimechukua muda mwingi sana kuweza kukomeshwa labda, unadhani ni nini kinachochea pengine jamii kuendeleza vitu kama hivi kwa ufupi tu?

Catherine Ruge: Unajua mila ni imani kama ilivyo imani ya dini, unaelewa? Kwamba unaamini kwenye Uislamu au unaamini kwenye Ukristo, kwa hiyo kumuondoa mtu kwenye ile imani yake inachukua muda. Lakini sababu nyingine ambayo imesababisha kuchelewa [kutokomezwa kwa vitendo hivi] ni kwamba ilitokea kwamba Serikali haikuwa imejihusisha sana na hili jambo, ikawa imeachia NGOs zaidi, unaelewa? Yaani, Serikali haikujitoa kwamba iko tayari kushughulikia hili jambo kwa umakini, kwa hiyo hizi harakati zilianza kufanywa na NGOs kama utasoma historia ya hizo harakati.

Sasa NGOs inaweza ikawa NGO ya nje au zinashirikiana na za hapa za Tanzania ile, lakini ule umiliki [wa harakati] unakuwa kwanza hakuna. Hicho ni kitu moja. Mbili, kwa sababu ni kitu ambacho kinaingizwa kutoka nje ya jamii au nchi [kwa hiyo] jamii inaona kwamba hili sio jambo letu, umeelewa, kwamba wanakuja hapa [African Medical and Research Foundation] AMREF natoa mfano wa AMREF kwa sababu ni watu ambao nimefanya nao kazi, mimi ni balozi wa AMREF dhidi ya ukeketaji Afrika. Kwa hiyo, mimi naenda pia kufanya hizi shughuli [za utetezi] kwenye nchi nyingine pia za Afrika lakini mimi ni balozi na kuna mabalozi pia wengi, nadhani tupo kama kumi.

Sasa utakuta AMREF wanaleta mradi, unaona, hilo ni shirika la nje [linalojihusisha na masuala ya afya] kwa hiyo watu wanaona kama hawa ni watu wamekuja tu na nini, [jamii] haiwachukulii kwa umakini. Wanashirikiana sawa na wazawa lakini hakuna ule umakini ambao ungeweza kuutarajia. Kwa hiyo, unakuta labda ni mradi kweli [wenye lengo la kutatua tatizo lakini] ikiisha watu wanaendelea na mambo yao kama kawaida.

Kwa hiyo, moja ni elimu kwa sababu [haya mambo ni ya] kiimani na inachukua muda [kuyaondosha]. Kwa hiyo, elimu lazima iendelee kutolewa. Kwa hiyo, ndio sababu kumuondoa mtu kwenye imani yake inachukua muda. Lakini kitu cha pili ni hiyo kwamba mara nyingi miradi mbalimbali ilikuwa inafanywa na wahisani au na wafadhili au na NGO za nje. Kwa hiyo, Serikali imeanza kujihusisha kwa umakini zaidi [kwenye hivi vitendo vya ukeketaji] miaka ya 2000.

Hapo ndo Serikali ikaanza kuchukua nafasi yake na kukawa na-, bila shaka sheria ilikuwepo lakini ilikuwa haitekelezwi. Sasa wakaanza kutekeleza sheria kwamba mtu anaye keketa mtoto anaweza kushtakiwa na pia akahukumiwa. Kwa hiyo, hukumu zimeanza kutolewa. Ni miaka ya 2000 tu ndo wameanza kutoa hizo hukumu, zile hukumu mtu anafungwa miaka saba, miaka kumi, miaka 15, [ambao] ni wazazi pamoja na wale mangariba [wanaotekeleza hizi mila].

Kwa hiyo, tuseme sababu ninazoziona ni hizo mbili: mikakati ilikuwa ikifanywa na watu wa nje zaidi ya Serikali lakini pia imani ni ngumu kumuondolea mtu. Na mpaka sasa hivi watu wanaendelea kukeketa na kukeketwa lakini sio kwa kiwango kile kilichokuwepo maana zamani ilikuwa ni ukienda Disemba kijijini acha kabisa! 

The Chanzo: Zamani maana yake ni lini? 

Catherine Ruge: Miaka ya 1990, miaka ya tisini maana mimi nilinusurika [kukeketwa] mwaka 1994, umeona? Kwa hiyo, miaka hiyo ya tisini. Mimi nimeanza kushuhudia kwa mara ya kwanza mtu anakeketwa mwaka 1990.

The Chanzo: Sawa sawa. 

Catherine Ruge: Kwa hiyo, imeenda 1990 yote imeisha, 2000 mwanzoni imeendelea mpaka 2003 pia nimeshuhudia 2004 nimeshuhudia hivyo vitendo vinafanyika. Kwa hiyo, kuanzia kati kati ya 2000 nadhani ndio kulikuwa na mikakati ya makusudi inayotekelezwa na Serikali kukomesha hivyo vitendo.

The Chanzo: Sawa sawa. Turudi kwenye siasa. Kama ulivyoelezea wewe mwenyewe mwaka 2015 ulijihusisha na siasa, namaanisha zile siasa haswa za ushindani, ikiwemo kumpigia kampeni mgombea wa CHADEMA kwenye Jimbo la Serengeti, sivyo?

Catherine Ruge: Ndio. 

The Chanzo: Sawa sawa. Na tunafahamu kwamba mwaka 2020 uligombea kwa tiketi ya CHADEMA kwenye Jimbo hilo hilo na kusema kweli kumekuwa na mazungumzo mengi ya changamoto ambazo wagombea wanawake wanakumbana nazo wanapotaka kugombania nafasi za uongozi wa kisiasa. Lakini nataka kusikia kutoka kwako, yaani maana yake ni nini kwa hapa Tanzania kuwa mgombea mwanamke na mpinzani au mtu ambaye anatoka upinzani? Kwa sababu wewe ulikuwepo kwenye 2020, kinyang’anyiro cha 2020 na tunafahamu changamoto ambazo ulipitia ni nyingi sitaki kuzisema hapa lakini nataka useme wewe mwenyewe, what does it mean to be a female opposition candidate in Tanzania? 

Catherine Ruge: Ni majanga, unaelewa, yaani sijui hata nitumie neno gani. Yaani sio kitu rahisi kuwa mgombea mwanamke halafu unatokea upinzani. [Unakuwa] unapambana na vitu vingi. Mosi, inabidi upambane na utamaduni, umeelewa? Upambane na utamaduni. [Utamaduni] namaanisha mila, imani na desturi [zilizopo] kwenye jamii zetu. Kwamba mwanamke hana uwezo wa kuwa kiongozi. Na hiyo unaweza kupambana nayo kuanzia kwenye ngazi ya familia, unaelewa, kwa sababu naweza kukupa mfano.

Mimi binafsi tu kutoka kwenye familia [nilipata changamoto]. Kwa sababu familia yetu sisi ni kubwa sana. Baba yangu alikuwa ana wake watatu, unaelewa, mimi mama yangu ni mke wa pili. Kwa hiyo, kuna ishu za ndo za mitara, unaelewa, kwa hiyo mule mule kwa baba yako kuna kuwa kuna changamoto wanakuona kwamba wewe huwezi, bado kuna baba wakubwa, kuna baba wadogo, unaelewa, watoto wa shangazi, binamu. Mule mule [kwenye familia yenu] unaanza kupata changamoto kwamba yaani wanakuwa kama hawakuamini. [Utasikia wanasema]: “Kwa nini usigombee viti maalumu, unaenda jimboni, tena kwa upinzani? Huwezi kutangazwa.”

Kwa hiyo, bado kunakuwa na ile imani kwamba mwanamke hawezi lakini bado kuna ile imani kwamba ukiwa upinzani huwezi kutangazwa. Kwa hiyo, kwanza unaanza kupambana na mfumo dume, unaanza kupambana na imani na desturi [za mfumo dume]. Mfumo dume unapambana na wanaume ndani ya chama na utakuja pia kuukuta mfumo dume kwenye jamii kwa ujumla, [yaani] wapiga kura wote. Sasa kwenye kura za maoni mimi nilipambana na wagombea wengine wanaume watano siyo mchezo. Kwa hiyo kwenye kura za maoni unapambana na wanaume kwa hiyo bado unajiona mnyonge.

Lakini wapiga kura [nao wana changamoto zao]. Kwa mfano, jimbo ninalotoka asilimia 80 ya wapiga kura walikuwa wanaume, asilimia 20 tu ndo wanawake, unaelewa? Kwa hiyo, haikuwa jambo rahisi [kugombea]. Cha kwanza unaanza kupambana na mfumo dume [ambayo ni] asilimia 80 ya wapiga kura wako ni wanaume, wanakwambia, “Wewe mwanamke utatwambia nini?” Umeona. Wanasema, “Hatuwezi sisi kuongozwa na wanawake sisi kwenye utamaduni wetu.” Walikuwa wanasema kabisa hivyo, yaani, [wanasema], “Sisi hatuwezi kuongozwa na mwanamke, hatuwezi kuongozwa na Msaghane.” Msaghane ni mtu ambaye hajakeketwa.

Kwa hiyo, unaona hapo unapambana na mila na desturi [na] unapambana na mfumo dume. Mimi walikuwa wananiambia, “Hatuwezi sisi kuongozwa na Msaghane,” [yaani] mtu ambaye hajakeketwa. Kwa hiyo, hiyo tu inakuvunja moyo. Lakini mimi nilikuwa imara sana. Yaani mimi ili uweze kunivunja moyo inabidi ufanye kazi kubwa sana kwa sababu nimeshavunjwa vunjwa katika safari yangu karibia miaka ishirini na tano [ya harakati]. Nimevunjwa vunjwa hapa kati kati kwa hiyo imefika mahali siwezi kuvunjika tena yaani huwezi kunivunja kwa maneno.

Lakini nikatumia ushawishi wangu, nikawa nawaelezea nawajengea hoja kwa nini wanichague mimi, kwa nini wanichague mimi kama mwanamke. Nawaambia, “Mimi ni mama, mimi ni mwanamke mimi na mama, mimi ni mlezi natambua changamoto za makundi yote za wanawake, za watoto, za wanaume za wazee kwa hiyo nitawasaidia. Lakini tumekuwa na wabunge wangapi kwenye historia ya nchi yetu?  Kwenye historia ya jimbo letu? Tumekuwa na wabunge wangapi wanaume niambieni wamefanya nini? Mimi nimekuwa mbunge wa viti maalumu miaka mitatu nimefanya hiki na hiki na hiki na nilitengeneza vitu ambavyo nimenunua nikagawa jimbo zima.”

Kwa hiyo, wakawa wanaambizana, “Nyie kama huyu alikuwa mbunge wa viti maalumu amefanya hivi, amekuwa mbunge wa viti maalumu wa mkoa mzima wa Mara katika jimbo letu amefanya haya, basi huyu atatusaidia akiwa mbunge wa Jimbo. Kama alikuwa anaweza kutembelea majimbo yote kumi aangalie changamoto hivi akiwa mbunge wa Jimbo moja tu la Serengeti akili yake yote iwe hapa, nguvu zake zote ziwe hapa atafanya mambo mengi.”

Na mimi nilikuwa nimefanya vitu vinavyoonekana. Nimejenga mabweni. Nimejenga shule. Nimesidia kama kuna hospitali nimepeleka mabati, nimepeleka saruji, unaona? Nimejenga madarasa kwenye shule ambazo zilikuwa zinahali mbaya. Kwa hiyo, mimi vitu vyangu vilikuwa vinaoneka kwa macho, unaweza kuona. Na nawambia, “Mimi sikuwa na mfuko wa jimbo nilikuwa natumia pesa zangu za mshahara. Kwa hiyo nikiwa na mfuko wa jimbo nitafanya zaidi. Nitakutana na watu. Mimi ni msomi nitaandika proposal. Niliandika proposal nimejenga hili bweni, nimeandika proposal nimejenga haya madarasa nini nitashindwa?”

Kwa hiyo, mimi walikuwa wananitukana kweli kabisa. Walikuwa wananitukana na ninamshukuru Mungu alikuwa ananipa hekima nilikuwa siwezi kupanda jukwaani nikamtuka mgombea mwingine lakini fikiria waliokuwa wananituka mimi ni wanawake wenzangu. Kwa hiyo, wanaume walikuwa wanawapa maneno ya kuongea wanawake wanapanda jukwaani wananambia wewe, samahani kusema hivi, ashakumu sio matusi, “Huyu ni malaya tu, Msaghane hajakeketwa atakujaje kutuongoza? Aende akatafute bwana aolewe, aende akalee watoto.” Hayo ndio maneno ambayo nilikuwa nayapata.

Lakini bado nilikuwa napata changamoto kutoka kwenye Dola au Serikali. Yaani sasa nakuja kwamba ni mgombea wa upinzani. Mimi, kati ya wabunge nadhani waliopata changamoto, hasa wabunge wanawake, wagombea ubunge wanawake, nadhani mimi naongoza. Toka siku ya kwanza kabisa naenda kurudisha fomu ya chama nilipigwa mabomu msafara wangu ulitawanywa. Siku narudisha fomu nilisindikizwa na vijana wenye bodaboba 246, watu zaidi ya elfu moja ikawa ni changamoto nikakamatwa, nikaja tena nikakamatwa tena nikapigwa na polisi nikawekwa ndani nipo kwenye kampeni nikafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi.

Mimi nilipigwa mpaka mimi sasa hivi nina shida [hapa] wanaita lower west. Nina shida kabisa, tatizo kubwa ambapo nikipata hela itabidi niende nje kwa ajili ya matibabu sababu ni tatizo. Kwa sababu nilipigwa na ile wanaita kitu gani kama ile nanii ya kuchezea baseball kama unaijua, sio rungu lakini ni kama rungu ina kitu fulani kinene mbele [kama hii]. Mimi nimebebwa, siwezi hata kutembea, nimebebwa napelekwa kwa [Mkuu wa Jeshi la Polisi] IGP [Simon Sirro] kwa sababu ilikuwa kesi mbaya [kiasi ya kwamba] siwezi kutembea.

Nimebebwa, nikatoka nikapelekwa hospitali, IGP akasema mpelekeni hospitali, nimepelekwa hospitali nimelazwa kesho yake wanakuja kunichukua wakanibeba wanaenda kunisomea makosa ya uhujumu uchumi, unaweza kuamini hilo? Kwa hiyo, na kosa ni kwamba nilienda kudai mabadiliko ya ratiba [ya kampeni] kwa Mkurugenzi [wa Uchaguzi] na nikasema mimi siondoki hapa mpaka unipe barua kwa sababu wewe kuniambia kwamba CCM wamekataa niandikie CCM wamekataa ili mimi nikate rufaa kwa sababu niliumwa kwa siku tatu nikalazwa, daktari akaniambia nipumzike siku nyingine tatu.

Kwa hiyo, siku sita sikufanya kampeni, ratiba imebadilika yaani mikutano sijafanya karibia 12 maana nilikuwa nafanya mikutano miwili kwa siku. Kwa hiyo, lazima nibadilishe ratiba hawataki kunibadilishia ratiba. Hapo kati kati mikutano yangu inazuiliwa kila siku, kugombana na Polisi, vyombo vyangu [vya kampeni] vimekamatwa vipo Polisi, watu wangu wamekamatwa yaani mimi Polisi pale ilikuwa ni kama ni kila siku naenda ni kama sijui wapi, sehemu unayoenda kila siku.

Watanikamata asubuhi watanitoa jioni, wakinikamata jioni watanitoa asubuhi yaani hayo ndo yalikuwa maisha yangu kwenye kampeni. Nisipokamatwa mimi, watu wangu wanakamatwa. Ni lazima niende asubuhi. Nilipoteza muda nashindwa kwenda kwenye mikutano maana lazima nikawatoe watu wangu, unaona? Kwa hiyo, jamani tuna matatizo.

Siku ya uchaguzi jamani sasa ndio usisema mabomu jimbo zima, hata kwenda kwenye kituo cha kuhesabia kura mimi nimeenda wameshahesebu kasha sita na mawakala wametolewa. Siku hiyo pia ya uchaguzi nilikamatwa niliwekwa ndani takribani masaa mawili, [mimi] na watu wangu kisa nimeuliza tu kuna diwani wa viti maalumu alikuwa anaenda kuwaandikia watu zaidi ya kumi, mtu mmoja anaingia anaandika anatoka anaingia kwenye kituo fulani haulizwi, hafanywi nini. Kwenda kuuliza imekuwa shida. Kwa hiyo, nikapandwa na hasira nikampiga kibao yule dada, yaani unajua nilishikwa na hasira yaani huwezi kuelewa kwa sababu nilikuwa naona kabisa nnaibiwa uchaguzi mbele ya macho yangu. Kwa hiyo, wakaniweka kwenye kituo kama masaa mawili baadae wakanitoa, unaona? Kwa hiyo, kwa kweli nimepitia mambo mengi machafu.

The Chanzo: Na hapo maana yake ujumbe ninao upata ni kwamba ukigombea kama mwanamke ambaye pia ni kutoka chama cha upinzani unapata kile wazungu wanaita double jeopardy, kwamba kwa upande mmoja kuna jamii ambayo mfumo dume umekita mizizi lakini kwa upande mwingine una dola. Kitu ambacho kusema kweli pengine mtu ambaye anagombea, mwanamke anayegombea kupitia chama tawala changamoto hii ya kupambana na dola hakumbani nayo, sivyo?

Catherine Ruge: Ndio. 

The Chanzo: Sawa, na labda sasa kwa sasa, labda pengine hivi sasa nchini unatathimini vipi hali ya kisiasa, tunafahamu kwamba BAWACHA kuna harakati nyingi inazifanya kupigania masuala ya Katiba Mpya, Tume Huru [ya Uchaguzi na harakati zingine]. Kwa ujumla tu, unatathimini vipi hali ya kisiasa ya Tanzania, hususan chini ya uongozi mpya wa Rais Samia Suluhu Hassan?

Catherine Ruge: Sawa, labda niseme unajua hamna kitu kibaya kama kuweka mfano ambao ni hasi. [Rais mstaafu hayati John] Magufuli aliweka mfano mbaya sana wa utawala wa kidikteta kwamba nchi hii haina Katiba, haina sheria yoyote. Kwa hiyo, yeye alikuwa anatawala kama mtu mmoja. Anachoamua ndio anafanya. Akiamua leo amfukuze fulani, akiamua leo amfunge fulani, akiamua ambambikizie mtu kesi [anafanya tu] yaani kwa hiyo nchi nzima ilikuwa inaendeshwa na mtu mmoja na sio kwamba taasisi [za utawala] zilikuwa zinajisimamia na kufuata Katiba. Kwa maana Serikali inasimama peke yake, Bunge linasimamia Serikali lakini pia Mahakama inatafsiria sheria na kusimamia haki. Haikuwa hivyo [chini ya Rais Magufuli].

Sasa Samia amekuja, na kwenye siku zake 100 za kwanza alikuwa anajaribu kusafisha, kujaribu kuweka vitu kwenye utaratibu mzuri. Lakini baadae kitu ambacho alisahau ni kwamba anafanya kazi kwenye ule ule mfumo ambao Magufuli alikuwa ameuweka. Kosa kubwa sana ambalo alifanya ni kuamua kuendelea na mfumo ule ule kwamba Baraza la Mawaziri litaendelea kuwa lile lile, akaamua kumbakiza IGP yule yule, [Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama] CDF yule yule, [na] Diwani Athumani [Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa] yule yule mtu wa system.

Kwa hiyo, hizo ndio taasisi ambazo zinakusaidia wewe Rais kufanya kazi zako vizuri. Sasa kwa nini unaenda kufanya kazi kwenye mfumo ambao ulikuwa unaamini kutokufuata sheria kwa miaka mitano, kutokufuata Katiba kwamba hii ndio uwe mtindo wa maisha, ndio mfumo wa kuendesha nchi wewe unaiacha halafu wewe unataka peke yako, mtu mmoja, uwabadilishe wale watu na mfumo ubadilike? Haiwezekani. Kwa hiyo, akajikuta na yeye sasa hana chaguo jingine kwa sababu yeye ndio mtu mmoja kwenye hilo kundi la watu wengi akajikuta anarudi kwenye mfumo ule ule wa Magufuli ambao unanyima haki kwa vyama vya siasa kwa kuwazuia wasifanye shughuli za kisiasa, kukanyaga Katiba, kufunga watu akiaamini kwamba hiyo itafanya kazi.

Kitu kingine ambacho watu wanaofanya nao kazi wanataka kuhalalisha ni kwamba Magufuli alikuwa sahihi, yaani wanataka kuhalalisha kila kitu alichokuwa anafanya Magufuli ni sawa sawa. [Kitu] ambacho sio sawa. Huwezi kuendelea na aina ya uongozi ambayo ni mbaya, inaumiza watu, na unanyima watu haki. Bunge asilimia 99 ni bunge lililoingia bungeni kwa mtutu wa bunduki. Bunge nchi zote ni Bunge linalotetea wananchi. Lakini hapa Tanzania imekuwa tofauti. Bunge linaitetea Serikali hivi uliona wapi?

Eti wananchi wanalalamikia tozo, mbunge anasimama, badala ya kuwatetea wananchi wanaoumia anaitetea Serikali kwamba ni lazima tutoze tozo tuumie maumivu kwa muda mfupi tutapata hela tutafanya nini. Mwingine anakuja kufanya mahesabu kwamba hizi hela tutajenga vituo vya afya tutafanya hili. Tumekusanya kodi miaka sita unashindwa kujenga mashimo ya vyoo, unashindwa kujenga vituo vya afya unafikiri tozo za miamala ya simu itakusaidia? Kwanza, [tozo zenyewe] si endelevu, yaani sustainable.

Kwa hiyo, mimi ninachotaka kusema ni kwamba hakuna haki, hakuna utawala wa kidemokrasia. Leo unaweza ukamuweka kiongozi mkuu wa upinzani jela bila kosa. Unamkamata kihuni, hutaki wanawake wafanye mazoezi, yaani jogging. Nilikuwa Njombe, nilikuwa na ziara Kanda ya Nyasa na kikao cha Tunduma kimevurugwa na Polisi nadhani umeona kwenye mitandao ya kijamii kimevurugwa na Polisi, hata RPC [wa Songwe] ni mwanamke amekuja kusema, mpo kwenye mkoa wangu. Mkoani kwako? Songwe siyo mkoa wako. Sio mkoa wako, ule ni mkoa wa watu wa Songwe wewe sijui umetolewa uko wapi kwanza sio mtu wa Songwe. Halafu anakuja kusema mkoani kwangu, unaona? Fikiria basi hicho kiburi kwamba ni mkoani kwangu, unaweza kufikiria? Kwamba sio kwamba yupo pale kwa niaba ya wananchi, yeye anachukulia kwamba Songwe ni mkoa wake anaumiliki na anaweza kufanya maamuzi yoyote juu ya mkoa husika, hebu pata hiyo picha?

Tukaenda ofisini tukafanya kikao. Jana tunakuja Njombe tukakubaliana tunakuja Njombe nipo njiani sijafika Njombe napigiwa simu naambiwa kwamba, “Polisi wamekuja wamekutafuta. Wametuambia tuondoke. Wametuambiwa tuondoke na hatuwezi kufanya kikao hatuna kibali.” Sasa nikawauliza, hiki ni kikao cha ndani tunaombaje kibali? Bahati nzuri kuna dada mmoja yupo pale ni mwanasheria, yule dada anaitwa Singrada, hii ni mara ya nne nadhani anakamatwa. Akaanza kujibishana nao kwa hoja, unaona? Kwa hiyo, walivyoona anawazidi hoja wakamkamata. Yaani, badala ya wao wamjibu kwa hoja wakamkamata. Akawa anawapa rejea kutoka kwenye Katiba, akisema kwamba hakuna sheria inayozuia vikao vya ndani, kwa hiyo walichokifanya kuwaogopesha wale wanawake waondoke wakamkamata na wale wanawake wakaogopa wakaondoka. Mimi nikafika pale ofisini nikafanyia kikao ofisini, unaona? Kwa hiyo, unaweza ukaona bado utawala wa Magufuli bado unaendelea yaani kuna kivuli cha Magufuli kinaendelea. 

The Chanzo: Sawa sawa. 

Catherine Ruge: Watu bado wanataka kuhalalisha kwamba kile [Rais Magufuli] alikuwa anakifanya ilikuwa sahihi. [Kuhusu hoja ya kwamba] tuna Rais mwanamke, ngoja nizungumzie kuhusu Rais mwanamke anavyokandamiza haki. Mimi siamini eti kwamba Samia haoni vitu vinavyotokea. Anaona. Kwa sababu yupo kwenye mitandao ya kijamii, magazeti yanandikwa, watu wake wanampa taarifa, vyombo vya ulinzi na usalama vinampa taarifa.

Eti leo unawazuia wanawake wasifanye mazoezi [kwenye] nchi ambayo inaongozwa na mwanamke, wanawake wanakandamizwa, hii maana yake ni nini? Haheshumu haki za wanawake ambazo ndio haki za binadamu, unaona? Mimi naona hakuna hata utawala wa sheria, hamna haki hamna demokrasia. Unaona waandishi wanakamatwa, wachora vibonzo wanakamatwa. Kwa hiyo, hamna uhuru wa vyombo vya habari, hakuna uhuru wa kujieleza na hakuna demokrasia.

The Chanzo: Nataka kukuuliza, na umegusia kwa mfano suala la Mwenyekiti wa CHADEMA taifa Freeman Mbowe kukamatwa na sasa hivi tunafahamu yupo rumande wakati kesi yake inaendelea, na umegusia Jeshi la Polisi kwa mfano kuzuia nyinyi kufanya vikao vya ndani, kufanya hizo jogging na kufanya shughuli zenu kama za chama. Unadhani ni kwa kiasi gani hizi hatua zinaathiri ujenzi wa chama chenu kama chama cha upinzani? 

Catherine Ruge: Zinatuathiri kwanza kumuweka Mwenyekiti ndani. Unajua Mwenyekiti ndio anatoa muongozo, Mwenyekiti wa taasisi yoyote, chama chochote. Kwa hiyo, kwa kiongozi wetu mkuu kuwa ndani kwa kweli inatuathiri sana kwa sababu mnakosa ile dira, miongozo, ushauri wake. Kwa hiyo, tunaathirika na kuna baadhi ya maamuzi hamuwezi kufanya bila kumshirikisha Mwenyekiti.

Kwa hiyo, inaweza ukafikia pengine tuna maamuzi ya kufanywa lakini inabidi icheleweshwe mpaka tumshirikishe Mwenyekiti na inachukua muda mpaka uende kule [gerezani] lakini bado kule [nako] hauko huru [kuongea naye kwani] unaongea nae na maaskari wako hapa. Kwa hiyo, kuna vitu vingine ambavyo ni siri unaweza usiwe tayari kuweza kuviongea mbele ya Mwenyekiti.

Lakini ile hali ya yeye kuwepo ndani tu inatuweka kwenye taharuki, yaani inatuweka kwenye hali fulani ambayo tunakuwa hatuna furaha. Hatuna furaha. Yaani unakuwepo kwenye hali ambayo nakosa lugha ya kuielezea. Lakini ni hali ambayo inatuweka kwenye taharuki. Yaani hatupumui kuona kuona Mwenyekiti yupo ndani. Lakini pia haya mambo ya kukamatwa wanawake [niyasemee nayo]. Unajua wanawake siyo watu wa fujo. Haya masuala ya kukamata yanaathiri sana wanawake.

Kwa mfano, mimi naona kwa sababu mimi ni Katibu wa Baraza la Wanawake, nashughulika na wanawake kila siku. Kwa mfano ikitokea watu mna shughuli leo, watu wakikamatwa halafu mkawa mnashughuli wiki inayofuata ukiwaita wanawake watajitokeza wachache, mahudhurio yatakuwa hafifu kwa sababu unakuwa unawajengea uoga. Na sio tu wanawake hata wanaume kwa sababu, kwa mfano, sasa hivi watu ambao wapo kwenye mstari wa mbele ni wanawake lakini wanaume si wapo? Kwa mfano, CHADEMA si kuna wanaume kina [Baraza la Vijana CHADEMA] BAVICHA kuna [Baraza la Wazee CHADEMA] BAZECHA. Lakini bado pamoja na kwamba wanawake wanaogopa lakini bado sisi tumeendelea kuwa wajasiri ukilinganisha na wanaume, umeelewa? Kwa hiyo [haya mambo] yanaathiri sana, yanaweka uoga na vitisho kwenye nyoyo za wanachama. 

The Chanzo: Na Unazungumziaje haya yote kwenye muktadha, unajua Disemba 9 mwaka huu Tanzania itakuwa inatimiza miaka 60 tangu ipate uhuru wake. 

Catherine Ruge: Inatimiza miaka 60? 

The Chanzo: Miaka 60 ndio. Kwa hiyo unazungumziaje uhuru ambao tumeambiwa tumeupata kutoka kwa wakoloni kwenye muktadha wa kile ambacho wanawake wa CHADEMA au CHADEMA kama chama kwa ujumla kinakumbana nacho kutoka kwenye vyombo vya dola hapa nchini? Unadhani tuna huo uhuru ambao tumeupata kutoka kwa wakoloni wa kuweza kujiamulia mambo yetu wenyewe kama wananchi? 

Catherine Ruge: Hapana, kwani hakuna uhuru bila haki. Hakuna amani bila haki. Kwa hiyo, pamoja na kwamba tunasherehekea, tunasherehekea tu kama maadhimisho. Ni kama tunasherehekea maadhimisho ya ndoa lakini huko ndani ndoa chungu. Kwa hiyo, unahesabu tu miaka lakini ndani huko unapambana, unalia, unapigwa, maisha magumu unanyanyasika. Kwa hiyo, ndio kinachotokea. Mwanamke ananyanyasika [kwenye ndoa] ni sawa na sisi Watanzania tunanyanyasika, hasa vyama vya upinzani maana sisi tumekuwa tukifanywa kama raia daraja nambari mbili.

Kwa hiyo, ninachoweza kusema ni kwamba bado kama nchi tuna fursa, hususan chini ya Rais mwanamke kutengeneza Tanzania mpya yenye uhuru, yenye haki, [na] yenye demokrasia. Yaani bado tuna hiyo fursa. Mama Samia, kama Rais, bado ana hiyo fursa yeye kama mwanamke, kama mama, na sisi wanawake tumejaliwa karama mbalimbali na mwenyezi Mungu ambazo tunaweza kuzitumia kuendesha jamii, kuendesha familia, na kuendesha nchi

Kwa sababu nchi ni kama familia yako. Kwa hiyo, [kama kiongozi ujiulize] unaweza kuifanyia familia yako kama wewe ni mama ni mama wa Tanzania mama wa Watanzania wote. Sasa jichukulie, je, jinsi ambavyo unavyowafanyia wananchi wa Tanzania ni sawa sawa unavyowafanyia watoto wako? Kwa hiyo, kama unawafanyia watoto wako vizuri unaweza  kuwafanyia pia wananchi vizuri.

Kwa hiyo, bado mimi nadhani [Rais Samia] achukue hii fursa ya tunavyoenda kusherekea miaka 60 ya uhuru aweze kutafakari kama kweli hivi kweli hii Tanzania ni huru, tunasherehekea kweli kile ambacho tunakiishi?  Tunasherehekea uhalisia ulioko huko nje? Ni kweli tuna uhuru hii miaka sitini tunayosherekea kweli ni uhuru kweli kweli? Kwa hiyo, bado tuna uhuru wa kukaa, kutafakari na kuamua kubadilisha hiki kilichopo, kubadilisha huu mfumo uliopo.

[Rais Samia] akae kwenye meza ya mazungumzo na wapinzani. Sisi ni washirika wake. Maana sisi ni washirika wake. Sisi sio adui. Sisi ni washirika wa Serikali. Sisi sio adui. Sisi ni Serikali inayosubiri muda wake, yaani the government on waiting. Sisi tunatoa sera mbadala kwa Serikali na umeona mambo mengi ambayo sisi tumeyazungumza hasa tukiwa bungeni, Serikali imeyafanyia kazi.

Kwa hiyo, sisi tunaisaidia Serikali kufikia malengo na hivyo kuisadia kuleta ustawi kwa wananchi. Sasa kwa nini sisi tuwe maadui? Kwa hiyo, bado [Rais Samia] ana fursa ya kukaa na wapinzani. Akae na viongozi wa upinzani wafanye mazungumzo na kuangalia namna bora ya kuendesha shughuli mbalimbali za nchi. Pia sisi tuweze kumshauri namna bora ya kuendesha Serikali na ikawa nchi yenye uhuru, haki, demokrasia na amani na tukawa ni taifa lenye furaha kama ambavyo mataifa mengine yapo.

The Chanzo: So, labda kwa kukatisha tu haya mazungumzo ili uendelee na mambo mengine, ukiachana na maisha yako ya kisiasa labda au kwenye harakati, usipokuwepo labda barabarani ukikabiliana na Polisi wanaowazuia kufanya mazoezi, au pengine hotelini unapokabiliana na askari wanaotaka kuzuia kufanya kikao chenu cha ndani, una maisha gani mengine nje ya siasa, pengine una vitu gani unavyovipenda? 

Catherine Ruge: Sawa. Mimi ni mama wa watoto wawili-, unamaanisha maisha nje ya siasa, sivyo? 

The Chanzo: Ndivyo 

Catherine Ruge: Mimi ni mama wa watoto wawili na muda mwingi nakuwa sipo na watoto wangu kwa sababu nakuwa kwenye shughuli za kisiasa, kwenye ziara kwenye nini, nitalala polisi, nipo ndani na nini. Kwa hiyo, muda mchache ninaoupata natumia na watoto wangu. Yaani muda mchache ninaoupata natumia kukaa na watoto wangu. Na mimi ni ni mtu wa kukaa nyumbani. Kwa hiyo, muda mwingi nakuwepo nyumbani na watoto wangu. Napenda kupika. Napikia watoto wangu. Napikia familia yangu.

Na pia napenda kusoma. Mimi siangalii TV, mimi siyo shabiki wa TV. Kwa hiyo, nasoma vitabu vyangu. Nasoma vitu ambavyo vipo kwenye mitandao, vitu ambavyo najua vitanipanua mawazo vitafanya nini. Nasoma taarifa mbalimbali nadhani unaona ninavochambua taarifa mbali mbali. Kwa hiyo hivyo ndo vitu nafanya kwenye maisha yangu nje ya siasa. Napenda kulala pia, sio uvivu lakini kwa sababu nakuwa sipati muda mwingi wa kupumzika. Kwa hiyo, kama nikipata muda napumzika, siyo kulala usingizi lakini napenda kukaaa kitandani. Nakipenda sana kitanda changu. Baada ya watoto wangu ni kitanda changu.

The Chanzo: Nashukuru sana Catherine kwa muda wako na kusema kweli kuja kwenye podcast yetu na kuzungumza na wewe na nakutakia kila la kheri kwenye mapambano yako ya kujenga Tanzania ya haki na ya kidemokrasia. 

Catherine Ruge: Asante sana pia na nakutakia Jumamosi njema.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 responses

  1. Interview nzuri. Majibu ya kina. Yana funzo hasa kuhusu mtu kujisimamia dhidi ya kitu asichotaka, na kufuata njia aliyokusudia. Catherine ametoa mfano kwa wengi.

    Asante The Chanzo!

  2. Nimefurahia sana mazungumzo yenu. Asante sana kwa Catherine na pia kwako ndugu Khalifa.
    Tuletee mahojiano mengi mengine kama haya.
    Asante sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts